Je, Una Miguu Isiyotulia?
Je, Una Miguu Isiyotulia?
NI USIKU. Umejilaza na kustarehe kitandani. Kisha waanza kuhisi—kana kwamba mdudu anatambaa miguuni. Huwezi kupuuza jambo hilo. Kuamka na kutembea ndiyo njia pekee ya kutuliza hali hiyo. Kutembea kunatuliza, lakini mara tu ulalapo tena tatizo linaanza. Unataka kulala lakini wapi. Ikiwa hilo ni tatizo lako hauko peke yako. Kwa mfano, huenda yapata asilimia 15 ya watu katika Marekani wana tatizo hilo.
Ingawa huenda madaktari wengi hawautambui au kuutibu ifaavyo, huu si ugonjwa mpya. Katika mwaka wa 1685 daktari mmoja aliandika juu ya wagonjwa ambao walikuwa ‘wakitatizwa sana’ na mikono na miguu hivi kwamba “walishindwa kupata usingizi kana kwamba walikuwa Mahali penye Mateso makali.”
Sababu moja inayofanya iwe vigumu kutambua ugonjwa huo ni kwamba hakuna mbinu yoyote ya maabara ya kupima kuwepo kwa ugonjwa huo mwilini. Hujulikana tu kwa dalili zake. Daktari mwenye ujuzi huenda akauliza hivi: “Je, unahisi mtambao huo kwenye mguu mmoja au miguu yote miwili? Je, wewe huhisi mtambao huo kwenye mikono? Je, hisia hiyo hutulia unapoamka na kutembea, unapooga, au unapokanda miguu? Je, hisia hiyo isiyopendeza hutokea baada ya kuketi kwa muda mrefu, kama vile garini au katika ndege? Je, hukutatiza zaidi wakati wa usiku? Je, kuna washiriki wengine wa familia wenye tatizo hilo? Je, mwenzi wako hukuambia kwamba wewe hukutua miguu yako unapokuwa umelala? Ikiwa jibu lako kwa baadhi ya maswali haya ni ndiyo, daktari huenda akakata kauli kwamba una ugonjwa wa miguu isiyotulia (RLS).
Walio na Ugonjwa Huo
Kwa baadhi ya watu, RLS ni tatizo dogo lenye kutokeza dalili mara kwa mara. Kwa watu wengine ni tatizo kubwa sana, linalowafanya wakose usingizi daima na kuwa wachovu mchana na hivyo kuvuruga shughuli zao za kila siku. Mtu mmoja mwenye ugonjwa huo alisema hivi: “Mimi huhisi kana kwamba minyoo wanatambaa kwenye miguu yangu. Nahitaji kufurukuta miguu yangu ili kutuliza hisia hiyo.”
Ugonjwa wa RSL huathiri watu wa jinsia zote na hali huwa mbaya zaidi katika watu wazee. Mara nyingi ugonjwa huu hutambuliwa katika
watu waliofikia umri wa miaka yao ya 50, ingawa dalili huwa zimejitokeza miongo mingi mapema. Nyakati nyingine dalili huenda zilianza utotoni. Kwa kawaida RLS husumbua watoto bila kutambuliwa. Kwa kuwa watoto wenye ugonjwa huo huwa hawatulii au daima husogea-sogea, wanasemwa tu kuwa “watendaji kupita kiasi.”Ingawa wataalamu wanauona ugonjwa wa RSL kuwa kasoro ya neva, ni vigumu kuwa na uhakika kuhusu chanzo chake. Kinachosababisha ugonjwa huo mwilini mwa watu wengi hakijulikani. Hata hivyo, ugonjwa wa RLS umehusianishwa na mambo fulani. Kwa mfano, ugonjwa wa RLS unarithiwa katika familia, kupitia chembe za urithi kutoka kwa wazazi hadi kwa watoto wao. Baadhi ya wanawake wajawazito hupata dalili za ugonjwa wa RLS, hasa wakiwa karibu kujifungua. Baada ya kujifungua dalili hizo kwa kawaida hupotea. Nyakati nyingine, matatizo ya kiafya, kama vile uhaba wa madini ya chuma mwilini au ukosefu wa vitamini fulani, hutokeza dalili zenye kusumbua za ugonjwa wa RLS. Maradhi yanayodumu yanaweza pia kutokeza dalili za ugonjwa wa RLS—hasa kushindwa kwa figo kufanya kazi, ugonjwa wa sukari, ugonjwa wa baridi-yabisi, ugonjwa wa hitilafu ya mishipa ya fahamu, kuharibika kwa neva kwenye mikono na miguu.
