Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Fungu Muhimu la Wauguzi

Fungu Muhimu la Wauguzi

Fungu Muhimu la Wauguzi

“Mwuguzi ni mtu ambaye hutia nguvu, hutia moyo, na hulinda—mtu ambaye yuko tayari kutunza wagonjwa, waliojeruhiwa, na wazee.”—Kichapo Nursing in Today’s World—Challenges, Issues, and Trends.

INGAWA hisani ni muhimu, haitoshi kumfanya mtu awe mwuguzi stadi. Wauguzi stadi pia huhitaji mazoezi yenye kina na uzoefu mwingi. Takwa moja la maana ni kuwa na masomo na uzoefu wa mwaka mmoja hadi minne au zaidi. Lakini ni sifa gani zinazomfanya mtu awe mwuguzi stadi? Yafuatayo ni baadhi ya majibu kutoka kwa wauguzi wenye uzoefu waliohojiwa na wachapishaji wa Amkeni!

“Daktari huponya, lakini mwuguzi hutunza mgonjwa. Mara nyingi hilo huhitaji kutia nguvu wagonjwa ambao wameumia kihisia-moyo na kimwili, kwa mfano, wakati wanapojulishwa kwamba wana ugonjwa wa kudumu au wako karibu kufa. Lazima uwe mama kwa mtu mgonjwa.”—Carmen Gilmartín, Hispania.

“Ni lazima uweze kuhisi maumivu na uchungu ambao mgonjwa anahisi na utake kusaidia. Fadhili na uvumilivu wahitajiwa. Lazima sikuzote utake kujifunza mengi juu ya uuguzi na mambo ya kitiba.”—Tadashi Hatano, Japani.

“Katika miaka ya karibuni, wauguzi wamehitaji ujuzi mwingi zaidi wa kitaaluma. Kwa hiyo, tamaa ya kujifunza na uwezo wa kuelewa yanayosomwa ni muhimu. Pia, wauguzi wanahitaji kuamua bila kukawia na kuchukua hatua haraka hali inapodai hivyo.”—Keiko Kawane, Japani.

“Ukiwa mwuguzi, lazima uonyeshe uchangamfu. Lazima uwe mvumilivu na uonyeshe huruma.”—Araceli García Padilla, Mexico.

“Mwuguzi bora lazima awe mwenye bidii ya kusoma, mwelekevu, na stadi kwelikweli. Ikiwa mwuguzi si mwenye kujitolea—ikiwa yeye si mwenye hisani au hapendi ushauri kutoka kwa wengine walio wa ngazi za juu kitiba—mwuguzi huyo hatafaa wagonjwa na wafanyakazi wenzake.”—Rosângela Santos, Brazili.

“Sifa kadhaa ni za lazima: kubadilika kulingana na hali, uvumilivu, na subira. Pia lazima uwe mwenye kukubali maoni ya wengine, ukiwa na uwezo wa kupatana na wafanyakazi wenzako na wale wa ngazi za juu kitiba. Lazima uwe mwepesi kupokea stadi mpya ili udumishe ustadi.”—Marc Koehler, Ufaransa.

“Lazima upende watu na utake kikweli kusaidia wengine. Lazima uweze kukabiliana na msongo kwa sababu katika kazi ya uuguzi, usipofanya kazi yako vizuri mambo yataharibika. Lazima uweze kubadilikana ili ufanye kazi hiyohiyo wakati mwingine ukiwa na wafanyakazi wenzako wachache—bila kuridhia ubora.”—Claudia Rijker-Baker, Uholanzi.

Mwuguzi Akiwa Mtunzaji

Kichapo Nursing in Today’s World chasema kwamba “uuguzi hushughulika na kutunza mtu katika hali mbalimbali zinazohusiana na afya. Hivyo basi, sisi huhusianisha mambo ya tiba na uponyaji wa mgonjwa na uuguzi na utunzaji wa mgonjwa huyo.”

Kwa hiyo, mwuguzi ni mtunzaji. Basi ni wazi kwamba, mwuguzi lazima ajali. Zamani kidogo, wauguzi waliohitimu wapatao 1,200 waliulizwa, “Ni jambo gani la maana zaidi kwako katika kazi yako ukiwa mwuguzi?” Kuandaa utunzaji bora ndilo lililokuwa jibu la asilimia 98.

