Mitakawa Iliokoa Uhai Wao
Mitakawa Iliokoa Uhai Wao
KATIKA miezi ya mwisho ya Vita ya Ulimwengu ya Pili huko Ulaya, Wanazi walizuia meli zote zilizokuwa zikileta shehena za chakula katika majiji yote makubwa magharibi ya Uholanzi. Matokeo yalikuwa mabaya sana, kama watu wengi walioishi pindi hiyo wawezavyo kuthibitisha.
Kwa kawaida mtu anahitaji kalori 1,600 hadi 2,800 hivi kwa siku. Lakini kufikia Aprili 1945, baadhi ya wakazi wa Amsterdam, Delft, The Hague, Leiden, Rotterdam, na Utrecht waliishi kila siku kwa migawo ya chakula chenye jumla ya kalori 500 hadi 600 kwa siku. Yaaminika kwamba kama tokeo, wakati wa Njaa ya Majira ya Baridi Kali ya mwaka wa 1944/1945, angalau raia 10,000 walikufa kutokana na utapiamlo.
Susan Monkman, aliyenusurika alisema kwamba familia yake iliishia kula vitunguu vya mitakawa. “Vitunguu vya mitakawa vilikuwa na ncha kali ajabu,” asema Monkman. “Havikulainika haidhuru kadiri vilivyochemshwa. Hata hivyo tulifurahi kuvitafuna taratibu na kwa uangalifu. Baadaye, koo zetu zilituwasha kwa siku nyingi.” Ili kupunguza mwasho huo, karoti chache au kiazi sukari, ikiwa vilipatikana, vilichanganywa na vitunguu hivyo.
Kipimo cha gramu 100 cha vitunguu vya mitakawa kina kalori 148, gramu 3 za protini, gramu 0.2 za mafuta, na gramu 32 za kabohidrati. Kwa hiyo, mlo usio na ladha wa vitunguu vya mitakawa huenda ulizuia Waholanzi wengi wasife njaa.
Ukatili mbaya wa mwanadamu kumwelekea mwanadamu mwenzake, mifano mingi ikiwa imekaziwa kikiki akilini mwa wengi, huonyesha kadiri wanadamu wanavyohitaji sana utimizo wa ahadi hii ya Biblia: “Lakini ziko mbingu mpya na dunia mpya ambazo tunangojea kulingana na ahadi yake [Mungu], na katika hizo uadilifu utakaa.”—2 Petro 3:13.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Internationaal Bloembollen Centrum, Holland