Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Paris Lisilo na Michoro ya Mikwaruzo?

“Kikosi cha kazi hupendeza sana,” lataarifu gazeti la Ufaransa la Le Figaro. Kina “magari ya mizigo 17 yaliyo na vifaa vyote, mabasi madogo 7 ambayo yamekusudiwa kazi ya kuondoa michoro ya mikwaruzo, pikipiki 12, na wafanyakazi 130 hivi ambao wanasaidiwa na wapelelezi 16 ambao wana kazi ya kutafuta michoro ya mikwaruzo.” Jeshi hilo jipya la Paris la kuondoa michoro ya mikwaruzo, lina kazi ya kuondoa asilimia 90 ya michoro iliyo katika kuta, milango na madirisha jijini Paris kwa muda wa mwaka mmoja—michoro hiyo imefunika eneo la “meta 200,000 za mraba za kuta za majengo ya manispaa na ya umma, na eneo la meta 240,000 za mraba za nyumba za watu binafsi.” Ikiwa miradi ya jiji hilo itatimizwa, kufikia Februari 2001 michoro yote ya ukutani itakuwa imeondolewa, isipokuwa meta 24,000 za mraba kwenye nyumba za binafsi, na “michoro mipya itaondolewa kabla ya siku 12 kupita baada ya kuonekana.” Usafishaji huo wote utagharimu dola milioni 72 za Marekani.

Idadi ya Wanaokula Mno Sasa Yalingana na Idadi ya Wasiolishwa vya Kutosha

“Idadi ya watu wanene kupita kiasi ulimwenguni sasa yalingana na idadi ya watu wenye njaa, wasiolishwa vya kutosha,” lasema gazeti la The New York Times, linapozungumzia uchunguzi wa Taasisi ya Worldwatch. Watu bilioni 1.2 hawana lishe ya kutosha na ni wenye njaa na sasa idadi yao yalingana na idadi ya watu wanaokula mno. Leo kuna watu wengi ulimwenguni pote ambao hawana lishe ya kutosha kuliko wakati mwingine wowote, na idadi ya wasiolishwa vya kutosha na wanaokula mno inaongezeka katika jamii zote. “Leo, hatufanyi kazi ya mwili ya kutosha ili kutumia kalori zote ambazo tunakula, na kalori zisizotumiwa na mwili hutokeza mafuta,” akasema Lester R. Brown, msimamizi wa Worldwatch, akirejezea idadi inayoongezeka ya watu wanene kupita kiasi. “Upasuaji 400,000 wa kuondoa mafuta mwilini ulifanywa Marekani mwaka uliopita. Hilo laonyesha jinsi ambavyo mambo yamekwenda kombo.”

Wamarekani Wana Wanyama-Vipenzi Wengi Zaidi ya Wote

Asilimia 40 ya wanyama-vipenzi milioni 500 walioko ulimwenguni wako Marekani. “Katika nchi hiyo yenye paka milioni 70, mbwa milioni 56, ndege milioni 40, samaki milioni 100, buku au wanyama wengineo wadogo milioni 13, na wanyama watambaazi milioni 8, karibu asilimia 60 hivi ya nyumba zina angalau mmojawapo wa wanyama hao,” lasema gazeti la National Geographic. Uingereza inafuata Marekani kwa idadi ya wanyama-vipenzi, hasa paka na mbwa. “Hata hivyo, samaki-vipenzi milioni 21 wamechukua nafasi ya kwanza nchini Ufaransa, kuzidi jumla ya idadi ya paka na mbwa,” lasema gazeti hilo.

