Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Je, Maoni Tofauti Ni Muhimu?

“Wengi wetu hatupendi kutafuta maoni tofauti kwa mambo ya kitiba. Lakini, itikio la jinsi hiyo laweza kusababisha wagonjwa wengi kufa,” lasema gazeti The News la Mexico City. Mara nyingi wagonjwa huhisi kwamba daktari wao atachukizwa iwapo watatafuta maoni tofauti. Kinyume cha hilo “madaktari walio wengi hawachukizwi na wagonjwa wenye kuuliza,” lasema gazeti hilo. “Iwapo daktari wako ni mwenye kuchukizwa jihadhari.” Leo, kutafuta maoni tofauti huonwa na madaktari na makampuni ya kutoa bima kuwa uhakikishio wa kupata matibabu bora. Dakt. Michael Andrews, msimamizi wa Shirika la Magonjwa ya Uvimbe la Georgia, alisema kwamba yeye huwatia moyo wagonjwa wake kutafuta maoni tofauti kwa sababu wao hurudi wakiwa na uhakika zaidi kwa ushauri wake. Mkurugenzi wa shirika fulani la afya ya umma alisema hivi: “Wagonjwa wanapaswa kukumbuka kwamba ni miili yao wenyewe inayohusika.”

Marafiki Hatari

Kwa mujibu wa ripoti katika jarida la The Journal of the American Medical Association, madereva vijana huelekea zaidi kufanya aksidenti kunapokuwa na abiria ndani ya gari. Wachunguzi katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, Maryland, Marekani, waligundua kwamba uwezekano wa kijana mwenye umri wa miaka 16 kufa kwenye aksidenti uliongezeka kwa asilimia 39 akiwa na abiria mmoja, kwa asilimia 86 akiwa na wawili, na kwa asilimia 282 akiwa na abiria watatu au zaidi. Sababu kuu katika ripoti hiyo ilikuwa ni “tabia hatari za uendeshaji-gari . . . , hasa wakiwepo marika zake.” Tabia hizo hatari zinatia ndani mwendo wa kasi sana, kufuata magari mengine karibu sana, kutosimama penye taa, kuendesha gari wakiwa wametumia dawa za kulevya au vileo, na kukengeushwa fikira na abiria wenye kuchezeana kwa fujo.

‘Hekima Huongezeka Kadiri Wanavyozeeka’

Watafiti wamegundua kwamba sehemu fulani za ubongo hutokeza chembe mpya kadiri watu wanavyozeeka, laripoti gazeti The Times la London. Hapo awali iliaminika kwamba ubongo haukuwa na uwezo wa kutokeza chembe mpya katika watu wazima. “Ufunguo wa kuchochea ubongo kutokeza chembe mpya ni kuhakikisha una shughuli nyingi,” lasema gazeti la The Times. Uchunguzi wa hivi karibuni wa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 65 ulipata kwamba kusoma pamoja na urafiki na watu wengine ulichangia kuchochea ukuzi mpya wa chembe za ubongo na miunganisho yake. Wachunguzi hao walipata kwamba kuwa na ushirika pamoja na watu wengine kuliwapa watu “afya bora, maisha marefu na uradhi zaidi.” Mwanasayansi wa mfumo wa neva Susan Greenfield asema hivi: “Kadiri uzoefu wako wa maisha ulivyo mwingi ndivyo ilivyo mingi miunganisho yako. Hivyo watu huongeza hekima kadiri wanavyozeeka.”

