Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Watoto Wanastahili Kupendwa na Kuthaminiwa

Watoto Wanastahili Kupendwa na Kuthaminiwa

Watoto Wanastahili Kupendwa na Kuthaminiwa

“MWONYESHE mtoto upendo kidogo, naye atakuonyesha mwingi zaidi.” Ndivyo alivyoandika John Ruskin, mwandishi na mchambuzi Mwingereza wa karne ya 19. Huenda wazazi wengi wakakubali kwamba inanufaisha kuwapenda watoto wako, si kwa sababu tu watakupenda lakini hasa kwa sababu upendo wako utakuwa na matokeo mazuri.

Mathalani, kitabu Love and Its Place in Nature kilisema kwamba bila upendo “watoto huelekea kufa.” Naye Ashley Montagu, mwanthropolojia mashuhuri aliyezaliwa Uingereza, alifikia hatua ya kusema: “Mtoto asiyependwa ni tofauti sana kibiokemia, kifiziolojia, na kisaikolojia na yule anayependwa. Yule asiyependwa hata hukua kwa njia tofauti sana na yule anayependwa.”

Gazeti la Toronto Star liliripoti juu ya uchunguzi mmoja uliofikia mkataa kama huo. Lilisema hivi: “Watoto wanaolelewa bila kukumbatiwa kwa ukawaida, kuguswa au kutomaswa kwa pongezi . . . wana kiasi kikubwa isivyo kawaida cha homoni za mkazo.” Kwa kweli, kutojali hali yao ya kimwili wakati wa utoto “kwaweza kuathiri vibaya na kwa muda mrefu uwezo wao wa kujifunza na kumbukumbu lao.”

Uchunguzi huo unakazia uhitaji wa kuwapo kwa wazazi. La sivyo, mzazi atasitawishaje uhusiano madhubuti kati yake na mtoto? Lakini inasikitisha kwamba hata katika sehemu zenye utajiri ulimwenguni, mwelekeo uliopo sasa ni kumwandalia mtoto mahitaji yake bila wazazi kuwapo. Watoto huagizwa waende shuleni, shule ya Jumapili, waende kufanya kazi, waende kwenye kambi za watoto za michezo, na kupewa fedha na kuambiwa waende sehemu za tafrija. Mamilioni ya watoto ambao huwa wametengwa mbali na kiini cha familia na kuachwa peke yao, kwa asili huanza kuhisi—hata bila kusema—wamepuuzwa tu, hawathaminiwi, na hawapendwi, na kuhisi wamezingirwa na jumuiya ya watu wazima wasiojali. Hisia hiyo iliyoenea miongoni mwa watoto yaweza kuwa kisababishi cha kuwapo kwa takriban watoto 3,000 wa mitaani huko Berlin. Kielelezo halisi cha jambo hilo ni kijana aitwaye Micha, yeye alisema hivi: “Hakuna mtu aliyenihitaji tena.” Vivyo hivyo kijana mmoja Mjerumani mwenye umri wa miaka tisa alilalamika hivi: “Laiti ningekuwa mbwa wetu.”

Kuna Njia Nyingi za Kuwatendea Watoto Vibaya

Kutowajali watoto ni njia moja ya kuwatendea vibaya inayoonyesha ukosefu wa kile kinachoitwa na Biblia “shauku ya kiasili.” (Waroma 1:31; 2 Timotheo 3:3) Kwaweza kuongoza kwenye njia mbaya hata zaidi za kuwatendea vibaya. Mathalani, tangu Mwaka wa Kimataifa wa Mtoto mnamo 1979, uangalifu mkubwa umeelekezwa kwa matatizo ya kuwatendea watoto vibaya kimwili na kingono. Bila shaka, si rahisi kukusanya takwimu sahihi, na isitoshe hali hutofautiana kila mahali. Lakini hapana shaka yoyote kwamba makovu ya kutendewa vibaya kingono wakati wa utoto hayawezi kupona kwa urahisi wanapokuwa watu wazima.