Mahakama Kuu ya Japani Yamtetea Shahidi

Mahakama Kuu ya Japani imeamua kwamba “Madaktari-wapasuaji waliingilia haki ya kujiamulia ya mwanamke mmoja walipomtia damu wakati wa upasuaji, huku wakivunja ahadi yao ya kutofanya hivyo hata kama angekufa,” lasema gazeti la Daily Yomiuri. “Ilikuwa mara ya kwanza kwa Mahakama Kuu kuamua kwamba haki ya mgonjwa kujiamulia matibabu ni haki ya binadamu.” Misae Takeda, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alitiwa damu mwaka wa 1992 alipokuwa angali ameduwazwa na dawa za kutuliza maumivu baada ya upasuaji wa kuondoa uvimbe hatari katika ini. Mahakimu wanne wa Mahakama Kuu waliamua kwa kauli moja kwamba madaktari walikosea kwa sababu hawakumweleza mwanamke huyo kwamba huenda wangemtia damu ikiwa wangeona ni ya lazima wakati wa upasuaji, na hivyo wakamnyima haki yake ya kuamua kama atakubali upasuaji huo au la. Uamuzi wa Februari 29, 2000 ulisema hivi: “Mgonjwa anapokataa kutiwa damu kwa sababu ya itikadi yake ya kidini, mapenzi ya aina hiyo lazima yaheshimiwe.” Watu wa ukoo waliendeleza kesi baada ya kifo cha Misae mwaka wa 1997.—Ukitaka kujua zaidi, tafadhali soma gazeti la Mnara wa Mlinzi la Desemba 15, 1998, ukurasa wa 26-29.

Kuhifadhi Mimea na Wanyama wa Dunia

“Kuhifadhi mimea na wanyama wengi waliomo duniani wasitoweke si jambo gumu,” lasema gazeti la Daily News la New York City. “Wanasayansi waliohesabu mimea na wanyama katika misitu ya Dunia inayoendelea kupungua, wameona jambo la kushangaza: Zaidi ya theluthi ya mimea na wanyama wa dunia wanapatikana kwenye sehemu ndogo tu, asilimia 1.4 ya dunia.” Watafiti hao wadokeza kwamba jitihada zaidi za kuhifadhi zifanywe hasa katika maeneo 25 yenye mimea na wanyama wengi zaidi katika nchi kama Brazili, Madagaska, Borneo, Sumatra, Milima Andes yenye joto, na Karibea. Sehemu nyingi kati yake zina misitu ya mvua. “Tukitumia milioni chache za mamia ya dola za Marekani kila mwaka ili kuhifadhi sehemu hizo zinazohitaji uangalifu wa haraka, twaweza kuhakikisha kwamba tumehifadhi aina zote za mimea na wanyama Duniani,” akasema Russell Mittermeier, msimamizi wa shirika la Conservation International. Ingawa asilimia 38 ya sehemu hizo tayari zimehifadhiwa kisheria, uchimbuaji wa madini, ukataji-miti na ulishaji-wanyama bado huendelea katika maeneo hayo.

Upungufu wa Makasisi Waenea

“Upungufu wa makasisi” umeenea toka sehemu za mashambani za Marekani hadi katika majiji makubwa, lasema gazeti la The New York Times. Makala hiyo yasema hivi inapotaja mfano wa sinagogi lililojengwa miaka 110 iliyopita ambalo limejaribu kupata rabi kwa miaka mitatu bila kufanikiwa: “Tatizo la sinagogi hilo si la kipekee. Mbali na masinagogi, makanisa ya Kikatoliki na Kiprotestanti vilevile yana matatizo ya kuajiri makasisi.” Mapadri wa parokia wamepungua kwa asilimia 12 kuanzia mwaka wa 1992 hadi 1997. Msemaji wa Kanisa la Kianglikana asema kwamba hali ni mbaya sana, kwa sababu miongoni mwa makasisi 15,000, wale waliozaliwa baada ya mwaka wa 1964 hawafiki 300. Zaidi ya asilimia 22 ya makanisa ya Dini ya Kiyahudi Iliyogeuka hayana rabi wa kudumu. Miaka mitano tu iliyopita, kulikuwako marabi wengi kuliko masinagogi. Baadhi ya makasisi wanalaumu “uchumi mzuri” ambao “huvuta [watu] kwenye shughuli zenye mapato mazuri zaidi.” Wengine husema ni kwa sababu ukasisi “hauvutii watu kama awali.” Rabi Sheldon Zimmerman, msimamizi wa Hebrew Union College, aonya hivi: “Tusipoongeza kwa njia fulani idadi ya wale wanaochagua kazi ya kidini, mwishowe jambo hilo litakuwa balaa kwa utendaji wa dini.”

