Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kukabiliana na Matatizo ya Tezi-kibofu

Kukabiliana na Matatizo ya Tezi-kibofu

Kukabiliana na Matatizo ya Tezi-kibofu

“Nilipokuwa na umri wa miaka 54, nilianza kukojoa mara nyingi na nyakati nyingine kila baada ya dakika 30. Hali hiyo ilinifanya nimwone daktari, na ikagunduliwa kwamba tezi-kibofu yangu ilihitaji kuondolewa.” Visa kama hivyo ni vya kawaida katika kliniki za tezi-kibofu ulimwenguni pote. Mwanamume aweza kufanya nini ili kuepuka magonjwa ya tezi-kibofu? Anahitaji kumwona daktari lini?

TEZI-KIBOFU ni tezi inayoshabihi tunda la mjoho iliyo chini ya kibofu na kuzingira njia ya mkojo. (Ona picha ya nyonga ya mwanamume.) Kwa mwanamume wa kawaida, tezi-kibofu huwa na uzito wa gramu 20 na iliyo kubwa zaidi huwa na kimo cha sentimeta 4, upana wa sentimeta 3, na uhimili wa sentimeta 2. Kazi yake ni kutengeneza umajimaji unaofanyiza takriban asilimia 30 ya shahawa. Umajimaji huu, wenye asidi sitriki, kalisi, na vimeng’enya, huenda ukaboresha mwendo wa shahawa na uwezo wake wa kutungisha mimba. Zaidi ya hayo, umajimaji huo wa tezi-kibofu unatia ndani zinki, ambayo wanasayansi hudhani kwamba huzuia mshipa wa uume kuambukizwa magonjwa.

Jinsi ya Kutambua Tezi-Kibofu Gonjwa

Dalili mbalimbali za magonjwa katika nyonga ya wanaume hutokana na maumivu au uvimbe katika tezi-kibofu. Prostatitis—maumivu katika tezi-kibofu—yaweza kusababisha homa, matatizo ya kukojoa, na maumivu katika mifupa ya nyonga au katika kibofu. Iwapo tezi-kibofu imevimba sana, yaweza kumzuia mgonjwa kukojoa. Ikiwa uvimbe umesababishwa na bakteria, ugonjwa huo unajulikana kama bacterial prostatitis, na unaweza kuwa mkali mno au wa kudumu. Kwa kawaida unahusianishwa na maambukizo katika mrija wa mkojo. Hata hivyo, katika visa vingi, kinachosababisha maumivu hayo hakijulikani, na kwa sababu hiyo ugonjwa huo unajulikana kama prostatitis isiyosababishwa na bakteria.

Matatizo ya kawaida ya tezi-kibofu hutia ndani kukojoa mara nyingi zaidi, kukojoa usiku, mkojo kutoka polepole, na kuhisi kuwa na mkojo daima. Dalili hizo huashiria ugonjwa uitwao benign prostatic hyperplasia (BPH)—uvimbe wa tezi-kibofu usio na kansa—unaoweza kuathiri wanaume wenye umri wa zaidi ya miaka 40. Uwezekano wa kupatwa na BPH huongezeka kadiri umri unavyoongezeka. Unapatikana katika asilimia 25 ya wanaume wenye umri wa miaka 55 na asilimia 50 ya wanaume wenye umri wa miaka 75.

Tezi-kibofu yaweza pia kushambuliwa na uvimbe wenye kansa. Mara nyingi, kansa ya tezi-kibofu hugunduliwa wakati wa kufanyiwa uchunguzi wa kawaida wa kitabibu, hata pasipo dalili za ugonjwa. Katika visa vibaya zaidi, mkojo waweza kukataa kutoka na kuvimbisha kibofu. Iwapo kansa imeenea kwenye viungo vingine, huenda kukawa na maumivu ya mgongo, dalili za ugonjwa wa neva, na kuvimba miguu kwa sababu ya kuziba kwa mfumo wa limfu. Katika mwaka wa hivi karibuni, Marekani pekee iliripoti visa vipya 300,000 hivi vya kansa ya tezi-kibofu na vifo 41,000 vilivyosababishwa na ugonjwa huo. Wanasayansi wanaamini kwamba asilimia 30 ya wanaume wenye umri wa kati ya miaka 60 na 69 na asilimia 67 ya wanaume wenye umri wa kati ya miaka 80 na 89 watapatwa na kansa ya tezi-kibofu.