Njia ya Bahari ya Kaskazini

Robert Thorne mfanya-biashara wa viungo aliyeishi katika karne ya 16 alikuwa na wazo la kutafuta njia ya bahari kati ya Ulaya na Mashariki ya Mbali kupitia eneo la Aktiki. Leo, wazo hilo la Thorne limefua dafu kwa sababu ya ongezeko la joto ulimwenguni pote, laripoti gazeti The Times la London. Maji ya ufuo wa Urusi na Siberia Mashariki sasa huwa bila barafu yoyote katika miezi yote ya kiangazi, ikiwezesha meli kusafiri kutoka Bahari ya Kaskazini, kuzunguka ncha ya kaskazini ya dunia na kuingia bahari ya Pasifiki kupitia Mlango-Bahari wa Bering. Wakati njia hii imezibwa na barafu, meli kutoka Ulaya hulazimika kutumia Mfereji wa Suez, kuzunguka kusini mwa Afrika, au kuvuka Mfereji wa Panama ili kufika Mashariki ya Mbali. Kutumia njia ya bahari ya kaskazini kunaleta faida kubwa kiuchumi. Hufupisha maradufu safari ya kutoka Hamburg, Ujerumani, na Yokohama, Japani—kwa umbali usiozidi kilometa 13,000 za ubaharia.

Matatizo Katika Kupima Damu

“Zaidi ya nusu ya nchi za ulimwengu hushindwa kupima ifaavyo damu wanayopokea, na hivyo kuzidisha hatari ya kueneza UKIMWI na maradhi mengine,” yasema ripoti moja ya shirika la habari la Associated Press. Ripoti hiyo, iliyotegemea habari kutoka kwa Shirika la Afya Ulimwenguni, yadai pia kwamba “asilimia 5 hadi 10 ya watu wenye virusi vya UKIMWI waliambukizwa ugonjwa huo kupitia kutiwa damu mishipani.” Hata hivyo, UKIMWI ni mojawapo ya magonjwa yanayopitishwa kwa njia hiyo. Kila mwaka, watu wapatao milioni 8 hadi milioni 16 huambukizwa mchochota wa ini aina ya B na watu wapatao milioni 2 hadi milioni 4 huambukizwa mchochota wa ini aina ya C kupitia kutiwa damu mishipani na kutumia sindano zenye viini. Sababu moja inayotolewa ya kutopima damu ifaavyo ni kwamba kufanya hivyo hugharimu pesa nyingi. Kupima magonjwa hayo katika kila painti ya damu hugharimu kiasi cha dola 40 hadi dola 50 za Marekani. Hata hivyo, upimaji huo “si salama wakati wote, hasa unapofanywa na watu wasio na uzoefu au wenye vifaa duni,” yasema ripoti hiyo.

Kuwatendea Vibaya Watoto Katika India

Gazeti The New Indian Express laripoti kwamba mtoto mmoja anaingizwa katika umalaya kila dakika kumi huko India. Hilo lamaanisha kwamba watoto 50,000 wa Kihindi wanalazimishwa kuingia katika biashara ya ngono kila mwaka. Warsha moja juu ya kutendwa vibaya kingono kwa watoto katika jimbo la Kerala iligundua jambo lenye kushtua. Madaktari wa huko “hukataa kushughulikia visa vya ubakaji kwa sababu hawana uzoefu wa mambo hayo wala hawataki kuhusishwa,” lasema gazeti hilo. Katika visa fulani, hata wazazi huwa wamechangia tatizo hilo. Msimamizi wa Makao Makuu ya Ulinzi, Sreelekha, alisema: “Wazazi hukataa kuripoti kwa polisi visa vya [ubakaji] kwa sababu ya kuogopa fedheha na kutengwa na jumuiya.”

Kula Pamoja Mkiwa Familia Huboresha Afya

Mojawapo ya njia bora zaidi za wazazi kuhakikisha kwamba watoto wao wana afya bora ni kula pamoja nao mlo wa jioni, lasema gazeti Globe and Mail. Kwa mujibu wa Dakt. Matthew Gillman wa Chuo cha Tiba cha Harvard, “milo ya jioni ya familia huwa na vyakula vyenye afya zaidi kuliko vile ambavyo vingeliwa na watoto na wabalehe.” Watoto wanaokula pamoja na familia wanaelekea kula kiasi kinachopendekezwa cha matunda na mboga, ili kupata vitamini na madini wanayohitaji, na kupunguza kiasi cha sukari na mafuta wanayokula. Watafiti waligundua pia kwamba kula mlo wa jioni mkiwa familia husitawisha mazungumzo kuhusu vyakula vinavyofaa na huwafanya watoto wawe na mazoea mazuri ya kula—mazoea ambayo yatawafaa wanapokuwa mbali na nyumbani. Uchunguzi huo mpya, ulio sehemu ya mradi wa utafiti unaoendelea unaofanya majaribio kwa watoto wapatao 16,000 wenye umri wa kati ya miaka 9 na 14, uligundua kwamba “ni watoto wawili tu kati ya watoto watano wenye umri wa kwenda shuleni wanaokula mlo wa jioni pamoja na wazazi wao siku nyingi, na mtoto mmoja kati ya watano hali nao kamwe,” lasema gazeti the Globe.