Kutendewa vibaya kwa njia yoyote ile huwafanya watoto waone kwamba hawapendwi wala kuthaminiwa. Na yaonekana tatizo hilo linaongezeka. Kwa mujibu wa gazeti la Ujerumani Die Welt, “watoto wengi zaidi na zaidi wanakomaa na kuwa wasiojiweza kijamii.” Laongezea hivi: “Watoto hukosa makao yenye uchangamfu. Kulingana na [Gerd Romeike, mkurugenzi wa kituo cha kuwaelekeza watoto huko Hamburg], uhusiano wa kihisia-moyo baina ya watoto na wazazi unadhoofika zaidi, au hata haupo kabisa. Watoto kama hao huhisi hakuna anayewajali, na hamu yao ya kupata ulinzi hukosa kutimizwa kabisa.”

Watoto wanaonyimwa haki ya kupendwa na kuthaminiwa waweza kuwa na uchungu, nao waweza kudhihirisha mfadhaiko wao kuelekea wale wasiowajali au labda kuelekea jamii nzima. Mwongo mmoja kamili uliopita, ripoti moja ya kikosi maalum cha Kanada ilikazia uhitaji wa kuchukuliwa kwa hatua mara moja la sivyo kizazi kizima “kinachofikiri jamii haiwajali” kitaharibika.

Vijana wasiopendwa wala kuthaminiwa waweza kushawishiwa kutoroka nyumbani ili kuepuka matatizo yao, na kutumbukia katika matatizo makubwa zaidi katika miji yenye kujaa uhalifu, dawa za kulevya, na ukosefu wa adili. Kwa kweli, zaidi ya miaka 20 iliyopita, polisi walikadiria kwamba watoto watoro wapatao 20,000 wenye umri usiozidi miaka 16 walikuwa wakiishi kwenye eneo moja tu la jijini nchini Marekani. Walitajwa kuwa “mazao ya familia zilizovunjika na ukatili, uliosababishwa mara nyingi na wazazi ambao ni waraibu wa vileo au dawa za kulevya. Wao hufanya ukahaba ili kujiruzuku kisha, baada ya kupigwa na makuwadi na kudhalilishwa, huishi kwa hofu ya kushambuliwa endapo watajaribu kutoroka magenge hayo.” Inasikitisha kwamba hali hiyo yenye kuchukiza ingali yaendelea licha ya jitihada za moyo mnyofu za kuibadili.

Watoto wanaokua katika hali zilizotajwa hapo juu huwa watu wazima wasio na usawaziko, mara nyingi hushindwa kuwalea watoto wao wenyewe ifaavyo. Kwa sababu ya kutopendwa na kutothaminiwa, baadaye wao huwa na watoto wenye sifa kama zao—wanaohisi hawathaminiwi wala kupendwa. Mwanasiasa Mjerumani alieleza hivi kinagaubaga: “Watoto wasiopendwa huwa watu wazima wenye chuki kali.”

Bila shaka, mamilioni ya wazazi wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba watoto wao wanajua kwamba wanathaminiwa na wanapendwa. Mbali na kuwaambia hivyo, wao huthibitisha hilo kwa kuwatunza watoto wao kwa upendo na kupendezwa nao kibinafsi kama anavyostahili kila mtoto. Hata hivyo, matatizo yangalipo—matatizo ambayo kwa wazi hayawezi kusuluhishwa na mzazi mmoja-mmoja. Kwa mfano, katika sehemu fulani ulimwenguni, mifumo ya kiuchumi na ya kisiasa ya wanadamu wasio wakamilifu hushindwa kuwaandalia watoto matibabu ifaavyo, elimu ya kutosha, na chakula cha kutosha, hali kadhalika kuwalinda kutokana na tatizo kubwa la ajira ya watoto na hali mbaya za kuishi. Na mara nyingi hali hizo huchochewa na pupa, ufisadi, ubinafsi, na watu wazima wasiojali.