Nyakati nyingine wauguzi hupunguza thamani yao kwa wagonjwa. Carmen Gilmartín, aliyenukuliwa hapo juu, mwuguzi mwenye uzoefu wa miaka 12, aliambia Amkeni! hivi: “Wakati mmoja nilimwambia rafiki yangu kwamba sikuhisi kuwa na sifa ya kutosha kutunza walio wagonjwa sana. Nilijiona kuwa mwenye kutoa msaada mdogo tu. Lakini rafiki yangu akanijibu: ‘Mwenye kutoa msaada mdogo tu’ anayethaminiwa sana, kwa kuwa mtu awapo mgonjwa, wewe ukiwa mwuguzi mwenye huruma ndiwe unayehitajiwa kuliko kitu kingine chochote.’”

Ni wazi kwamba, kutoa utunzaji huo kwaweza kuleta mkazo mwingi sana kwa mwuguzi ambaye hufanya kazi kwa muda wa saa kumi au zaidi kila siku! Ni nini kilichowachochea watunzaji hawa wenye roho ya kujitolea wawe wauguzi?

Kwa Nini Uwe Mwuguzi?

Wachapishaji wa gazeti la Amkeni! walihoji wauguzi kote ulimwenguni na kuwauliza, “Ni nini kilichokuchochea uwe mwuguzi?” Yafuatayo ndiyo baadhi ya majibu yao.

Terry Weatherson ana uzoefu wa miaka 47 ya uuguzi. Sasa yeye ni mwuguzi wa mambo ya afya na mtaalamu katika Idara ya Urolojia ya hospitali moja huko Manchester, Uingereza. “Nililelewa katika Ukatoliki nami nilihudhuria shule ya bweni ya Katoliki,” asema. “Nikiwa msichana, niliamua nataka kuwa mtawa wa kike au mwuguzi. Nilitamani kusaidia wengine. Huenda ukauita wito. Kama uonavyo, nilichagua uuguzi.”

Chiwa Matsunaga kutoka Saitama, Japani, amekuwa na kliniki yake kwa miaka minane. Asema hivi: “Nilifuata maoni ya baba yangu kwamba ‘ni vema kujifunza ustadi utakaokuwezesha kupata kazi katika maisha yako yote.’ Ndipo nikachagua kazi ya uuguzi.”

Etsuko Kotani kutoka Tokyo, Japani, mwuguzi mkuu mwenye uzoefu wa miaka 38 ya uuguzi, alisema: “Nilipokuwa shuleni, baba yangu alizirai na kupoteza damu nyingi. Nilipokuwa nikimtunza baba yangu hospitalini, niliamua kwamba nataka kuwa mwuguzi ili niweze kusaidia watu wagonjwa wakati ujao.”

Wengine walichochewa na hali yao wenyewe walipokuwa wagonjwa. Eneida Vieyra, mwuguzi huko Mexico, asema hivi: “Nilipokuwa na umri wa miaka sita, nililazwa hospitalini kwa majuma mawili kwa ugonjwa wa mkamba, tangu wakati huo niliamua nataka kuwa mwuguzi.”

Ni dhahiri, kuwa mwuguzi hutaka kujitolea zaidi. Acheni tuchunguze kwa ukaribu zaidi magumu na thawabu za utaalamu huu wenye kutokeza.

Shangwe za Kuwa Mwuguzi

Ni nini zilizo shangwe za uuguzi? Jibu la swali hilo lategemea utaalamu wa mtu katika uuguzi. Kwa mfano, wakunga huhisi wamethawabishwa kila wanapozalisha bila matatizo. “Ni jambo zuri ajabu kuzalisha mtoto mwenye afya ambaye umeangalia ukuzi wake,” asema mkunga mmoja kutoka Uholanzi. Jolanda Gielen-Van Hooft, pia kutoka Uholanzi, asema hivi: “Kuzalisha ni mojawapo ya mambo mazuri ambayo wenzi—na mfanyakazi wa kitiba—aweza kufurahia. Ni mwujiza!”

