Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Viumbe Wanaoruka wa Baharini

Viumbe Wanaoruka wa Baharini

Viumbe Wanaoruka wa Baharini

HUNYIRIRIKA kwa madaha katika maji ya mwambao karibu na visiwa vya bahari. Wanaweza kupatikana katika vilindi vya bahari, ziwe zina maji yenye uvuguvugu au baridi, na hata katika maziwa na mito fulani. Ni nani hao? Ni jamii ya taa, viumbe wa baharini ambao huonekana ni kana kwamba wanaruka!

Si lazima uwe mpiga-mbizi au mvuvi ili ufurahie uzuri wa taa anayeruka, wala si lazima uwe majini. Kama asemavyo Bart, mwanabiolojia wa viumbe wa baharini, mara nyingi watu wanaoenda ufuoni huona taa wenye mabawa wakiruka kutoka majini.

Kuna mamia ya aina za taa, walio na ukubwa mbalimbali, kuanzia sentimeta chache hadi meta kadhaa. Unaweza kuona wanafanana na papa, kiumbe wa jamii yao. Mayai ya taa, tofauti na ya samaki wengi, hutungishwa ndani ya mwili wa taa wa kike. Skate, ambao ni washiriki wa jamii ya taa hutaga mayai yaliyotungishwa, ilhali mayai ya taa wengine huanguliwa ndani ya mwili wa kike na wachanga huzaliwa wakiwa hai—samaki wachanga wanaofanana kabisa na wazazi wao.

Miongoni mwa aina inayojulikana sana ni taa aina ya stingray, wenye mwili ulio na gegedu bila mifupa, na pezi kila upande linaloanzia kichwani hadi mkia uanziapo. Stingray wanaweza kuwa na umbo la almasi au la mviringo, au wanaweza kuonekana kama tiara yenye mkia. Miili yao iliyo bapa mara nyingi hushindwa kuzuia nguvu za maji. Mwendo wa mapezi yao ulio kama mawimbi huwapa nguvu za kunyiririka majini kana kwamba wanaruka bila kujisukuma. Taa wanapokuwa hawaogelei, hulala na kujificha kwenye sehemu ya chini ya bahari yenye mchanga.

Macho ya stingray yako juu ya vichwa vyao, ilhali midomo yao iko chini. Wana meno magumu na taya zenye nguvu, zinazowawezesha kurarua makaka. Ndiyo sababu hawapendwi mahali ambapo chaza huzalia, kwa kuwa wao hupenda kula samaki-gamba. Stingray huliwa na wanadamu na nyakati nyingine hutumiwa kwa chakula badala ya makombe ya pwani.

Jina lao la kuwatofautisha stingray latokana na miiba yenye sumu kwenye sehemu ya juu ya mkia wao mrefu. Miiba hiyo yaweza kuchoma kwa uchungu na kutoa sumu taa huyo anapokanyagwa, asiposhikwa kwa uangalifu, au anapotishwa na adui. Mara nyingi miiba hiyo huvunjika ndani ya vidonda, na kufanya iwe vigumu kuitoa, na inaweza kusababisha maambukizo mabaya kidonda hicho kisipotibiwa vizuri. Ikiwa utawahi kuchomwa na taa, osha sehemu hiyo vizuri kwa maji—maji ya baharini ikiwezekana. Loweka kidonda ndani ya maji moto kabisa kadiri uwezavyo, na upesi iwezekanavyo. Maji moto hukomesha sumu hiyo na kupunguza maumivu. Kisha mwone daktari mara moja.

Ingawa mikia yao yenye miiba yaweza kukutisha, kwa kawaida stingray si wachokozi na hutumia mikia yao wakati tu wanapotishwa. Bart, aliyetajwa mwanzoni mwa makala, aliona stingray kuwa wenye urafiki wakati yeye na mke wake walipoogelea nao katika Visiwa vya Cayman kwenye eneo ambapo yasemekana taa wenye urafiki huogelea. Aripoti hivi: “Tulikuwa tukipiga magoti chini, katika maji yenye kina cha meta tano hivi. Tulipoanza kuwalisha, stingray walituzingira! Labda kulikuwa na stingray 30 au 40 wa saizi zote waliozingira kikundi chetu. Taa hao walianza kutafuta chakula kuanzia magotini mwetu na kuelekea kifuani na mgongoni na juu ya vichwa vyetu, wakiogelea kwa uanana na kutusumbua tuwape chakula hata ikiwa ni kidogo sana. Ilishangaza kuona jinsi viumbe hao wazuri wanavyoweza kutiishwa. Hata walitulia tuliposugua tumbo zao walipokuwa wakituzunguka.” Bart alitaja kwamba taa hao wamejitiisha sana hivi kwamba katika miaka yote ambayo watu wamekuwa wakiogelea pamoja nao, hakuna mtu aliyewahi kushambuliwa.

Wale ambao miongoni mwetu si wapiga-mbizi wazoefu waweza kufurahia taa kwenye maji yasiyo na kina au kwenye matangi-samaki ulimwenguni pote. Matangi-samaki mengi yana sehemu ambazo unaweza kugusa-gusa stingray, lakini miiba yao imeondolewa ili kuzuia hatari. Ron Hardy, mmiliki wa Gulf World, katika Panama City, Florida asema hivi: “Mojawapo ya mifano bora tuliyo nayo ya uwezo wa kuonyesha wanyama walio hai ni kidimbwi chetu chenye stingray wanaoweza kuguswa-guswa. Yaonekana watu huogopa sana stingray lakini utaona wakibadili maoni yao wajifunzapo habari kamili kutokana na simulizi letu! Baada ya kugusa mmoja, wanaanza kustaajabia uzuri wa taa. Kwa kweli, hata wengine hukosa kuona maonyesho ya dolfini, ambayo hufuata baada ya hapo, ili waendelee tu kugusa-gusa stingray.”

Labda kwa kuwa sasa umejifunza habari fulani kuhusu taa, woga wako umepungua. Hata hivyo, kumbuka kwamba mara nyingi hujificha kwenye sehemu ya chini yenye mchanga isiyo na kina, na iliyo na maji yenye uvuguvugu. Kwa hiyo unapotembea kwa shida katika sehemu kama hizo, kokota miguu yako badala ya kuiinua. Kwa njia hiyo utawaonya taa kwamba unakaribia na hivyo utaepuka kukanyaga taa na labda kuumwa na kiumbe huyo mzuri anayeruka wa baharini.

[Picha katika ukurasa wa 16]

“Stingray”

[Picha katika ukurasa wa 16]

Yaonekana watu huogopa “stingray,” lakini mtazamo wao hubadilika wanapojifunza habari kamili kuwahusu

[Picha katika ukurasa wa 17]

“Manta ray”

[Hisani]

© Francois Gohier/ Photo Researchers