Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Malengo ya Olimpiki Yanazorota

Malengo ya Olimpiki Yanazorota

Malengo ya Olimpiki Yanazorota

BARON Pierre de Coubertin alipopendekeza kuanzishwa upya kwa Michezo ya Olimpiki, aliweka malengo fulani yanayofaa. Hata, kanuni inayoongoza michezo ya Olimpiki ya kisasa, inayodhaniwa kuwa ilibuniwa na Coubertin, hutaarifu hivi: “Jambo muhimu zaidi katika Michezo ya Olimpiki si kushinda bali kushiriki . . . Jambo la maana si kutia fora bali kupambana vyema.”

Coubertin aliamini kwamba kushiriki mashindano yafaayo kungeweza kusitawisha sifa bora, kudumisha akili timamu, na kuendeleza mwenendo mnyoofu. Hata alitaja ‘dini ya michezo.’ Yeye alidhani kwamba Michezo ya Olimpiki ingeweza kufunza watu kuishi kwa amani.

Lakini kufikia wakati Coubertin alipokufa mwaka wa 1937, matumaini ya kufikia malengo hayo yalikuwa yamedidimia. Tayari michezo hiyo ilikuwa imeahirishwa pindi moja kwa sababu ya vita ya ulimwengu, na kulikuwa na wasiwasi mkubwa wa kuzuka kwa vita nyingine kuu. Leo, malengo ya michezo ya Olimpiki yamezorota hata zaidi. Mbona yanazorota?

Michezo ya Olimpiki na Dawa za Kulevya

Kwa miongo mingi wanariadha wametumia dawa za kulevya ili kuwawezesha kutia fora, na Michezo ya Olimpiki imekumbwa na tatizo hilo pia. Kwa kweli, sasa miaka 25 tangu kuanzishwa kwa ule unaoonwa kuwa upimaji makini wa matumizi ya dawa za kulevya, wanariadha katika Michezo ya Olimpiki wangali wanaendelea kutumia dawa za kulevya zilizopigwa marufuku.

Baadhi ya wanariadha hutumia steroidi za kuongeza nguvu mwilini ili kuwashinda wenzao. Wengine hutumia dawa zinazochochea utendaji wa mwili. Homoni za ukuzi wa binadamu hutumiwa mno na wakimbiaji wa mbio za masafa mafupi na wanariadha wengine wa mashindano magumu sana kwa sababu huwasaidia kupata nguvu haraka baada ya mazoezi makali, pia hujenga misuli. Wakati huohuo, wakimbiaji wa masafa marefu, waogeleaji, na wale wanaoteleza thelujini kwa safari ndefu hupenda kutumia homoni iliyogeuzwa maumbile ya erythropoietin kwa sababu inazidisha ustahimilivu wao kwa kuchochea damu itokeze chembe nyingi nyekundu.

Ndiyo sababu, Dakt. Robert Voy, aliyekuwa mkurugenzi wa upimaji wa matumizi ya dawa za kulevya wa Kamati ya Olimpiki ya Marekani, anawaita wanariadha “maabara inayotembea.” Yeye aongezea hivi: “Michezo ya Olimpiki imekuwa mahali pa majaribio kwa wanasayansi, wanakemia, na madaktari wasio na ujuzi.” Vipi juu ya upimaji? Dakt. Donald Catlin, mkurugenzi wa maabara moja ya kupima utumiaji wa dawa za kulevya huko Marekani, asema: “Mwanariadha anayejiona kuwa na busara na anayetaka kutumia dawa za kulevya amegeukia dawa nyingine tusizoweza kupima.”

Rushwa na Ufisadi

Kwa kuwa ni majiji machache tu yanayoweza kufaulu kupata kibali cha kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki, baadhi yake hufanya juu chini ili kupata fursa hiyo. Miaka miwili hivi iliyopita, Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Olimpiki (IOC) ilikumbwa na kashfa. Maadili ya wale waliohusika katika uteuzi yalitiliwa shaka kwa sababu ya madai ya kwamba washiriki wa IOC walipokea rushwa ya dola 400,000 za Marekani ili kukubali ombi la Jimbo la Salt Lake la kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi Kali ya mwaka wa 2002.

