Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka Maumivu Makali Hadi Unusukaputi

Kutoka Maumivu Makali Hadi Unusukaputi

Kutoka Maumivu Makali Hadi Unusukaputi

KABLA ya miaka ya 1840, wagonjwa hawakuingia ndani ya chumba cha upasuaji wakiwa na wasiwasi. Walikuwa na hofu kuu! Kwa nini? Kwa sababu unusukaputi haukuwepo. Katika kitabu chake “We Have Conquered Pain,” Dennis Fradin asema hivi: “Imesemwa kwamba madaktari-wapasuaji waliingia chumba cha upasuaji wakiwa wameshika mikononi mwao chupa mbili za mvinyo—moja kwa ajili ya mgonjwa na nyingine ya daktari ili aweze kustahimili mayowe ya mgonjwa.”

Kumlevya Mgonjwa au “Kumpumbaza”!

Madaktari, madaktari wa meno, na wagonjwa, walijaribu mbinu yoyote ya kupunguza maumivu wakati wa upasuaji. Madaktari wa Kichina na wa Kihindi walitumia bangi. Kasumba na vileo vilitumika katika sehemu nyingi za ulimwengu. Dioscorides, daktari wa Ugiriki ya kale —mtu wa kwanza kutumia neno “unusukaputi”—aliona dawa iliyotengenezwa kutokana na mmea wa mandragora na divai kuwa na uwezo wa unusukaputi. Madaktari wa baadaye hata walijaribu njia ya kupumbaza akili ya mgonjwa.

Na bado, njia hizo hazikuondoa maumivu ifaavyo. Kwa sababu hiyo, madaktari-wapasuaji na madaktari wa meno walifanya kazi yao haraka iwezekanavyo; hata uzoefu wao ukaja kupimwa kwa wepesi wao. Ingawa hivyo, wagonjwa waliteseka sana wajaposhughulikiwa na madaktari wepesi. Matokeo yakawa kwamba watu waliamua kuvumilia magonjwa mbalimbali, haidhuru ni uvimbe au kinywa chenye kujaa meno yenye kuoza, badala ya kukabili maumivu ya upasuaji au kung’olewa jino.

Mafuta Matamu ya Salfa na Gesi-Chekeshi

Katika mwaka wa 1275, daktari Mhispania Raymond Lullus, huku akifanya majaribio ya kemikali, alitokeza umajimaji fukivu, wenye kushika moto kwa urahisi aliouita mafuta matamu ya salfa. Katika karne ya 16, daktari Mswisi anayejulikana sana kwa jina Paracelsus aligundua kwamba kuku waliovuta hewa ya mafuta matamu ya salfa walilala na hawakuhisi maumivu kabisa. Lullus na Paracelsus hawakufanya majaribio hayo kwa wanadamu. Katika mwaka wa 1730, Frobenius, mwanakemia Mjerumani, aliupa umajimaji huo jina lake la kisasa, etha, ambalo ni neno la Kigiriki linalomaanisha “ya kimbingu.” Hata hivyo, miaka 112 ilipita kabla ya dutu za etha zenye uwezo wa kusababisha unusukaputi kuthaminiwa kikamilifu.

Wakati huohuo, Joseph Priestley, mwanasayansi Mwingereza, aligundua gesi ya oksidi nitrasi katika mwaka wa 1772. Mwanzoni, gesi hiyo ilidhaniwa na watu kuwa yenye kufisha, hata ikitumiwa kwa vipimo vidogo. Hata hivyo, katika mwaka wa 1799, Humphry Davy, mwanakemia na mvumbuzi Mwingereza, aliamua kuhakikisha jambo hilo kwa kujaribu gesi hiyo yeye binafsi. Alishangazwa kugundua kwamba gesi hiyo ilimfanya aangue kicheko, na hivyo akaipa jina la ziada gesi-chekeshi. Davy aliandika kuhusu uwezekano wa kutumia oksidi nitrasi katika unusukaputi, lakini hakuna mtu aliyefuatilia jambo hilo wakati huo.

Etha na Vikusanyiko vya Gesi-Chekeshi

Vituko vya Davy alipovuta gesi-chekeshi—ambayo alikuja kuwa mraibu wake kwa kipindi fulani—vilijulikana sana. Punde si punde watu wakaanza kuvuta gesi hiyo ili kujifurahisha. Hata wanasarakasi wasafiri, ikiwa sehemu ya programu yao, waliomba wajitoleaji kutoka kwa watazamaji waje jukwaani na kuvuta gesi-chekeshi kwa zamu. Wakiwa chini ya uvutano wa gesi hiyo, walishindwa kujizuia na punde si punde vitimbi vyao vyenye kupita kiasi vilichekesha watazamaji sana.