Rachid Assam kutoka Dreux, Ufaransa, ni mwuguzi wa Serikali aliyehitimu, mtaalamu wa usukaputi mwenye umri wa miaka 40 hivi. Kwa nini yeye hufurahia uuguzi? Kwa sababu ya “uradhi wa kuchangia kwenye mafanikio ya upasuaji na kuwa mshiriki wa kazi ambayo inasisimua na sikuzote inasonga mbele,” asema. Isaac Bangili, pia kutoka Ufaransa, alisema: “Mimi hufurahia shukrani nyingi tupokeazo kutoka kwa wagonjwa na familia zao, hasa katika hali za dharura tunapofaulu kuponyesha mgonjwa ambaye tulifikiria kwamba hangepona.”

Wakati mmoja Terry Weatherson aliyetajwa mapema, alipokea shukrani kama hizo. Mjane mmoja alimwandikia hivi: “Muda hauwezi kupita kabla sijataja tena faraja tuliyopata kutokana na utulivu wako wakati wote wa ugonjwa wa Charles. Uchangamfu wako uliondoa huzuni yetu, nao ulikuwa tegemezo ambalo katika hilo tulipata kuimarishwa.”

Kukabili Magumu

Lakini pamoja na shangwe za uuguzi huja magumu mengi. Makosa hayaruhusiwi! Iwe ni kumpa mgonjwa dawa au kutoa damu au kuingiza chombo cha kupitishia maji mwilini au hata kumsogeza mgonjwa tu, lazima mwuguzi awe mwangalifu kabisa. Hapaswi kufanya makosa, hasa katika nchi ambazo unaweza kushtakiwa kisheria. Lakini nyakati nyingine mwuguzi hujikuta katika hali ngumu. Kwa mfano, tuseme mwuguzi anahisi kwamba daktari amemwandikia mgonjwa dawa isiyofaa au ametoa amri ambazo hazitamfaa mgonjwa, mwuguzi anaweza kufanya nini? Je, ashindane na daktari? Jambo hilo lahitaji moyo mkuu, busara, na hekima—nalo huhitaji kujasiria. Kwa kusikitisha, madaktari fulani huwa si wepesi kukubali madokezo ya wale wanaowaona kuwa chini yao.

Wauguzi fulani wamegundua nini kuhusu jambo hilo? Barbara Reineke kutoka Wisconsin, Marekani, mwuguzi aliyesajiliwa na kufanya kazi kwa miaka 34, aliambia Amkeni!: “Lazima mwuguzi awe na moyo mkuu. Kwanza kabisa, ana wajibu kisheria kwa dawa zozote au tiba anayotoa na madhara yoyote yanayosababishwa nazo. Lazima aweze kukataa kutekeleza amri fulani kutoka kwa daktari ikiwa anahisi inakiuka kiwango chake cha kazi aliyofunzwa au kama anaamini kwamba amri hiyo si sahihi. Uuguzi si kama ulivyokuwa siku za Florence Nightingale au hata miaka 50 iliyopita. Wakati huu mwuguzi anahitaji kutambua wakati wa kukataa maagizo ya daktari na wakati wa kumsisitizia daktari amwone mgonjwa hata kama ni usiku wa manane. Na ikiwa umekosea, basi lazima usiwe mwepesi sana kukasirika daktari akikudhihaki.”

Tatizo jingine ambalo wauguzi wanalazimika kukabili ni jeuri kazini. Ripoti moja kutoka Afrika Kusini yasema kwamba wauguzi “wako katika hatari ya juu sana ya kutendwa vibaya na kwa ukali sana kazini. Hata, yaelekea wauguzi wanashambuliwa sana kazini kuliko walinzi wa gereza au maofisa wa polisi na asilimia 72 ya wauguzi hawahisi wakiwa salama.” Hali kama hiyo yaripotiwa huko Uingereza ambapo asilimia 97 ya wauguzi katika uchunguzi wa karibuni walijua mwuguzi ambaye alikuwa ameshambuliwa mwaka uliopita. Ni nini ambacho husababisha jeuri hiyo? Mara nyingi, tatizo huja kutoka kwa wagonjwa ambao hutumia dawa za kulevya au wamekuwa wakitumia kileo au wako na mkazo mwingi au walioathiriwa na huzuni.

