Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Mimi Ni Mwembamba Sana?

Kwa Nini Mimi Ni Mwembamba Sana?

Vijana Huuliza . . .

Kwa Nini Mimi Ni Mwembamba Sana?

JUSTIN ni mwembamba na mwenye afya nzuri hata hivyo hapendi mwili wake. “Najaribu kuongeza uzito wangu,” yeyeanakiri.Kwasasaanakulamilo mitano kwa siku, yenye jumla ya kalori 4,000. Hata hivyo, yeye anataka kuongeza uzito wa misuli peke yake. Yeye aongezea hivi: “Mimi na rafiki yangu huamka mapema siku fulani-fulani katika juma na kwenda katika ukumbi wa mazoezi ili kuinua vitu vizito kabla ya kwenda kazini.”

Vanessa ni mwembamba pia. Lakini ameridhika kabisa na uzito wake. “Nilipokuwa mchanga zaidi, watoto walinidhihaki na kusema mimi ni mwembamba kama sindano,” Vanessa akumbuka. “Lakini sasa sijali tena. Nimeridhika na mwili wangu.”

‘Ridhika na mwili wako.’ Hilo lasikika kuwa shauri zuri. Lakini huenda likawa shauri unaloshindwa kutumia. Ukiwa kijana, huenda ukawa katika “mchanuko wa ujana.” (1 Wakorintho 7:36) Kipindi cha ubalehe hufadhaisha zaidi kwa sababu mabadiliko ya haraka sana ya mwili hutukia. Wakati wa ubalehe, sehemu nyingine za mwili huenda zikakua haraka kushinda sehemu nyingine; mikono yako, miguu, na uso huenda zikaonekana hazina usawaziko. * Hilo laweza kukufadhaisha na kukufanya uhisi huvutii. Pia vijana wote hawakui kwa njia ileile. Hivyo marika zako huenda wakawa na miili mikakamavu au umbo la kike, ilhali wewe ungali waonekana mwembamba.

Ingawa mengi yamesemwa kuhusu vijana wanaojiona kuwa wanene kupita kiasi, mara nyingi vijana wanaodhani ni wembamba mno hawatiliwi maanani. Huenda ikawa hivyo miongoni mwa makabila fulani na katika nchi fulani ambako wembamba hauonwi kuwa urembo. Katika maeneo hayo msichana mwembamba huenda akadhihakiwa sana kwa sababu ya kuwa “sindano.”

Vipi wavulana? Mchunguzi aitwaye Susan Bordo asema kwamba, “uchunguzi wa maoni ya wanawake juu ya umbo la mwili wao uliofanywa miaka mingi kabla ya miaka ya 1980 ulidokeza kwamba wanawake wanapojitazama kwenye kioo wao huona tu dosari.” Namna gani wanaume? Bordo aendelea kusema hivi: “Wanaume wanapojitazama kwenye kioo wao huona umbo lenye kuridhisha au hata bora zaidi kuliko umbo lao halisi.” Lakini mtazamo huo umeanza kubadilika katika miaka ya karibuni. Akitaja kuwa zaidi ya robo ya wenye kufanyiwa upasuaji unaonuiwa kuboresha sura ni wanaume, Bordo asema kwamba ongezeko hilo la vijana wanaozingatia kuwa na umbo zuri linasababishwa na wale wanaume wenye umbo “kamilifu” wanaoonyeshwa kwenye matangazo ya kibiashara ya nguo za ndani katika Marekani na nchi nyinginezo za Magharibi. Bila shaka, wavulana matineja wameathiriwa. Huenda wakahisi wamepungukiwa wanapoona kwamba hawana miili mikakamavu kama ya wanaume waonyeshaji-mitindo.

Kwa hivyo, ikiwa wewe ni mwembamba huenda ukajiuliza ‘Nina kasoro gani?’ Ukweli ni kwamba huenda ukawa huna kasoro yoyote.

Sababu ya Wewe Kuwa Mwembamba

Wembamba ni jambo la kawaida kabisa kwa vijana wengi. Mara nyingi husababishwa tu na ule ukuzi wa haraka na uvunjaji wa kasi wa kemikali mwilini unaotukia wakati wa ubalehe. Kwa kawaida uvunjaji huo wa kemikali utapungua kadiri unavyokua. Hata hivyo, ikiwa wewe ni mwembamba sana licha ya kula milo yenye lishe, basi ni vema kumwona daktari ili kuhakikisha huna matatizo ya kiafya, kama vile ugonjwa wa sukari, unaoweza kusababisha kupungua kwa uzito.

