Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuzuru Duka la Dawa za Kichina

Kuzuru Duka la Dawa za Kichina

Kuzuru Duka la Dawa za Kichina

KWOK KIT amekuwa mgonjwa kwa siku kadhaa, na ameamua kumwona daktari. Kwa kuwa yeye ni Mchina, anapendelea daktari wa dawa za mitishamba ya Kichina. Rafiki mmoja wa familia anamjua daktari fulani aliye na duka la dawa za mitishamba karibu na hapo. Yule rafiki anamwambia Kwok Kit kwamba huyo daktari atamchanganyia mitishamba fulani ambayo itamtibu.

Kama ilivyo katika nchi nyingine za Kusini-Mashariki mwa Asia, kumtembelea daktari katika China ni tofauti na nchi za Magharibi. Katika nchi za Magharibi kutembelea daktari huanza kwa kupanga naye siku na wakati wa kuonana, kwenda ofisini mwake, kupimwa, na kupewa agizo la dawa. Kisha lazima mgonjwa aende kwenye duka la dawa na kununua dawa alizoagizwa. Daktari wa Kichina hana mambo mengi. Unapotembelea duka la mitishamba utampata mtaalamu wa mitishamba ambaye pia ni daktari wa mitishamba ya Kichina. Anaweza kukupima, kutambua ugonjwa wako, kukupa kiasi cha dawa unachohitaji, na kukueleza jinsi utakavyoitumia—atafanya yote hayo katika ziara yako ya muda mfupi! *

Je, Mitishamba Ni Dawa?

Ingawa watu wengi wa nchi za Magharibi wamezoea dawa za tembe, vidonge, na sindano, dawa hizo zimetokea hivi karibuni tu. Kwa maelfu ya miaka, watu wametegemea njia za asili kutibu magonjwa yao. Kwa mfano, madaktari wa Kiyahudi katika nyakati za Biblia walitumia vitu kama mafuta, manukato, na divai kuwa dawa. (Isaya 1:6; Yeremia 46:11; Luka 10:34) Tini kavu zilizochemshwa zilitumiwa kutibu majipu.—2 Wafalme 20:7.

Kwa kweli, watu wa nchi zote au vikundi vya watu wametumia mitishamba na michanganyo mingine kutibu maradhi pindi moja. Hata viungo mbalimbali vinavyotumiwa katika mapishi vilitumika mwanzoni kama dawa. Hilo halimaanishi kwamba matumizi hayo yalikuwa na mafanikio siku zote. Tofauti na hilo, mara nyingi ushirikina na kutojua kulihusika. Hata hivyo, njia hizo zimetumika kutibu wagonjwa kwa maelfu mengi ya miaka. Hata baadhi ya dawa za kisasa zimetokana na mimea.

Dhana na Tiba ya Kichina

Kutibu maradhi kwa kutumia mitishamba ni sehemu muhimu ya historia ya China. Mapokeo hutaja kwamba Huang Di, yule Mtawala wa Manjano, ndiye aliyebuni Nei Jing, kile kitabu cha dawa za kutibu maradhi yasiyohitaji upasuaji, ambacho kingali kinatumiwa na madaktari wa China. * Kitabu hicho, ambacho tarehe yake ya kuandikwa yabishaniwa, kina mambo yenye kufanana na yale ambayo yangejadiliwa katika kitabu cha tiba kutoka Magharibi. Hakijadili tu jinsi ya kutambua maradhi, dalili, visababishi vya maradhi, dawa inayohitajika, na kuzuia maradhi bali pia kina habari kuhusu mwili na viungo vyake na utendaji wa mwili.

Elimu na utendaji wa tiba ya Kichina umeathiriwa sana na dhana ya yin-yang, kama usanii mwingine wowote wa Kusini-Mashariki mwa Asia. Katika tiba hiyo, yin huwakilisha baridi na yang huwakilisha joto—semi hizo mbili pia huwakilisha mambo mengine yenye kutofautiana. * Zaidi ya hayo, sehemu za mwili zenye kuhusianishwa na tiba ya vitobo, hutumiwa wakati wa kupima na kutibu ugonjwa. Mitishamba na vyakula vikiwa baridi au moto hupewa mgonjwa ili kusawazisha yin-yang katika mwili wake.

Kwa mfano, mtu anayeugua homa aonwa kuwa mwenye joto, na hivyo mitishamba yenye kudhaniwa kuwa na uwezo wa kutia baridi hupewa mgonjwa huyo. Ingawa huenda yin-yang isitajwe waziwazi, kanuni yake bado hutumiwa kuamua njia ya kumtibu mgonjwa. Lakini daktari wa Kichina hutambuaje aina ya ugonjwa? Na duka la mitishamba likoje? Ili kupata majibu ya maswali hayo, mbona tusiandamane na Kwok Kit atembeleapo duka alilopendekezewa na rafikiye?

