Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Yellowstone Chimbuko la Maji, Mwamba, na Moto

Yellowstone Chimbuko la Maji, Mwamba, na Moto

Yellowstone Chimbuko la Maji, Mwamba, na Moto

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Marekani

Unapozungumza juu ya sehemu za kwanza na zilizo bora kupita zote—hifadhi ya kitaifa ya kwanza ulimwenguni, chemchemi ya maji moto inayofikia kimo cha juu zaidi na iliyo maarufu zaidi ulimwenguni, na ziwa la milimani lililo kubwa zaidi huko Amerika Kaskazini. Haikosi unazungumza juu ya Yellowstone.

HUKU tukiwa na hamu nyingi sana mimi na mke wangu tuliendesha gari hadi kwenye lango la kaskazini la Hifadhi ya Kitaifa ya Yellowstone huko Wyoming, Marekani. Tangu utotoni, jina Mkongwe Mwaminifu na maneno kama vile “chemchemi ya maji moto” na “bubujiko la maji moto” yalituvutia sana. Je, tungeona tuliyotarajia?

Kwenye lango kuu la kuingilia kwenye hifadhi, tuliona tao kubwa la jiwe. Sehemu yake ya juu ilikuwa na maandishi haya: “Kwa manufaa na furaha ya watu.” Hifadhi ya Yellowstone iliyofunguliwa mnamo mwaka wa 1872, ilikuwa hifadhi ya kitaifa ya kwanza ulimwenguni.

Tulianzia kwa Chemchemi Kubwa Mno za Maji Moto, ng’ambo tu ya mpaka kutoka Montana. Tuliweza kuona wazi kwamba joto kutoka duniani lilikuwa likifanya kazi kubwa sana. Maji yalichemka na kububujika kutoka katika vidimbwi na mabonde. Mawingu makubwa ya mvuke yaliibuka nyufani. Matuta ya madini ya rangi ya waridi yanayoitwa travertine yalishabihi nta ya mshumaa inayotiririka.

Ni Nini Kinachochemka Chini ya Yellowstone?

Hifadhi ya Yellowstone ina chemchemi 10,000 hivi za maji moto zenye kustaajabisha. Mpaka wa Mabara * hugawanya uwanda wa juu wa Milima ya Rocky. Maji hutiririka kuelekea magharibi na mashariki na pia hupenya ardhini. Tulijifunza kwamba maji hayo yanayopenya ardhini ndiyo yanayotokeza maajabu katika Yellowstone. Wakati mmoja milipuko mikali ya volkano ilisambaratisha uwanda huo. Maelfu ya miaka iliyopita, mlipuko mmoja mkali wa volkano uliacha shimo kubwa sana lenye upana wa kilometa 75 kwa kilometa 45. Mwamba ulioyeyuka, au magma, ambao ungali chini ya ardhi unachemsha Yellowstone.

Mabango ya maelezo yaliyo katika hifadhi hiyo yanaeleza kwamba maji yaliyo juu hupenya polepole miamba yenye vitundu hadi kwenye tabaka la mwamba ulio moto kupindukia, juu tu ya magma. Humo maji husukumwa nje tena. Joto hilo husukuma maji juu. Vikwazo vilivyo mwambani vinapozuia maji moto kupanda juu, msongamano wa maji huzidi na kufanyiza chemchemi ya maji moto. Mahali pengine unyevu hutoka ukiwa mvuke. Nyufa hizo ndogo huitwa fumarole. Matope hububujika kwenye vidimbwi ambako gesi za asidi na maji hugeuza udongo kuwa matope na udongo wa mfinyanzi. Ni mandhari yenye kustaajabisha kama nini!

Mkongwe Mwaminifu

Tulipoona kuchemka kwa maji moto ardhini kwenye Chemchemi Kubwa Mno za Maji Moto, tulikisia kwamba tulikuwa karibu sana na chemchemi maarufu ya maji moto ya Mkongwe Mwaminifu. Lakini tulipochunguza ramani yetu ya usafiri tuligundua kwamba chemchemi ya Mkongwe Mwaminifu ilikuwa kilometa 80 upande wa kusini. Hifadhi ya Yellowstone ni kubwa zaidi ya tulivyowazia; ina ukubwa wa ekari milioni 2.2.