Nani Wanaoelekea Kupatwa na Ugonjwa Huo?

Uchunguzi unafunua kwamba uwezekano wa kupatwa na kansa ya tezi-kibofu huongezeka haraka sana baada ya umri wa miaka 50. Katika Marekani, aina hii ya kansa inawapata wanaume wa asili ya Kiafrika mara mbili zaidi ya wanaume wazungu. Idadi ya watu wenye ugonjwa huo hutofautiana kote ulimwenguni, ikiwa juu sana katika Amerika Kaskazini na nchi za Ulaya, idadi ya kadiri katika Amerika Kusini, na idadi ndogo katika Asia. Jambo hilo ladokeza kwamba huenda mazingira au ulaji ukasababisha kusitawi kwa kansa ya tezi-kibofu. Hivyo, iwapo mwanamume ahamia nchi yenye visa vingi, huenda hatari ya kupatwa na ugonjwa huu ikaongezeka.

Wanaume walio na watu wa ukoo wenye kansa ya tezi-kibofu wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupatwa na ugonjwa huu. Kulingana na Shirika la Kansa la Marekani, “ikiwa baba yako au ndugu yako ana kansa ya tezi-kibofu, basi uwezekano wa wewe kupatwa na ugonjwa huu unaongezeka maradufu.” Baadhi ya mambo yenye kuhatarisha ni uzee, jamii, taifa, historia ya kitiba ya familia, chakula, na kutofanya mazoezi. Wanaume wanaokula chakula chenye mafuta mengi na ambao hukaa kitako wako katika hatari zaidi ya kupatwa na kansa ya tezi-kibofu.

Kuzuia Magonjwa ya Tezi-Kibofu

Ingawa wanasayansi hawajui hasa kisababishi cha kansa ya tezi-kibofu, wanaamini kwamba chembe za urithi na homoni huenda zikasababisha ugonjwa huo. Jambo la kufurahisha ni kwamba tunaweza kudhibiti mambo mawili yanayohatarisha kupatwa na ugonjwa huu—chakula na kutofanya mazoezi. Shirika la Kansa la Marekani lapendekeza “upunguze kula vyakula vyenye mafuta mengi yanayotoka kwa wanyama na kula vyakula vinavyotokana na mimea.” Shirika hilo lapendekeza pia kula “angalau matunda na mboga mara tano kila siku” kutia ndani mkate, nafaka, pasta, bidhaa nyingine za nafaka, wali na maharagwe. Nyanya, balungi, na matikiti maji yana dutu za karotini—zinazozuia kuharibiwa kwa chembe na huenda zikapunguza hatari ya kupatwa na kansa ya tezi-kibofu. Wataalamu fulani hudai pia kwamba aina fulani ya mitishamba na madini huenda yakawa na matokeo mazuri.

Shirika la Kansa la Marekani na Shirika la Urolojia la Marekani yaamini kwamba kupimwa kansa ya tezi-kibofu kwaweza kuokoa maisha. Matibabu yataelekea kufaulu iwapo kansa inagunduliwa mapema. Shirika la Kansa la Marekani lapendekeza wanaume wenye umri unaozidi miaka 50, au 45 katika vikundi vilivyo hatarini zaidi, wafanyiwe uchunguzi wa kitiba kila mwaka. *

