Inategemea Dhamiri
Inategemea Dhamiri
SINEMA mashuhuri ya 1944 Arsenic and Old Lace ilionyesha jinsi wanaume wazee-wazee fulani walivyokufa haraka baada ya kunywa divai ya msambuku iliyoongezwa aseniki. Sinema hiyo ni mfano halisi wa maoni yaliyo ya kawaida kwamba sikuzote aseniki ni sumu hatari, inayotenda kazi haraka. Kwa kweli, vifo vya ghafula vilivyoonyeshwa kwenye sinema hiyo havikusababishwa na aseniki, bali na sumu kali ya kusisimua neva na sianidi ambazo ziliongezwa pia kwenye divai hiyo.
“Athari za sumu ya aseniki hazidhihiriki mara moja,” asema Dakt. Robert E. Gallagher katika kichapo The New England Journal of Medicine. Hata hivyo, aongezea kwamba “sumu ya aseniki inayosababishwa na maji machafu ya kunywa na vichafuzi vya viwandani ni tatizo kubwa linalokumba afya ya umma katika sehemu nyingi za ulimwengu, ambako hufanya watu wapatwe na maradhi mbalimbali, kutia ndani kansa ya ngozi, kibofu, mapafu, na ini.”
Kwa kufikiria habari iliyo juu, unaweza kuelewa ni kwa nini si jambo la kawaida kwa wanatiba kumpatia mtu dawa ya aseniki. Lakini chunguza kwa uangalifu jambo hili lililoonwa kutoka Kanada. Ona jinsi dhamiri ya mgonjwa mmoja anayeitwa Darlene, ya madaktari wake, wauguzi na mfamasi aliyehusika ilivyotofautiana wakati ilipopendekezwa kwamba atiwe damu mishipani kisha atibiwe kwa aseniki. Darlene asimulia kisa chake kama ifuatavyo.
“Katika Mei 1996, nilikuwa na matatizo fulani ya kuchubuka sana, kuvuja damu, na kutokwa damu kwenye ufizi isivyo kawaida. Mtaalamu wangu wa damu Dakt. John Matthews, katika Kingston, Ontario, alipima tatizo hilo na kusema kuwa ni kansa hatari sana iliyo nadra iitwayo promyelocytic leukemia (APL). Baada ya kunipima mara kadhaa, kutia ndani kupima mafuta ya mifupa, kwa fadhili Dakt. Matthews alieleza maana ya APL na jinsi ya kutibu ugonjwa huo. Mpango wa kawaida wa tiba ulihusisha kubadilishwa damu pamoja na tiba ya kemikali, lakini dhamiri yangu iliyozoezwa na Biblia haingeniruhusu nikubali kutiwa damu mishipani.
“Badala ya kupoteza wakati wenye thamani kwa kujaribu kunifanya nibadili msimamo wangu, madaktari walitumia hekima na kutafuta tiba ya aina tofauti. Tiba hiyo iliyorekebishwa ilihusisha kitu kilichotokana na vitamini-A, pamoja na tiba ya kemikali ya kiasi. Ugonjwa wangu wa damu ulitulia kwa miezi mitatu, kisha ukarudi kwa nguvu sana. Singeweza kuvumilia maumivu ya kichwa yaliyosababishwa na kuvimba kwa ubongo. Zaidi ya hayo, tiba hiyo haikuwa ikifanya kazi mwilini mwangu. Wakati huo ndipo daktari alipotuambia kwamba ikiwa sitatiwa damu mishipani basi sitatibiwa. Tuliambiwa kwamba ningeishi kwa muda unaopungua majuma mawili.
