Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Kazi ya Kudumu” Imepatwa na Nini?

“Kazi ya Kudumu” Imepatwa na Nini?

“Kazi ya Kudumu” Imepatwa na Nini?

GRAHAM * alifanya kazi kwenye kampuni moja kubwa huko Australia kwa muda wa miaka 37. Akiwa mwenye umri unaokaribia miaka 60, alipewa kwa ghafula notisi ya majuma machache na kufahamishwa kwamba hahitajiki tena kazini. Tunaweza kuelewa hisia zake za wasiwasi, mshangao na mfadhaiko kuhusu hali yake ya wakati ujao. ‘Ni nini kimeipata “kazi [yangu] ya kudumu” ambayo nilifikiri ni imara hadi nitakapofikia umri wa kustaafu?’ akajiuliza Graham.

Bila shaka, si ajabu kupoteza kazi, wala si jambo jipya. Hata hivyo, kupoteza kazi kunakoendelea ulimwenguni pote ni jambo jipya kwa kizazi cha sasa cha wafanyakazi. Kwa hakika, kuna sababu nyingi za kupoteza kazi, lakini sababu kuu yaelekea kuwa ile inayojulikana kama kupunguza idadi. Huku kupunguza idadi ni nini na kulianzaje?

Mabadiliko Katika Mahali pa Kazi

Leo uchumi umezidi kuwa wa kimataifa. Hilo lilieleweka katika Marekani hasa katika miaka ya 1970 makampuni ya huko yalipong’amua kwamba wateja walio wengi walikuwa wakinunua magari, vifaa vya elektroniki, na bidhaa nyingine nyingi kutoka nchi nyingine.

Ili kumudu ushindani huo na kupunguza gharama ya uzalishaji wa bidhaa, makampuni ya Marekani yalianza kupunguza idadi ya wafanyakazi na kuboresha njia za uzalishaji na vifaa vyao. Utaratibu uliotumiwa katika kuwapunguza wafanyakazi ukaja kuitwa kupunguza idadi. Utaratibu huo umefasiriwa kuwa “kupunguza idadi ya wafanyakazi katika kampuni fulani, kwa kutumia njia mbalimbali kama kufuta kazi, kuwapa wafanyakazi marupurupu ili kuwashawishi kustaafu mapema, kuhamisha, na kutojaza nafasi za wafanyakazi wanaokufa.”

Katika miaka fulani iliyopita ni wafanyakazi wa viwandani walioathiriwa na kupunguzwa huko. Lakini mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990, tatizo hilo likaanza kuwaathiri wafanyakazi wengi wa ofisini, hasa wafanyakazi wa vyeo vya chini. Punde si punde mwelekeo huo ukaathiri nchi zote zilizositawi kiviwanda. Uchumi ulipozidi kuzorota, serikali pamoja na waajiri wengine wakawa wakitafuta mbinu za kupunguza gharama kwa kupunguza wafanyakazi zaidi.

Wafanyakazi walio wengi waweza kupoteza kazi wakati wowote. Ofisa mmoja wa chama cha wafanyakazi asema hivi: “Watu ambao wamefanya kazi kwa uaminifu kwa miaka 10, 15, 20 wameona mikataba yao ya kazi ikifutiliwa mbali na wao kufutwa ghafula.” Katika kitabu chake Healing the Downsized Organization, Delorese Ambrose anasema kwamba katika mwaka wa 1956 mtajo “mtu wa kampuni” ulitungwa kumfafanua ya mfanyakazi wa kawaida. Delorese aongezea kusema hivi: “Awe alikuwa mfanyakazi wa chini au meneja, alikuwa tayari kutolea kampuni yake mali zake, maisha yake, uaminifu-mshikamanifu wake ili kupata ulinzi—kazi ya kudumu. Kwa wazi, mapatano hayo hayapo tena katika mashirika ya sasa.”

Mamilioni ya wafanyakazi kotekote duniani wamepoteza kazi zao kupitia mpango wa kupunguza wafanyakazi, na hakuna kikundi cha wafanyakazi ambacho hakijaathiriwa. Katika Marekani pekee, idadi ya wafanyakazi walioachishwa kazi ni kubwa sana, mamilioni wakiwa wamepoteza kazi zao za kudumu. Jambo sawa na hilo limefanyika katika nchi nyingine nyingi. Hata hivyo, takwimu hizo pekee haziwezi kueleza kihoro cha watu hao.

Athari Mbaya

Graham, aliyetajwa mwanzoni mwa makala hii, alisema: “Unapatwa na umivu halisi la kiakili.” Alilinganisha kufutwa kwake kazi na “ugonjwa au pigo lenye kuchubua.”

Uaminifu-mshikamanifu usipothawabishwa, watu huhisi wamesalitiwa kwa sababu juhudi zao zote kwa kampuni ile hazikuthaminiwa. Wanapoteza itibari, hasa iwapo mameneja wengi wakubwa wanapata donge nono baada ya kupunguza wafanyakazi wa kampuni. Isitoshe, mtu aliyepoteza kazi kwa ghafula hushindwa kulipia rehani, madeni mengine, kutimiza mahitaji ya afya kwa washiriki wa familia, kulipa ada za shule, kudumisha kiwango chake cha maisha, hobi, na kuwa na mali za kibinafsi. Matokeo ni kukata tamaa na kujiona hafai.

Kwa kuwa kazi imara na yenye kuridhisha huchangia sana kujistahi, unaweza kuwazia pigo linalowapata walemavu, watu wasio na ustadi wa kazi, au watu wazee wanapopoteza kazi. Uchunguzi uliofanywa huko Australia ulifunua kwamba watu walio na umri wa miaka kati ya 45 na 59 ndio walio katika hatari ya kupoteza kazi. Ilhali watu walio katika kikundi hicho ndio huona ugumu zaidi kubadilikana kulingana na hali.

