Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuchunguza Matibabu ya Asili

Kuchunguza Matibabu ya Asili

Kuchunguza Matibabu ya Asili

“Kuanzisha mjadala wa kitaaluma kati ya matabibu wa matibabu yasiyo ya asili na wale wa matibabu ya asili ni muhimu sana katika kuboresha tiba ya wagonjwa wanaochagua matibabu ya asili.”

TAARIFA hiyo ilichapishwa katika jarida la The Journal of the American Medical Association (JAMA) katika toleo lake la Novemba 11, 1998. Makala hiyo ilisema hivi: “Uhitaji [wa mjadala] watarajiwa kuongezeka kadiri matibabu ya asili yanavyoongezeka, hasa makampuni ya bima ya afya yanapotoa malipo ya bima kwa matibabu hayo.”

Wagonjwa wengi zaidi wanatumia matibabu ya asili pamoja na matibabu mengine yasiyo ya asili. Lakini, wagonjwa wengine hawamfahamishi daktari wao. Kwa hiyo, gazeti la Tufts University Health & Nutrition Letter la Aprili 2000 lilisihi hivi: “Wapaswa kuhangaikia hali njema yako kwa kushirikiana na daktari wako badala ya kujifanyia mambo.” Liliongezea kusema: “Iwe atakubali uchaguzi wako au la, yaelekea utanufaika kwa kumpasha habari hiyo.”

Habari hiyo ilisemwa kwa sababu ya hatari za kiafya zinazoweza kuzuka unapochanganya mitishamba fulani na madawa yasiyo ya asili. Wataalamu wengi wa afya hujitahidi sana kutoruhusu maoni yao binafsi kuhusu utunzaji wa afya yawazuie kushirikiana na wataalamu wa matibabu ya asili kwa manufaa ya mgonjwa, kwa sababu wanang’amua kwamba baadhi ya wagonjwa wao wanachagua matibabu hayo.

Tutazungumzia kifupi baadhi ya matibabu ya asili kusudi tuwafahamishe wasomaji wetu kuhusu matibabu hayo ambayo sasa yanatumiwa na watu wengi zaidi katika nchi nyingi. Hata hivyo, tafadhali kumbuka kwamba Amkeni! halipendekezi yoyote ya matibabu hayo wala matibabu mengine yoyote.

Matibabu ya Mitishamba

Yaelekea kwamba matibabu haya ndiyo yanayopendwa sana kati ya matibabu yote ya asili. Licha ya kwamba mitishamba imetumiwa kwa matibabu kwa karne nyingi, ni mimea michache sana ambayo imechunguzwa kwa uangalifu na wanasayansi. Ni mimea michache sana na bidhaa zake ambazo zimechunguzwa sana hivi kwamba usalama na uwezo wake wa kuponya umethibitishwa. Habari zilizo nyingi kuhusu mitishamba hutegemea matokeo ya matumizi ya kale.

Lakini katika miaka ya majuzi, kumekuwako na uchunguzi kadhaa wa kisayansi unaoonyesha umuhimu wa mitishamba fulani katika kutibu matatizo kama vile mshuko-moyo wa kiasi, kupoteza kumbukumbu kwa sababu ya uzee, na dalili za uvimbe hafifu wa tezi-kibofu. Mtishamba mmoja uliochunguzwa ni black cohosh, ambao nyakati nyingine huitwa black snakeroot, bugbane, au rattleroot. Wahindi Wekundu walichemsha mizizi yake na kuitumia kuhusiana na matatizo ya hedhi na uzazi. Kwa mujibu wa gazeti la Harvard Women’s Health Watch la Aprili 2000, uchunguzi wa hivi karibuni unadokeza kwamba bidhaa ya black cohosh ya Ujerumani ambayo inauzwa madukani inaweza “kutuliza dalili za koma-hedhi.”

Yaonekana kwamba uhitaji mkubwa wa matibabu hayo ya kiasili hutegemea dhana ya kwamba ni salama kuliko madawa ya kemikali. Ijapokuwa hilo laweza kuwa kweli mara nyingi, mitishamba fulani ina athari mbaya, hasa inapotumiwa pamoja na madawa mengine. Kwa mfano, mtishamba unaojulikana sana ambao unasifiwa kuwa tiba ya kiasili ya mvilio wa damu na ya kupunguza uzito wa mwili unaweza kuzidisha shinikizo la damu na mpigo wa moyo.

