Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka Olympia Hadi Sydney

Kutoka Olympia Hadi Sydney

Kutoka Olympia Hadi Sydney

WENGI huiona Michezo ya Olimpiki kuwa mashindano ya riadha yaliyo muhimu zaidi ulimwenguni pote. “Hakuna mashindano mengine ya michezo yanayovutia watu wengi kama mashindano hayo,” chasema kichapo The World Book Encyclopedia. “Mamilioni kadhaa ya watu huhudhuria michezo hiyo, na mamia ya mamilioni ya watu kotekote ulimwenguni huitazama kwenye televisheni.”

Historia Fupi

Michezo ya Olimpiki ilianza maelfu ya miaka iliyopita. Wagiriki wa kale walifanya sherehe za kitaifa zilizochanganya dini na michezo kwa kuwa waliamini kwamba wanariadha walipendeza nafsi za wafu. Michezo hiyo ilitia ndani ile ya Isthmia, Nimea, Olimpiki, na Pithia. Kati ya michezo hiyo, Michezo ya Olimpiki ndiyo iliyokuwa mashuhuri zaidi, kwa kuwa ilimstahi Zeusi, aliyeonwa na Wagiriki kuwa mfalme wa miungu.

Yaonekana kwamba michezo ya awali ya Olimpiki ilikuwa na shindano moja tu, shindano la mbio. Lakini mwishowe ilikuja kutia ndani mashindano mengine, kama vile mbio za magari ya farasi na majaribio makali ya ustahimilivu. Wageni walimiminika kutoka kila pembe kwa ajili ya michezo hiyo. Ili kuhakikisha kwamba wako salama, makubaliano ya kusimamisha vita kwa muda kabla na baada ya michezo hiyo yalifanywa.

Roma ilipoanza kutawala, Michezo ya Olimpiki ilianza kudidimia. Kwa kweli, Waroma wengi walidharau riadha. Lakini Maliki Nero alipenda riadha. Alijiunga na michezo hiyo mwaka wa 67 W.K., na kushinda kila shindano aliloshiriki. Yaonekana kwamba washindani wenzake walimruhusu ashinde ili wasimkasirishe! Kwa vyovyote vile, kufikia mwaka wa 394 W.K., Michezo ya Olimpiki ilikuwa imekomeshwa.

Kuanzishwa Upya kwa Michezo ya Olimpiki

Karne 15 baadaye, mabaki yaliyochimbuliwa na waakiolojia Wajerumani katika uwanda wa Olympia la kale yaliamsha upendezi wa watu kwa michezo hiyo. Kisha, Baron Pierre de Coubertin, Mfaransa mwenye umri wa miaka 29, akapendekeza kuanzishwa upya kwa michezo hiyo. Kwa hiyo, mwaka wa 1896 Michezo ya Olimpiki ya kwanza ya kisasa ilifanyika huko Athens. Tangu mwaka huo, Michezo ya Olimpiki imefanywa kila baada ya miaka minne, isipokuwa mara chache sana.

Leo wengi hutazamia kwa hamu michezo hiyo. Mwaka huu, itakuwa huko Sydney, Australia, kuanzia Septemba 15 hadi Oktoba mosi. Itatia ndani michezo 28, mashindano 292, na vipindi 635, kukiwa na wanariadha zaidi ya 10,300 watakaoshiriki.

Lakini katika miaka ya majuzi, Michezo ya Olimpiki imekumbwa na ubishi mwingi. Hata watu wengi husema kwamba malengo ya Michezo ya Olimpiki yanazorota. Kuchunguza mambo ya siri kutafunua mambo mengi yenye kushtua sana.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Scala/Art Resource, NY