Liliokoa Maisha Yake
Liliokoa Maisha Yake
Toleo la “Amkeni!” la Desemba 22, 1999, lilikuwa na kichwa kikuu “Utekaji-Nyara—Sababu Ni Tisho la Tufeni Pote.” William Louis Terrell alisema kwamba toleo hilo la “Amkeni!” liliokoa maisha yake.
PUNDE tu baada ya kuwadia saa nne asubuhi siku ya Ijumaa Machi 10, 2000, Terrell alitekwa nyara kutoka nyumbani kwake na Joseph C. Palczynski, Jr. akiwa ameelekezewa bunduki. Makala hizo za Amkeni!, ambazo Terrell alisema kwamba alikuwa akizikumbuka alipokuwa ametekwa nyara, zilikuwa na mashauri yafuatayo kutoka kwa wataalamu kuhusu mambo ya kufanya utekwapo nyara:
“Uwe mwenye ushirikiano; epuka tabia ya kuwa mkaidi. Mateka wanaoonyesha uadui mara nyingi hutendwa kikatili, na wanakabili hatari kubwa zaidi ya kuuawa au kutengwa na wengine ili kuadhibiwa.
“Usihofu. Kumbuka kwamba wahasiriwa wengi huokoka utekaji-nyara.
“Piga gumzo ikiwezekana na jaribu kuanzisha mawasiliano. Ikiwa watekaji-nyara wanatambua sifa zako, hawataelekea kukudhuru au kukuua.
“Wajulishe [watekaji-nyara] mahitaji yako kwa njia ya upole.”
“Urafiki umekuwa ulinzi kwa mateka, kama ielezwavyo na kitabu Criminal Behavior: ‘Kadiri mhasiriwa na mtekaji wanavyojuana, ndivyo hupendana zaidi. Tukio hilo laonyesha kwamba baada ya muda fulani huenda mkosaji asimdhuru mateka.’”
William Terrell, mwenye umri wa miaka 53, na ambaye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alifuata mashauri hayo kadiri alivyoweza kwa muda wa karibu saa 14 alizokuwa ametekwa nyara, karibu muda huo wote alikuwa ameelekezewa bunduki. Kisa kilianza hapo Palczynski alipobisha mlango wa nyumba ya Terrell iliyoko eneo la mashambani karibu na ile inayoitwa Barabara Kuu ya 95, baada ya gari ambalo Palczynski alikuwa ameiba kuishiwa na petroli.
Baada ya mgeni huyo kuelezea shida yake, Terrell aliamua kumsaidia. Palczynski aliomba glasi ya maji kisha akaomba asafirishwe hadi
Baltimore, Maryland, Marekani. Terrell akamjibu kwamba angepanga mtu fulani ampeleke kwa gari hadi jiji la Fredericksburg, Virginia, ambako angeweza kupanda basi ambalo lingemfikisha alikokuwa akienda. Terrell alipomletea huyo mgeni glasi ya maji, alielekezewa bunduki. Palczynski akamwamuru Terrell ampeleke kwa gari alikotaka kwenda.Kufuata Mashauri
Wakati wa safari hiyo kwenye Barabara Kuu ya 95, Terrell alifuata amri ya Palczynski ya kumtaka aendeshe gari katika mwendo uleule na kuepuka kuvuta uangalifu wa watu wengine. Akiwa mwenye utulivu, Terrell alianza kuzungumza na Palczynski mwenye umri wa miaka 31, akionyesha kupendezwa naye kibinafsi na pia akataja hali zilizofanya wakutane. Palczynski alimweleza Terrell kwamba siku tatu zilizokuwa zimepita, alikuwa ameenda kumtembelea rafikiye msichana aliyeitwa Tracy, ambaye alikuwa amevunja uhusiano pamoja naye. Akiwa huko aliwapiga risasi na kuwaua marafiki wawili wa Tracy kutia ndani na jirani aliyejaribu kumzuia asimchukue Tracy. Baadaye Tracy aliponyoka.