Pia kuna mitishamba ambayo humfanya mgonjwa avuje damu nyingi zaidi. Endapo mitishamba hiyo itatumiwa pamoja na madawa ya kitiba ya “kuifanya damu iwe nyepesi,” basi hali hatari yaweza kuzuka. Watu wenye magonjwa ya kudumu, kama vile ugonjwa wa sukari au shinikizo la damu, au wale wanaotumia madawa mengine wapaswa kujihadhari kuhusu kutumia mitishamba.—Ona sanduku lililoonyeshwa.

Hangaiko jingine kuhusu mitishamba ni ukosefu wa uhakikishio wa usafi katika kutengeneza bidhaa hizo. Katika miaka ya karibuni kumekuwako na ripoti za bidhaa zilizochanganywa na metali nzito na vitu vingine vyenye sumu. Kwa kuongezea, bidhaa nyingine za mitishamba zimegunduliwa kuwa na vitu vichache au hata kukosa vitu vyote vilivyotajwa kwenye kibandiko chake. Mifano hiyo yakazia uhitaji wa kununua bidhaa za mitishamba, vilevile bidhaa zozote za afya, kutoka kwa vyanzo vinavyojulikana na vinavyotegemeka.

Nyongeza za Lishe

Imeripotiwa kwamba nyongeza za lishe, kama vile vitamini na madini, zimesaidia sana kuzuia na kutibu matatizo kadhaa ya afya, kutia ndani upungufu wa damu na kudhoofika kwa mifupa—na hata kuzuia kasoro fulani za kurithiwa. Vidonge vya vitamini na madini vinavyopendekezwa na serikali kwa matumizi ya kila siku vinaonwa kuwa salama zaidi na vyenye kufaa zaidi.

Kwa upande mwingine, kumeza vidonge vingi kupita kiasi ili kutibu magonjwa fulani kwaweza kuwa hatari kwa afya. Kwaweza hata kuvuruga ufyonzaji au utendaji wa virutubishi vingine na vyaweza pia kusababisha athari mbaya. Uwezekano huo, vilevile ukosefu wa uthibitisho wa kutosha kuunga mkono matumizi ya vitamini zenye nguvu sana, haupasi kupuuzwa.

Homeopathy

Matibabu ya homeopathy [matibabu ya kutumia viini vya ugonjwa wenyewe] yalibuniwa katika miaka ya 1700 yakiwa matibabu yenye kutuliza yasiyo makali, tofauti na yale yaliyopendwa nyakati hizo. Tiba ya homeopathy hutegemea kanuni ya “dawa sawa kwa ugonjwa sawa” na nadharia ya kutumia kiasi kidogo tu cha dawa. Matibabu ya homeopathy hutayarishwa kwa kupunguza kabisa nguvu za madawa yanayotumiwa kuponya—nyakati nyingine, hupunguzwa nguvu sana hata kufikia kusalia kiwango cha chini cha molekuli ya madawa hayo.

Hata hivyo, madawa ya homeopathy yalikuwa na matokeo katika kutibu matatizo kama vile pumu, mizio, na kuharisha kwa watoto wachanga kuliko madawa ya kutuliza. Madawa ya homeopathy huonwa kuwa salama sana, kwa kuwa yamepunguzwa nguvu kabisa. Makala moja iliyochapishwa katika toleo la Machi 4, 1998, la jarida la JAMA lilisema hivi: “Homeopathy yaweza kuwa matibabu muhimu na yanayofaa wagonjwa wengi wenye magonjwa ya kudumu ambayo hayawezi kupimwa kwa njia muafaka. Endapo yatumiwa kwa kiasi, matibabu ya homeopathy yanaweza kukamilisha matibabu ya kisasa yakiwa, ‘njia nyingine ya tiba.’” Lakini, huenda likawa jambo la hekima kutumia madawa mengine yasiyo ya asili ya matibabu, kunapokuwa na hali hatari ya dharura.

Matibabu ya Maungo

Kuna matibabu kadhaa ya asili ya kurekebisha maungo ya mwili. Matibabu ya maungo ni miongoni mwa matibabu ya asili yanayopendwa sana, hasa katika Marekani. Yanategemea wazo la kwamba mtu aweza kupona haraka uti wa mgongo unapolainishwa. Ndiyo sababu wataalamu wa matibabu ya maungo huwa hodari sana katika kurekebisha na kulainisha pingili za uti wa mgongo wa wagonjwa wao.

Matibabu yasiyo ya asili wakati mwingine hushindwa kutuliza maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo. Lakini wakati mwingine, baadhi ya wagonjwa wanaopata matibabu ya maungo huridhika sana. Ni nadra sana kupata uthibitisho wa kuunga mkono matumizi ya kurekebisha maungo katika kutibu matatizo mengine mbali na maumivu.