Mara nyingi si rahisi kubainisha ukarimu na rushwa ya peupe kwani majiji yanayowania nafasi ya kuwa mwenyeji wa michezo huwakabidhi zawadi kemkemu wale wanaoteua mahali pa kufanyia michezo hiyo. Washiriki wapatao 20 wa IOC walituhumiwa katika kashfa ya Jimbo la Salt Lake, na 6 kati yao waliachishwa kazi hatimaye. Kwa habari ya Michezo ya mwaka wa 2000 itakayofanyika Australia, jitihada yote ya kudumisha sifa njema ilitokomea wakati msimamizi wa Kamati ya Olimpiki ya Australia alipokiri hivi: “Kwa kweli, hatukufaulu kupata fursa hiyo kwa sababu ya umaridadi wa jiji wala wa vifaa vya michezo peke yake.”

Maisha ya ubadhirifu ya baadhi ya maofisa wakuu wa IOC yamezidisha shaka. Mswisi aliyekuwa msimamizi wa Shirikisho la Kimataifa la Upigaji-Makasia, Tommy Keller, pindi moja alisema kwamba kwa maoni yake maofisa fulani wa michezo huona Michezo ya Olimpiki kuwa njia ya “kutosheleza fahari yao ya kibinafsi.” Aliongezea kusema kwamba yaonekana wanachochewa na “pupa ya fedha na tamaa ya makuu.”

Uchumaji wa Fedha Nyingi Sana

Hakuna mtu awezaye kubisha kuwa Michezo ya Olimpiki huchuma fedha nyingi sana. Kwa kawaida, huvutia watazamaji wa televisheni chungu nzima na matangazo ya kibiashara yenye kuleta faida, ni mambo yanayowaletea wafadhili wa michezo hiyo kiasi kikubwa sana cha fedha.

Fikiria Michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 1988, iliyodhaminiwa na makampuni tisa ya kimataifa ambayo yalilipa IOC jumla ya zaidi ya dola milioni 100 za Marekani ili kupata idhini ya kutangaza michezo hiyo ulimwenguni pote. Michezo ya mwaka wa 1996 ya Majira ya Kiangazi huko Atlanta ilichuma jumla ya dola milioni 400 za Marekani kutokana na matangazo. Bila kutia ndani idhini kwa vituo vya televisheni. Kituo kimoja cha mfumo wa televisheni huko Marekani kililipa zaidi ya dola bilioni 3.5 za Marekani ili kupata idhini ya kutangaza Michezo ya Olimpiki kati ya mwaka wa 2000 na 2008, na iliripotiwa kwamba wafadhili 11 ulimwenguni pote watahitaji kulipa dola milioni 84 za Marekani kila mmoja kwa kipindi cha miaka minne. Hivyo, watu fulani wamesema kwamba ijapokuwa hapo awali Michezo ya Olimpiki ilikuwa ikidhihirisha ufanisi wa mwanadamu, leo michezo hiyo huwapa wanadamu wenye pupa fursa ya kuchuma fedha nyingi sana.

Mbona Kuna Kasoro?

Baadhi ya wataalamu husema kwamba kuzorota kwa Michezo ya Olimpiki kulisababishwa na matukio mawili makuu mapema miaka ya 1980. La kwanza ni uamuzi wa kuidhinisha kila shirikisho la kimataifa la michezo kuweza kuteua wanariadha wanaofaa kushiriki Olimpiki. Ijapokuwa IOC ilikuwa imeruhusu tu wanariadha wasiolipwa kushiriki, mashirikisho hayo yalianza kuruhusu wanariadha wanaolipwa kushiriki mashindano mbalimbali ya Olimpiki. Lakini wanariadha wanaolipwa walijiona kuwa bora. Hungeweza kupokea donge nono kutoka kwa watangazaji kwa ‘kupambana vyema’ tu, kwa hiyo punde si punde ushindi ukawa jambo muhimu kupita yote. Si ajabu kwamba wazo hilo limeendeleza matumizi ya dawa za kulevya za kuwawezesha kutia fora.

