Unaweza Kupata Wapi Elimu Bora Zaidi?
Unaweza Kupata Wapi Elimu Bora Zaidi?
“Kama vile bonge la marumaru liwezavyo kutokeza sanamu maridadi, ndivyo elimu ilivyo kwa nafsi.”—Joseph Addison, 1711.
JE, ULIWAHI kwenda shuleni? Watu wengi waweza kujibu ndiyo—lakini si kila mtu. Tunapoingia kwenye karne ya 21, mamilioni yasiyohesabika ya watoto hawapokei elimu ya msingi. Na imekuwa hivyo kwa muda mrefu, hivi kwamba leo takriban watu wazima bilioni moja hawajui kusoma wala kuandika.
Lakini, kupata elimu nzuri ni uhitaji wa msingi. Badala ya kuiona elimu kuwa anasa isiyopatikana, wengi leo huiona kuwa haki ya watoto na watu wazima pia. Lakini elimu nzuri yaweza kupatikanaje bila rasilimali zifaazo? Vipi ikiwa kuna uhaba wa vitabu, uhaba wa walimu wenye ujuzi, na uhaba wa shule?
Kwa kweli, watu waweza kupata wapi elimu bora inayomtia moyo kila mtu kushiriki, inayopanua ujuzi wao kuhusu ulimwengu unaowazunguka, na kuwapa viwango vya kiroho vinavyoweza kugeuza maisha yao? Ni elimu gani inayokazia viwango vifaavyo vya maadili, inayoonyesha jinsi ya kupata maisha bora, na kuandaa tumaini hakika la wakati ujao? Je, kila mtu aweza kwelikweli kupata elimu ya aina hiyo?
Msingi wa Elimu Bora Zaidi
Japo laonekana kuwa jambo la kushangaza, twaweza kujibu kwa uhakika ndiyo, elimu bora yapatikana kwa wote. Kwa sababu, kuna kifaa chenye uwezo mkubwa wa kuelimisha kinachoweza kuandaa msingi wa elimu hiyo. Ni “kitabu cha mafunzo” ambacho kimeheshimiwa kwa sababu ya kudumu kwa muda mrefu zaidi, nacho chaweza kupatikana kikiwa kizima au kwa sehemu, katika lugha zaidi ya 2,200 ulimwenguni pote. Kwa kweli kila mtu duniani anaweza kukipata katika lugha anayoweza kuelewa. Ni kitabu kipi hicho?
Ni Biblia, kitabu ambacho kimesifiwa kote kuwa kitabu muhimu zaidi ambacho kimewahi kuandikwa. “Kila mtu ambaye anaijua Biblia kabisa aweza kwa kweli kuitwa mtu aliyeelimika,” akaandika msomi mmoja wa mapema karne ya 20 William Lyon Phelps. “Hakuna elimu nyingine yoyote wala utamaduni, uwe mpana au sanifu kadiri gani, unaoweza . . . kuchukua mahali pake barabara.”
Biblia ni mkusanyo wa vitabu vilivyoandikwa kwa kipindi cha miaka ipatayo 1,600. Kuhusu maktaba hiyo muhimu ya vitabu, Phelps aliongezea hivi: “Dhana zetu, hekima yetu, falsafa yetu, fasihi yetu, sanaa yetu, maadili yetu, hutoka kwenye Biblia kuliko kwa vitabu vinginevyo vyote kwa ujumla. . . . Naamini kwamba ujuzi wa Biblia pasipo elimu ya chuoni ni muhimu zaidi kuliko elimu ya chuoni pasipo Biblia.”
Leo kazi isiyo na kifani ya kutoa elimu ya Biblia inaendeshwa ulimwenguni pote na jamii ya Kikristo ya Mashahidi wa Yehova. Elimu hiyo inatia ndani mengi zaidi ya kufundisha kusoma na kuandika tu. Inatokeza maendeleo ya kiakili na ya kiadili. Inaathiri mtazamo wa watu kuhusu wakati ujao kwa njia yenye kujenga, na kuandaa msingi wa kuwa na tumaini lifaalo la wakati ujao la kwamba hali ya wakati ujao itakuwa bora kuliko ya wakati uliopita.
Tafadhali jifunze kuhusu programu hiyo ya elimu inayoongoza kwenye uhai kwa kusoma makala ifuatayo.