Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jitihada Inayoendelea ya Kutafuta Suluhisho

Jitihada Inayoendelea ya Kutafuta Suluhisho

Jitihada Inayoendelea ya Kutafuta Suluhisho

TANGU kuanzishwa kwake, Shirika la Umoja wa Mataifa limependezwa na watoto na matatizo yanayowakumba. Mwishoni mwa mwaka wa 1946, Shirika hilo lilianzisha Hazina ya Dharura ya Watoto ya Ulimwenguni Pote ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) ikiwa hatua ya muda ya kutunza watoto walio katika maeneo yaliyoharibiwa na vita.

Mnamo mwaka wa 1953 hazina hiyo ya dharura ikabadilishwa kuwa shirika la kudumu. Ijapokuwa sasa linajulikana kama Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa, lingali linatumia herufi za awali, UNICEF. Kwa hiyo, kwa zaidi ya nusu karne, shirika la UNICEF limekuwa likiwaandalia watoto kotekote ulimwenguni chakula, mavazi, na matibabu na limekuwa likijitahidi kutimiza mahitaji ya watoto kwa ujumla.

Mahitaji ya watoto yalikaziwa sana mwaka wa 1959 wakati Shirika la Umoja wa Mataifa lilipokubali Azimio la Haki za Mtoto. (Ona sanduku, kwenye ukurasa wa 5.) Ilitumainiwa kwamba azimio hilo lingewachochea wengi kupendezwa na matatizo ya watoto na kuyasuluhisha kwa kutia moyo umma uunge mkono, kifedha na kwa njia nyinginezo.

Lakini “miaka ishirini baadaye,” chasema kichapo cha Collier’s 1980 Year Book, “‘haki’ hizo—hususan zile zinazohusiana na lishe, afya, na masilahi ya kimwili—bado hazikutimizwa kwa wengi wa watoto wapatao bilioni 1.5 walio duniani.” Hivyo basi kwa sababu ya uhitaji ulioongezeka wa kusuluhisha matatizo ya watoto na kupatana na miradi yake ya azimio, Shirika la Umoja wa Mataifa lilitangaza mwaka wa 1979 kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Mtoto. Mashirika ya kiserikali, kiraia, kidini, na ya kutoa misaada ulimwenguni pote yaliitikia hima-hima jitihada za kutafuta suluhisho.

Je, Ulikuwa “Mzaha Mtupu” Tu?

Jambo la kusikitisha ni kwamba watoto walio katika nchi zinazositawi walikuwa katika hali mbaya wakati wa Mwaka wa Kimataifa wa Mtoto, ikasema ripoti moja ya UNICEF. Mwishoni mwa mwaka huo, takriban watoto milioni 200 walikuwa bado na utapiamlo, na nusu ya watoto wapatao milioni 15 wenye umri usiozidi miaka mitano waliokufa yamkini walikufa kutokana na utapiamlo. Watoto 15 kati ya 100 waliozaliwa kila dakika mwaka huo katika nchi zinazositawi, walikufa kabla ya kufikia umri wa mwaka mmoja. Watoto waliokamilisha elimu ya msingi hawakuzidi asilimia 40. Ikizungumzia ripoti hiyo ya UNICEF, safu ya mhariri katika gazeti la Indian Express ililalamika kwamba Mwaka wa Mtoto uligeuka kuwa “mzaha mtupu.”

Watu fulani mmoja-mmoja walitarajia kutofaulu huko. Mathalani, mwanzoni kabisa mwa mwaka huo, Fabrizio Dentice aliandika hivi katika gazeti la L’Espresso: “Mwaka wa Mtoto hautoshi kusuluhisha matatizo hayo.” Gazeti hilo lilitaarifu hivi: “Mtindo wa maisha wa sasa ndio unaotutumbukiza katika hali hii, huo ndio unaohitaji kubadilishwa.”

Katika jitihada inayoendelea ya kutafuta suluhisho kwa matatizo ya watoto, mkutano wa kimataifa ulifanywa katika makao makuu ya UM mwezi wa Septemba 1990. Ulikuwa mojawapo ya mikutano mikubwa zaidi ya viongozi wa ulimwengu katika historia yote. Zaidi ya viongozi 70 wa serikali walihudhuria. Mkutano huo ulifuatia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, uliokubaliwa Novemba 20, 1989, na kuanza kutekelezwa Septemba 2, 1990. Kufikia mwisho wa mwezi huo, mkataba huo ulikuwa umetiwa sahihi na mataifa 39.