Katibu-mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alitaja baadhi ya matatizo makuu yanayowakabili watoto leo alipoandika hivi: “Mamilioni ya watoto wanaendelea kunyong’onyea ndani ya ufukara wenye kudhalilisha na kuumiza; mamia ya maelfu huteseka kutokana na athari za mapambano na michafuko ya kiuchumi; makumi ya maelfu hulemazwa vitani; wengi zaidi ni yatima au hufa kutokana na UKIMWI.”

Lakini si habari yote isiyopendeza! Mashirika ya UM, kama vile Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) na Shirika la Afya Ulimwenguni, yamejitahidi sana kuboresha hali ya watoto. Annan alisema: “Watoto wengi wanazaliwa wakiwa na afya na wengi wanakingwa na maradhi; wengi wanaweza kusoma na kuandika; wengi wako huru kujifunza, kucheza na kuishi maisha ya kawaida kuliko ilivyodhaniwa hata miongo michache iliyopita.” Hata hivyo, alionya hivi: “Huu si wakati wa kuridhika na mafanikio tuliyokwisha kutimiza.”

Wale Wanaostahili Uangalifu wa Pekee

Baadhi ya watoto wanastahili uangalifu wa pekee. Mapema katika miaka ya 1960, ulimwengu ulishtuka kusikia ripoti kutoka kwa zaidi ya nchi 12 kuhusu kuzaliwa kwa maelfu ya wale wanaoitwa watoto wenye kasoro ya thalidomide. Wanawake wajawazito walipotumia dawa ya thalidomide ambayo hutuliza maumivu na kuleta usingizi, ilitokeza athari zisizotarajiwa zilizowafanya wajifungue watoto wasio na viungo au wenye viungo vilivyodhoofika kabisa. Mikono na miguu kwa kawaida ilishabihi vikono vya nyangumi tu.

Miongo minne baadaye, chombo kinachoelekea kuwalemaza watoto ni bomu linalotegwa ardhini. * Watu fulani wanakadiria kwamba takriban mabomu hatari ya ardhini milioni 60 hadi milioni 110 yamesambaa ulimwenguni pote. Watu wapatao 26,000 huuawa au kulemazwa kila mwaka—kutia ndani watoto wengi. Tangu mwaka wa 1997, Jody Williams aliposhinda Tuzo ya Amani ya Nobeli kwa ajili ya kampeni yake ya kupiga marufuku mabomu ya kutegwa ardhini, tatizo hilo limekaziwa fikira sana. Lakini sehemu zilizotegwa mabomu ya ardhini bado ziko. Mwanasiasa mmoja Mjerumani alisema hivi kuhusu jitihada za kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini ulimwenguni pote: “Ni kama kujaribu kuzoa maji kutoka kwenye birika kubwa la kuogea kwa kijiko cha chai huku maji yakitiririka kutoka mferejini.”

Kikundi kingine cha watoto wanaohitaji uangalifu wa pekee ni wale wasio na wazazi. Yehova Mungu, Muumba wa mwanadamu, alikusudia watoto walelewe na kutunzwa kwa upendo na mama na baba. Mtoto anahitaji na anastahili kulelewa kwa njia hiyo yenye usawaziko.

Makao ya yatima na mashirika ya kuwatafutia watoto wazazi walezi hujaribu kushughulikia mahitaji ya watoto wasio na wazazi wote wawili. Hata hivyo, inasikitisha kwa kuwa baadhi ya watoto wenye mapendeleo haba, wanaohitaji sana wazazi walezi ndio wanaopuuzwa zaidi mara nyingi—wale walio wagonjwa, wenye matatizo ya kusoma, walemavu, au wa asili ya kigeni.

Mashirika yameanzishwa ili kuwatia moyo watu kuchanga fedha kwa kawaida na hivyo “kuwa mzazi mlezi” wa mtoto anayeishi katika nchi maskini. Fedha zinazochangwa zinatumiwa kumwelimisha mtoto huyo au kumwandalia mahitaji ya lazima ya maisha. Wakipenda, wanaweza kutumiana picha na barua ili kuimarisha uhusiano wao. Ingawa mpango huo unasaidia sana, si suluhisho madhubuti kwa tatizo hilo.