Duka la Kipekee la Mitishamba

Ajabu iliyoje! Leo itambidi Kwok Kit kusubiri kabla ya kumwona daktari. Yaonekana kuna mweneo wa mafua, na wagonjwa wawili wamemtangulia Kwok Kit. Acheni tuchunguze duka hili tunaposubiri.

Tulipokuwa tukiingia tuliona kwanza marundo ya vitu vikavu—uyoga, kombe, chaza, tini, kokwa, na vyakula vingine—vikiwa ndani ya mapipa yasiyo na vifuniko yaliyo karibu na mlango. Naam, hata vyakula vyapatikana hapa. Hata hivyo, huenda vingine ni baadhi ya dawa.

Mbele zaidi, twaona kaunta za glasi zenye vitu zikiwa pande zote mbili za duka hili jembamba. Ndani ya kaunta hizo mna mitishamba adimu au ya kipekee, madini, na viungo vilivyokaushwa vya wanyama, vyenye bei ghali sana. Tutazamapo kwa uangalifu zaidi, twaona pembe za kulungu, lulu, mijusi na farasi-maji waliokaushwa, na vitu vingine vya kipekee. Hadi miaka ya hivi karibuni, pembe za kifaru, nyongo ya dubu, na viungo vingine vya wanyama kama hivyo vilionyeshwa kwenye kaunta hizi za glasi, lakini kuwa na viungo hivyo kumepigwa marufuku.

Katika sehemu nyingine ya duka, tunapata vifurushi vyenye michanganyo ya mitishamba inayotumiwa kutibu magonjwa ya kawaida kama vile mafua, mchafuko wa tumbo pamoja na michanganyo mingine ya mitishamba ya Kichina ikiwa ndani ya chupa. Ukimweleza tu msaidizi wa mwenye duka au karani tatizo lako, atapendekeza bidhaa iliyo ndani ya chupa au kifurushi cha mchanganyo wa mitishamba halafu akupe mawaidha ya jinsi ya kuitayarisha nyumbani.

Kwenye upande mmoja wa ukuta ulio nyuma ya msaidizi wa mwenye duka, tunaona chupa kubwa zimepangwa kwenye rafu zikiwa na aina mbalimbali ya mizizi, majani, na vijiti vilivyokaushwa. Wateja wanajua mitishamba hii na wanaweza kuinunua kwa ajili ya kujitibu au kwa ajili ya mapishi. Kwenye upande wa pili wa duka, kuna kabati inayofika kwenye dari yenye safu nyingi za saraka zilizochakaa. Kabati hii inaitwa baizigui au “kabati yenye watoto 100,” kwa sababu kabati hiyo ya mitishamba yaweza kuwa na saraka 100 au zaidi. Kuwepo kwa saraka hizi humwezesha mwenye duka kupata upesi dawa zinazotumiwa kwa ukawaida, na zile zinazopendwa zaidi ndizo huwekwa mahali ambapo ni rahisi kufikiwa. Kwa kawaida hakuna alama yenye kuonyesha vilivyomo ndani ya saraka. Wasaidizi wenye uzoefu wanajua mahali hasa mitishamba ya kila aina imewekwa.

Tazama ustadi wa msaidizi anapopima mitishamba kwa mteja huyu wa kike. Anatumia mizani ya Asia iliyo hafifu lakini isiyo na hitilafu—mti wenye vipimo ukiwa na sinia yenye kuning’inizwa kwa kamba tatu upande mmoja na jiwe la mizani lenye kusogezwa likiwa upande ule mwingine. Anafahamu kwamba baadhi ya mitishamba yaweza kusababisha kifo ikitumiwa kupita kiasi na hivyo lazima awe mwangalifu anapoipima. Si aina zote za mitishamba zinazohitaji kupimwa kwa mizani. Sasa tunamwona akichota kwa mkono kiasi kidogo cha mitishamba kadhaa kutoka kwa saraka mbalimbali na kuiweka ndani ya karatasi. Naam, umewaza sawa, agizo hili la mitishamba linatia ndani makoa ya nyenje. Anapokuwa akifunga mkusanyo huo, anamweleza mwanamke huyo jinsi atakavyotumia mitishamba hiyo.

