Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mlima Ulipotaka Kuungana na Bahari

Mlima Ulipotaka Kuungana na Bahari

Mlima Ulipotaka Kuungana na Bahari

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA VENEZUELA

KATIKATI ya Caracas, mji mkuu wa Venezuela, na bahari kuna mlima mmoja wenye urefu wa meta 2,000 uitwao El Ávila. Upande wake wa kaskazini kuna kishoroba cha mwambao chenye kukaliwa na idadi kubwa ya watu. Hapo ndipo palipo na uwanja wa ndege ulio mkuu zaidi nchini Venezuela, na ili kwenda Caracas kutoka kwa uwanja huo, watalii hulazimika kusafiri kupitia barabara iliyochimbwa chini ya mlima huo.

Baada ya mvua ya mafuriko iliyonyesha mwezi wa Desemba mwaka uliopita, El Ávila ulishindwa kustahimili maji hayo mengi. Sehemu fulani za mlima ziliporomoshwa na maji yenye kutiririka kwa kasi. Kama mtu mmoja alivyosema, ilionekana kana kwamba mlima wote ulitaka kuungana na bahari. Makao—nyumba kubwa na ndogo—zote zilifunikwa na maji, matope, miamba, na miti. Vitanda, friji, televisheni, na hata watu fulani walifagiliwa mbali. Mwanamume mmoja mzee alisema kwamba alidhani mwisho wa ulimwengu ulikuwa umewadia.

Hatimaye, mvua ilikoma kunyesha na mafuriko yakaanza kupungua. Kulingana na kadirio fulani, huenda watu 50,000 walikufa, na watu wengine 400,000 wakaachwa bila makao. Kwa sababu hiyo, tukio hili limetajwa kuwa “msiba mbaya zaidi wa asili kuwahi kutokea katika historia yote ya Venezuela.”

Kuponea Chupuchupu

Mnamo Desemba 15, Juan Carlos Lorenzo na baba yake walikuwa wamenaswa katikati ya mito miwili iliyofurika. Waliacha gari lao na kujiunga na watu wengine 35 waliokuwa ndani ya nyumba moja. Hata hivyo, punde si punde, maji yalianza kuvuja na kuongezeka kwa haraka. Watu wote walipanda kwenye paa. Wakati huohuo, mawe makubwa na miti ilikuwa ikiipiga nyumba ile. Muda si muda, kuta za orofa ya kwanza na ya pili za nyumba hiyo zikaporomoka, zikasalia nguzo na paa tu. Nyumba hiyo isiyokuwa imara ilianza kuyumbayumba kutokana na kudundwa na yale mawe na miti.

Helikopta ilifika mahali pale, lakini haikuweza kutua kwenye paa hilo hafifu. Helikopta hiyo ilipokuwa ikitokomea, Juan Carlos na baba yake waliagana kwa machozi, kwa kuwa waliamini hawana budi kufa. Kisha helikopta mbili zikawasili. Kwa kumnyanyua mtu mmoja baada ya mwingine, watu wote waliokuwa kwenye paa waliokolewa, huku marubani wakiwa wanazizungusha-zungusha helikopta hizo juu ya paa kwa ustadi mwingi. Baada tu ya helikopta kuondoka, nyumba hiyo iliporomoka na kuzama ndani ya maji hayo yenye msukosuko. Waliponea chupuchupu!

Maelfu ya watu walihamishwa kutoka eneo hilo—kwa ndege ndogo, kwa magari, na kwa meli za kijeshi zenye uwezo wa kutia nanga karibu na ufuo wa bahari. Misafara mirefu ya watu—wengine wakiwa wamebeba watoto wadogo mabegani mwao—waliongozwa kwa kamba ndani ya maji ili kufikia meli. Ingawa watu wachache waliweza kuokoa vitu vyao vichache, wengi waliondoka bila kitu chochote ila nguo walizokuwa wamevalia.

Kutoa Msaada

Mipango ya kutoa msaada ilianzishwa mara tu habari ya msiba huo ilipofika kwenye ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova katika Venezuela. Hata hivyo, barabara zilikuwa zimezibwa na vifusi au kufagiliwa mbali na maji. Baada ya siku chache, upande mmoja wa barabara kuu ulifunguliwa ili utumiwe kwa mambo ya dharura, na magari ya Mashahidi yakiwa yamebeba madawa na wataalamu yaliruhusiwa kupita. Ofisa mmoja alisema hivi baadaye: “Serikali inafahamu wazi kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuleta msaada na kuwahamisha watu kutoka eneo hilo.”

Mashahidi waliunda vikundi vya kuwatafuta watu wenye kuhitaji msaada. Mipango ya kuwasafirisha walioathiriwa hadi Caracas ilifanywa, na wengi wao walifika huko bila kuwa na kitu chochote. Vituo vilisimamishwa kote katika mji ili kugawanya chakula, nguo, na dawa kwa watu waliokuwa na uhitaji. Lakini wengi wao hawakuhitaji tu chakula na nguo. Walihitaji sana makao. Ndugu zao Wakristo waliwakaribisha kwa furaha katika nyumba zao.

Hata muda mrefu baada ya msiba huo, watu bado walikuwa wakiishi pamoja na marafiki na watu wengine wa ukoo. Joel na Elsa, ni Mashahidi wanaoishi katika nyumba ndogo huko Puerto Cabello. Mwezi mmoja baada ya mvua hiyo kubwa, bado waliishi na watu wengine 16. Watu wengi walikuwa wamepoteza si makao yao tu bali pia kazi zao za kuajiriwa. Mahali pao pa kazi hapakuwapo tena.

Kwa kusikitisha, sehemu zilizokuwa zenye shughuli nyingi za kitalii na miji yenye bandari zilikuwa zimeharibiwa kabisa. Baadhi ya magari yalikuwa nusu udongoni, mengine yalikuwa yamerundikwa kwenye kuta, mengine kwenye vigingi na mengine yalikuwa yamebanwa kwenye milango na madirisha ya majengo. Tabaka ya matope yaliyokauka—sehemu nyingine zikiwa na kina cha meta tatu—yaliinua usawa wa barabara hivi kwamba mtu alipotembea juu yake angeona ndani ya nyumba za ghorofa au hata paa za nyumba!

Watu fulani katika Venezuela walisema kwamba msiba huo uliwafunza somo muhimu—wasitumaini vitu vya kimwili. (Luka 12:29-31) Wengi kati yao wakaja kuthamini shauri hili la Yesu Kristo: “Komeni kujiwekea akiba ya hazina duniani, ambako nondo na kutu hula kabisa, na ambako wezi huvunja na kuiba. Badala ya hivyo, jiwekeeni akiba ya hazina mbinguni, ambako wala nondo wala kutu haili kabisa, na ambako wezi hawavunji na kuiba. Kwa maana ilipo hazina yako, ndipo moyo wako utakapokuwa pia.”—Mathayo 6:19-21.

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

VENEZUELA

Caracas

Eneo lililokumbwa na msiba

KOLOMBIA

[Picha katika ukurasa wa 17]

Rubén Serrano, na mabaki ya nyumba yake

[Picha katika ukurasa wa 18]

1. Wajitoleaji walikusanya misaada katika Caracas

2, 3. Washiriki wa Kutaniko la Maiquetía waliondoa matope yaliyokauka yenye kina cha meta mbili kutoka katika Jumba lao la Ufalme

4. Mashahidi hawa walipoteza makao yao kisha wakajitolea kujijengea na kujengea wengine nyumba nyingine mpya

5. Mojawapo ya nyumba zinazokaribia kukamilika katika San Sebastián de los Reyes