Wafumaji Hodari

“Hariri ya buibui ni mojawapo ya vitu vigumu zaidi Duniani,” lasema gazeti New Scientist. Kila uzi waweza kurefuka mara mbili hadi mara nne ya urefu wake kabla ya kukatika na ni wenye nguvu sana hivi kwamba imesemekana kwamba uzi wenye unene wa penseli unaweza kusimamisha ndege aina ya jumbo jet ikipaa hewani. Wachunguzi wamekuwa wakitafuta kufahamu siri ya buibui ya kufuma ili itumiwe katika viwanda mbalimbali. Kwa mfano, fulana zisizoweza kupenywa na risasi hufumwa kwa Kevlar, ambacho ni kitambaa kilichotengenezwa katika maabara “kwa asidi nzito ya sulfuri iliyopashwa moto karibu kuchemka,” lasema gazeti hilo. Lakini ingawa kutengeneza uzi wa Kevlar hutokeza bidhaa zenye sumu na ambazo haziwezi kuharibiwa kwa urahisi baada ya kutumika, buibui hutengeneza uzi wa hariri kwa kutumia “protini na maji ya kawaida chini ya hali za asidi na halijoto sawa na zile za kinywa cha mwanadamu.” Isitoshe, mchanganyiko huu wa protini na maji hutokeza uzi unaostahimili mvua. Ndiposa, gazeti New Scientist lasema: “Licha ya uchunguzi wa miaka mingi, bado hariri ya buibui ni fumbo.”

Uchafuzi Nyumbani

“Hewa ya ndani ya nyumba yako yaelekea kuchafuliwa mara kumi zaidi ya hewa ya bustani lako,” lasema gazeti The Times la London. Uchunguzi uliofanywa kwenye nyumba 174 katika Uingereza na Kituo cha Utafiti wa Majengo ulionyesha kwamba kiasi cha mvuke wa fomaldehidi, kutoka kwa fanicha zenye mbao za vibanzi na kemikali nyingine ndani ya nyumba, kilikuwa mara kumi zaidi ya kilivyokuwa nje ya nyumba. Nyumba 12 zilizochunguzwa zilikuwa na hali mbaya ya hewa kulingana na viwango vya usafi wa hewa vinavyokubaliwa na Shirika la Afya Ulimwenguni. Fanicha ya sanisia, mikeka ya plastiki, vifaa vya ujenzi na vya kurembesha, sabuni zenye kemikali, au vifaa vya kupasha joto na vya kupikia vyaweza kutokeza kaboni monoksaidi, nitrojeni dioksidi, mvuke wa benzini, au michanganyiko mingine ya kaboni inayotokeza mvuke. Mvuke wa benzini, unaojulikana kwa kusababisha kansa, ulio katika sabuni ya maji na moshi wa sigareti, ni njia nyingine kuu ya uchafuzi wa ndani ya nyumba. Mhariri wa gazeti Health Which?, Charlotte Gann, asema kwamba watu wengi hutumia asilimia 80 hadi 90 ya wakati wao wakiwa ndani ya nyumba. Yeye ashauri kwamba “kupunguza kidogo matumizi ya bidhaa zenye kemikali, kufungua madirisha machache na kukagua vifaa vyenye kutumia gesi” kutaboresha usafi wa hewa ndani ya nyumba.