Jambo la kutokeza ni kwamba kuna ripoti chache za athari zitokanazo na kurekebishwa maungo na tabibu mwenye uzoefu. Hata hivyo, mtu apaswa pia kukumbuka kwamba ulainishaji wa shingo huhusianishwa na hatari ya kuibuka kwa matatizo mengine makubwa sana, kama vile kiharusi na kupooza. Ili kupunguza hatari ya kuibuka kwa matatizo hayo, wataalamu fulani hupendekeza kwamba mtu apimwe kabisa ili kujua njia mahususi ya ulainishaji iliyo salama kwake.

Kukanda Mwili

Manufaa ya kukanda mwili yamejulikana kwa muda mrefu katika tamaduni karibu zote. Hata Biblia inaripoti zoea hilo. (Esta 2:12) “Mbinu za kukanda mwili hutimiza fungu muhimu katika matibabu ya kale ya Kichina na ya Kihindi,” lasema jarida la British Medical Journal (BMJ) la Novemba 6, 1999. “Kukanda mwili huko Ulaya kulianzishwa na Per Hendrik Ling mapema katika karne ya 19, alipobuni mbinu ambayo sasa inaitwa kukanda mwili kwa Sweden.”

Yasemekana kwamba kukanda mwili hulegeza misuli, huboresha mzunguko wa damu, na kuondoa kemikali zinazorundamana kwenye tishu. Sasa madaktari huagiza wagonjwa wenye matatizo kama vile maumivu ya mgongo, maumivu ya kichwa, na matatizo ya mmeng’enyo wa chakula waweze kukandwa mwili. Watu wengi wanaokandwa mwili hueleza jinsi kunavyowatuliza. Dakt. Sandra McLanahan asema kwamba “asilimia themanini ya ugonjwa inasababishwa na mkazo, na kukanda mwili hupunguza mkazo.”

“Mbinu nyingi za kukanda mwili hazina hatari kubwa ya kusababisha athari mbaya,” likaripoti jarida la BMJ. “Hali zinazoweza kukufanya uepuke kukandwa mwili kwa sehemu kubwa hutegemea maarifa ya kawaida (kwa mfano, kuepuka kusugua majeraha ya kuchomeka au kukanda kiungo chenye mshipa unaovuja damu kindani) . . . Hakuna uthibitisho wowote kwamba kukanda miili ya wagonjwa wenye kansa hueneza ugonjwa huo mwilini.”

“Kadiri ukandaji-mwili unavyozidi kupendwa, ndivyo wateja wanavyozidi kuhangaikia ujuzi wa matabibu wa kukanda mwili, na bila shaka hilo lafaa,” asema E. Houston LeBrun, aliyewahi kuwa msimamizi wa Shirika la Marekani la Tiba ya Kukanda Mwili. Jarida la BMJ lilishauri kwamba ili kuepuka tabia isiyo ya kitaaluma, “wagonjwa wapaswa kuhakikisha kwamba matabibu hao wamesajiliwa na shirika lifaalo linalotoa leseni.” Ripoti moja ya mwaka uliopita ilisema kwamba matabibu walikuwa wamepewa leseni katika majimbo 28 huko Marekani.

Matibabu ya Vitobo

Matibabu ya vitobo (Acupuncture) yameenea sana kotekote ulimwenguni. Japo “matibabu ya vitobo” yanatia ndani mbinu kadhaa mbalimbali, kwa kawaida huhusisha kutumia sindano nyembamba sana ambazo hudungwa sehemu hususa za mwili ili kutokeza hisia inayoponya. Utafiti uliofanywa katika miongo kadhaa iliyopita wadokeza kwamba matibabu ya vitobo yaweza kufanya kazi nyakati nyingine kwa kutokeza kemikali katika mishipa ya fahamu, kama vile protini za endorphin, ambazo zinaweza kutuliza maumivu na uvimbe mchungu.

Utafiti fulani wadokeza kwamba matibabu ya vitobo yaweza kutibu magonjwa kadhaa na ni salama kuliko unusukaputi. Shirika la Afya Ulimwenguni linatambua kwamba matibabu ya vitobo hutibu magonjwa 104. Na kamati iliyoteuliwa na Taasisi za Kitaifa za Afya za Marekani ilitaja uthibitisho wa kwamba matibabu ya vitobo ni tiba inayokubalika ya kutuliza maumivu ya baada ya upasuaji, maumivu ya misuli, mkakamao wa misuli wakati wa hedhi, kichefuchefu na kutapika kunakosababishwa na tiba ya kemikali au ujauzito.