Karibu na wakati huo, matumizi ya etha kwa ajili ya kujifurahisha yakavutia watu wengi. Hata hivyo, siku moja daktari mmoja mchanga huko Marekani aitwaye Crawford W. Long, aligundua kwamba rafiki zake hawakuhisi maumivu baada ya kujeruhiwa wakipepesuka chini ya uvutano wa etha. Mara moja akafikiria jinsi ya kuitumia katika upasuaji. Na kama kwa mpango, miongoni mwa watu wenye “kupata raha ya etha,” kulikuwa na mwanafunzi aitwaye James Venable, ambaye alitaka vivimbe viwili vidogo alivyokuwa navyo vipasuliwe. Lakini kwa kuhofia maumivu, Venable alikuwa akiahirisha upasuaji. Kwa sababu hiyo, Long akadokeza apasuliwe akiwa chini ya uvutano wa etha. Venable akakubali, na katika Machi 30, 1842, akafanyiwa upasuaji bila kuhisi maumivu yoyote. Hata hivyo, Long hakutangaza ugunduzi wake mpaka mwaka wa 1849.

Madaktari wa Meno Pia Wagundua Unusukaputi

Mnamo Desemba 1844, daktari mmoja wa meno wa huko Marekani aitwaye Horace Wells, alienda kwenye sarakasi ambapo mtu mmoja aitwaye Gardner Colton alifanya maonyesho na oksidi nitrasi. Wells alijitolea kujaribu gesi hiyo lakini hakulewa kiasi cha kushindwa kung’amua lililokuwa likitendeka. Aliona mjitoleaji mwingine ambaye licha ya kugonga miguu yake kwenye benchi ngumu na kuvuja damu, hakuhisi maumivu yoyote. Usiku huo Wells akakata kauli kujaribu kutumia oksidi nitrasi katika hospitali yake ya meno—lakini kwanza aijaribu yeye mwenyewe. Alifanya mipango Colton alete gesi hiyo na daktari mwenzake wa meno aitwaye John Riggs ang’oe gego lake la mwisho lenye kasoro. Aling’olewa gego hilo bila kuhisi maumivu yoyote.

Wells aliamua kujulisha umma kuhusu huo ugunduzi wake kwa kutumia mbinu hiyo mbele ya madaktari wenzake. Lakini, alikuwa mwenye wasiwasi sana hivi kwamba alitumia gesi haba na mgonjwa akapiga yowe jino lilipokuwa liking’olewa. Bila kukawia watazamaji wakaanza kumzomea. Hata hivyo, ingewapasa kupata habari kutoka kwa mgonjwa mwenyewe, kwa sababu alikiri baadaye kwa Wells kwamba ingawa alipiga yowe, alikuwa amehisi maumivu kidogo tu.

Katika Septemba 30, 1846, Mmarekani mwenzake aliye daktari wa meno William Morton, aling’oa jino bila mgonjwa kuhisi maumivu yoyote, akitumia etha—msombo uleule aliotumia Long katika mwaka wa 1842. Morton alisaidiwa kutayarisha etha aliyotumia na mwanakemia mashuhuri aitwaye Charles Thomas Jackson. Tofauti na Long, Morton aliandaa wonyesho wake wa peupe wa dutu zenye kutoa unusukaputi za etha kwa mgonjwa mwenye kufanyiwa upasuaji. Katika Oktoba 16, 1846, Morton alimtia mgonjwa nusukaputi huko Boston, Massachusetts. Kisha daktari-mpasuaji, Dakt. Warren, akafanya upasuaji—kuondoa uvimbe chini ya taya la mgonjwa. Upasuaji huo ulifanikiwa ajabu. Habari ya jambo hilo ikasambaa haraka sana katika Marekani na Ulaya.

Ugunduzi Zaidi

Baada ya ugunduzi huo wenye kutokeza, majaribio ya gesi nyinginezo uliendelea. Klorofomu, iliyogunduliwa katika mwaka wa 1831, ilitumiwa kwa mafanikio katika mwaka wa 1847. Upesi, ikawa dawa ya unusukaputi inayopendwa na watu wengi katika maeneo fulani. Punde si punde klorofomu ikatumiwa kwa wanawake wenye kujifungua, kutia ndani Malkia Victoria wa Uingereza, mnamo Aprili 1853.

