Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wajue Nyuki Wasiouma wa Australia

Wajue Nyuki Wasiouma wa Australia

Wajue Nyuki Wasiouma wa Australia

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

JE, UMEWAHI kutulizwa na mvumo wenye kuburudisha wa nyuki wenye bidii wanaporuka kutoka kwa ua moja hadi jingine katika mwangaza wenye kung’aa wa jua mwanzoni mwa masika? Kwa kweli, ni wadudu maridadi. Laiti hawangekuwa wakiuma!

Waweza kushangaa kujua kwamba kuna nyuki wasiouma. Wanajulikana kama nyuki wasiouma wa Australia, nao wanapatikana katika sehemu nyingi mashariki mwa Australia. Nyuki wasiouma wana urefu wa milimeta nne tu. Wana rangi nyeusi, pia wana manyoya mengi meupe katika uso na ubavuni. Wengi wao wana madoadoa madogo ya manjano kwenye sehemu za nyuma za kidari za mwili wao. Kuna angalau jamii kumi za nyuki wasiouma kwenye pwani ya kaskazini ya Queensland kuteremka hadi kusini mwa New South Wales. Baadhi yao hata wamepatikana katika Eneo la Kaskazini la kitropiki kwenye bara hilo.

Fikiria manufaa wanazopata warina-asali. Mfugaji mmoja wa nyuki asema: “Mimi huhitaji kuvalia kifuniko cha uso na fulana inayofunika shingo ninaposhughulikia [jamii nyingine za nyuki], lakini sihitaji kujikinga na chochote ninaposhughulikia [nyuki wasiouma]. Dakika tano baada ya kufunua mzinga, nyuki hao waendelea na shughuli zao kana kwamba sipo.”

Mizinga ya nyuki wasiouma ni tofauti sana na ile ya nyuki wengine wanaotoa asali. Hata, mara nyingi huitwa viota. Badala ya kuhifadhi asali na chavuo katika sega la asali la kawaida lenye pande sita, nyuki wasiouma hutengeneza vitundu vingi vyenye umbo la yai. Vitundu hivyo hufunikwa vikisha jaa, halafu vitundu vingine hutengenezwa juu yake au kando yake.

Ndani ya Kiota

Acheni tuchunguze kiota, makao ya nyuki wasiouma wapatao 15,000. Lakini, uwe mwangalifu kwa kuwa nyuki hao wanaweza kukuuma kidogo kwa taya zao ingawa hawaumizi.

Pembeni mwa kiota hicho twaona utendaji mkubwa ajabu. Nyuki hao wanafanya kazi kwa umoja kabisa. Kila mmoja wao anafahamu barabara jambo la kufanya na mahali pa kulifanyia. Twaona nyuki mmoja mdogo akilainisha na kung’arisha kitundu kipya cha asali, kana kwamba anaiga kwa usahihi kabisa mchoro fulani. Kando yetu nyuki wanne zaidi wanafunika kitundu ambacho kimetoka tu kujazwa asali. Kiambaza chenye pande tatu hutumiwa kama fremu inayotegemeza vitundu vya asali. Uhandisi huu bora kabisa hutegemeza uzito wa asali.

Sasa twaingia chumba cha pili nasi twaona nyuki mmoja aliye mkubwa kuliko nyuki wengine. Huyu ndiye malkia mwenye fahari tosha! Anapendeza kama nini, akiwa na rangi nyeusi-nyangavu na duara za kidhahabu huku akiwa amezingirwa na kundi kubwa la nyuki wengine wenye shughuli nyingi! Sasa malkia aanza kutaga mayai katika vijumba 60 alivyotayarishiwa. Anataga kwa ustadi na kwa uangalifu mkubwa kama nini, anashabihi mama anayemlaza mtoto wake mchanga kitandani! Angalia pia namna wafanyakazi wanavyofunika hima-hima vijumba hivyo baada ya malkia kutaga mayai ndani yake. Kazi hiyo yakamilika baada ya dakika chache tu.