Ili kufika palipo na Mkongwe Mwaminifu, tulifuata njia inayopinda-pinda kuelekea magharibi mwa hifadhi hiyo; njiani watalii huona mabonde matano ya chemchemi za maji moto. Punde si punde tulianza kuzoea harufu ya salfa na mawingu ya mvuke yenye kupaa hewani.

Sawa na mamilioni ya watu waliozuru Mkongwe Mwaminifu kabla yetu, tulitaka kujua wakati ambapo chemchemi hiyo ingeanza kufoka. Daima tulifikiri kwamba ilifoka kwa ukawaida mahususi—baada ya kila dakika 57 kamili. Lakini tulipotazama huku na huku, tuliona ishara inayosema kwamba chemchemi hiyo ilikisiwa kufoka tena karibu saa 6:47 alasiri. Muda unaozidi saa nzima ungepita, na huo ulikuwa wakati wa kukisiwa tu! Tulimuuliza Rick, askari wa hifadhi, kuihusu.

“Muda barabara wa kufoka kwa Mkongwe Mwaminifu haujulikani,” akasema. “Wakati wa kufoka hubadilika-badilika kila mara, na umeongezeka kadiri miaka inavyopita kwa sababu ya matetemeko ya ardhi na kwa sababu watu wasiojali hutupa takataka kwenye tundu lake. Leo hufoka baada ya kila dakika 80 hivi kwa wastani. Wafanyakazi wetu wanaweza tu kukisia mfoko mmoja baada ya mwingine.”

Sasa iliwadia saa 6:30 alasiri. Tulitembea kuelekea Mkongwe Mwaminifu ili kuona mfoko uliokisiwa kutokea. Mamia ya watu waliketi kwenye eneo la watazamaji au walikuwa wakielekea huko. Tulisubiri mfoko wa Mkongwe Mwaminifu kwa dakika kumi. Lakini chemchemi hiyo ilipofoka, ilikuwa na umaridadi ambao hauwezi kuonyeshwa na picha iwayo yote. Baada ya kububujika mara kadhaa kana kwamba kuondoa uchafu kooni, chemchemi hiyo ilizidisha kasi. Kila mtu alipiga makofi. Mfoko huo wa maji ulidumu kwa dakika tatu hivi, lililotupendeza zaidi ni kwamba kilele cha maji kilifika juu sana. Maji na manyunyu hayo yalikuwa yakiporomoka hatua kwa hatua huku yakifikia kimo cha meta 37 hadi meta 46. Mwangaza wa jua ulipenya manyunyu hayo na kusambaratika kwa maumbo mbalimbali.

Mfoko ulipotulia tulirejea kwenye ukumbi wa hoteli iliyo karibu. Lakini chemchemi ya Mkongwe Mwaminifu iliendelea kudhihirisha kuwapo kwake. Kwa siku nzima, wakati ilipokisiwa kufoka ulipokaribia, wageni wote waliacha shughuli zao na kutoka nje ili kuona mfoko huo. Tuliona mifoko kadhaa yenye ukubwa na kimo na umaridadi mbalimbali, hususan mmoja ambao maji yake yaliyumbayumba katika mwangaza wa machweo. Tulijionea wenyewe kuwa chemchemi hiyo kongwe ya maji moto ni aminifu kwelikweli.

“Duniani kote kuna chemchemi za maji moto zisizozidi 500, na takriban 300 kati yake ziko katika Hifadhi ya Yellowstone,” akatuambia Rick, askari wa hifadhi. “Na chemchemi 160 kati yake ziko katika bonde hili dogo, Bonde la Juu la Chemchemi za Maji Moto, lenye urefu wa kilometa mbili tu. Chemchemi nyingine za maji moto hutokea na kutokomea—hutenda au ni bwete—lakini chemchemi ya Mkongwe Mwaminifu ingalipo.” Hata hivyo, jirani ya Mkongwe Mwaminifu, chemchemi ya Grand, hurusha maji kufikia kimo cha meta 60. Chemchemi ya Steamboat yaweza kurusha maji meta 120, mara tatu ya kimo cha Mkongwe Mwaminifu—lakini yaweza kubaki bwete kwa miaka mingi. Chemchemi iitwayo Echinus, katika bonde la Norris, mara kwa mara huwanyunyizia watazamaji maji vuguvugu.