Pia wauguzi lazima wakabiliane na uchovu wa kimwili unaosababishwa na mkazo wa akili. Upungufu wa wafanyakazi ni mojawapo ya sababu hizo. Mwuguzi mwenye kujali anapokosa kumpa mgonjwa utunzi wa kutosha kwa sababu ya kazi nyingi, mkazo wa akili huongezeka. Kujaribu kukabiliana na hali hiyo kwa kuepuka vipindi vya pumziko na kufanya kazi saa za ziada hufanya tatizo hilo kuwa mbaya zaidi.

Ulimwenguni pote hospitali nyingi hazina wafanyakazi wa kutosha. “Hatuna wauguzi katika hospitali zetu,” ndivyo inavyosema ripoti katika gazeti Mundo Sanitario la Madrid. “Mtu yeyote aliyehitaji utunzaji wa kitiba anatambua umuhimu wa wauguzi.” Ni sababu gani iliyotolewa ya upungufu huu? Uhitaji wa kuokoa pesa! Ripoti hiyohiyo ilisema kwamba hospitali za Madrid zilikuwa na upungufu wa wauguzi 13,000!

Jambo jingine linalosababisha mkazo wa akili ni kwamba vipindi vya kuwa kazini ni virefu na mshahara ni kidogo. Kichapo The Scotsman kilisema: “Zaidi ya mmoja kati ya wauguzi wa Uingereza watano na robo ya wasaidizi wa wauguzi wana kazi nyingine ya pili ili kuwasaidia kupata riziki, kulingana na muungano wa utumishi wa umma, Unison.” Wauguzi 3 kati ya 4 wanahisi kwamba hawalipwi vizuri. Tokeo likiwa kwamba, wengi wamefikiria kujiuzulu.

Kuna mambo mengine kadhaa yanayochangia mkazo wa akili wa wauguzi. Tukikata kauli kutokana na maelezo ambayo Amkeni! lilipata kutoka kwa wauguzi ulimwenguni pote, kifo cha wagonjwa chaweza kuwashusha moyo sana. Magda Souang, aliyelelewa Misri, hufanya kazi Brooklyn, New York. Alipoulizwa ni nini kilichofanya kazi yake iwe ngumu, alijibu hivi: “Kushuhudia wagonjwa wapatao 30 wenye ugonjwa usio na tiba ambao nilikuwa nimewauguza kwa miaka kumi, wakifa. Hilo huchosha.” Si ajabu kichapo kimoja kilisema hivi: “Kuendelea kutumia jitihada zako na hisia-moyo zako kutunza wagonjwa wanaokufa kwaweza kuumiza hali ya mtu ya afya na kihisia-moyo.”

Wakati Ujao wa Wauguzi

Ukuzi na uvutano wa tekinolojia huongeza mkazo katika kazi ya uuguzi. Ugumu uliopo ni kupatanisha tekinolojia na ubinadamu, njia ya kibinadamu ya kushughulika na wagonjwa. Hakuna mashine inayoweza kuchukua mahali pa ufundi na huruma ya mwuguzi.

Jarida moja lasema hivi: “Uuguzi ni utaalamu wa milele. . . . Maadamu binadamu yupo, sikuzote kutakuwa na uhitaji wa utunzaji, huruma, na uelewevu.” Uuguzi hutimiza uhitaji huo. Lakini kuna sababu kubwa hata zaidi ya kuwa na mtazamo wenye tumaini kuhusu mambo ya kiafya. Biblia huonyesha kwamba wakati utakuja ambapo hakuna mtu atakayesema, “Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24) Madaktari, wauguzi, na hospitali hazitahitajiwa katika ulimwengu mpya ambao Mungu ameahidi.—Isaya 65:17; 2 Petro 3:13.

Pia Biblia huahidi kwamba “Mungu . . . atafuta kabisa kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala ombolezo wala kupaaza kilio wala umivu halitakuwapo tena kamwe. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.” (Ufunuo 21:3, 4) Hata hivyo, kwa wakati huu, twapaswa kushukuru kwa utunzi wote na kujitolea ambako mamilioni ya wauguzi ulimwenguni pote wanafanya, ambapo bila wao, kukaa hospitalini kungechukiza! Basi swali hili lafaa kama nini, “Wauguzi—Tungefanyaje Bila Wao?”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

Florence Nightingale —Mtangulizi wa Uuguzi wa Kisasa

Florence Nightingale alizaliwa mwaka 1820 huko Italia na wazazi Waingereza matajiri, naye alidekezwa sana. Kijana Florence alikataa kuolewa naye akafuatia masomo yanayohusu afya na utunzaji wa watu maskini. Ujapokuwa upinzani wa wazazi wake, Florence aliajiriwa kazi katika shule moja ya kufunza wauguzi huko Kaiserswerth, Ujerumani. Baadaye, alisomea Paris, na akiwa na umri wa miaka 33, akawa mkurugenzi wa hospitali ya wanawake huko London.