Uchunguzi wapasa utie ndani kupimwa kwa antijeni hususa za tezi-kibofu katika damu (PSA). Antijeni hiyo ni protini inayofanyizwa katika chembe za tezi-kibofu. Na kiwango chake huongezeka kukiwa na magonjwa ya tezi-kibofu. Shirika la Kansa la Marekani lasema kwamba “iwapo kiwango chako cha antijeni ya tezi-kibofu (PSA) si cha kawaida, mwombe daktari akueleze uwezekano wa kupatwa na kansa na uhitaji wa kufanyiwa uchunguzi zaidi.” Uchunguzi wa mkundu kwa kutumia kidole (DRE–digital rectal exam), hutiwa ndani pia. Kwa kutia kidole ndani ya mkundu wa mgonjwa, daktari aweza kutambua hali isiyo ya kawaida katika tezi-kibofu, kwa kuwa tezi hiyo iko upande wa mbele wa mkundu. (Ona picha ya nyonga ya mwanamume kwenye ukurasa wa 20.) Uchunguzi wa mkundu kwa sauti-mno (TRUS) ni muhimu “iwapo PSA au DRE yaonyesha kuna kasoro fulani” na daktari ahitaji kuamua kama atapendekeza uchunguzi wa kisehemu cha tezi-kibofu ufanywe. Uchunguzi huu ni wa dakika 20 hivi.

Zaidi ya kugundua kansa ya tezi-kibofu, uchunguzi wa kila mwaka wa urolojia waweza kugundua mapema kuwepo kwa ugonjwa wa BPH, uliotajwa mwanzoni, jambo hilo litazuia kutumika kwa tiba yenye kuumiza. (Ona sanduku “Tiba Mbalimbali za BPH.”) Mwenendo safi kiadili ni ulinzi dhidi ya magonjwa yenye kupitishwa kingono, ambayo yanaweza kusababisha magonjwa ya tezi-kibofu.

Bila shaka kuna uhitaji wa kutunza na kulinda tezi-kibofu yako. Mwanamume aliyetajwa mwanzoni wa makala hii alieleza kwamba amepona kabisa baada ya upasuaji. Yeye anaonelea kwamba “wanaume wote wapasa kufanyiwa uchunguzi wa kitiba wa kila mwaka unaonuiwa kuzuia ugonjwa huo,” hata kama hawana dalili zozote za ugonjwa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Ikiwa uko katika kikundi hiki, unaweza kusoma habari katika sanduku “Fahirisi ya Dalili za Ugonjwa wa Benign Prostatic Hyperplasia (BPH).”

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

Fahirisi ya Dalili za Ugonjwa wa Benign Prostatic Hyperplasia (BPH)

Maagizo: Jibu maswali yafuatayo kwa kutia duara nambari ifaayo.

Maswali namba 1 hadi 6 yatajibiwa:

0—Hakuna

1—Chini ya mara 1 kati ya 5

2—Chini ya nusu ya wakati

3—Takriban nusu ya wakati

4—Zaidi ya nusu ya wakati

5—Takriban wakati wote

1. Katika mwezi uliopita, ni mara ngapi ulihisi kwamba mkojo haukutoka kabisa baada ya kumaliza kukojoa? 0 1 2 3 4 5

2. Katika mwezi uliopita, ni mara ngapi umelazimika kukojoa tena baada ya kuwa umekojoa muda usiozidi saa mbili? 0 1 2 3 4 5

3. Katika mwezi uliopita, ni mara ngapi umeona kwamba mkojo umejikata-kata ulipokuwa ukikojoa? 0 1 2 3 4 5

4. Katika mwezi uliopita, ni mara ngapi ulishindwa kuzuilia mkojo? 0 1 2 3 4 5

5. Katika mwezi uliopita, ulikojoa mara ngapi kwa njia hafifu? 0 1 2 3 4 5

6. Katika mwezi uliopita, ni mara ngapi ulihitaji kulazimisha mkojo? 0 1 2 3 4 5

7. Katika mwezi uliopita, ni mara ngapi, kwa wastani, ulilazimika kuamka ili kukojoa, kuanzia wakati ulipolala hadi kuamka asubuhi? (Tia duara mara ulizofanya hivyo.) 0 1 2 3 4 5

Jumla ya nambari zilizotiwa duara ndiyo kiwango cha dalili za ugonjwa wa BPH ulizo nazo. Kidogo: 0-7; Kadiri: 8-19; Mbaya Sana: 20-35.

