Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kiungo Kilichotoka Sehemu za Mbali Sana za Dunia

Kiungo Kilichotoka Sehemu za Mbali Sana za Dunia

Kiungo Kilichotoka Sehemu za Mbali Sana za Dunia

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HUNGARIA

“MCHUZI huu ni mtamu kama nini! Uliukoleza kwa kiungo kipi?” Huenda ukaitikia jinsi hiyo uonjapo mchuzi unaoliwa kwa ukawaida katika Hungaria. Ladha yake ya kipekee yatokana na paprika, kiungo kinachotengenezwa kutoka kwa mpilipili ulioletwa Hungaria kutoka sehemu za mbali sana za dunia.

Historia yadokeza asili ya mpilipili kuwa Amerika Kusini. Vyombo vya udongo vinavyopatikana kwenye makaburi ya Wainka—yaaminiwa vimedumu kwa maelfu ya miaka—vimerembwa kwa picha za mpilipili. Pilipili hata zinapatikana miongoni mwa vyakula vilivyozikwa pamoja na maiti zilizohifadhiwa za Wainka.

Baadhi ya wanahistoria huamini kwamba daktari mmoja aliyesafiri Marekani pamoja na Columbus alileta mbegu za mpilipili Hispania katika mwaka wa 1493. Vyovyote iwavyo, Hispania ndiyo nchi ya kwanza katika Ulaya kukuza pilipili kwa kiasi kikubwa. Kutoka huko mpilipili ulifika Uingereza na kusini mwa Ufaransa, ambako ulitumika zaidi kama maua kuliko kikolezo au chakula! Baadaye, wafanya-biashara Wagiriki walipeleka mipilipili kwenye nchi zilizo kando ya Bahari ya Mediterania na Bahari Nyeusi.

Mpilipili umekuwepo Hungaria tangu karne ya 16. Mojawapo kati ya majina yake, “pilipili ya Uturuki,” hudokeza kuwa yaelekea Waturuki ndio waliouleta Hungaria. Kwa vyovyote vile, paprika nyekundu ya Hungaria, inayonukia vizuri, na yenye ladha tamu hupendwa sana na wapenzi wa viungo kotekote ulimwenguni.

Mipilipili husitawi kwenye mashamba tambarare yenye udongo wa hudhurungi wenye mchanga na mwangaza mwingi wa jua. Wakulima hutayarisha mashamba ili kupanda mwishoni mwa kiangazi, baada tu ya kuvuna zao la mwaka uliotangulia. Mipilipili fulani hutokana na mbegu; na mingine hupandwa ikiwa miche. Miche ya mipilipili inayonuiwa kupandwa hukuzwa kwanza kwenye kibanda cha kukuzia mimea chenye mazingira yenye kudhibitiwa. Humo hiyo miche michanga humwagiliwa maji, hutiliwa mbolea, na kupaliliwa kwa uangalifu. Kabla ya kupandwa, miche hiyo huzoezwa kustahimili hali za kawaida hatua kwa hatua.

Baada ya majuma sita au manane, ni wakati wa kuhamisha miche hiyo ya mipilipili hadi kwenye mashamba. Katika Hungaria shughuli hiyo hufanyika mwanzo-mwanzo mwa mwezi wa Mei. Katika kipindi hicho mimea hiyo bado huhitaji kutunzwa kwa uangalifu—ili wakulima wavune zao lenye afya lazima waimwagilie maji, wainyunyizie dawa na waipalilie.

Kuvuna huanza mwishoni mwa mwezi wa Agosti au mwanzoni mwa Septemba. Pilipili mbichi hugeuka na kuwa nyekundu nyangavu ikiisha iva. Iwapo pilipili zote haziivi wakati uleule, basi huvunwa kwa mikono wala si kwa mashine. Bila kujali njia inayotumiwa kuivuna, pilipili hufanyiwa mabadiliko mengi ya sura na ya kemikali kabla hujaitumia kwa mapishi. Kwa mfano, baada ya pilipili kuvunwa, kiasi kikubwa cha umajimaji wake hupotea, na sukari na vitamini C hupungua. *

Baada ya kuvunwa, lazima pilipili ziachwe zikauke na kuiva zaidi. Njia ya kidesturi ya kufanya hivyo imekuwa ni kuzianika kwenye kamba. Hata hivyo, siku hizi imekuwa kawaida kuweka pilipili ndani ya magunia marefu yenye matundu yanayoruhusu hewa kupenya. Magunia hayo huning’inizwa kwenye chaga au ndani ya maghala. Mara tu zikisha iva kikamili, pilipili husagwa hadi kuwa ungaunga ambao hutokeza kiungo kile kitamu sana kinachojulikana kwa neno la Kihungaria la pilipili—paprika.

Aina fulani za paprika zaweza kuwa kali sana, hasa kwa sababu ya kuwapo kwa aina fulani ya kemikali iitwayo capsaicin. Bidhaa hii ya asili hata imetumiwa kuwa dawa ya kutibu maumivu kama ya tumbo na ya viungo. Kwa vyovyote vile, ladha ya kipekee ya paprika—iwe kali au ya kiasi—ni mojawapo tu ya sifa zake. Kwa upande wa umaridadi, rangi ya mlo inayotokana na paprika huvutia macho. Kuku huweza kutaga mayai yenye kiini chenye rangi nyangavu zaidi wanapokula chakula kilichotiwa paprika!

Je, ungependa kuonja mlo uliokolezwa kwa paprika? Kwa nini usijaribu mapishi ya mchuzi wa Hungaria yanayoonyeshwa chini? Sisi Wahungaria husema, jó étvágyat!—furahia mlo wako!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Pilipili moja inaweza kuwa na kiasi cha vitamini C kinachozidi mara tano au sita kile kilicho katika chungwa au limau.

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

MCHUZI WA HUNGARIA

Nyama isiyo na mifupa robo kilo, katakata vipande vidogo vidogo

Mafuta kijiko kimoja kikubwa

Kitunguu kimoja cha kadiri, katakata

Vidole viwili vikubwa vya kitunguu saumu, ponda-ponda

Vijiko viwili vikubwa vya paprika tamu

Chumvi vijiko viwili vya chai

Kisibiti robo kijiko cha chai (ukipenda)

Viazi viwili vya kadiri, osha, menya, katakata vipande vidogo vidogo

Pilipili mbichi ndogo, ondoa mbegu, katakata

Nyanya mbili ndogo, menya, ondoa mbegu, katakata vipandevipande

Gramu 100 za tambi-mayai zilizokaushwa

Pasha moto mafuta kwenye sufuria, kisha ongeza kitunguu. Kaanga hadi kiwe laini. Ongeza kitunguu saumu na paprika, koroga na uongeze maji kidogo ili visiungue. Sasa weka nyama na chumvi na ukoroge vema. Funika sufuria na uache utokote polepole. Koroga mara kwa mara, ongeza maji tu mchuzi unapoelekea kuungua. Ongeza kisibiti ukipenda. Nyama iwapo laini, ongeza pilipili, nyanya, na maji lita mbili. Acha uchemke, funika, acha utokote polepole kwa muda wa dakika 15. Ongeza viazi na acha utokote polepole hadi viazi viive (dakika 10 hadi 15). Weka chumvi ya kutosha. Pakua mchuzi ukiwa ungali moto pamoja na tambi-mayai zilizotayarishwa kando. Waweza kuliwa na watu wanne hadi sita hivi.