Mayai Yanapoanguliwa

Mayai yanapoanguliwa, kila funza mdogo aliyeanguliwa (au, kiluwiluwi) hula chakula kilichotiwa kwenye kijumba alichotayarishiwa. Baada ya kuwa mkubwa na kuzidi kijumba chake cha nta, funza huyo husokota kifukofuko cha hariri atakamoishi. Katika kifukofuko hicho funza hukomaa na kuwa nyuki (baada ya kuwa pupa). Baadaye, huibuka kutoka kwenye kifukofuko hicho na kuanza kazi—yaani, baada ya kutunzwa sana na nyuki kadhaa walezi. Inakuwaje kwa vile vijumba vya nta? Vinakusanywa mara moja, na kutengenezwa upya. Vifukofuko hivyo havihitajiwi tena baada ya nyuki kuibuka ndani yake. Vikiachwa humo vitachafua kiota tu. Kwa hiyo nyuki wengi wasafishaji huokota vifukofuko vinavyosalia na kuvitengeneza upya.

Jamii nyingi za nyuki wasiouma hutengeneza dutu fulani ya ujenzi inayoitwa cerumen. Hutengenezwa kwa nta inayotoka katika miili ya nyuki wenyewe na kuchanganywa na utomvu na nta wanayokusanya kutoka kwa mimea na miti. Dutu ya cerumen hutumiwa kujengea fremu yenye nguzo na mihimili na mitambaapanya, na viunganishi vilivyoimarishwa. Wanapotengeneza asali na vitundu vya chavuo katika fremu hiyo, nyuki huruka huku na huku ndani ya vitundu hivyo, wakilainisha na kushindilia cerumen hiyo. Kisha vitundu hivyo hufunikwa na kuhifadhiwa vinapojaa. Yaonekana kwamba nyuki hao hujua kisilika umuhimu wa mimea kulingana na msimu na hatari za kubadilika kwa halihewa. Inaonekana wanajua vizuri sana kwamba kukusanya na kuhifadhi chakula ni muhimu sana kwa uhai wao.

Nyuki hutoka kiotani na kwenda kutafuta vifaa vya kujengea vilevile mbochi na chavuo. Nyuki huruka na kusafiri kwa ustadi sana mara tu atokapo katika kiota. Nyuki anajua vitu vya kukusanya na mahali anapoweza kuvipata.

Kuanza Makao Mapya

Kiota husongamana sana kadiri kundi linavyokua. Sasa inakuwaje? “Hatuna budi kujenga nyumba nyingine” yaelekea ndio ujumbe kwa jamii hiyo ya nyuki. Nyakati nyingine, nyuki mmoja mpelelezi hutumwa kwenda kutafuta shimo linalofaa kujengwa kiota. Kisha “wahandisi” huja kukagua mahali hapo. Kwa kawaida wataalamu 30 hadi 50 hukagua ndani ya shimo hilo kwa saa kadhaa, kana kwamba wanachora plani ya nyumba kwa mistari na vijiti. Halafu, wakisha amua kwamba msingi huo unafaa, wanarejea nyumbani ili kutoa ripoti. Kisha, kwa kawaida katika muda wa saa 48, “wajenzi” wenyewe huwasili. Kundi hilo laweza kuwa na zaidi ya nyuki elfu moja—lakini halina malkia. Upesi wanaanza kazi, wakileta vifaa vya ujenzi na chakula kutoka kwa kiota cha awali.

Ili kutayarisha chumba cha malkia kwenye kiota hicho kipya, ni sharti chumba cha kutagia mayai kijengwe kwa hali ya kuweza kudumisha halijoto inayofaa—ya nyuzi Selsiasi 28 hivi. Ili kutimiza takwa hilo, nyuki wafanyakazi hulazimika kufunika kiota chote kwa cerumen, kana kwamba wanafunika kiota kwa blanketi. Ni kana kwamba nyuki hao wenye hekima wanajua kuwa ni lazima mayai yapashwe joto. Sasa kila kitu ki tayari, na siku ya tisa hivi, malkia mpya, ambaye amelelewa kwenye kiota cha awali aletwa kwenye kiota kipya. Mara moja, anaanza kutaga mayai yatakayotokeza nyuki zaidi kwenye kiota chake.

Pole kwa pole, nyuki waliotoka kwa kiota cha awali hufa na mahali pao kuchukuliwa na nyuki wengine wapya, wachanga kutoka kwa makao hayo mapya. Muda si muda, nyuki wa kiota hiki watalazimika kujenga makao mengine mapya. Na hivyo mzunguko mwingine wenye kustaajabisha uliobuniwa na Muumba asiye na kifani huendelea!

[Picha katika ukurasa wa 13]

Badala ya kujenga sega lenye pande sita, nyuki wasiouma hutengeneza vitundu vingi vyenye umbo la yai

[Picha katika ukurasa wa 14]

Kuna angalau jamii kumi za nyuki wasiouma huko Australia