Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Rangi Inayovutia ya Kauri ya Koryo

Rangi Inayovutia ya Kauri ya Koryo

Rangi Inayovutia ya Kauri ya Koryo

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KOREA

MNAMO mwaka wa 1995 tunu moja iligunduliwa katika Maktaba ya Truman katika Missouri, Marekani. Ilikuwa nini? Chupa ndogo ya kauri ya maji yenye mchoro wa maua na rangi nzito yenye kung’aa. Ingawa urefu wake ni sentimeta 23 tu, chupa hiyo imekadiriwa kuwa na thamani ya takriban dola 3,000,000 za Marekani. Ni mojawapo ya vyombo vya ufinyanzi kutoka Korea vinavyojulikana kama kauri ya Koryo, na Rais wa hapo zamani wa Marekani Harry Truman alikabidhiwa chombo hicho na serikali ya Korea katika mwaka wa 1946.

Kwa nini kauri ya Koryo ni yenye thamani sana? Kwa nini iko tofauti na kauri nyinginezo?

Mbinu ya Pekee

Mtajo “kauri ya Koryo” hurejezea aina fulani ya pekee ya kauri iliyotengenezwa kwa mara ya kwanza wakati wa kipindi cha historia ya Korea kiitwacho Koryo (918-1392 W.K.). * Neno la Kikorea la aina hiyo ya kauri, ch’ongja, humaanisha kauri ya buluu. Wachina walioishi wakati huo waliisifu sana kauri hiyo, kwa maneno kama vile “iliyo bora zaidi chini ya mbingu.” Rangi hiyo nzito yenye kung’aa ya buluu na chanikiwiti huifanya kauri ya Koryo iwe ya pekee sana.

Rangi hii ya buluu na chanikiwiti yenye kuvutia hutokana na kuchanganywa kwa rangi ya udongo na chuma. Kila chombo kilichomwa mara mbili. Mwanahistoria wa usanii wa Korea Yang-Mo Chung asema kwamba kupitia mbinu hiyo kila chombo kilitengenezwa kwa udongo wenye chuma. Mwanzoni kilichomwa kwenye moto wa nyuzi Selsiasi 700 hadi nyuzi Selsiasi 800. Kisha chombo kilipakwa mchanganyiko wenye kung’aa wa kalisi ya kaboni na asilimia 1 hadi 3 ya chuma. Kisha, chombo kilichomwa tena—pindi hii kwa moto wa nyuzi Selsiasi 1,250 hadi nyuzi Selsiasi 1,300 na kiasi cha hewa kilichopunguzwa. *

Kuchunguza kwa makini kauri ya Koryo hufunua kwamba michoro yake maridadi huonekana ni kana kwamba inapatana kiasili na umbo lake. Vyombo maarufu sana vya kauri kama vile chupa, mabirika ya chai, sahani, na mitungi huwa na michoro ya usanii inayoshabihi michoro katika nguo na hata ngoma za kitamaduni za Wakorea. Michoro hiyo ya usanii hushabihi pia mambo ya asili. Wafinyanzi waliunganisha michoro ya milima, miti, maua, samaki, ndege, wadudu, na watu na kufanyiza mandhari nzuri ajabu kwenye vyombo hivyo vya kauri. Mpangilio wa baadhi ya michoro yao yenye mistari imeigwa na michoro ya wafinyanzi wa kisasa.

Sasa acheni tuchunguze rangi zinazotumiwa katika michoro ya kauri. Michoro iligandishwa kwa kauri kwa kutumia rangi nyeusi na nyeupe. Mwanzoni, wafinyanzi wa Koryo waliiga ufundi kutoka China. Lakini punde si punde walianza kubuni michoro yao wenyewe. Kielelezo kimoja maarufu cha ubuni huo ni mbinu ya kugandisha iitwayo sanggam. Katika mbinu hii, mchoro uliochaguliwa huchongwa kwenye chombo ambacho kinafanyiwa kazi, na nakshi hizo kujazwa na udongo mweupe au mwekundu. Kisha chombo huchomwa. Wakati huu udongo mweupe hubaki mweupe kama theluji, lakini udongo mwekundu hugeuka kuwa mweusi.

Uchunguzi wa makini wa chombo hiki cha kauri utaonyesha miatuko laini. Je hii ni kasoro? Miatuko hiyo hutokezwa na nini? Jinsi mchoro ulivyo wenye mambo mengi ndivyo mpako wa kung’arisha uwavyo mwembamba ili mchoro uweze kuonekana wazi. Na kwa sababu mpako huo huwa mwembamba sana na mgumu, miatuko laini hutokea—yakiwa matokeo ya kutafuta urembo wa hali ya juu. Kwa hiyo, miatuko hiyo ikaja kuonwa kuwa sehemu ya asili ya kauri ya Koryo na wala si kasoro. Kwa hakika, hata baadhi ya wafinyanzi wa kisasa hutumia kimakusudi udongo wenye kuatuka.