Hivi majuzi shirika la UNICEF lilisema hivi, “Mkataba huo umepata kuwa mkataba mashuhuri sana wa haki za wanadamu kuwahi kukubaliwa, na hivyo kutetea kwa dhati zaidi watoto ulimwenguni pote.” Kwa kweli, kufikia Novemba 1999, Mkataba huo ulikuwa umetiwa sahihi na mataifa 191. Shirika la UNICEF lilijisifu hivi: “Kulikuwa na maendeleo makubwa katika kuzingatia na kutetea haki za watoto katika mwongo uliofuata kuanzishwa kwa Mkataba wa Haki za Mtoto kuliko kipindi kingine chochote katika historia ya mwanadamu.”

Licha ya maendeleo hayo, Rais wa Ujerumani Johannes Rau alichochewa kusema: “Inasikitisha kwamba hata katika nyakati zetu ni lazima tukumbushwe kuwa watoto wana haki.” Au kukumbushwa kwamba wangali na matatizo makubwa! Likikiri mnamo Novemba 1999 kwamba “kungali na mengi ya kufanywa,” UNICEF lilieleza hivi: “Ulimwenguni pote, takriban watoto milioni 12 wenye umri usiozidi miaka mitano hufa kila mwaka, hasa kutokana na mambo yanayoweza kuzuiwa. Watoto wapatao milioni 130 katika nchi zinazositawi hawahudhurii shule za msingi . . . Watoto wapatao milioni 160 wana utapiamlo mbaya au wa kadiri. . . . Watoto wengi wasiotakiwa hutaabika sana katika makao ya yatima na vituo vingine, bila kuelimishwa wala kutunzwa kiafya ifaavyo. Mara nyingi watoto hao hutendewa vibaya kimwili. Takriban watoto milioni 250 wameajiriwa kazi fulani.” Hali kadhalika walitaja watoto milioni 600 wanaoishi maisha fukara pamoja na watoto milioni 13 ambao watampoteza angalau mzazi mmoja kutokana na UKIMWI kufikia mwisho wa mwaka wa 2000.

Yaonekana viongozi wa kisiasa wameshindwa kupata suluhisho lenye kuridhisha kwa matatizo hayo. Lakini, matatizo hayawapati watoto wanaoishi katika nchi zinazositawi peke yake. Katika nchi za Magharibi watoto wengi hukabili matatizo ya aina nyingine.

[Blabu katika ukurasa wa 4]

“Inasikitisha kwamba hata katika nyakati zetu ni lazima tukumbushwe kuwa watoto wana haki”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

Azimio la UM la Haki za Mtoto:

● Haki ya kuwa na jina na kuwa raia wa nchi.

● Haki ya kuonyeshwa shauku, upendo, na uelewevu na kuandaliwa mahitaji ya kimwili.

● Haki ya kupata lishe ya kutosha, makao, na huduma za kitiba.

● Haki ya kutunzwa kwa njia ya pekee iwapo ni mlemavu, iwe kimwili, kiakili, au kijamii.

● Haki ya kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupata ulinzi na msaada chini ya hali zote.

● Haki ya kulindwa dhidi ya aina zote za ukatili, kupuuzwa, na kutumiwa vibaya.

● Haki ya kupewa fursa kamili ya michezo na tafrija na fursa sawa ya kupata elimu ya msingi bila malipo, ili kumwezesha mtoto asitawishe vipawa vyake na kuwa mshiriki wa jamii mwenye manufaa.

● Haki ya kutumia uwezo wake kamili katika mazingira ya uhuru na adhama.

● Haki ya kulelewa kwa njia ya kusitawisha uelewevu, ustahimilivu, na urafiki kati ya watu, amani, na udugu wa ulimwenguni pote.

● Haki ya kufurahia haki hizo bila kujali jamii, rangi, jinsia, dini, maoni ya kisiasa au mengineyo, kabila au taifa, mali, uzawa, au hadhi nyingineyo.

[Hisani]

Summary based on Everyman’s United Nations

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

UN PHOTO 148038/Jean Pierre Laffont▼

UN photo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]

Picha kwenye ukurasa wa 4 na 5 Giacomo Pirozzi/Panos Pictures