[Hisani]

From the American Urological Association

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Tiba Mbalimbali za BPH

DAWA: Aina mbalimbali za dawa hutumiwa, ikitegemea dalili za kila mgonjwa. Ni daktari wako pekee anayepaswa kukupa maagizo ya dawa hizo.

KUCHUNGUZWA KWA UANGALIFU: Mgonjwa achunguzwa kitiba mara kwa mara na hatumii dawa.

UPASUAJI:

(a) Katika upasuaji wa sehemu ya tezi-kibofu kupitia mrija wa mkojo (TURP), daktari-mpasuaji huingiza kupitia mrija wa mkojo chombo chenye ukanda wa umeme (resectoscope) ambao hukata tishu na kufunga mishipa ya damu. Hakuna upasuaji wa nje unaohitajika. Upasuaji huo ni wa dakika 90 hivi. Upasuaji huo hauna athari kama upasuaji wa kawaida.

(b) Upasuaji wa tezi-kibofu kupitia mrija wa mkojo (TUIP) wafanana na ule wa TURP. Hata hivyo, upasuaji huu hutia ndani kupanua mrija wa mkojo kwa kufanya mikato kadhaa midogo mahali ambapo mrija wa mkojo unapoungana na kibofu na katika tezi-kibofu pia.

(c) Upasuaji wa kawaida hufanywa iwapo upasuaji kupitia mrija wa mkojo hauwezi kufanywa kwa sababu tezi-kibofu imevimba sana. Upasuaji wa kawaida hulazimu sehemu ya nje kukatwa.

(d) Upasuaji wa leza hutumia miali ya leza ili kuyeyusha tishu yoyote inayoziba tezi-kibofu.

Mgonjwa ahitaji kuamua binafsi aina ya tiba atakayopendelea. Ripoti ya karibuni katika gazeti la The New York Times ilisema kwamba baadhi ya wataalamu wanasita hata kufanya uchunguzi wa kansa ya tezi-kibofu, hasa katika wanaume wazee sana, kwa sababu “ugonjwa huenda ukasitawi polepole bila kutokeza madhara makubwa kwa afya ilhali tiba yake mara nyingi huwa na athari mbaya sana.”

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Maswali ya Kumwuliza Daktari Wako Kabla ya Upasuaji

1. Unapendekeza aina gani ya upasuaji?

2. Kwa nini nahitaji upasuaji huo?

3. Je, kuna aina nyingine ya tiba iliyo badala ya upasuaji?

4. Upasuaji huu una manufaa zipi?

5. Upasuaji huu una athari zipi? (Kwa mfano, kuvuja damu au kutoweza kufanya ngono)

6. Matokeo yatakuwa nini nisipofanyiwa upasuaji huu?

7. Naweza kupata wapi maoni ya ziada?

8. Una uzoefu mkubwa kadiri gani wa kufanya upasuaji huu bila kutia damu mishipani?

9. Upasuaji utafanyiwa wapi? Je, madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo wanaheshimu haki za mgonjwa kuhusu utiaji-damu mishipani?

10. Nitahitaji aina gani ya unusukaputi? Je, mtaalamu wa nusukaputi ana uzoefu wa upasuaji bila kutia damu mishipani?

11. Itanichukua muda gani kupona?

12. Upasuaji utagharimu pesa ngapi?

[Mchoro katika ukurasa wa 20]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mchoro wa nyonga ya mwanamume

Kibofu

Tezi-kibofu

Mkundu

Mrija wa mkojo

[Picha katika ukurasa wa 23]

Chakula chenye afya na mazoezi ya kiasi yaweza kupunguza hatari ya kupata kansa ya tezi-kibofu