Ingawa ni nadra sana kupata athari mbaya kutokana na matibabu ya vitobo, watu fulani huhisi uchungu, hufa ganzi, au huhisi mwasho. Kufisha ifaavyo viini vilivyo kwenye sindano au kutumia sindano zinazotupwa baada ya tiba kwaweza kupunguza hatari ya maambukizo. Wanatiba wengi wa vitobo hukosa ujuzi wa kitiba unaohitajiwa ili kupima ugonjwa ifaavyo au kupendekeza matibabu mengine yafaayo. Si jambo la hekima kupuuza ukosefu huo wa ujuzi wa kupima ugonjwa, hasa ikiwa unachagua matibabu ya vitobo kutuliza dalili za magonjwa ya kudumu.

Machaguo Ni Mengi Sana

Hayo ni matibabu machache tu kati ya matibabu mengi ambayo sasa hurejezewa katika sehemu nyingine kuwa matibabu ya asili. Baadhi ya matibabu hayo, pamoja na mengine ambayo hayakuzungumziwa, huenda yakaonwa kuwa matibabu yasiyo ya asili wakati ujao, kama yalivyo sasa katika sehemu nyingine za ulimwengu. Bila shaka, matibabu mengine huenda yakatokomea au hata kuchukiwa.

Jambo la kusikitisha ni kwamba maumivu na magonjwa ni mambo yanayowasumbua sana wanadamu, kama tu Biblia inavyotaarifu kwa usahihi: “Twajua kwamba viumbe vyote vinafuliza kupiga kite pamoja na kuwa katika maumivu pamoja hadi sasa.” (Waroma 8:22) Bila shaka wanadamu wanatarajiwa kutafuta kitulizo. Lakini twaweza kugeukia wapi? Tafadhali fikiria maoni fulani ambayo yanaweza kukusaidia unapochagua matibabu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Kuchanganya Mitishamba na Madawa—KUNA HATARI ZIPI?

Mara kwa mara watu wameonywa dhidi ya kuchanganya madawa au kuyatumia pamoja na vileo. Je, kuna hatari pia kutumia mitishamba fulani pamoja na madawa ya kitiba? Zoea hilo limeenea kadiri gani?

Makala moja katika jarida la The Journal of the American Medical Association iliripoti juu ya “matumizi ya madawa ya kitiba pamoja na mitishamba.” Ilisema hivi: “Kati ya asilimia 44 ya watu wazima waliosema kwamba walitumia kwa kawaida madawa ya kitiba, takriban mtu 1 (asilimia 18.4) kati ya watu 5 alikiri kutumia angalau dawa 1 ya mitishamba, kibonge chenye vitamini nyingi, au vyote viwili.” Ni muhimu kujua hatari ziwezazo kusababishwa na zoea hilo.

Wale wanaotumia madawa fulani ya mitishamba wanapaswa kuwa na tahadhari wapatapo matibabu yanayohitaji unusukaputi. Dakt. John Neeld, msimamizi wa Shirika la Amerika la Wataalamu wa Unusukaputi alieleza hivi: “Watu fulani wameripoti kwamba mitishamba fulani inayopendwa sana, kama vile ginseng na St. John’s wort, yaweza kusababisha mabadiliko makubwa ya shinikizo la damu. Hilo laweza kuwa hatari sana wakati wa unusukaputi.”

Daktari huyo akaongezea kusema: “Mitishamba mingine kama vile ginkgo biloba, tangawizi na feverfew, yaweza kuvuruga kuganda kwa damu, na kuzusha hatari kubwa sana wakati wa tiba ya unusukaputi wa ngozi ya nje inayofunika ubongo na ya mshipa mkuu wa ufahamu katika uti wa mgongo—iwapo damu inavuja karibu na uti wa mgongo, yaweza kumfanya mgonjwa apooze. Mtishamba wa St. John’s wort waweza pia kuzidisha athari za madawa fulani ya kulevya au madawa ya unusukaputi.”

Kwa wazi, ni muhimu sana kujua hatari iwezayo kukupata unapotumia mchanganyiko wa mitishamba fulani na madawa. Wanawake wajawazito na wale wanyonyeshao wapaswa hasa kujihadhari na madhara yawezayo kuwapata watoto wao wachanga kwa sababu ya mchanganyo wa mitishamba fulani na madawa. Hivyo basi, wagonjwa wanatiwa moyo kuzungumza na madaktari wao kuhusu madawa wanayotumia, yawe ya asili au yasiyo ya asili.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Mitishamba fulani imesaidia sana kutibu matatizo ya afya

“Black cohosh”

“Saint-John’s-wort”

[Hisani]

© Bill Johnson/Visuals Unlimited

[Picha katika ukurasa wa 7]

Ili kufaulu, wagonjwa wanapaswa kushirikiana na wataalamu wa matibabu