Mfano mwingine wa kupendeza wa hatua ambayo imechukuliwa kuwasaidia watoto wasio na wazazi ni shirika ambalo mnamo mwaka wa 1999, lilisherehekea nusu karne tangu kuanzishwa kwake.

Makao ya Watoto ya SOS

Mnamo mwaka wa 1949, Hermann Gmeiner alianzisha kile alichokiita Makao ya Watoto ya SOS, huko Imst, Austria. Kutoka mwanzo huo mdogo, shirika lake limesitawi na kuwa na vijiji maalum 1,500 hivi vya watoto na makao mengine kama hayo katika nchi 131 za Afrika, Amerika, Asia, na Ulaya.

Gmeiner alitumia kanuni nne za msingi katika kazi yake—mama, ndugu, nyumba, na kijiji. “Mama” ndiye msingi wa “familia” ya watoto watano au sita—labda hata zaidi. Anaishi nao na kujaribu kuwaonyesha upendo na utunzaji unaotarajiwa kutoka kwa mama mzazi. Watoto huishi pamoja katika “familia” moja na “mama” yuleyule hadi wakati uwadiapo wa kutoka “nyumbani.” “Familia” hiyo ina watoto wenye umri mbalimbali. Wakiwa na “ndugu” na “dada” wenye umri mkubwa na mdogo, watoto hujifunza kuwajali wengine, na hivyo kuwasaidia waepuka kuwa na ubinafsi. Jitihada hufanywa ili watoto hao waje kuwa sehemu ya “familia” wakiwa wachanga iwezekanavyo. Ndugu na dada wa kimwili huwekwa pamoja kwenye “familia” moja.

Vijiji huwa na “familia” 15 hivi, kila familia ikiishi katika nyumba yake. Watoto wote huzoezwa kumsaidia “mama” yao kwa kufanya kazi muhimu za nyumbani. Japo huenda wasiwe na baba, mpango hufanywa wa kupata msaada kutoka kwa mwanamume fulani ambaye hutoa ushauri wa baba na nidhamu inayohitajiwa. Watoto hao huhudhuria shule za karibu. Kila “familia” hupokea kiasi hususa cha fedha kila mwezi ili kulipia gharama zake. Chakula na mavazi hununuliwa madukani. Lengo ni kuwaweka watoto hao katika maisha halisi ya familia pamoja na matatizo yake yote na shangwe yake, na hivyo kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida kadiri iwezekanavyo. Hilo huwatayarisha kuwa na familia zao wenyewe wanapokuwa watu wazima.

Jitihada za Kutafuta Suluhisho Bora

Mashirika ya kuwatafutia watoto wazazi walezi, makao ya yatima, Vijiji vya Watoto vya SOS, UNICEF, na mashirika au vikundi vingine kama hivyo hutimiza wajibu muhimu vinapojaribu kuwasaidia watoto wenye mapendeleo haba. Lakini hakuna shirika hata moja linaloweza kupinga uhakika wa kwamba baadhi ya watu wana mapendeleo haba. Hata wakipenda, hawawezi kumpa mtoto mlemavu viungo vya mwili vyenye afya, hawawezi kurekebisha akili ya mtoto mwenye akili punguani, kumrudisha tena mtoto kwa wazazi wake waliotengana au kutalikiana, au kumrejesha kwenye kumbatio lenye upendo la mzazi wake aliyekufa.

Hata wakijaribu jinsi gani, wanadamu hawawezi kusuluhisha matatizo ya watoto kwa njia bora. Lakini yatasuluhishwa! Naam, na huenda itakuwa karibuni zaidi ya uwezavyo kutarajia. Lakini jinsi gani?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 17 Ona mfululizo “Mabomu ya Ardhini—Ni Nini Kinachoweza Kufanywa?” kwenye toleo letu la Mei 8, 2000.

[Picha katika ukurasa wa 8]

Mtoto anahitaji na anastahili upendo wa wazazi wote wawili