Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Piramidi za Mexico

Piramidi za Mexico

Piramidi za Mexico

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA MEXICO

WATU wengi leo wanafahamu piramidi za Misri. Huko Amerika pia, waakiolojia wamegundua majengo yanayofanana na piramidi, hasa katika Mexico. Piramidi za Mexico zimedumu kwa karne nyingi na zina mafumbo mengi sawa na zile za Misri.

Piramidi ya Misri ni kaburi lililochongwa ndani ya rundo kubwa la mawe yaliyopangwa sawasawa. Vijia vilivyomo huelekeza kaburini, sehemu muhimu zaidi ya piramidi. Lakini, piramidi ya Mexico ni rundo kubwa la udongo ambalo lina hekalu kileleni na kuna ngazi nje yake zinazoelekea kileleni. Ni piramidi chache sana zilizopatikana Amerika ambazo zilikuwa makaburi.

Teotihuacán—“Mji wa Miungu”

Mojawapo ya sehemu mashuhuri zaidi zenye piramidi huko Mexico ni Teotihuacán. Teotihuacán ulio kilometa 50 hivi kaskazini-mashariki ya Mexico City, ungali fumbo kwa wanaanthropolojia na waakiolojia. Mji huu mkuu wa kale uliachwa na wajenzi wake zaidi ya miaka 500 kabla ya kuibuka kwa utamaduni wa Waazteki. Jina Teotihuacán, la lugha ya Nahuatl, humaanisha “Mji wa Miungu” au “Mahali Ambapo Wanadamu Wanakuwa Miungu.” Yadhaniwa kwamba Waazteki waliupa mji huo jina hilo walipouzuru.

Mmoja wa wahariri wa gazeti la National Geographic, George Stuart, aeleza kwamba “Teotihuacan ulikuwa mji halisi wa kwanza katika Kizio cha Magharibi . . . Uliibuka karibu na mwanzo wa enzi ya Ukristo, ukadumu kwa karne saba, kisha ukatokomea na kuwa wa kihistoria. Katika upeo wa ufanisi wake, wapata mwaka wa 500 A.D., inakadiriwa kwamba ulikuwa na kati ya watu 125,000 na 200,000.”

Piramidi ya Jua iliyo mashuhuri iko karibu katikati ya mji. Ina kitako cha meta 220 kwa 225, na ngazi zake tano zinapanda kufikia urefu wake wa sasa wa meta 63 hivi. Lazima upande zaidi ya vidato 240 ili ufike kilele cha piramidi hiyo. Upande wa kaskazini wa mji huo wa kale kuna Piramidi ya Mwezi, yenye kimo cha meta 40. Vilele vya piramidi hizo mbili kuu vilikuwa na mahekalu hapo awali.

Katika miongo ya karibuni mengi yamejulikana kuhusu piramidi hizo. Hata hivyo, kama Stuart asemavyo, “bado hatujui chochote kuhusu asili ya Wateotihuacan, lugha waliyozungumza, utaratibu wa jamii yao, na kilichofanya watokomee.”

Sehemu Nyingine Zenye Piramidi

Katikati ya Mexico City, kuna Hekalu Kuu la Waazteki unaloweza kuzuru. Ingawa hakuna piramidi yoyote karibu, mabaki ya piramidi iliyokuwa msingi wa Hekalu Kuu bado yaweza kuonekana. Waakiolojia wamechimbua madhabahu mawili ambayo yalitumiwa kutolea dhabihu za wanadamu.

Chichén Itzá ni mojawapo ya sehemu zenye piramidi zinazotembelewa sana katika Mexico. Jimbo la Wamaya lina magofu mengi ya kale, lakini magofu hayo hufikika kwa urahisi kwa sababu yako karibu na mji wa Mérida huko Yucatán. Ingawa majengo hayo yalijengwa katika eneo la Wamaya, yanaonyesha kwamba wakati mmoja Watolteki walikuwa na uvutano katika majimbo hayo. Majengo fulani hudhihirisha ujuzi wa hali ya juu sana wa hisabati na wa elimu ya nyota wa wajenzi wake.

Katika Palenque, wageni waweza kuona kijiji kikubwa chenye kuvutia cha Wamaya kinachozingirwa na jangwa la Chiapas. Miongoni mwa piramidi nyingi na majengo mna Jumba la Mfalme na Hekalu la Michoro. Hekalu la Michoro “ni mojawapo ya mahekalu maarufu zaidi katika Mesoamerica yote kwa sababu mbali na kuwa kituo cha hekalu kama mengineyo, lilikuwa nguzo ya ukumbusho wa wafu,” chaeleza kitabu cha The Mayas—3000 Years of Civilization. “Ndani yake mna ngazi ya chini inayoelekeza kwenye kaburi lenye kuvutia sana lililowahi kupatikana katika eneo la Wamaya.” Kaburi hilo lilijengwa kwa ajili ya gavana mmoja aliyeishi katika karne ya saba—Pacal, au Uoxoc Ahau.

Hizo ni baadhi tu ya piramidi zilizo Mexico. Magofu na piramidi nyingine ziko kotekote nchini. Kuna piramidi kubwa nchini Guatemala na Honduras pia. Majengo hayo yote ya kale yanaonyesha kwamba wakazi wa Mesoamerica walitamani kujenga sehemu zao za ibada mahali palipoinuka. Walter Krickeberg, mtungaji wa kitabu Las Antiguas Culturas Mexicanas, aliandika hivi: “Desturi ya kujenga mahekalu kwenye misingi yenye ngazi ilianza na ibada ya kale ya sehemu zilizoinuka.” Aongezea kusema: “Ingawa sisi huona mbingu kuwa ‘chumba,’ kwa watu wengine iliwakilisha mlima ambapo jua lilichomoza asubuhi na kutua jioni; miteremko yake ina ngazi kama jengo kubwa sana. Hivyo, ‘mlima huo wa kuwaziwa’. . . uligeuzwa kuwa piramidi yenye ngazi na, kulingana na hekaya na desturi, uligeuzwa kuwa ishara ya mbingu miongoni mwa makabila mengi ya Mesoamerica.”

Dhana hiyo yaweza kuwakumbusha wanafunzi wa Biblia lile simulizi la Biblia kuhusu Mnara wa Babeli, uliokuwa katika jiji lililokuja kuitwa Babiloni. Andiko la Mwanzo 11:4 husema hivi juu ya wajenzi wa mnara huo: “Wakasema, haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina.” Waakiolojia wamegundua piramidi zinazoitwa zigurati karibu na magofu ya Babiloni.

Ibada iliyoanzia Babiloni ilienea katika sehemu nyingi za ulimwengu, na yaelekea ilifika katika eneo lililokuja kuitwa Mexico. Si jambo la kushangaza kupata kwamba zigurati na vilevile dini na mazoea ya Babiloni, zilikuwa vigezo vya piramidi za kifumbo na zinazovutia sana za Mexico.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Teotihuacán

[Hisani]

▲CNCA.-INAH.-MEX Reproducción Autorizada por el Instituto Nacional de Antropología e Historia▶

[Picha katika ukurasa wa 17]

Palenque