Lakini alikabili ushindani mkubwa zaidi alipojitolea kutunza askari waliojeruhiwa katika Krimea. Akiwa huko, yeye na kikundi chake cha wauguzi 38 walilazimika kusafisha hospitali iliyokuwa imejaa panya. Kazi hiyo ilikuwa ngumu sana, kwa kuwa mwanzoni, hakukuwa na sabuni, beseni za kuoshea, wala taulo, na vitanda vya kutosha, hakukuwa na magodoro, wala bendeji. Florence na kikundi chake walijitahidi kupambana na ugumu huo, na kufikia mwisho wa vita, alikuwa amefanya mabadiliko makubwa ulimwenguni katika uuguzi na usimamizi wa hospitali. Mwaka wa 1860, alianzisha Shule ya Uuguzi ya Nightingale kwenye St. Thomas’ Hospital huko London—shule ya kwanza ya uuguzi isiyoshirikishwa na dini. Kabla ya kifo chake mwaka wa 1910, alikuwa mgonjwa kitandani kwa miaka mingi. Hata hivyo, aliendelea kuandika vitabu na vijitabu katika jitihada za kuboresha viwango vya utunzaji wa afya.

Watu fulani hupinga sifa ya kipekee anayopewa Florence Nightingale wakisema kwamba wengine walistahili sifa nyingi pia kwa yale waliyotimiza katika kazi ya uuguzi. Kwa kuongezea, sifa yake imebishaniwa sana. Kulingana na kitabu A History of Nursing, wengine hudai kwamba alikuwa “mwepesi wa kubadili tabia, mkandamizaji, mwenye kushikilia kauli yake, mwenye hamaki, na mwenye kutawala,” ilhali wengine walivutiwa na “akili nyingi na uvutio wake, uwezo wake wenye kushangaza, na sifa tofauti-tofauti za utu wake.” Hata awe alikuwa na utu wa aina gani, jambo moja ni la hakika: Mbinu zake katika uuguzi na usimamizi wa hospitali zilienea katika nchi nyingi. Anajulikana kuwa mtangulizi wa utaalamu wa uuguzi kama tuujuavyo leo.

[Picha]

Hospitali ya St. Thomas’ baada ya kuanzishwa kwa Shule ya Uuguzi ya Nightingale

[Hisani]

Courtesy National Library of Medicine

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Sifa za Ustahili za Uuguzi

Mwuguzi: “Ni mtu ambaye hasa amejifunza mambo ya msingi ya sayansi ya uuguzi na ambaye hutimiza viwango kadhaa vilivyowekwa vya kielimu na vya ustadi wa kitiba.”

Mwuguzi aliyesajiliwa: “Ni mwuguzi aliyehitimu ambaye ameidhinishwa kisheria (aliyesajiliwa) kufanya kazi baada ya mtihani uliotolewa na baraza la serikali la wafunzi wa uuguzi . . . na ameidhinishwa kisheria kutumia cheo cha uteuzi cha Mwuguzi Aliyesajiliwa.”

Mwuguzi mtaalamu wa afya: “Ni mwuguzi aliye na ujuzi wa hali ya juu, ufundi, na ana kiwango cha kutosha katika ustadi hususa wa uuguzi.”

Mwuguzi-mkunga: “Ni mtu aliyeelimishwa katika sehemu mbili, ya uuguzi na ya ukunga.”

Mwuguzi asiye na leseni: “Ni mtu ambaye amekuwa na uzoefu katika kuuguza wagonjwa lakini si mhitimu wa aina yoyote ya shule ya uuguzi.”