Jitihada za Kufufua Ufinyanzi wa Kauri za Koryo

Baada ya Korea kuvamiwa na Wamongol mapema katika karne ya 13, ufinyanzi wa kauri za Koryo ulididimia kwa haraka. Hatimaye, wafinyanzi wakaacha kufinyanga vyombo hivyo maridadi, na mbinu zao za usanii zikapotea. Leo, kwa sababu ya bei kubwa ya vyombo vya kauri vya Koryo na pia uhaba wake, wafinyanzi wa kisasa wameazimia kufufua mbinu hiyo. Kwa kuchunguza vigae vya kauri za kale, wafinyanzi wamefaulu kutokeza vyombo vyenye umbo na saizi kama ya vyombo vya kale, na hata wafinyanzi fulani wamedai kwamba wametokeza vyombo vyenye rangi ya kuvutia sana kama kauri ya kale ya Koryo. Hata hivyo, ni vigumu sana kuchanganya udongo wa mfinyanzi ulio sawa na ule wa kale—mchanganyiko uliofanyizwa na vifaa vya asili tu.

Wafinyanzi wa kisasa wanatatizwa pia kuiga mambo mengine, kama vile kujua vyombo hivyo vilichomwa jinsi gani na kwa muda gani. Watafiti katika Vyuo vya Utafiti wa Kauri katika Korea wamefanya majaribio na vifaa mbalimbali wakitumia mbinu mbalimbali katika jitihada ya kufufua rangi yenye kuvutia sana ya kauri ya Koryo.

Katika miaka ya karibuni, vyombo tunu vya kauri ya Koryo vilivyopotea vimegunduliwa. Kwa mfano, katika mwaka wa 1995 mvuvi mmoja aliyekuwa amesikia kwamba vigae vya ufinyanzi vilikuwa vikinaswa kwenye nyavu, aliamua kujaribu kutumia mbinu hiyo. Akiandamana na wavuvi wengine, alianza kutafuta vyombo hivyo vya ufinyanzi. Hatimaye alifaulu kuvua vyombo 129 hivi vya kauri ya Koryo. Kufuatia kufanikiwa kwa wavuvi hao, Ofisi ya Hifadhi za Turadhi ya Korea iliunda kundi la kuchunguza. Waligundua meli iliyokuwa imezama ikiwa na shehena ya vyombo vya kauri, na katika muda wa miezi kadhaa walifaulu kupata vyombo 463! Bila shaka ugunduzi huo uliwasisimua sana watafiti wa kauri na wanahistoria wa usanii.

Kufurahia Usanii wa Kauri ya Koryo Leo

Waweza kufurahiaje umaridadi wa kauri ya Koryo leo? Waweza kuzuru maonyesho ya usanii wa Korea katika majumba ya makumbusho yanayojulikana sana ulimwenguni, kama vile British Museum au Metropolitan Museum of Art huko New York. Licha ya hilo utakapozuru Korea, unaweza kufika kwenye mji wa Kangjin, mahali ambapo idadi kubwa ya tanuru za kale za kauri ya Koryo zinapatikana. Ama waweza kuhudhuria maonyesho ya kauri ya kila mwaka katika Mkoa wa Kyŏnggi. Huko unaweza kujionea kauri ya Koryo ikifinyangwa. Waweza pia kujaribu kufinyanga. Je, waweza kuwazia ukifinyanga chombo wewe mwenyewe, ukitie alama au mchoro, ukichome kwenye tanuru, na hatimaye uwe na chombo kilichomalizika mkononi?

Bila shaka waweza pia kununua kauri ya kisasa ya Koryo katika maduka makubwa au maduka ya kuuzia vitu vya ukumbusho. Humo, jagi za maua, seti za vikombe vya chai, na vyombo vya aina mbalimbali vimeonyeshwa—ama vyombo vilivyofinyangwa na wafinyanzi au vilivyotengenezwa kiwandani. Labda huenda ukapendezwa kuwaandalia wageni wako chai ya Kikorea katika vikombe vya kauri ya Koryo huku jagi yenye maua mengi ikiwa imepamba meza yako.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Jina la kisasa Korea limetokana na jina Koryo.

^ fu. 7 Kiasi cha hewa inayoingia ndani ya tanuru kilipunguzwa na hivyo kutokeza kaboni monoksidi.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Jagi ya awali ya karne ya 12

[Hisani]

The Collection of National Museum of Korea

[Picha katika ukurasa wa 18]

Picha ya kauri ya Koryo ikionyesha mchoro wa pekee