“Siku chache zilizofuata zilikuwa za majonzi, huku nikipimwa damu mara nyingi zaidi, na kumtembelea wakili ili kuzungumzia wasia wangu, na mipango ya maziko. Katika kipindi hicho, Dakt. Matthews alituambia kuhusu tiba fulani isiyo ya kawaida ambayo imetumiwa kwa mafanikio na madaktari wa kitiba wa
China kutibu APL, na ambayo iliripotiwa katika majarida mashuhuri ya sayansi kama vile Blood na Proceedings of the National Academy of Sciences. Walipokuwa wakifanya utafiti, daktari huyo na mwenzake walikuwa wamesoma katika jarida fulani la kitiba kwamba ‘huenda wengi wakashangaa kujua kwamba aseniki trioksidi imetumiwa kwa mafanikio kwa kutiwa mishipani, bila kusababisha sumu, ili kutibu maradhi hatari ya promyelocytic leukemia (APL).’“Sasa nilihitaji kuchagua kati ya mambo mawili—ama nikiuke dhamiri yangu na kukubali kutiwa damu mishipani au nikubali dawa hii isiyojulikana sana yenye aseniki. Nilichagua dawa ya aseniki. * Sikujua kwamba jambo hilo lingesumbua sana dhamiri za madaktari, wauguzi, mfamasi, na hata maofisa wa hospitali.
“Baada ya hapo wafanyakazi wa hospitali walienda kuhakikishiwa na wenye kuidhinisha matumizi ya aseniki trioksidi kama inaweza kutumiwa. Ndipo wangekubali kutumia tiba hiyo. Hapo mwanzoni mfamasi hakutaka kushirikiana, kwa kuwa alitilia shaka usalama wa dawa hiyo kwa dhamiri safi. Matabibu wangu, Dakt. Matthews na Dakt. Galbraith, walihitaji kutoa maelezo mazuri na yenye kusadikisha kuhusu tiba hiyo. Hatimaye, baada ya kupewa uthibitisho wa kitiba wa kutosha kuhusu tiba hiyo, wasimamizi wa hospitali na mfamasi walihisi kwamba wanaweza kushirikiana.
“Mfamasi alikubali kutayarisha dawa hiyo ya aseniki na kuua vijidudu ili kuitia ndani ya mishipa mara moja. Lakini sasa dhamiri za wauguzi hazingewaruhusu kuangika mfuko wenye dawa hiyo ya kutiwa mishipani yenye kutiliwa shaka. Walikuwa hapo tu wakati madaktari walipoangika lita kadhaa za umajimaji huo. Wauguzi waliniomba nikubali damu. Walikuwa wamesadiki kwamba ningekufa, kwa hiyo niliwaomba watumie ujuzi wao kunitibu na wakati uleule wastahi msimamo wangu wa kudhamiria kukataa damu. Niliwashukuru, nikawakumbatia na kuwaomba wasahau hisia zao. Tulidumisha uhusiano mzuri. Tiba ya aseniki trioksidi iliendelea kwa miezi sita, na nikaendelea kupata nafuu. Kisha madaktari walikubali kwamba ningeweza kuendelea kutumia dawa zilizobakia nikiwa nyumbani.
“Mipango ya kunitembelea nyumbani ilifanywa na Shirika la Wauguzi la Victoria, ambalo huhudumia wagonjwa nyumbani. Kwa mara nyingine tena dhamiri ikahusika. Wao pia walisitasita kunitia umajimaji huo. Mikutano, barua, na makala za kitiba kutoka kwa majarida mashuhuri ya kitiba yalibadili hali. Hatimaye wauguzi walikubali kushirikiana nami. Mnamo Septemba 1997, nilimaliza dawa zangu.
“Ni kweli, kansa niliyokuwa nayo yaweza kunirudia. Daktari anasema kwamba ni kama kuishi katika hatari kubwa sana. Lakini nimejifunza kupata shangwe kila siku, bila kuacha kamwe mahali pangu pa ibada na kuwa na shughuli nyingi katika kushiriki tumaini linalotegemea Biblia kuhusu wakati ambapo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.
Wataalamu wa kitiba wana daraka zito la kuandaa utunzaji bora wa afya. Kwa kawaida wao hutibu watu kwa bidii na kwa kudhamiria kulingana na utaalamu na ujuzi wao wa kisasa. Kama ionyeshwavyo na jambo hili lililoonwa, madaktari, wauguzi, na wataalamu wengine wa kitiba wanaweza kutimiza mengi kwa kuwa wenye kubadilikana na kujali masadikisho na dhamiri ya mgonjwa ambaye ni mtu mzima mwenye ujuzi.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 8 Ingawa gazeti Amkeni! linaripoti jambo hili, haliungi mkono dawa au tiba yoyote hususa.
[Picha katika ukurasa wa 20]
Darlene Sheppard