Uokoaji wa Ajabu
Uokoaji wa Ajabu
Na mleta-habari wa Amkeni! katika BENIN
“WALE wanaume watatu wangali hai kwa sababu Mashahidi wa Yehova waliwaokoa!” Hizo ndizo habari zilizosambaa upesi kote katika mji wa Calavi, katika nchi ya Benin iliyo Afrika Magharibi, Jumatano, Aprili 19, 2000. Wanaume hao watatu walikuwa nani, na Mashahidi wa Yehova waliwaokoaje?
Mwendo wa saa 12:30 asubuhi, Philippe Elegbe na Roger Kounougbe walikuwa wakijitayarisha kufanya kazi katika uwanja wa kusanyiko la Mashahidi wa Yehova unaopakana na ofisi ya tawi ya Benin ya Watch Tower Society. Mamia ya watu wangekusanyika hapo jioni hiyo kwa ajili ya Ukumbusho wa kila mwaka wa kifo cha Yesu Kristo. * Ghafula, kishindo kikubwa mno kilivuruga utulivu na amani asubuhi hiyo. Mara moja, Philippe na Roger walitambua kwamba aksidenti ilikuwa imetokea kwenye barabara kuu.
Muda mfupi baadaye walimsikia mtu akipaaza sauti: “Wafanyakazi wangu watatu wamefunikwa na mifuko yenye sementi!” Philippe na Roger wakatimua mbio kuelekea kwenye barabara kuu. Walipofika waliona lori lenye uzito wa tani 20 likiwa limepinduka. Mifuko mingi sana yenye kujaa sementi ilikuwa imeanguka kutoka kwenye lori hilo.
Josué Didolanvi, ambaye alikuwa akifanya kazi pia kwenye uwanja wa kusanyiko, alikuwa tayari amefika palipotokea aksidenti, alikuwa akimvuta mtu aliyebanwa kati ya chumba cha dereva cha lori na mifuko yenye sementi. Dereva, aliyejiponyoa kutoka kwenye lori hilo, alikuwa ameshtuka sana. Lakini bado alikuwa na nguvu za kusema kwa sauti: “Kungali na watu wawili chini ya mifuko hiyo yenye sementi!” Watazamaji kadhaa walianza kuondoa mifuko hiyo, lakini waliacha baada ya muda kwa sababu ya joto kali la sementi. Sementi hiyo ilikuwa imetoka tu kwenye tanuri kiwandani!
Wafaulu Kuwaokoa
Philippe, Roger, na Josué walianza kujikakamua kuondoa rundo hilo la mifuko ya sementi, mmoja baada ya mwingine. Walihisi maumivu makali mikononi kwa sababu ya joto na uzito wa mifuko hiyo yenye uzani wa kilogramu 50. Jambo baya hata zaidi ni kwamba sementi ilikuwa ikimwagika kutoka kwenye mifuko iliyopasuka, na kutokeza malengelenge kwenye vidole vyao na hata ikawa vigumu kupumua. “Mikono yangu ilikuwa ikichomeka, hasa vidole vyangu,” Josué akasema baadaye. “Lakini niliendelea kufikiri kwamba bado kulikuwa na nafasi ya kumwokoa yeyote aliyekuwa amefunikwa na mifuko hiyo.”
Baada ya kuondoa mifuko 40 hivi, waokoaji hao watatu waliona mkeka wa majani makavu. Walipigwa na butwaa kuwakuta wanaume wawili—wakiwa chini ya mkeka huo. Walikuwa hai! Aksidenti ilipotokea, wanaume hao walikuwa wamelalia mkeka huo ambao ulifunika mifuko yenye sementi kwenye lori. Walipodondoka kutoka kwenye lori, mkeka uliwafunika, na hivyo ukawakinga na joto kali sana la mifuko hiyo yenye sementi iliyokuwa juu yao.
Wakati na baada ya uokoaji, umati mkubwa wa watu ulikusanyika hapo kutazama. Wote walistaajabu kwa sababu Philippe, Roger, na Josué waliweza kuondoa rundo la mifuko yenye sementi yenye uzito wa tani mbili haraka sana chini ya hali ngumu. Walivutiwa pia kwa sababu wanaume hao watatu walijitolea mhanga kuwasaidia watu wasiowajua hata kidogo. Punde si punde yaonekana kila mtu katika Calavi alipata habari za tendo lao la kishujaa.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Mashahidi wa Yehova hutii amri ya Yesu kwa kuadhimisha ukumbusho huo mtakatifu kila mwaka.—Luka 22:19.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Roger akiwa ameshika ule mkeka wa majani makavu baada ya uokoaji