Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Hasira ya Madereva Wanaotahiniwa

Kwa mujibu wa gazeti International Herald Tribune la Paris, “kushambuliwa kwa ‘wakaguzi’ 500 wanaowatahini madereva katika Ufaransa kwa maneno na kupigwa, kumeongezeka kwa asilimia 150 tangu 1994.” Idadi isiyozidi asilimia 60 ya watahiniwa wa udereva hufaulu mtihani huo wa dakika 20, na karibu watu wote ambao hawakufanya mtaala wa hali ya juu wa masomo ya udereva hufeli mtihani huo. Watu wasiofaulu huelekeza hasira yao kwa wakaguzi, wao hupigwa ndondi na kuburutwa kutoka garini wakiwa wameshikwa nywele. Hata mkaguzi mmoja, aliwahi kukimbizwa na mwanamume mmoja akiwa na sindano mkononi, aliyodai kuwa na damu yenye virusi vya UKIMWI. Hivi karibuni mwanamume mmoja wa miaka 23 alimfyatulia mkaguzi risasi za mpira baada ya kufeli mtihani. Ili kuepuka jeuri hiyo, wakaguzi wanapendekeza madereva wajulishwe matokeo ya mtihani wao kupitia barua badala ya kuelezwa ana kwa ana.

Wanafunzi Walio na Mkazo

Gazeti la Asian Age la huko Mumbai, laripoti kwamba kipindi cha mitihani ya mwisho wa mwaka hutokeza mkazo mkubwa kwa watoto wengi huko India. Kujifunza harakaharaka kwa ajili ya mtihani na mkazo wa kupata maksi nzuri hulemea wanafunzi wengi na idadi ya wale wanaowaona madaktari wa magonjwa ya akili huwa maradufu wakati wa mitihani. Katika jitihada ya kuwasaidia watoto wao kupata maksi nzuri, baadhi ya wazazi hukatiza aina zote za tafrija. “Watoto huwekwa chini ya mkazo mkubwa na wazazi wao. Pia kuna kushindana na wanafunzi wengine,” asema daktari wa magonjwa ya akili V. K. Mundra. Anaongezea kusema kwamba wazazi wengi “hawafahamu kwamba kumfanya mtoto astarehe kiakili kutamsaidia kujifunza vizuri zaidi.” Dakt. Harish Shetty asema kwamba mkazo wa mtihani “umewakumba hata watoto wa darasa la kwanza hadi la saba.”

Nguruwe-Mwitu Waja Mjini

Nguruwe-mwitu, ambao kwa kawaida ni waoga na huishi msituni, wamegundua kwamba hawapati tu chakula kwa wingi mijini bali pia ulinzi kutokana na wawindaji, lasema gazeti la kila juma la huko Ujerumani, Die Woche. Nguruwe-mwitu wa kike hata wamezalia ndani ya mji wa Berlin. Wakiwa na njaa wanazurura sehemu nyingine mbali na misitu au bustani za umma. Wanaharibu pia bustani za kibinafsi, kwa kutafuna maua. Nguruwe-mwitu hao ambao wanaweza kufikia uzito wa kilogramu 350, huwaogopesha wenyeji wengi, ambao katika visa fulani wamekimbilia usalama juu ya miti au ndani ya vyumba vya kupigia simu. Wanyama hao wamesababisha aksidenti za barabarani chungu nzima. Wanapofika nyumbani kutoka kazini, wenyeji wengi wamekumbana na wanyama hao wavamizi. Mtu mmoja aliuliza hivi: “Nitawezaje kuingia ndani ya nyumba huku nguruwe-mwitu wapatao 20 wakiwa wamesimama kati ya gari langu na mlango wa mbele wa nyumba yangu?”

