Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Upasuaji Bila Damu—Kisa Kilichofanikiwa

Upasuaji Bila Damu—Kisa Kilichofanikiwa

Upasuaji Bila Damu—Kisa Kilichofanikiwa

Baada ya kuchapishwa kwa toleo la Amkeni! la Januari 8, 2000, lililozungumzia tiba na upasuaji bila damu, wahariri walipokea barua ifuatayo yenye kutia moyo.

“Toleo hilo la Amkeni! lilinikumbusha hali iliyonikumba mimi na mume wangu kuhusiana na binti yetu, Janice. Baada tu ya kuzaliwa, matatizo matano ya moyo yaligunduliwa, tatizo kubwa zaidi lilikuwa kuvurugika kwa mishipa mikubwa ipelekayo damu moyoni. * Kwa kuwa alihitaji kupasuliwa, tulimpata daktari-mpasuaji wa moyo anayetibu watoto huko Buffalo, New York, Marekani, ambaye alikuwa tayari kumfanyia upasuaji bila damu.

“Janice alifanyiwa upasuaji kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miezi minne—ili kupunguza damu inayoingia mapafuni mwake. Miezi mitano baadaye, alifanyiwa upasuaji wa pili—waliutia ganzi moyo wake ili damu yake izunguke ifaavyo. Upasuaji huo wote ulifanywa bila damu, na ulifanikiwa sana!

“Sasa Janice ana umri wa miaka 17 na ana afya bora kabisa. Tunashukuru sana madaktari-wapasuaji wenye ujasiri walio tayari kuheshimu msimamo wetu kuhusu damu. Kwa kweli, wao ni, ‘Watangulizi wa Tiba,’ kama mnavyowaita kwenye toleo la Januari 8. Kuhusu swali mlilouliza katika gazeti hilo, Je, upasuaji bila damu ni njia badala iliyo salama? Twaweza kujibu kwa usadikisho kwamba bila shaka ni salama!”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Katika hali hiyo, mshipa wa damu wa upande wa kushoto wa moyo huwa mahali pa mshipa unaopeleka damu mapafuni. Hivyo, damu yenye oksijeni nyingi inayopasa kusambazwa mwilini hupelekwa tu kwenye mapafu. Kisa kama hicho kiliripotiwa kwenye toleo letu la Kiingereza la Aprili 8, 1986, ukurasa wa 18-20.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Baada ya upasuaji

[Picha katika ukurasa wa 31]

Janice akiwa na wazazi wake leo