Mtaalamu mashuhuri wa matatizo ya kula, Steven Levenkron, aliliambia gazeti la Amkeni! hivi: “Nakumbuka msichana mmoja aliyeelekezwa kwangu akiwa na tatizo la kujinyima chakula, na kwa hakika alionekana kuwa mwenye tatizo la kula. Lakini upesi niligundua kwamba tatizo lake halikuwa la kiakili bali la kimwili. Daktari wake alikuwa ameshindwa kutambua kwamba alikuwa na ugonjwa hatari uitwao Crohn, unaoshambulia matumbo. Msichana huyo angekufa kwa sababu ya kutogunduliwa kwa ugonjwa huo.” Ikiwa unaugua ugonjwa wa sukari au ugonjwa mwingine wowote unaopunguza uzito, litakuwa jambo la hekima kufuata kwa makini ushauri wa daktari.

Bila shaka, nyakati nyingine wembamba waweza kuwa ni ishara ya mfadhaiko wa kihisia-moyo. Katika kitabu chake kiitwacho Anatomy of Anorexia, Dakt. Levenkron ameandika juu ya madai ya watafiti fulani kwamba idadi kubwa “ya watu wanaougua ugonjwa wa sukari na ambao hutegemea sana insulini wana matatizo ya kula, kama vile kula kupita kiasi, hamu ya kula isiyo ya kawaida, na kujinyima chakula.” Daktari mwenye ujuzi aweza kuthibitisha kama una tatizo la kula au la. *

Madokezo Yenye Kutumika

Tuseme kwamba tayari umemwona daktari na kwamba wewe ni mwembamba lakini mwenye afya nzuri. Sasa utafanya nini? Katika Ayubu 8:11, Biblia husema hivi: “Je! hayo mafunjo yamea pasipo matope na makangaga kumea pasipo maji?” Kama vile tu mmea husitawi kwenye udongo na mazingira yafaayo, vivyo hivyo unahitaji mlo kamili ikiwa unatazamia kukua na kuwa mtu mzima mwenye afya bora. Jambo hilo ni muhimu uwe unajaribu kupunguza au kuongeza uzito.

Hata hivyo, usithubutu kula milo yenye mafuta mengi ukitazamia kuongeza uzito upesi. Mtaalamu wa mambo ya lishe, Susan Kleiner alipokuwa akifanya utafiti kuhusu ulaji wa wanyanyuaji wa vitu vizito wakati wa mazoezi yao, aligundua kwamba wao hula chakula chenye kalori 6,000 kila siku! Lakini Kleiner asema kuwa, “jambo lenye kutia wasiwasi alilogundua katika uchunguzi huo ni kwamba walikula kwa wastani, zaidi ya gramu 200 za mafuta kila siku. Kiasi hicho cha mafuta ni sawa na kile kilicho katika gramu 250 za siagi! Watu walio wengi waweza kuwa wagonjwa wakila kiasi hicho cha mafuta hata kwa muda mfupi. Kiasi hicho kikubwa cha mafuta chaweza kusababisha ugonjwa wa moyo kinapotumiwa kwa muda mrefu.”

Kulingana na Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), msingi wa mlo kamili ni vyakula vyenye wanga kama vile mkate, nafaka, mchele, na pasta. Vyakula vinavyofuata kwa umuhimu ni mboga na matunda. Idara hiyo ya kilimo yapendekeza kwamba nyama na bidhaa zinazotokana na maziwa zitumiwe kwa kiasi tu.

Huenda ukajaribu kuandika orodha ya milo ili uweze kujua aina na kiasi unachokula. Beba daftari ndogo, andika chochote unachokula na wakati unapokila kwa juma moja. Huenda ukashangaa kugundua kwamba huli sana kama unavyodhania, hasa ikiwa wewe ni mtu mwenye shughuli nyingi. Ukiwa kijana chipukizi, unaweza kwa urahisi kutumia kalori 3,000 au zaidi kila siku! Huenda pia ukang’amua kwamba milo yako si kamili inavyopaswa—ikiwa imejaa vyakula vingi vinavyotayarishwa haraka kama vile hambaga na piza bila mboga na matunda ya kutosha.