Ndoa za Vijana

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kitaifa ya Afya kwa Jamii, katika India asilimia 36 ya ndoa za vijana ni za wale wenye umri wa kati ya miaka 13 na 16. Gazeti la Asian Age la huko Mumbai laripoti kuwa uchunguzi huo uligundua kwamba asilimia 64 ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 17 na 19 ama walikuwa tayari wamejifungua au walikuwa wajawazito. Ripoti hiyo yasema kwamba uwezekano wa wasichana wanaojifungua wakiwa na umri wa miaka 15 hadi 19 kufa kutokana na mimba ni maradufu zaidi ya wale wenye umri wa miaka 20 hadi 24. Zaidi ya hayo, magonjwa yanayoambukizwa kingono yameongezeka maradufu miongoni mwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 katika miaka michache iliyopita. Wataalamu wanasema kwamba matatizo hayo yanayozidi kuongezeka husababishwa na kutojua na habari potovu kuhusu mambo ya ngono kutoka kwa marika na vyombo vya habari.

Tiba Yasababisha Ugonjwa Mwingine

Gazeti la The Economist lasema kwamba “miaka thelathini iliyopita, Wamisri watatu kati ya watano walikuwa na ugonjwa wa kichocho, ugonjwa wenye kudhoofisha mwili unaosababishwa na vimelea walio katika konokono wa majini.” Kampeni ya kupambana na kichocho kwa kutumia dawa za kisasa imepunguza sana tisho la ugonjwa huo. Hata hivyo, yaonekana kwamba mojawapo ya kampeni zilizofanywa awali huenda “iliambukiza mamilioni ya watu mchochota wa ini aina ya C, ugonjwa wenye kufisha ambao huenda ukachukua mahali pa kichocho na kuwa tatizo kuu la afya huko Misri.” Sababu ilikuwa kwamba sindano za kutibu kichocho “zilitumiwa tena na tena bila kuchemshwa ifaavyo. . . . Wanasayansi hata hawakutambua virusi vya mchochota wa ini aina ya C (HCV) katika damu hadi kufikia mwaka wa 1988,” gazeti hilo lasema. Uchunguzi mbalimbali waonyesha kwamba Misri ina “idadi kubwa zaidi ya watu ulimwenguni wana mchochota wa ini aina ya C.” Wamisri milioni 11 hivi—takriban mtu 1 kati ya 6—wanasemekana kuwa na ugonjwa huo, ambao hukomaa na kuwa ugonjwa wa kudumu wa ini katika asilimia 70 ya visa na kuua katika asilimia 5 ya visa. Likitaja ugonjwa huo kuwa “ambukizo lililo kuu sana la virusi lililowahi kufanywa na madaktari,” makala hiyo yaongezea hivi: “Liwazo ni kwamba, bila kuwepo kwa kampeni hizo kubwa, watu wengi zaidi wangalikufa kwa kichocho.”

Uchafuzi Watokeza Kuenea kwa Wadudu Wenye Kuuma

Uchafuzi wa maji yaelekea umechangia kutokea kwa tatizo la wadudu wenye kuuma karibu na Mto Chili, ambao unapita katikati ya Arequipa, mmojawapo wa miji mikubwa zaidi nchini Peru. Wenyeji wamenunua dawa zote za kuwafukuza wadudu kutoka madukani katika jitihada ya kupambana na wadudu hao wadogo wenye kuuma. Kulingana na gazeti El Comercio la huko Lima, kuenea kwa wadudu hao yadhaniwa kumesababishwa na kutupwa kwa kemikali katika Mto Chili. Kemikali za sumu zimewaua chura wengi mtoni ambao “kwa miaka mingi wamekuwa njia ya asili ya kuwapunguza wadudu hao,” lasema gazeti hilo.

