Louis Braille—Kuwaangazia Nuru Wafungwa wa Giza
Louis Braille—Kuwaangazia Nuru Wafungwa wa Giza
UNATHAMINI kwa kadiri gani uwezo wa kusoma na kuandika? Baadhi ya watu huenda wakaona uwezo wa kusoma na kuandika kuwa jambo la kawaida tu, lakini huo ndio msingi wenyewe wa elimu yetu. Bila uwezo wa kusoma, akiba kubwa sana ya ujuzi haifikiki.
Kwa mamia ya miaka, vipofu hawakuweza kusoma. Hata hivyo, katika karne ya 19, kijana mmoja mwenye juhudi, alipoona taabu yao alisukumwa kubuni njia ya mawasiliano iliyompa yeye na mamilioni wengine fursa mpya.
Tumaini Latokana na Msiba
Louis Braille alizaliwa mwaka wa 1809 katika kijiji cha Coupvray, huko Ufaransa, kilichoko umbali wa kilometa 40 hivi kutoka Paris. Baba yake, Simon-René Braille alikuwa fundi wa lijamu na hatamu. Huenda ikawa Louis alipokuwa mchanga alicheza katika karakana ya babake mara nyingi. Hata hivyo, siku moja aksidenti mbaya ilitukia. Louis alichukua chombo chenye ncha kali—labda msharasi—akajichoma jicho kwa sababu ya kutokuwa mwangalifu. Jicho lake halikupona. Jambo baya hata zaidi lilitukia, mchochota ulienea kufikia jicho lake lingine. Louis akawa kipofu alipokuwa na umri wa miaka mitatu tu.
Ili kumsaidia Louis, wazazi wake na kasisi wa parokia, Jacques Palluy, walifanya mpango ili Louis aweze kuhudhuria masomo katika shule ya mahali hapo. Louis alielewa mengi aliyosikia. Hata, akawa kiongozi katika darasa lake kwa miaka kadhaa! Hata hivyo, yale ambayo kipofu anaweza kujifunza yana mipaka anapojifunza kwa utaratibu wa elimu unaokusudiwa watu wasio vipofu. Kwa hiyo, mwaka wa 1819, Louis aliandikishwa katika Chuo cha Kifalme cha Vijana Vipofu.
Mwanzilishi wa chuo hicho, Valentin Haüy, alikuwa mmojawapo wa watu wa kwanza kuanzisha mpango wa kusaidia vipofu kusoma. Tamaa yake ilikuwa kupinga dhana ya wengi ya kwamba haiwezekani kuelimisha vipofu shuleni. Majaribio ya kwanzakwanza ya Haüy yalitia ndani kugandamiza herufi kubwa kwenye karatasi nzito. Ingawa njia hiyo ilikuwa sahili mno, jitihada hizo ziliweka msingi kwa maendeleo ya baadaye.
Braille alijifunza kusoma herufi hizo kubwa za vitabu vya maktaba ndogo ya Haüy. Hata hivyo, aligundua kwamba njia hiyo ya kujifunza ilikuwa ya polepole bila matokeo mazuri. Herufi zilikusudiwa kusomwa kwa macho—wala si kwa vidole. Jambo la kupendeza ni kwamba mtu mwingine aliyetambua matatizo hayo alikuwa karibu kutokea.