Vipi vijalizo-chakula vilivyo ghali sana? Huenda visihitajike. Wataalamu wengi huamini kuwa unaweza kupata lishe yote yenye kuhitajiwa na mwili kwa kula vyakula vinavyofaa. Kwa vyovyote vile, epuka utatuzi wa haraka kama vile kutumia dawa za kujenga misuli ziitwazo steroidi. Kwa kusikitisha, kutumia dawa hizo si tatizo miongoni mwa wavulana pekee. Gazeti la The New York Times laripoti hivi: “Kuongezeka kwa matumizi ya [steroidi] miongoni mwa wasichana, jambo ambalo wachunguzi wengi hudhania kwa kiasi fulani kuwa kinyume cha tatizo la kujinyima chakula, limefikia kiwango kile kilichokuwa cha wavulana katika miaka ya 1980.” Idadi yenye kushtua ya wasichana 175,000 katika Marekani wanakiri kuwa wanatumia steroidi za kujenga misuli. Dawa hizo zimeshirikishwa na athari mbaya sana, zinazotia ndani kuwa na nywele zisizotakikana usoni, kuvurugika kwa vipindi vya hedhi, na kansa ya matiti katika wanawake, kansa ya tezi-kibofu katika wanaume, na kuziba kwa ateri na kansa ya ini katika wanaume na wanawake. Steroidi hazipasi kamwe kutumiwa bila usimamizi na maagizo ya daktari.

Kuwa Mnyenyekevu na Kuona Mambo Kihalisi

Biblia hutuambia ‘twende kwa unyenyekevu na Mungu wetu.’ (Mika 6:8) Unyenyekevu ni kutambua mipaka ya uwezo wako. Unyenyekevu utakusaidia uone mambo yanayohusiana na umbo lako kwa njia halisi. Hapana ubaya wowote kwa mtu kutaka kuwa na umbo zuri. Lakini kuhangaikia umbo lako kupita kiasi hakunufaishi mtu yeyote—isipokuwa labda wauza-nguo za mitindo na wanaouza vyakula maalumu. Wataalamu wa mazoezi ya viungo wanasema kwamba mwanamume wa kawaida hana chembe za urithi za kumfanya awe na mwili wenye nguvu isivyo kawaida, haidhuru ukamili wa chakula anachokula au hata kiasi cha mazoezi anayofanya. Na iwapo wewe ni msichana, huenda mwili wako usiwe na umbo unalotaka hata ule kiasi gani cha chakula.

Jambo la kupendeza ni kwamba huenda unalohitaji tu ni kuchagua mavazi yanayositiri yale unayoona kuwa upungufu katika mwili wako. Epuka mavazi yanayokazia mno mambo usiyopenda ya mwili wako. Watu fulani hudokeza kuvalia mavazi yenye rangi nyangavu, kwa kuwa mavazi yenye rangi inayokaribia nyeusi humfanya mtu mwembamba kuonekana mwembamba zaidi.

Kumbuka pia kwamba utu wako ni muhimu zaidi ya umbo lako. Kwa vyovyote vile, tabasamu yenye kupendeza pamoja na matendo yenye fadhili yatakufanya uwe mwenye kuvutia wengine kuliko misuli iliyojengeka au mtindo fulani wa mavazi. Ikiwa marafiki wako hukufanyia mzaha daima kuhusu umbo lako, tafuta watu wanaothamini utu wako wa ndani—kile kinachotajwa na Biblia kuwa “yule mtu wa siri wa moyoni.” (1 Petro 3:4) Hatimaye, usisahau kamwe kwamba “wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo.”—1 Samweli 16:7.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Ona makala “Vijana Huuliza . . . Je! Ninakua kwa Njia ya Kawaida?” katika toleo la Amkeni! la Septemba 22, 1993.

^ fu. 12 Ona makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Ninahangaikia Sana Uzito Wangu?” na “Naweza Kushindaje Kuhangaikia Sana Uzito?,” katika toleo letu la Aprili 22, 1999 na la Mei 22, 1999.

[Picha katika ukurasa wa 14]

Baadhi ya vijana hujichukia kwa sababu ni wembamba