Kwa kusikitisha, sifa ya dawa ya unusukaputi yenye kutia ganzi mwili wote imeharibiwa kwa kiasi fulani. Kulikuwa na bishano kali juu ya ni nani—Long, Wells, Morton, au Jackson, yule mwanakemia mashuhuri aliyemsaidia Morton—anayestahili kukwezwa zaidi kwa kugundua unusukaputi (hilo, bila shaka, halitii ndani misombo yenyewe ya kemikali). Hakuna mwafikiano umewahi kupatikana, lakini kwa kusababu kunakofaa, watu wengi wametambua mchango wa wanaume hao wote wanne.

Wakati huohuo, maendeleo ya dawa ya unusukaputi ya kutia ganzi sehemu fulani tu ya mwili yaliendelea kufanywa. Unusukaputi unaotumiwa huruhusu wagonjwa kubaki na fahamu zao huku sehemu fulani ya mwili wao ikiwa imetiwa ganzi. Leo, madaktari-wapasuaji wa meno hutumia kwa ukawaida aina hii ya dawa ya unusukaputi wanaposhughulikia meno na ufizi wa meno, na madaktari wengine huzitumia wanapofanya upasuaji mdogo na kutibu majeraha. Wataalamu wa unusukaputi hutumia kwa ukawaida nusukaputi kutia ganzi sehemu fulani mwilini kwa wanawake wenye kujifungua.

Baada ya muda, utaalamu wa unusukaputi umesitawi na kuwa tiba maalumu. Wataalamu wa unusukaputi wa kisasa hushughulika na kutayarisha mgonjwa kwa upasuaji. Hutia wagonjwa nusukaputi kwa kutumia vyombo vya kisasa na dawa maalum za nusukaputi ambazo ni msombo wa kemikali kadhaa pamoja na oksijeni. Kwa kweli, wagonjwa wengi huenda hata wasijue kwamba daktari amewatia gesi za nusukaputi kwa sababu mara nyingi gesi hizo hutumiwa baada tu ya mgonjwa kutiwa ganzi na dawa nyingine ya nusukaputi kupitia mishipani. Mtaalamu wa unusukaputi pia hushughulika na kutuliza maumivu baada ya upasuaji.

Basi, iwapo utahitaji kufanyiwa upasuaji wakati ujao, epuka kuwa mwenye wasiwasi kupita kiasi. Ebu wazia ukiwa umelala kwenye meza sahili ya upasuaji karne mbili zilizopita. Mlango wafunguliwa na daktari atakayekufanyia upasuaji aingia akiwa amebeba chupa mbili za mvinyo. Mara moja, vifaa vya unusukaputi vya kisasa havitishi tena, sivyo?

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

TIBA YA VITOBO—Kitulizo cha Maumivu Kutoka Mashariki

Tiba ya vitobo ni tiba ya kale ya Kichina inayosemekana kuwa hutuliza maumivu. Wataalamu hudunga sehemu mbalimbali za mwili kwa sindano, kwa kawaida mbali na eneo linalotibiwa. Mara baada ya sindano kudungwa mwilini, huenda zikazungushwa au kupitishiwa mkondo wa umeme usio na nguvu nyingi. Kichapo Encyclopædia Britannica chasema kwamba tiba ya vitobo “inatumiwa kwa ukawaida katika China kama nusukaputi wakati wa upasuaji. Wageni kutoka Magharibi wameshuhudia upasuaji tata (na ambao kwa kawaida ni wenye maumivu mengi) ukifanyiwa wagonjwa wa Kichina wakiwa na fahamu huku tiba ya vitobo ikiwa ndiyo nusukaputi pekee.”

Tiba ya vitobo yapasa kutolewa tu na mtaalamu aliyehitimu kitiba. Kulingana na Encyclopedia Americana, “madhara makubwa yametukia baada ya sindano za tiba ya vitobo kudunga moyo au mapafu, na mchochota wa ini, sehemu fulani kuambukizwa, na matatizo mengine huenda yakatokea iwapo sindano zisizo safi zatumiwa.” Bila shaka, matumizi ya unusukaputi huwa na athari zake sawa na upasuaji wenyewe—bila kujali aina ya unusukaputi inayotumiwa.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Utaalamu wa unusukaputi umesitawi na kuwa tiba maalumu

[Hisani]

Courtesy of Departments of Anesthesia and Bloodless Medicine and Surgery, Bridgeport Hospital - CT

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

Ukurasa wa 2 na wa 21: Reproduced from Medicine and the Artist (Ars Medica) by permission of the Philadelphia Museum of Art/Carl Zigrosser/ Dover Publications, Inc.