Kumkimbia Nyati

Asubuhi iliyofuata tuliipitia broshua moja ya watalii. Ilisema: “Chini ya matabaka membamba ya udongo yenye kuvunjika kwa urahisi, mna vidimbwi vya maji moto sana; maji yaliyomo ni moto kupita kiasi. Kila mwaka, wageni wanaozurura ovyoovyo kwenye maeneo yenye vidimbwi vya maji moto hutumbukia humo na kuchomeka vibaya sana na wengine hufa.” Broshua nyingine ya watalii ilisema: “Onyo: Wageni wengi wamepigwa pembe na nyati. Nyati anaweza kuwa na uzito wa kilogramu 900 naye aweza kukimbia kwa kasi ya kilometa 50 kwa saa, mara tatu zaidi ya unavyoweza kukimbia.” Tulitumaini kwamba hatungekutana na nyati na kulazimika kumkimbia!

Wanyama hupishwa njia katika Yellowstone. Mnyama anapotokea, magari husimama mara moja, kunakuwa na misongamano ya magari mahali pasipotazamiwa. Msongamano mmoja ulikuwa unakwisha tulipowasili tu, na watalii walikuwa wakirejea kwenye magari yao. Tulipomwuliza mwanamke mmoja umati huo ulikuwa ukitazama nini, yeye alisema: “Kongoni dume mkubwa wa Amerika, lakini ameenda.”

Baadaye tuliwaona kulungu wa Ulaya wakijaribu kuwabembeleza ndama wao wa majuma mawili wavuke kijito. Walikuwa wakielekea kwenye hifadhi ya chini kutoka milimani ambako waliishi wakati wa majira ya baridi. Ndama hao hawakutaka kwenda—hawakuwa tayari kuvuka maji. Mama hao waliendelea kuwasihi ndama wao, na hatimaye wakavuka.

“Uduni Wangu, Kutojiweza Kwangu”

Kisha tukaendesha gari kuelekea Korongo Kuu la Yellowstone. Tulishuka garini sehemu mbalimbali za kuangalilia mandhari kwenye ukingo wenye kimo cha meta 360 na kutazama kule chini—nyakati nyingine kwa kusitasita. Katika jarida la safari zake la mwaka wa 1870, Nathaniel Langford alisema juu ya “uduni wangu, kutojiweza kwangu” huku akikodolea macho korongo hilo lenye urefu wa kilometa 32 na kuta zake za ngegu inayong’aa—chanzo cha jina la Mto Yellowstone—na maporomoko mawili makubwa mno ya maji. Tulijihisi tukiwa duni na wasiojiweza kama alivyojihisi.

Siku iliyofuata tulisafiri kuelekea mashariki. Mara nyingine tena mandhari ya hifadhi hiyo ikabadilika. Hapo palikuwa na msitu ulio penye mwinuko wa juu, na barabara ilivuka Mpaka wa Mabara mara mbili. Tuliendelea kuona nyati na wanyama wengine wakubwa, nyati akiwa amesimama kwa njia yake ya kawaida. Ilitusikitisha kwamba, hatukuona dubu wowote—ambao huwavutia sana watalii katika Yellowstone. Walienda wapi?

Watalii fulani wamejeruhiwa au kuuawa kwa sababu ya dubu kuwakaribia sana wanadamu katika miaka ya karibuni. Hali haikuwa nzuri kwa dubu pia. Kwa hivyo, mapema katika miaka ya 1970, Huduma za Hifadhi za Kitaifa zilifunga mahali pa kutupia takataka, na hivyo kuzuia dubu hao wasipate chakula kutoka kwa wanadamu. Hatua hiyo ilifanya dubu warejee porini. Mradi huo umefaulu. Sasa dubu hao hula chakula cha asili, nao wana afya bora zaidi. Hata hivyo, bado wao hukutana na watalii katika sehemu fulani-fulani, kama vile Fishing Bridge, ambapo watu na dubu hula, hulala, na kutafuta samaki.

