“Michezo Hatari”—Je, Ujihatarishe?
Maoni ya Biblia
“Michezo Hatari”—Je, Ujihatarishe?
“SIKU HIZI WENGI WETU TUMEACHA KUWA MASHABIKI TU ILI TURUKE KWA MIAVULI KUTOKA KATIKA NDEGE, TURUKE MILIMANI KWA KAMBA, TUSAFIRI KWA MITUMBWI KATIKA MAPOROMOKO YA MAJI NA KUPIGA MBIZI KATIKA MAJI YENYE PAPA.”—GAZETI LA THE WILLOW GLEN RESIDENT.
TAARIFA hiyo yaeleza mtazamo wa wengi kuelekea michezo. Kupendezwa kunakoongezeka sana kwa michezo kama vile kuruka kwa mwavuli kutoka katika ndege, kupanda milima yenye barafu, kuruka kwa mwavuli kutoka mlimani,nakuruka kutoka katika majengo, madaraja, na magenge, * kwaonyesha kwamba ulimwengu hupenda kujihatarisha. Ubao wa kutelezea thelujini, baiskeli za kuendeshwa popote, ubao wenye magurudumu, na viatu vyenye magurudumu hutumiwa pia kupandia milima iliyoinuka zaidi, miamba mirefu zaidi, na kuruka mbali zaidi kadiri mtu awezavyo. Gazeti la Time lasema kwamba idadi inayoongezeka ya watu wanaopenda “michezo hatari”—yaani, michezo inayohatarisha mchezaji mwenyewe—yaonyesha hamu ya mamilioni kushiriki “hatari, woga na ustadi ambao hufanya wanariadha hodari na mabingwa wanaoshiriki mwisho-juma wahisi kwamba wanashinda uwezo wao wa binafsi.”
Hata hivyo, kupendezwa huko kunakoongezeka huleta pia madhara makubwa ya kibinafsi. Watu wengi hujeruhiwa wakati michezo isiyo hatari inapofanywa kwa njia hatari. Huko Marekani, mwaka wa 1997, idadi ya waliopelekwa hospitalini ili kupata matibabu ya dharura kwa sababu ya kujeruhiwa walipotumia ubao wenye magurudumu kutelezea barabarani, iliongezeka kwa asilimia 33, idadi ya waliotumia ubao wa kutelezea thelujini iliongezeka kwa asilimia 31, na idadi ya waliopanda milima iliongezeka kwa asilimia 20. Matokeo katika michezo mingine ni mabaya hata zaidi, kwa kuwa watu wengi zaidi wanakufa kutokana na michezo hatari. Wanaopendekeza michezo hiyo wanajua hatari hizo. Mwanamke mmoja ashirikiye katika kuteleza thelujini kwa skii kwa njia hatari asema hivi: “Nafikiria kifo daima.” Mchezaji mwenye kulipwa wa kuteleza kwa ubao thelujini anasema
kwamba ikiwa “hujeruhiwi, basi hujikakamui vya kutosha.”Tukijua hayo, Mkristo apaswa kuonaje kushiriki katika michezo kama hiyo? Biblia yaweza kutusaidiaje kuamua ikiwa twapaswa kushiriki katika michezo hatari? Kuzingatia maoni ya Mungu kuhusu utakatifu wa uhai kutatusaidia kupata majibu kwa maswali hayo.
Maoni ya Mungu Kuhusu Uhai
Biblia yatuambia kwamba Yehova ni “chemchemi ya uzima.” (Zaburi 36:9) Mbali na kuumba wanadamu, yeye alituandalia yote tunayohitaji ili tufurahie maisha. (Zaburi 139:14; Matendo 14:16, 17; 17:24-28) Kwa hiyo, ni jambo la akili kukata shauri kwamba anatarajia tutunze kile alichotupatia kwa fadhili. Sheria na kanuni ambazo taifa la Israeli lilipewa zatusaidia kuelewa jambo hilo.