Jambo la pili kuu lilitukia mwaka wa 1983 wakati IOC iliponuia kuchuma faida kwa kutumia kile kilichoitwa na mtaalamu wake wa uuzaji, “alama muhimu zaidi isiyopata kutumiwa ulimwenguni”—duara za Olimpiki. Alama hiyo ilizua mashindano makali ya kibiashara ambayo yamekuwa ya kawaida katika Michezo ya Olimpiki. Jason Zengerle alisema: “Licha ya matumaini yote ya kudumisha amani na kuunganisha ulimwengu wote . . . , kwa kweli Michezo ya Olimpiki ni sawa tu na . . . mashindano mengineyo mashuhuri ya michezo.” Lakini je, hilo lamaanisha kwamba malengo yaliyopendekezwa na chama cha Olimpiki hayawezi kutimizwa?

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

MAMBO MUHIMU KUHUSU OLIMPIKI

Alama ya Michezo ya Olimpiki ni duara tano, zinazowakilisha mabara ya Afrika, Asia, Australia, Ulaya, na Amerika Kaskazini na Kusini. Kuunganika kwake huonyesha urafiki wa kimichezo wa watu wote.

Wito wa Michezo ya Olimpiki ni Citius, Altius, Fortius—maneno ya Kilatini yamaanishayo “haraka zaidi, juu zaidi, kwa ujasiri zaidi.” Tafsiri nyingine ya “kwa wepesi zaidi, juu zaidi, kwa nguvu zaidi” ilianzishwa na mwelimishaji mmoja Mfaransa.

Moto wa Michezo ya Olimpiki uliwaka kwenye madhabahu ya Zeusi michezo hiyo ilipokuwa ikiendelea hapo kale. Leo, mwenge huwashwa kwa miali ya jua huko Olympia, kisha husafirishwa hadi mahali pa michezo.

Desturi ya Michezo ya Olimpiki imekuwapo kwa milenia nyingi. Michezo ya kwanza kabisa ya Olimpiki kuwahi kurekodiwa ilifanyika mwaka wa 776 K.W.K., lakini wengi husema kwamba michezo hiyo ilianza mapema sana angalau karne tano kabla ya hapo.

[Hisani]

AP Photo/Eric Draper

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

MAHALI PATAKAPOANDALIWA OLIMPIKI HUKO SYDNEY

Tangu mwezi wa Septemba 1993, Sydney ilipopata kibali cha kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 2000, kumekuwa na pilikapilika za kulitayarisha jiji hilo kwa ajili ya kupokea makumi ya maelfu ya wageni. Kumekuwa na kazi nyingi za kusafisha mahali pa michezo, kujenga viwanja vya kisasa, kuzoa marundo ya takataka na kujenga vinamasi, bustani, na milango ya mito, inayoenea kwa umbali wa eka 1,900.

Kijiji cha Olimpiki cha Sydney, ambacho kimejengwa kuwa makazi ya wanariadha na maofisa wote, ndicho kijiji kikubwa zaidi ulimwenguni kinachotumia nishati ya jua. SuperDome—uwanja mkubwa zaidi wa michezo ya ndani na wa vitumbuizo katika Kizio cha Kusini—una mfumo mkubwa zaidi wa pekee wa nishati ya jua huko Australia, ambao hutenda kazi kwa nishati isiyotokeza moshi unaozidisha joto la dunia.

Mihimili mikubwa yenye kujipinda na kupitana ya Uwanja wa Olimpiki huchomoza angani nyuma ya SuperDome. Uwanja huo uliojengwa kwa gharama ya dola 435,000,000 za Marekani ndio uwanja wa Olimpiki ulio mkubwa zaidi ulimwenguni, unaweza kutoshea watu 110,000. Ndege nne aina ya Boeing 747 zaweza kuegezwa pamoja chini ya tao kuu la uwanja huo! Watazamaji hukingwa kutokana na miale ya urujuanimno ya jua na paa la vigae vinavyopenywa na nuru. “Kwa miezi kadhaa mwaka wa 2000,” akasema Alan Patching, msimamizi mkuu wa uwanja huo, “mahali hapa patakuwa kitovu cha utendaji cha Australia.” Kisha akatabiri: “Baadaye patakuwa mahali pa kipekee, kama lile Jumba la Opera.”

[Picha katika ukurasa wa 4]

Baron Pierre de Coubertin

[Hisani]

Culver Pictures

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 7]

AP Photo/ACOG, HO