Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matibabu Unayochagua

Matibabu Unayochagua

Matibabu Unayochagua

KATIKA kitabu chake kuhusu matibabu ya asili, Dakt. Isadore Rosenfeld alikazia jambo hili: “Matibabu yoyote au kitulizo chochote kinachotolewa kwa kikundi chochote kile cha watu walio na uhakika kwamba ‘yatafanya kazi’ yaweza kuboresha hali yao katika asilimia 50 ya visa.”

Hayo yaitwa matibabu ya kutuliza akili, yaani hata kidonge cha sukari chaweza kufanya kazi mradi tu mtu anaamini hivyo. Matibabu ya kutuliza akili yaweza kuponya matatizo ya kihisia, kama vile maumivu, kichefuchefu, uchovu, kizunguzungu, wasiwasi, na mshuko wa moyo. Jambo hilo hakika lafunua nini?

Kwanza, laonyesha kwamba kuwa na uhakika kwamba matibabu yoyote yale unayopokea yatafanya kazi, mara nyingi ni muhimu sana katika kupata nafuu. Wakati huohuo, yamkini ni jambo la hekima kuchunguza iwapo matibabu yoyote yale yanalenga kiini cha tatizo wala si dalili tu. Hilo laweza kufanywa kwa kuchunguza matokeo ya matibabu hayo kwa njia muafaka, kama vile majaribio katika maabara na picha za eksirei.

Lakini, bado kuna mengi awezayo mtu kufanya anapochagua matibabu fulani.

Hatua Muhimu Unazohitaji Kuchukua

Ni jambo la hekima kufanya utafiti kabla ya kufanya uamuzi. Uliza maswali. Matokeo ni nini? Ni nini faida, hasara, gharama na muda wa matibabu? Zungumza na watu waliopokea matibabu unayozingatia. Waulize ikiwa yaliwasaidia. Hata hivyo, kumbuka kwamba uthibitisho unaotegemea maoni ya watu tu unaweza kupotosha.

Matibabu ya asili huenda yasifae ikiwa yanamfanya mtu asusie matibabu yanayojulikana kuwa na matokeo, hata kama kiwango cha matokeo cha matibabu hayo yasiyo ya asili kiko chini. Uthibitisho wa madhara yanayoweza kutokea uliandikwa kwenye ripoti moja katika gazeti la The New England Journal of Medicine. Gazeti hilo lilieleza hali ya wagonjwa wawili wachanga wenye kansa ambao walikataa matibabu yasiyo ya asili huku wakitumia madawa mengine ya asili. Mgonjwa mmoja kati yao alikufa.

Watu wenye magonjwa ya kudumu au yaliyo hatari kwa uhai wapaswa kujihadhari kwa hekima kwa sababu wanaweza kutumbukia katika mtego wa walaghai ambao wanaeneza matibabu ya hila. Jihadhari na bidhaa zozote ambazo zasemekana kutibu magonjwa mbalimbali. Mfano wa hivi karibuni ulihusu vitamini mpya ambayo ilisemwa kuwa “ilisaidia kutibu kila tatizo kuanzia kwa matatizo ya kupumua na kudhoofika hadi magonjwa hatari kwa uhai.” Uchunguzi wa “vitamini” hiyo ulifunua kwamba yalikuwa maji ya chumvi tu.

Bila shaka matibabu fulani ya asili yanaweza kusaidia kudumisha afya bora. Hata hivyo, usitarajie muujiza. Ni jambo la hekima kuzingatia mno kula mlo wenye lishe, kulala vya kutosha, kufanya mazoezi ya kutosha, na kuwa mwangalifu unapochagua matibabu.

Tamaa Hiyo Yatimizwa

Bila shaka, hakuna matibabu yoyote ya wanadamu yanayoweza kukomesha magonjwa yote na kifo. Hiyo ni kwa sababu tumerithi matatizo hayo kutoka kwa mzazi wetu wa kwanza, mtu wa kwanza, Adamu. (Ayubu 14:4; Zaburi 51:5; Waroma 5:12) Matibabu mengi—ya kila aina—huenda yakasaidia, lakini ni vitulizo tu vya muda ambavyo vinaweza kuendeleza uhai na kuufanya ufurahishe kwa muda mfupi tu. Lakini kuna tiba hakika ya tatizo la afya mbaya, na mamilioni ya watu wameipata tayari.

Tiba hiyo imeandaliwa na Muumba wetu, Yehova Mungu, yule Daktari Mkuu. Kwa kudhihirisha imani kumwelekea na kutumia kwa faida thamani ya dhabihu ya fidia ya Mwanaye, Yesu Kristo, ambayo inafunika dhambi, utaweza kufurahia afya kamilifu na uhai udumuo milele katika ulimwengu usio na magonjwa! (Mathayo 20:28) Biblia huahidi kwamba katika ulimwengu huo mpya, “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.

[Blabu katika ukurasa wa 12]

Mamilioni wamepata tumaini hakika la pekee la afya kamilifu