Mwuguzi aliye na leseni: “Ni mhitimu wa shule ya uuguzi . . . ambaye ameidhinishwa kisheria afanye kazi akiwa mwuguzi aliye na leseni au wa kitaaluma.”

[Hisani]

Kutoka katika kichapo cha Marekani, Dorland’s Illustrated Medical Dictionary

UN/J. Isaac

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

‘Msingi wa Utunzi wa Kitiba’

Kwenye Mkutano wa kuadhimisha miaka 100 ya kuwepo kwa Baraza la Wauguzi Ulimwenguni, Juni 1999, Dakt. Gro Harlem Brundtland, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, alisema:

“Wauguzi wakiwa wataalamu wakuu wa afya, wako katika hali ya pekee ya kutetea kuwe na sayari yenye afya. . . . Kwa kuwa wauguzi na wakunga tayari wanajumuisha asilimia 80 ya wafanyakazi wa afya wenye ustahili katika mifumo mingi ya afya ya kitaifa, wanawakilisha wafanyakazi wenye uwezo wa kufanya mabadiliko ya lazima ili kutimiza mahitaji ya Afya kwa Wote katika karne ya 21. Kwa kweli, kazi yao katika utumishi wa afya hushughulikia utunzi wote wa mambo ya afya . . . Ni wazi kwamba wauguzi ndio msingi wa vikundi vingi vya utunzi wa mambo ya afya.”

Rais wa Mexico, Ernesto Zedillo Ponce de León, aliwasifu sana wauguzi wa Mexico katika hotuba yake aliposema: “Siku baada ya siku nyinyi nyote . . . hutoa ujuzi wenu wote, umoja wenu, utumishi wenu katika kulinda na kurudisha afya ya Wamexico. Siku baada ya siku nyinyi huwapa watu, si msaada wenu wa kitaalamu tu bali pia faraja inayotokana na tabia yenu yenye fadhili, na ya ubinadamu. . . . Nyinyi ni sehemu kubwa mno ya mashirika yetu ya afya . . . Wauguzi wetu wanahusika katika kila uhai unaookolewa, kila mtoto anayechanjwa, kila msaada wa uzalishaji unaotolewa, kila mazungumzo ya afya, kila uponyaji, kila mgonjwa anayepokea utunzi na tegemezo.”

[Hisani]

UN/DPI Photo by Greg Kinch

UN/DPI Photo by Evan Schneider

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 11]

Daktari Mwenye Kuthamini

Dakt. Sandeep Jauhar wa Hospitali ya Presibitari ya New York alikiri udeni wake kwa wauguzi stadi. Mwuguzi alimsadikisha kwa busara kwamba mgonjwa aliyeelekea kufa alihitaji afyuni. Daktari huyo aliandika hivi “Wauguzi wazuri hufundisha madaktari pia. Wauguzi walio katika wodi maalumu kama zile za kutunzia wagonjwa mahututi ni baadhi ya wataalamu waliozoezwa vizuri zaidi hospitalini. Nilipokuwa daktari mkufunzi, walinifundisha jinsi ya kuingiza katheta (neli ya kuingizia uoevu katika mishipa ya mwilini) na kurekebisha vyombo vya kupitishia hewa. Waliniambia ni dawa zipi za kuepukwa.”

Yeye aendelea kusema: “Wauguzi huandaa tegemezo muhimu la kisaikolojia na kihisia-moyo kwa wagonjwa, kwa sababu wao ndio hutumia wakati mwingi zaidi nao. . . . Mwuguzi nimtumainiye aniambiapo kwamba ni lazima nimwone mgonjwa fulani, mimi hufanya hivyo haraka sana.”

[Picha katika ukurasa wa 7]

“Nilitamani kusaidia wengine.”—Terry Weatherson, Uingereza.

[Picha katika ukurasa wa 7]

“Nilipokuwa nikimtunza baba yangu hospitalini, niliamua kwamba nataka kuwa mwuguzi.”—Etsuko Kotani, Japani.

[Picha katika ukurasa wa 7]

‘Kumzalisha mama ni mojawapo ya mambo mazuri sana awezayo kufanya mkunga.’—Jolanda Gielen-Van Hooft, Uholanzi.

[Picha katika ukurasa wa 8]

Wakunga hupata shangwe na uradhi wanaposaidia kuzalisha