Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Afya Bora—Je, Kuna Mwelekeo Mpya?

Afya Bora—Je, Kuna Mwelekeo Mpya?

Afya Bora—Je, Kuna Mwelekeo Mpya?

Afya ni suala muhimu sana kwa watu wengi. Nyakati nyingine, ni kana kwamba kuna maoni mengi ya kibinafsi kuhusu afya kama walivyo madaktari. Badala ya kuunga mkono upande wowote, Amkeni! linajaribu kuripoti kupitia kwa mfululizo huu wa makala kuongezeka kwa yale yanayoitwa matibabu ya asili. Hatupendekezi mojawapo ya matibabu tutakayozungumzia au mengine yoyote. Matibabu mengi hayatajwi—baadhi yake yanapendwa sana, mengine huzusha ubishi. Twaamini kwamba elimu kuhusu masuala ya afya ni muhimu kwa ujumla; maamuzi kuhusu masuala ya afya ni mambo ya kibinafsi.

KILA mtu ataka kuwa na afya bora. Lakini yaweza kuwa vigumu kuwa na afya bora, kama inavyothibitishwa na watu wengi wenye matatizo ya afya. Baadhi ya watu huona kwamba kuna wagonjwa wengi zaidi leo kuliko awali.

Madaktari wengi hutumaini sana kuponya magonjwa kwa kuwaagiza wagonjwa watumie madawa yanayotengenezwa na kutangazwa hima-hima na makampuni ya madawa. Jambo la kutokeza ni kwamba mauzo ya madawa ulimwenguni pote yameongezeka sana katika miongo ya karibuni, kutoka kwa mabilioni machache ya dola kwa mwaka hadi mamia ya mabilioni ya dola kwa mwaka. Tokeo limekuwa nini?

Madawa yanayoagizwa na madaktari kwa matibabu yamewasaidia watu wengi. Hata hivyo, baadhi ya watu wanaotumia madawa wangali na afya mbaya au hata imezorota. Kwa hiyo, hivi karibuni wengine wamegeukia njia nyingine za matibabu.

Matibabu Wanayogeukia Wengi

Katika sehemu ambako tiba ya kisasa isiyo ya asili imekuwa ikitumiwa kutibu magonjwa, watu wengi sasa wanageukia yale yanayoitwa matibabu ya asili, au ya ziada. “Yaonekana ukuta ambao umekuwa ukitofautisha kwa muda mrefu matibabu ya asili na matibabu yasiyo ya asili unaporomoka,” lasema gazeti la Consumer Reports la Mei 2000.

Jarida la The Journal of the American Medical Association (JAMA), la Novemba 11, 1998, lilisema hivi: “Matibabu ya asili, ambayo huonwa kuwa vizuizi vya magonjwa visivyofunzwa sana katika vyuo vya tiba wala kupatikana kwa ukawaida katika hospitali za Marekani, yamevutia vyombo vya habari nchini, wataalamu wa tiba, mashirika ya kiserikali, na umma.”

Hata hivyo, jarida la Journal of Managed Care Pharmacy lilieleza hivi mnamo mwaka wa 1997 kuhusu mwelekeo huo wa kisasa: “Hapo zamani madaktari wa matibabu yasiyo ya asili walikuwa wakishuku matibabu ya asili, lakini sasa shule 27 za tiba huko Marekani [ripoti ya karibuni zaidi yasema 75] zinaandaa mtalaa wa hiari wa matibabu ya asili, kutia ndani Chuo Kikuu cha Harvard, Chuo Kikuu cha Stanford, Chuo Kikuu cha Arizona, na Chuo Kikuu cha Yale.”

Jarida la JAMA lilitaja mambo ambayo wagonjwa wengi wanafanya ili kuboresha afya yao. Liliripoti hivi: “Mnamo mwaka wa 1990, takriban mtu 1 (asilimia 19.9) kati ya watu 5 waliopata ushauri wa daktari wa kitiba kuhusiana na ugonjwa fulani walitumia pia matibabu ya asili. Asilimia hiyo iliongezeka kufikia mtu 1 (asilimia 31.8) kati ya 3 mwaka wa 1997.” Makala hiyo ilisema hivi pia: “Uchunguzi wa kitaifa uliofanywa sehemu nyinginezo mbali na Marekani unadokeza kwamba matibabu ya asili yanapendwa sana katika nchi zote zilizositawi kiviwanda.”

Kwa mujibu wa JAMA, idadi ya watu waliotumia matibabu ya asili katika kipindi cha miezi 12 ya karibuni ilikuwa asilimia 15 nchini Kanada, asilimia 33 nchini Finland, na asilimia 49 nchini Australia. “Uhitaji wa matibabu ya asili umeongezeka sana,” lakiri JAMA. Hilo ni kweli hasa uzingatiapo uhakika wa kwamba ni nadra sana kampuni za bima kulipia gharama kwa matibabu ya aina hiyo. Makala hiyo ya jarida la JAMA ilimalizia kwa kusema: “Ikiwa malipo ya bima kwa matibabu ya asili yataongezeka wakati ujao, basi matumizi ya sasa huenda yasitoe picha kamili ya hali ya wakati ujao kuhusu idadi ya watu wanaopendelea matibabu hayo.”

Mwelekeo wa kuchanganya matibabu ya asili na yale yasiyo ya asili umekuwa desturi ya muda mrefu katika nchi nyingi. Dakt. Peter Fisher, wa Royal London Homeopathic Hospital, alisema kwamba matibabu maarufu ya asili yamekuwa “kama matibabu yasiyo ya asili katika sehemu nyingi. Sasa hakuna tena aina mbili za matibabu, ya asili na yale yasiyo ya asili,” akadai. “Kuna matibabu yanayofaa na yale yasiyofaa peke yake.”

Kwa hiyo, wataalamu wengi wa tiba leo wanatambua umuhimu wa matibabu yasiyo ya asili na yale ya asili. Badala ya kusisitiza kwamba mgonjwa atumie aina moja tu ya matibabu au nyingine, wanapendekeza kutumia njia yoyote ya matibabu kati ya njia zote zilizopo leo ambayo inaweza kumponya mgonjwa.

Ni nini baadhi ya njia za matibabu za yale yanayoitwa matibabu ya asili, au ya ziada? Baadhi ya matibabu hayo yalianzia wapi na lini? Na kwa nini watu wengi sana wanayatumia?