Je, kuna lolote awezalo kufanya mtu? Kufanya kazi ya muda au kazi yenye mapato ya chini ni afadhali kuliko kuwa bila kazi. Hapana shaka, hilo litaathiri kiwango chako cha maisha. Imethibitishwa kwamba ni theluthi tu ya watu waliopoteza kazi waliowahi hatimaye kupata kazi yenye mapato sawa na ile waliyopoteza. Hilo nalo huongeza mkazo kwa maisha ya familia.

Hata kazi yetu ya sasa huenda isiwe yenye kuridhisha. Hii ni kwa sababu wasiwasi wa kupoteza kazi wakati ujao una athari mbaya isiyoonekana. Kitabu Parting Company chasema hivi: “Kutazamia kupoteza kazi kwalingana na kuchagua njia ifaayo ya kupigwa dafrao na lori. Kwa kweli huna mpango wowote kwa sababu kwa kawaida hata huoni hilo lori—sawa na kufukuzwa kazi—kabla halijakukanyanga.”

Kukosa kazi za kuajiriwa kunaathirije vijana? Baada ya uchunguzi kufanywa na idara ya elimu na sayansi, kulikuwa na maoni haya: “Wonyesho muhimu wa kuwa kijana amekuwa mtu mzima ilikuwa ni kuajiriwa kazi ya kudumu, ambayo iliashiria mwanzo wa maisha ‘halisi’ ya mtu mzima, katika ulimwengu wa watu wazima, kulingana na viwango vya watu wazima, pamoja na kuwa na pesa za kutumia apendavyo.” Iwapo watu huhisi kuwa kuajiriwa kazi huashiria mwanzo wa kuwa mtu mzima, basi kukosa kazi ya kuajiriwa ni pigo kubwa sana kwa vijana.

Kupambana na Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa

Kupambana na hali ya kupoteza kazi ya kuajiriwa kumefananishwa na kutembea katika eneo lenye mabomu yanayotegwa ardhini. Kitabu Parting Company chasema kwamba hisia za kawaida za watu hao ni hasira, aibu, woga, huzuni, na kujihurumia. Ni vigumu sana kukabiliana na hisia hizo. Mwandikaji wa kitabu hicho asema hivi: “Umepewa mgawo mgumu—kupangia wakati wako ujao. Wewe hukuomba mgawo huo, na huenda hata hujui namna ya kuutekeleza, na ghafula unahisi huna mtu yeyote wa kukusaidia.” Na hasa kuwajulisha washiriki wa familia habari ya kufutwa kazi kwa ghafula ni jambo gumu sana.

Hata hivyo, kuna njia zenye kutumika za kupambana na athari ya kupoteza kazi. Hatua ya kwanza ni kupunguza kiwango chako cha maisha bila kukawia kwa kupangia kuishi maisha ya chini zaidi ya uliyozoea.

Yafuatayo ni madokezo yenye kutumika ambayo huenda yakakusaidia kupambana na tatizo hilo, hata kama hutalitatua kabisa. Kwanza, lazima ufahamu kwamba kupoteza kazi ghafula ni jambo la kawaida siku hizi. Kwa hiyo, bila kujali umri au uzoefu wako wa kazi, pangia kimbele uwezekano wa kupoteza kazi kwa njia unayoishi sasa.

Pili, uwe mwangalifu usijitwike mzigo mkubwa wa deni kwa sababu ya vitu visivyo vya lazima maishani. Ishi kulingana na mapato yako, na usiwaze kuwa utalipa madeni yako kupitia marupurupu ya kupandishwa cheo au nyongeza ya mshahara. Ujumbe wa uchumi wa leo ni kwamba hakuna matumaini yenye kutegemeka kwa wakati ujao.

Tatu, tafuta njia ya kufanya maisha yako yawe sahili na upunguze miadi yako ya kifedha. Hilo latia ndani kuepuka kukopa vitu ambavyo havihitajiki katika maisha sahili, yafaayo.

Nne, kagua miradi yako maishani, ya kiroho na ya kimwili, na ifanye ifae hali ya sasa. Halafu pima maamuzi yako yote kuhusu miradi yako na uone inavyoathiriwa.

Mwishowe, usitamani kuishi kama wengine katika eneo lako wanaoishi maisha ya juu kuliko wewe, usije ukanaswa na kuanza kuishi kama wao.

Hayo ni madokezo machache ambayo huenda yakakusaidia wewe na familia yako kuepuka mtego wa kutegemea mali zisizo hakika katika ulimwengu wenye wasiwasi na kuepuka mfadhaiko wa maisha ya leo.

Felix Rohatyn aliyekuwa mfanyakazi wa banki alinukuliwa akisema hivi: “Huu ni uovu mbaya katika jamii iwapo kupoteza kazi kwa mtu mmoja kunamtajirisha mwingine.” Uovu wa mfumo huu ni mbaya hivi kwamba karibuni mahali pake patachukuliwa na ulimwengu ambamo mtajo “kazi ya kudumu” utapata maana zaidi ya tunavyowazia.—Isaya 65:17-24; 2 Petro 3:13.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Jina limebadilishwa.

[Blabu katika ukurasa wa 14]

‘Huu ni uovu mbaya iwapo kupoteza kazi kwa mtu mmoja kunamtajirisha mwingine.’

[Picha katika ukurasa wa 15]

Tafuta njia za kufanya maisha yako yawe sahili