Mitishamba hutayarishwa na kutumiwa kwa njia mbalimbali. Nyingine huwa ya ungaunga. Mgonjwa huichanganya na maji moto na kuinywa. Nyingine huwa lahamu. Huchanganywa na asali au aina fulani ya kileo kabla ya kutumiwa. Hata hivyo, mwanamke huyu ameambiwa atumie njia iliyo ya kawaida zaidi, yaani, achemshe mitishamba. Hilo litambidi achemshe mitishamba hiyo ndani ya nyungu kwa muda wa saa moja hivi. Kisha anywe mchanganyiko huo kila baada ya saa kadhaa. Na iwapo mwanamke huyu ahitaji agizo jingine, atarudi tena hapa dukani na kupata kiasi kingine cha mitishamba.

Hatimaye zamu ya Kwok Kit ya kumwona daktari imewadia. La, daktari hatangulii kupima msukumo wa damu wala mpigo wa moyo wa Kwok Kit. Lakini anamwuliza Kwok Kit dalili za ugonjwa wake. Je, ana tatizo la kupata usingizi? Vipi mmeng’enyo wake wa chakula, hamu, tumbo, joto, hali na rangi ya ngozi yake? Daktari atazama kwa makini macho yake na kuchunguza rangi ya sehemu mbalimbali za ulimi wake. Sasa anapima mpigo wa moyo wa Kwok Kit kwenye sehemu mbalimbali za viganja vyote viwili akitumia nguvu mbalimbali, njia hii inadhaniwa kuonyesha hali ya viungo na sehemu mbalimbali za mwili. Hata, daktari anachunguza pia kama ana harufu isiyo ya kawaida! Uamuzi? Haishangazi kwamba Kwok Kit ana mafua. Anahitaji pumziko la kitandani na kunywa maji mengi pamoja na mitishamba iliyochemshwa. Mchanganyiko wa mitishamba ukisha chemshwa utakuwa mchungu, lakini utampa nafuu. Pamoja na habari kuhusu vyakula vya kuepuka, daktari amweleza kwa fadhili Kwok Kit aina ya plamu iliyohifadhiwa ambayo itaondoa ladha chungu mdomoni baada ya kunywa mitishamba.

Huyo, Kwok Kit aondoka na kifurushi chake cha mitishamba. Kumwona daktari pamoja na dawa kumemgharimu Kwok Kit dola za Marekani zisizozidi 20—bei nafuu kwelikweli. Ingawa mitishamba hiyo haitamponya mara moja, Kwok Kit apasa kupata nafuu baada ya siku chache. Lakini hapasi kutenda kama wengine ambao hukosea kwa kudhani kwamba kunywa mitishamba kupita kipimo huponya haraka. Ni kawaida kusikia habari za watu waliopatwa na madhara mabaya baada ya kutumia mitishamba fulani kupita kipimo.

Katika nchi fulani hakuna kanuni zenye kuongoza matumizi ya mitishamba wala madaktari wa mitishamba ya Kichina. Jambo hilo limetokeza madaktari bandia na hata kuuzwa kwa michanganyo hatari ya mitishamba ikisingiziwa kuwa dawa. Kwa hiyo, haishangazi kwamba wagonjwa wengi wa Kiasia hutegemea mapendekezo ya watu wa ukoo na marafiki wa karibu wanapohitaji kumuona daktari wa mitishamba ya Kichina.

Bila shaka, hakuna tiba yoyote—iwe ya mitishamba au ya kutoka Magharibi—iwezayo kutibu magonjwa yote. Hata hivyo, duka la dawa za Kichina na daktari wa mitishamba ni sehemu muhimu ya maisha katika Asia.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Amkeni! halipendekezi tiba fulani hususa. Wakristo wapaswa kuhakikisha kwamba tiba wanayochagua haipingani na kanuni za Biblia.

^ fu. 8 Mtawala wa Manjano, alikuwa mtawala mashuhuri sana kabla ya nasaba ya Zhou, na inadhaniwa kuwa alitawala kuanzia mwaka wa 2697 K.W.K hadi mwaka wa 2595 K.W.K. Hata hivyo, wasomi wengi wanaamini kwamba kitabu Nei Jing kiliandikwa mwishoni mwa nasaba ya Zhou, iliyotawala kuanzia mwaka wa 1100 K.W.K hivi hadi mwaka wa 250 K.W.K.

^ fu. 9 Herufi ya Kichina ya “yin” humaanisha “utusitusi” au “kivuli” na huwakilisha giza, baridi, mambo ya kike. Herufi ya “Yang,” kinyume cha yin, huwakilisha mambo maangavu, joto, mambo ya kiume.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Vitu vya kipekee, kutia ndani farasi-maji waliokaushwa, vinapatikana katika duka la mitishamba

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mizizi, majani, na vijiti vikavu hupimwa kwa umakini