Tahadhari Huhitajika Unaposugua Meno

“Inawezekana kusugua meno yako kupita kiasi,” yasema ripoti moja katika jarida la The Wall Street Journal. “Tatizo hilo lajulikana kama ‘mchubuo wa mswaki,’ na waweza kusababisha meno yawe mepesi kudhurika, kumomonyoka kwa ufizi wa meno na kudhoofika kwa shina la jino.” Inakadiriwa kwamba asilimia 10 hadi 20 ya watu wote Marekani “wameharibu meno au ufizi wao kwa kusugua meno kupita kiasi.” Wale wanaosugua meno kwa nguvu na wale wanaotumia mswaki mgumu ndio walio hatarini zaidi. “Wanajiletea madhara badala ya manufaa katika jitihada ya kusugua meno kikamili,” asema daktari wa meno Milan SeGall. Baadhi ya watu wanaelekea kupata tatizo hilo zaidi kwa sababu hawana mifupa ya kutosha ya kuimarisha meno yao. Hata watu ambao wamenyoosha au kusogeza meno yao kwa mabano, na wale wanaosaga au kukaza sana meno, wako hatarini pia. Ili kuepuka kuharibu meno, wataalamu wapendekeza yafuatayo: Tumia mswaki mwororo. Kwanza sugua meno ya nyuma, kwa kuwa hata mswaki mwororo huwa mgumu kwa kadiri fulani uanzapo na dawa ya meno hukwaruza zaidi. Shika mswaki taratibu kwa vidole vichache badala ya mkono wote. Weka mswaki kwa pembe ya digrii 45 kuelekea ufizi, na usugue polepole kwa kufuata umbo la yai badala ya kusugua mbele na nyuma.

Mnara Unaoegemea wa Pisa Wanyoshwa

Jitihada za kunyosha Mnara Unaoegemea wa Pisa zimefaulu kuunyosha mnara huo kwa sentimeta tano katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka, wasema ujumbe wa shirika la habari la The Associated Press. Wahandisi waamini kwamba kufikia mwezi wa Juni 2001, mnara huo utakuwa imara vya kutosha kuweza kufunguliwa kwa umma tena. Mara ya mwisho kwa watalii kupanda mnara huo uliojengwa katika karne ya 12 ni zaidi ya miaka kumi iliyopita. Wakati huo mwinamo wake ulionwa kuwa hatari na kazi ya kuunyosha ikaanza. Kazi hiyo imefikia hatua ya mwisho, na inadhaniwa kwamba itakapokuwa imemalizika, mnara huo utakuwa umenyoshwa kwa sentimeta 50. Kabla ya kufunguliwa, kilogramu 8,000 za risasi za kusawazisha uzito zilizowekwa kwenye msingi wa mnara huo wakati wa kunyoshwa zitaondolewa, na vilevile ile miviringo kumi ya feleji inayouzunguka mnara ili kuuimarisha itatolewa.

Faida ya Ziada ya Kumnyonyesha Mtoto Maziwa ya Mama

“Mbali na kumwandalia mtoto wako aliyezaliwa karibuni fingo za kinga dhidi ya kuhara, maambukizo ya masikio, na mizio, kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kwaweza kuzuia pia kansa,” lasema gazeti la Parents. Uchunguzi wa Kitovu cha Kansa cha Chuo Kikuu cha Minnesota ulipata kwamba watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama si rahisi kupata kansa ya damu—kansa inayowakumba sana watoto—kama watoto wanaolishwa kwa chupa. Hatari ya kupata kansa ya watoto walionyonyeshwa maziwa ya mama angalau kwa muda wa mwezi mmoja ilipunguka kwa asilimia 21, na ilipunguka kwa asilimia 30 kwa walionyonyeshwa kwa muda wa miezi sita au zaidi.