Sheria ya Kimusa iliamuru mtu achukue hatua fulani ili kulinda uhai wa wengine. Ikiwa mtu angekufa kwa sababu takwa hilo halikufuatwa, yule ambaye angeweza kuzuia kifo hicho angekuwa na hatia ya damu. Kwa mfano, mwenye nyumba aliamriwa kujenga ukuta kandokando ya dari tambarare la nyumba yake mpya. La sivyo, nyumba hiyo ingekuwa na hatia ya damu ikiwa mtu angeanguka kutoka darini na kufa. (Kumbukumbu la Torati 22:8) Ikiwa fahali bila kutarajiwa alimpiga mtu pembe hadi akafa, mwenye fahali hangeshtakiwa. Kwa upande mwingine, ikiwa ilijulikana kuwa fahali huyo ni hatari na mwenyewe alikuwa ameonywa lakini hakumchunga fahali huyo kwa njia inayofaa, basi endapo fahali huyo angempiga mtu pembe, mwenyewe angehesabiwa kuwa na hatia ya damu na angeweza kuuawa. (Kutoka 21:28, 29) Kwa kuwa uhai ni mtakatifu kwa Yehova, Sheria yake ilitaka uhai uhifadhiwe na kulindwa.
Watumishi waaminifu wa Mungu walielewa kwamba kanuni hizo zilihusu pia kujihatarisha mwenyewe. Katika simulizi moja la Biblia, Daudi alisema kwamba alitamani ‘kunywa maji ya kisima cha Bethlehemu.’ Mji wa Bethlehemu ulikuwa chini ya utawala wa Wafilisti wakati huo. Waliposikia tamaa ya Daudi, watatu kati ya wanajeshi wake wakaingia kambi ya Wafilisti kwa nguvu, wakateka maji katika kisima cha Bethlehemu, na kumletea Daudi. Daudi alifanya nini? Alikataa kunywa maji yale na badala yake akayamwaga ardhini. Akasema hivi: “Mungu wangu apishe mbali, nisifanye hivi; je! ninywe damu ya watu hao waliohatirisha nafsi zao? maana kwa hatari ya nafsi zao wameyaleta.” (1 Mambo ya Nyakati 11:17-19) Kwa Daudi kuhatarisha uhai kwa sababu ya kutosheleza tamaa yake kulikuwa jambo ambalo hangeweza kufanya kamwe.
Yesu alitenda sawa na Daudi wakati ambapo, yamkini katika njozi, Ibilisi alimshawishi kujitupa kutoka buruji ya hekalu ili kuona ikiwa malaika wangemlinda asiumie. Yesu alijibu hivi: “Lazima usimtie Yehova Mungu wako kwenye jaribu.” (Mathayo 4:5-7) Naam, Daudi na Yesu walitambua kwamba haikuwa sawa mbele ya Mungu kufanya lolote ambalo lingeweza kuhatarisha uhai wa binadamu.
Tukikumbuka mifano hiyo, twaweza kujiuliza, ‘Twaweza kubainishaje michezo hatari? Kwa kuwa tafrija ya kawaida, ambayo yenyewe si hatari, yaweza kufanywa kwa njia na kiasi cha hatari, twaweza kujuaje kiasi kilicho sawa?’
Je, Inafaa Kujihatarisha?
Kuchunguza kwa unyofu utendaji wowote ambao twapanga kushiriki kutatusaidia kujibu swali hilo. Kwa mfano, twaweza kujiuliza, ‘Ni watu wangapi wanaojeruhiwa katika mchezo huu? Je, nimezoezwa vya kutosha, au je, nina vifaa vyote vya usalama vinavyohitajika? Matokeo yatakuwa yapi nikianguka au nikikosa kupima mruko vizuri au vifaa vya usalama vikiwa na hitilafu fulani? Je, jambo hilo litasababisha majeraha madogo tu, au huenda likasababisha majeraha mabaya au kifo?’
Kujihatarisha bila sababu nzuri kwaweza kuathiri uhusiano wa Mkristo pamoja na Yehova na vilevile kustahili kwake kupata mapendeleo kutanikoni. (1 Timotheo 3:2, 8-10; 4:12; Tito 2:6-8) Kwa wazi, hata wanapofanya tafrija mbalimbali, Wakristo wafanya vyema kuzingatia maoni ya Muumba kuhusu utakatifu wa uhai.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Vitu vinne vifuatavyo vyahusika katika mchezo huo: jengo, mlingoti, daraja na genge. Mchezo huo wa kuruka kwa mwavuli kutoka kwa majengo, madaraja na magenge ni hatari sana hivi kwamba umepigwa marufuku na shirika la Marekani la Huduma ya Kitaifa ya Hifadhi ya Wanyama.