Jioni iliyofuata, Palczynski alimpiga risasi mtoto mwenye umri wa miaka miwili na kuvunja kabisa taya yake, alipokuwa akijaribu kuteka nyara gari moja. Gari lililokuwa likiendeshwa na Jennifer Lyn McDonel lilipigwa risasi pia. Kwa kusikitisha, risasi moja ilimpata Jennifer na kumwua na nyingine ikalenga kiti kilichokuwa kitupu cha mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja. Jennifer na mumewe, Thomas, walikuwa wakielekea kwenye Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova, ambako wote wawili wangetoa hotuba walizogawiwa katika mkutano jioni hiyo. Mama ya Jennifer, Sarah Francis, alieleza hivi: “Huo ndio usiku pekee ambao hawakuandamana na mtoto wao kwenye Jumba la Ufalme. [La sivyo] tungeomboleza watu wawili.”
Terrell alipokuwa akiendeleza mazungumzo kwa upole pamoja na mtekaji wake, Palczynski alisema kwamba yeye kamwe hakuwa na nia ya kumdhuru yeyote na kwamba alimpenda sana Tracy na alitaka tu kuwa naye. Terrell alieleza: “Nilimwambia kwamba hangeweza kubadili mambo yaliyopita lakini angeweza kubadili ya wakati ujao, na nikamtia moyo ajisalimishe. Nilimweleza kwamba ningemtembelea gerezani na kujifunza Biblia pamoja naye.” Baadaye iliripotiwa kwamba tangu Palczynski amalize masomo ya sekondari katika mwaka wa 1987, amekuwa gerezani au katika hospitali za wagonjwa wa akili ama chini ya uangalizi muda wote wa maisha yake isipokuwa miezi kumi pekee.
Akitumia uzoefu wake wa miaka mingi akiwa mzee Mkristo, Terrell aliendelea kugusa moyo wa kijana huyo mwenye kuvurugika akili kwa kutumia mifano halisi kutoka kwa Biblia. Mathalani, alisimulia kisa cha mtu mwema, Mfalme Daudi wa Israeli, aliyetamani sana mke wa Uria, mmoja wa askari katika jeshi lake. Mwanamke huyo alipopata mimba, Daudi alipanga Uria auawe vitani. Daudi alipojulishwa kwa busara dhambi zake, yeye alitubu kutoka moyoni na kupata tena kibali cha Mungu.—2 Samweli 11:2–12:14.
Terrell alianzisha urafiki pamoja na mtoro huyo, akimwita kwa jina lake la utani Joby. Walipotua penye duka, Terrell alitumwa kununua chakula na televisheni ndogo, lakini Palczynski alimwonya kwamba angewaua watu wengine zaidi iwapo angetoa habari kwa yeyote. Akifahamu hali ya kuvurugika akili ya mtoro huyo, Terrell alitii. Hatimaye, baada ya kutazama uhalifu wa Palczynski kwenye taarifa ya habari ya saa 5:00, Palczynski alimkumbatia Terrell na kuondoka polepole na kutokomea kwenye mtaa mmoja huko Baltimore.
Juma moja baadaye, Palczynski alizingirwa na polisi katika nyumba moja alimokuwa amewazuilia mateka. Terrell, ambaye alikuwa ametajwa na huyo mtoro, aliitwa ili kusaidia katika majadiliano. Kwa kusikitisha, majadiliano hayo hayakufaulu na katika Machi 22, Palczynski alipigwa risasi na kuuawa na polisi waliposhambulia nyumba ile. Hakuna mwingine aliyejeruhiwa.
Baadaye Terrell alijipatia nakala 600 za toleo hilo la Amkeni! ambalo anasema liliokoa maisha yake. Amewapa mamia ya watu nakala za gazeti hilo. Terrell anashukuru kwamba yeye husoma habari muhimu katika Amkeni! kwa ukawaida, na tuna hakika kwamba hata wewe utafanya vivyo hivyo.
[Picha katika ukurasa wa 26]
William Terrell