Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Karibu Kwenye Korongo la Shaba

Karibu Kwenye Korongo la Shaba

Karibu Kwenye Korongo la Shaba

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA MEXICO

KORONGO la Shaba ni ajabu ya asili iliyo katika safu ya milima iliyo kaskazini mwa Mexico inayoitwa Sierra Madre Occidental, nalo lina eneo la takriban kilometa 50,000 za mraba, eneo linalolingana na lile la nchi ya Kosta Rika.

Lakini jina lake si sahihi kabisa. Korongo la Shaba si korongo moja bali ni mfumo wa makorongo 20 yaliyoungana. Mojawapo ya makorongo hayo ni Korongo la Shaba, jina linalotumiwa kwa mfumo wote. Kulingana na mvumbuzi Richard Fisher, angalau makorongo matatu kati yake yana kina zaidi ya lile Korongo Kuu nchini Marekani. *

Kwa sababu ya ukubwa wa kupindukia wa Korongo la Shaba, watalii wengi huweza kufika sehemu chache tu kati ya sehemu zake nyingi za kiasili za kutazamia mandhari. Mandhari zinazovutia zaidi huelekeana na korongo la Shaba, Sinforosa, na Urique. Hata hivyo, baadhi ya watu huhisi kwamba mandhari zenye kustaajabisha zaidi huweza kuonwa kutoka sehemu ya kuangalilia mandhari ya Divisadero, ambapo waweza kuona mandhari ya muungano wa korongo la Shaba, Urique, na Tararecua.

Tabia Mbalimbali ya Nchi

Kubadilika ghafula kwa mwinuko huathiri tabia ya nchi na mimea katika Korongo la Shaba. Miguel Gleason alithibitisha jambo hilo binafsi wakati yeye na kikundi fulani walipoteremka kwenye Korongo la Urique. Aandika hivi katika gazeti la México Desconocido: “Tulianza kuhisi joto, na misitu ya misonobari ikatokomea, tukaanza kuona mimea ya kitropiki na ndizi, parachichi, na hata machungwa. Hatukuweza kuamini. Naweza kusema tu kwamba sijawahi tena kamwe maishani mwangu kuvuka kutoka kwa msitu wenye baridi hadi kwa eneo lenye joto la kitropiki kwa muda na mwendo mfupi hivyo.”

Nyanda za juu za makorongo hayo zimefunikwa na aina 15 za misonobari na aina 25 za mialoni. Pia kuna mipopla na mireteni kwenye Korongo la Shaba. Katika majira ya kiangazi, maua mengi mbalimbali hunawiri kwenye safu hiyo yote ya milima, baadhi yake hutumiwa kama chakula au mitishamba na wenyeji, ambao huitwa Watarahumara. Kwenye miinuko ya zaidi ya meta 1,800 juu ya usawa wa bahari, tabia ya nchi ya milima hiyo hubadilikabadilika kutoka halijoto ya wastani hadi baridi karibu mwaka wote. Kunakuwa na rasharasha na hata theluji mara kwa mara katika majira ya baridi kali.

Wageni wanapoteremka, huanza kuona miti mbalimbali na dungusi-kakati. Bondeni kuna tabia ya nchi ya kitropiki yenye majira ya baridi yenye kupendeza yaliyo na halijoto ya wastani ya nyuzi Selsiasi 17. Kwa upande mwingine majira ya kiangazi yaweza kuwa na joto kali mno, wakati halijoto inapobadilika kuanzia kwa nyuzi Selsiasi 35 hadi nyuzi Selsiasi 45, mvua tele hunyesha pia na kufanya mito ifurike.

Umaridadi wa eneo hilo huzidishwa na maporomoko mawili makubwa ya maji. Poromoko la Piedra Volada, mojawapo ya maporomoko marefu zaidi ulimwenguni, lina kimo cha meta 453, na Basaseachic lina kimo cha meta 246.

Kimbilio la Wanyama wa Pori

Wanyama wengi wa pori huishi katika Korongo la Shaba. Yasemekana kwamba asilimia 30 ya wanyama walio Mexico wanaishi katika eneo hilo. Hao watia ndani dubu mweusi, puma, fisi-maji, paa aina ya sprocket, mbwa mwitu wa Mexico, nguruwe-mwitu, paka-shume, raccoon, melesi, kicheche mwenye milia na vilevile popo, kuchakuro, na sungura.

Aina 400 za ndege wanaishi katika Korongo la Shaba, kutia ndani tai na kipanga aina ya peregrine. Korongo hizo ziko mahali muafaka kati ya Amerika ya Kaskazini na ya Kati, kwa hiyo ndege wanaohama huja hapa ili kuepuka majira ya baridi kali. Wengine hutua tu kwa muda kwa mapumziko kabla ya kuendelea na safari yao.

Bila shaka Korongo la Shaba humletea sifa Muumba wa maajabu yote ya asili, Yehova Mungu. Ni kama alivyosema Mfalme Daudi wakati mmoja, “Ee, BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako.”—1 Mambo ya Nyakati 29:11.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Korongo la Urique hufikia kina cha meta 1,879; Korongo la Sinforosa, meta 1,830; na Korongo la Batopilas, meta 1,800. Korongo Kuu lina kina cha takriban meta 1,617.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

Kutazama Mandhari Kutoka Kwenye Garimoshi

Reli ya Pasifiki-Chihuahua hufika umbali wa kilometa 941 kutoka Ojinaga kwenye mpaka wa Mexico na Marekani hadi bandari ya Topolobampo katika Bahari ya Pasifiki—na hivyo huvuka Korongo la Shaba. Kwa sababu ya mandhari ya eneo hilo, reli hiyo huonwa kuwa kazi bora sana ya uhandisi. Garimoshi linaposafiri kwenye reli hiyo huvuka daraja kubwa 37, daraja ndefu zaidi yenye urefu wa meta 500 huvuka Mto Fuerte. Daraja iliyo juu zaidi hufikia kimo cha meta 90 juu ya Mto Chínipas.

Garimoshi hilo hupitia pia kwenye njia 99 za ardhini. Njia ya ardhini iliyo ndefu zaidi huitwa El Descanso na ina urefu wa meta 1,810. Watalii huweza kufurahia mandhari yenye kuvutia ya Korongo la Shaba wanaposafiri kwa garimoshi.

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MAREKANI

MEXICO

CHIHUAHUA

Ojinaga

Chihuahua

ENEO LA KORONGO LA SHABA

La Junta

Creel

Divisadero

Topolobampo

[Picha katika ukurasa wa 15]

Poromoko la maji la Basaseachic

[Hisani]

© Tom Till

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mandhari kutoka Divisadero

[Hisani]

© Tom Till

[Picha katika ukurasa wa 17]

Watarahumara huishi kote katika korongo hilo

[Hisani]

George Hunter/ H. Armstrong Roberts

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ziwa Arareko

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

George Hunter/H. Armstrong Roberts