Tulikuwa tumeamua kumalizia safari yetu kwenye Fishing Bridge. Hapo ndipo tulipoona jambo la mwisho na lenye kustaajabisha zaidi katika hifadhi hiyo. Tulipotazama ng’ambo ya Ziwa Yellowstone—ziwa kubwa zaidi la mlimani huko Amerika Kaskazini—kwenye Milima ya Teton, kwa muda tulidhani kwamba tulikuwa kaskazini mwa Italia. Ziwa hilo na mandhari yake ilikuwa na fahari kama milima ya Alp. Lakini hatukuona dubu yeyote.

Wakati wa kuondoka katika Hifadhi ya Yellowstone ulikuwa umewadia. Tuliburudishwa na kuchangamshwa sana na mambo tuliyoona. Mambo tuliyoona yalizidi yale tuliyotarajia.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Mpaka wa Mabara ni sehemu ndefu iliyoinuka inayoenea kutoka Amerika Kaskazini hadi Kusini. Mito kutoka sehemu zote mbili hutiririka pande tofauti kabisa—kuelekea kwenye Bahari ya Pasifiki na kuelekea Bahari ya Atlantiki, Ghuba ya Mexico, na Bahari ya Aktiki.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

Mioto ya 1988

Mwishoni mwa Julai na Agosti mwaka wa 1988, mioto midogo katika Yellowstone iliungana na kuwa mioto mikubwa minane iliyoharibu sana hata wanadamu wakashindwa kuidhibiti. Sababu moja ilikuwa ukame, kwani majira ya kiangazi ya mwaka wa 1988 yalikuwa makavu zaidi katika historia yote ya Yellowstone. Sababu nyingine ilikuwa upepo mkali. Upepo mkali wenye kuvuma kwa kasi ya kilometa 80 kwa saa, ulieneza mioto hiyo kwa umbali wa kilometa 20 kwa siku. Upepo huo ulipeperusha makaa ya moto kwa umbali ambao wazima-moto hawajapata kuona tena. Makaa hayo ya moto yalianzisha mioto mipya.

Jumla ya wazima-moto wa kujitolea na wanajeshi 10,000 hivi na magari zaidi ya 100 ya kuzima moto yalisaidia katika jitihada kabambe za kuzima moto huo ambazo ziligharimu dola milioni 120 za Marekani. Helikopta na ndege zenye kubeba maji zilivurumisha takriban lita milioni 5 za kemikali za kudhibiti moto na lita milioni 40 za maji. Miali ya moto ilikiuka jitihada hizo na kusambaa kwa kasi sana kote katika hifadhi hiyo, nusura iangamize jamii fulani za watu. Siku baada ya siku wingu kubwa la moshi lilizagaa hewani. Kufikia mwishoni mwa majira ya kiangazi hifadhi yote ilishabihi eneo la kivita. Mioto hiyo ilizimwa na hewa baridi, dhoruba ya majira ya mvua, na theluji kiasi iliyozuka katikati ya mwezi wa Septemba, baada ya ekari milioni 1.4 za msitu kuchomeka.

Mioto hiyo haikuathiri sana wanyama, hivyo basi idadi ya watalii imeongezeka haraka tangu wakati huo. Moshi uliposambaratika, majani yaliyochipuka katika majira ya mvua yalirembesha mandhari hiyo mpya, na katika majira ya masika maua-mwitu yalichanua kwa utele hata kwenye maeneo mapya. Katika miaka iliyofuata kuibuka kwa mioto hiyo, miti mipya imesitawi na kufunika maeneo yaliyochomeka.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mkongwe Mwaminifu

Maporomoko ya Chini

[Hisani]

NPS Photo

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mto Firehole

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kidimbwi cha “Morning Glory”

[Hisani]

NPS Photo