Wazo Kutokana na Chanzo Kisichotazamiwa
Mnamo 1821, Louis Braille alipokuwa na umri wa miaka 12 tu, Charles Barbier, kapteni wa mizinga Mfaransa aliyestaafu, alitembelea chuo hicho. Huko alionyesha njia ya mawasiliano iitwayo maandishi ya usiku, baadaye ilikuja kuitwa sonography. Maandishi ya usiku yalianzishwa kwa kusudi la kutumiwa katika uwanja wa vita. Hayo yalikuwa maandishi yaliyosomwa kwa kuguswa, yalikuwa na vidutu vilivyokuwa vimepangwa kama umbo la mstatili wenye urefu wa vidutu sita na upana wa vidutu viwili. Njia hii ya kuandika maneno kwa kuyawakilisha na alama mbalimbali kulingana na matamshi yake, ilipendwa katika shule hiyo. Braille alijifunza kwa bidii njia hiyo na hata kuiboresha. Hata hivyo, Braille alihitaji kujikaza ili kufanya njia hiyo ya mawasiliano iwe yenye manufaa kwelikweli. Katika
kitabu chake cha kumbukumbu aliandika: “Iwapo upofu wangu wanizuia nisiweze kujifunza juu ya watu na matukio, mawazo na mafundisho, lazima nipate njia nyingine ya kujifunza.”Kwa hiyo, kwa miaka miwili iliyofuata, Braille alifanya kazi kwa bidii sana ili kurahisisha mfumo huo wa maandishi. Hatimaye, alibuni njia bora zaidi na sahihi akitumia mfumo wenye kikundi cha vidutu sita chenye urefu wa vidutu vitatu tu na upana wa vidutu viwili. Katika mwaka wa 1824, Louis Braille alipokuwa na umri wa miaka 15, alikuwa amekamilisha mfumo huo wa maandishi wenye vidutu sita. Punde baadaye, Braille alianza kufundisha katika Chuo cha Kifalme cha Vijana Vipofu, na mnamo 1829 alitangaza rasmi njia yake ya pekee ya mawasiliano inayoitwa leo kwa jina lake. Isipokuwa marekebisho madogo ya kuongeza ubora, mfumo wake umedumu bila kubadilika hadi leo.
Kueneza Maandishi ya Breli Ulimwenguni Pote
Mwishomwisho wa miaka ya 1820, kitabu cha kwanza kilichoeleza mfumo wa maandishi wa vidutu ambao Braille alibuni kilichapishwa; lakini wengi hawakuwa tayari kuutumia. Hata chuo chenyewe hakikutumia mfumo huo hadi mwaka wa 1854—miaka miwili baada ya kifo cha Braille. Hata hivyo, hatimaye mfumo huo bora ulipata kupendwa na wengi.
Mashirika kadhaa yamechapisha vichapo katika Breli. Mnamo 1912, Watchtower Society ilianza kuchapisha vichapo katika maandishi ya vipofu (Breli), wakati mfumo huo ulipokuwa ukiendelea kusanifishwa kwa ajili ya wasomao Kiingereza. Leo, Watchtower Society kwa kutumia uchapishaji wa hali ya juu, huchapisha mamilioni ya kurasa za Breli kila mwaka katika lugha nane. Hizo husambazwa katika zaidi ya nchi 70. Hivi majuzi, kwa sababu ya uhitaji unaoongezeka wa vichapo vya Biblia vya Breli, Watchtower Society iliongeza idadi ya vichapo vya Breli maradufu ya ilivyokuwa awali.
Leo, maandishi ya Breli yaliyo sahili na yaliyopangwa vizuri huwasaidia mamilioni ya vipofu kusoma—kwa sababu ya jitihada kubwa ya mvulana mchanga karibu miaka 200 iliyopita.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]
KUELEWA MFUMO WA MAANDISHI YA BRELI
Maandishi ya Breli husomwa kutoka kushoto hadi kulia, kwa kutumia mkono mmoja au miwili. Kila kikundi chenye vidutu 6 chaweza kuwa na mipangilio 63 ya vidutu. Kwa hiyo, vituo na herufi zote za alfabeti nyingi zaweza kuwa na mpangilio mahususi wa vidutu. Lugha kadhaa hutumia Breli iliyofupishwa, katika hiyo baadhi ya vikundi vyenye vidutu 6 huwakilisha herufi au maneno ambayo ni ya kawaida. Baadhi ya watu wamejua kusoma Breli vizuri sana hivi kwamba wanaweza kusoma maneno 200 kwa dakika moja!
[Picha]
Herufi kumi za kwanza hutumia vidutu vya mistari miwili ya juu tu
Herufi kumi zifuatazo huongeza kidutu cha kushoto-chini kwa kila moja ya herufi kumi za kwanza
Herufi tano za mwisho huongeza vidutu viwili vya chini kwa herufi tano za kwanza; herufi “w” ni ya pekee kwa kuwa iliongezwa kwenye alfabeti ya Kifaransa baadaye
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]
Picha: © Maison Natale de Louis Braille - Coupvray, France/Photo Jean-Claude Yon