Jitihada ya Kutafuta Kitulizo
Kwa kusikitisha, ugonjwa wa RLS hauna tiba, na dalili zake huzidi kuwa mbaya kadiri miaka inavyosonga. Ingawa hivyo, habari njema ni kwamba ugonjwa wa RLS waweza kutibiwa kabisa, mara nyingi bila matumizi ya dawa. Hakuna suluhisho moja kwa tatizo hili; linalofaa kwa mmoja huenda lisifae kwa mwingine. Wenye ugonjwa huo wanahitaji kutambua ni tabia zipi, utendaji upi, au ni dawa zipi zinazozidisha au kupunguza dalili zake.
Jambo la kufanya kwanza ni kuhakikisha kama kuna ugonjwa unaoweza kutibika unaosababisha dalili za RLS. Kwa wagonjwa wenye uhaba wa chuma au vitamini mwilini mwao, kutumia madini ya chuma au vitamini B12 pamoja na milo yao huenda likawa ndilo jambo linalohitajiwa tu ili kutuliza ugonjwa wa RLS.Hata hivyo, kutumia vitamini na madini kwa wingi kwaweza kuhatarisha afya yako. Hivyo, uamuzi wa kutumia madini ya chuma au vitamini za ziada wapasa kufanywa baada ya kushauriana na daktari.
Katika watu fulani kafeni huzidisha dalili za ugonjwa wa RLS. Kahawa, chai, chokoleti, na aina mbalimbali za soda huwa na kafeini. Kupunguza au kuacha kabisa kutumia kafeini, kwaweza kupunguza au hata kumaliza dalili zote za ugonjwa wa RLS. Unywaji wa vileo huzidisha dalili au muda wa kuwa na dalili hizo. Kupunguza au kuacha kabisa unywaji wa vileo, hutuliza maumivu ya watu wengine.
Kuishi na Ugonjwa wa RLS
Iwapo una ugonjwa wa RLS, kubadili mtindo wako wa maisha huenda kukawa na mafaa. Kwa sababu uchovu na kusinzia kwa kawaida hufanya dalili kuwa mbaya zaidi, inafaa sana kuwa na utaratibu usiobadilika wa kulala. Inapowezekana, lala mahali palipo kimya, patulivu na penye kustarehesha. Kulala na kuamka wakati uleule kila siku ni kwenye mafaa pia.
Kufanya mazoezi kwa ukawaida kutakusaidia kupata usingizi wa kutosha. Hata hivyo, kufanya mazoezi magumu saa sita kabla ya kulala kwaweza kuharibu usingizi wako. Wagonjwa fulani wa RLS wamepata kwamba mazoezi ya kiasi kabla tu ya kulala huboresha usingizi wao. Jaribu kufanya mazoezi tofauti-tofauti ili uweze kufahamu yanayokufaa.
Usijizuie unapohisi kutembea. Ukijaribu kujizuia kutenda, hali huzidi kuwa mbaya zaidi. Mara nyingi suluhisho linalofaa ni kutoka kitandani na kutembea huku na huku. Kutembea, kujinyoosha, kuoga mwili kwa maji baridi au moto, au kukanda miguu huwapa watu fulani nafuu. Iwapo utalazimika kuketi kwa muda mrefu, kama vile wakati wa kusafiri, itafaa ushughulishe akili yako kwa kusoma.
Vipi matibabu? Taasisi ya Ugonjwa wa RLS, iliyoko huko Raleigh, North Carolina, Marekani, yasema kwamba “huenda ikawa lazima kuanza kutumia dawa.” Kwa kuwa hakuna dawa moja yenye kufaa wagonjwa wote wa RLS, daktari wako atahitaji kutambua ile inayofaa hali yako. Wengine wamepata kwamba mchanganyo wa dawa huwafaa zaidi. Nyakati nyingine dawa iliyofanya kazi wakati fulani huenda iwe haifai tena. Na kwa sababu kutumia dawa na hasa mchanganyiko wa dawa ni hatari kwa afya, inafaa kushauriana na daktari wako kuhusu zile dawa zinazofaa kabisa hali yako.