Divai Kali Zaidi

Polisi pamoja na makundi yanayoelimisha umma juu ya madhara ya ulevi katika Uingereza wameonya kwamba kuzidishwa kwa kiasi cha alkoholi katika divai kwaweza kulewesha wasiozoea kunywa divai. Miaka kumi iliyopita, ni divai ya msimu au divai tamu pekee ndizo zilizokuwa na asilimia 13 au 14 za alkoholi. Lakini, sasa divai zenye kutumiwa kwa ukawaida zina kiwango cha juu cha alkoholi kufikia asilimia 14. Divai hizo hutoka hasa katika nchi kama vile Australia, Afrika Kusini, na Chile, ambapo hali ya hewa yenye joto hutokeza zabibu mbivu zaidi, tamu zaidi, zenye kufanyiza divai kali zaidi. Likiandika kuhusu jambo hilo, gazeti la The Sunday Times la London lilimnukuu mkurugenzi msaidizi wa taasisi inayoshughulikia Maswala ya Vileo, Mary-Ann McKibben: “Kiwango cha alkoholi katika divai chazidi kuongezeka na hutatiza wenye kutumia divai, ambao hawatilii maanani ongezeko hilo.”

Je, Ni Safi Kupita Kiasi?

Kulingana na Taasisi ya Madawa ya Mazingira na Usafi wa Kiafya Hospitalini katika Chuo Kikuu cha Freiburg, Ujerumani, kemikali za ziada za kuua bakteria zilizo katika bidhaa kadhaa za nyumbani huenda zikawa bila mafaa na hata kuwa hatari, laripoti gazeti la Ujerumani, Westfälische Nachrichten. “Kemikali hizo hazihitajiki kamwe,” asema mkuu wa Taasisi hiyo Profesa Franz Daschner. “Kinyume cha kuwa zenye mafaa, bidhaa hizo zaweza kudhuru wanaozitumia.” Mojawapo ya madhara ni kwamba baadhi ya bidhaa hizo zina kemikali zinazosababisha mizio mikali. Nguo zenye kuvunda hazihitaji kuwekwa ndani ya kemikali zenye kuua bakteria bali zahitaji tu kufuliwa, yasema ripoti hiyo. Daschner amalizia kwa kusema: “Kuosha kwa kutumia sabuni ya kawaida isiyo na madhara kunatosha kabisa.”

Msongo wa Kujipatanisha

Uchunguzi wa vijana 500 uliofanywa na serikali huko Uingereza unadokeza kwamba vijana “wanamenyeka chini ya msongo wa kujipatanisha na mitindo inayosifiwa sana katika matangazo ya biashara na katika vyombo vya habari,” laripoti gazeti The Guardian la London. Ingawa wasichana hukabiliana na mkazo huo kwa kuzungumza pamoja na marafiki zao wa karibu, wavulana huona vigumu kueleza hisia zao, tokeo ni kwamba wengi huonyesha hasira yao kupitia matendo ya jeuri au uhalifu. Wakiwa na hisia za kujiona kuwa bure na mshuko-moyo mkali, mwelekeo wa wavulana kujiua ni mara tatu zaidi ya wasichana wenye umri sawa. Kwa upande mwingine, mwelekeo wa wasichana kujidhuru kimakusudi au kuwa na matatizo ya kula kama vile, kujinyima chakula na kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida ni mara nne zaidi ya wavulana.

Wachezaji wa Kandanda Waliotupwa

“Zaidi ya asilimia 90 ya vijana wanaocheza kandanda wanaosajiliwa kutoka Afrika kuchezea klabu za kandanda za Ufaransa mwishowe hujikuta wakiwa wafanyakazi haramu [bila] tumaini la kuwa raia wa Ufaransa,” lasema gazeti la Marianne la Paris. Ripoti moja rasmi ya serikali ya Ufaransa ilishutumu wasajili fidhuli ambao husafiri kote ulimwenguni wakitafuta “vijana wenye vipawa.” Maelfu ya vijana wa Kiafrika, kutia ndani vijana wapatao 300 walio na umri usiozidi miaka 13, wamevutiwa na wazo la kuwa na kazi-maisha yenye fahari katika michezo. Hata hivyo, wengi wao hawatii sahihi mkataba rasmi na klabu yoyote ile na mwishowe hujikuta wakiwa maskini hohe-hahe. Gazeti hilo lasema hivi: “Kuna visa vingi zaidi vya kuhuzunisha katika faili za mawakili wa kandanda kuliko visa vya wale wenye kufaulu.”