Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Fumbo la Nan Madol

Fumbo la Nan Madol

Fumbo la Nan Madol

Ni nani waliojenga hii ‘Venisi ya Bahari za Kusini’? Waliijengaje? Kwa nini walihama?

JE, WAPENDA fumbo lenye kusisimua—lenye mambo ajabu ya kuvutia? Basi njoo uchunguze magofu ya Nan Madol, fumbo la karne nyingi ambalo limewatatanisha wageni wengi.

Nan Madol ni mzingile wenye kustaajabisha sana wa vijisiwa na mifereji ya mawe iliyotengenezwa na wanadamu miaka elfu moja iliyopita kwenye mwamba usio na kina pembeni mwa kisiwa cha Pohnpei * huko Mikronesia. Kadiri tunavyozidi kukikaribia majini, tunashindwa kuona magofu hayo kwa sababu yamefunikwa na mikoko na vichaka vya kitropiki vilivyosongamana. Mashua yetu inapozunguka taratibu penye mzingo, ghafula twakabili majengo hayo yaliyojengwa kwa uhandisi bora sana.

Kuta kubwa sana, nyingine zikiwa ndefu kama jengo kubwa la mjini, zaibuka kwanza. Kuta hizo kubwa, ambazo zimeinuka taratibu na kufanyiza pembe zilizo butu, zilijengwa kwa nguzo kubwa za gumawesi (basalt) zinazokingamana.

Jina Nan Madol humaanisha “Mahali pa Katikati,” na hilo hueleza vyema mizingile ya mifereji iliyotengenezwa na wanadamu inayozingira visiwa hivyo. Mabaharia wa Ulaya wa miaka ya 1800 yaelekea ndio waliokuwa wageni wa kwanza kufika Nan Madol. Waliduwazwa ajabu na mandhari hiyo kiasi cha kwamba walikiita kwa utani kitovu hicho cha kale cha kidini na cha kisiasa kuwa Venisi ya Bahari za Kusini. Lakini mabaharia hao hawakushuhudia kamwe fahari kamili ya Nan Madol, kwani kilikuwa kimehamwa kwa sababu zisizojulikana karne moja hivi kabla hawajawasili.

Watu wawili waliotuongoza walitueleza kwamba Kisiwa cha Nan Madol kina ukubwa wa ekari 200 hivi. Walieleza kwamba kila kimoja cha vijisiwa vyake 92, kilitumiwa kwa kusudi fulani mahususi. Baadhi yake vilitumiwa kuwa vituo vya makazi. Vingine vilitumiwa kwa minajili ya utayarishaji wa vyakula, utengenezaji wa mitumbwi, na kwa sherehe za kucheza dansi. Ingawa visiwa hivyo vilijengwa kwa maumbo na ukubwa mbalimbali, kisiwa cha kawaida kina umbo la mstatili na karibu kitoshane na uwanja wa soka. Vijisiwa vingi vina vichaka vikubwa, lakini mambo yanayoweza kugunduliwa yanavutia sana.

Ngome ya Wafalme

Mahali bora pa kupeleleza kwa makini fumbo la Nan Madol ni penye ngome kubwa inayoitwa Nan Douwas. Ingawa inawezekana kutembea kwenye maji ya bahari ili kutazama magofu hayo, ni afadhali kuyafikia kwa mashua. Kisiwa cha Nan Madol kilijengwa kusudi kitumiwe na vyombo vya majini, na mifereji yake ni mipana kama barabara kuu yenye njia nne. Pia haina kina sana. Maji yanapojaa humfika mtu kiunoni, hali ambayo bila shaka ililinda Nan Madol kutokana na meli za wavamizi karne zilizopita. Wale waliokuwa wakitutembeza waliendesha mashua kwa uangalifu kwenye njia za majini ili kuepuka kuharibu rafadha za mashua hiyo kwenye matumbawe yaliyo majini.

Tulipofika kwenye gati huko Nan Douwas, tulishuka na kupanda ngazi zilizoelekea moja kwa moja katika madhabahu ya kale. Kwa kufuata mwingilio huo wenye kuvutia sana tulipita kuta zenye upana wa meta 3 hadi 4 na urefu wa meta 8 hadi 9. Minara hiyo thabiti imestahimili dhoruba za kitropiki na hata vimbunga.

Ndani ya kuta hizo kubwa kupindukia, tuliona ua mkubwa sana unaozingira chumba cha mawe kilicho ardhini. Mahali hapa pa ibada ni chumba cha kuhifadhia maiti za wafalme ambamo maombolezo ya wafalme yalifanyiwa. Tulipopeleleza zaidi tuligundua sehemu iliyoonekana kuwa kijia kinachopita ardhini. Wale waliokuwa wakitutembeza walitutia moyo tujipenyeze kwenye mianya iliyo katika mawe hayo, na punde si punde tulikuwa tumejikunyata kwenye chumba kidogo chenye giza kilicho ardhini. “Mko gerezani,” mtembezaji mmoja akaeleza. “Humu ndimo walimowekwa wafungwa wa Nan Madol.” Tulipowazia namna ambavyo mfungwa alihisi “mwingilio” wa jela ulipofunikwa kabisa kwa jiwe lenye uzito wa tani mbili, tulifurahia kutoka humo.

Mawe ya Kujengea Yasiyo ya Kawaida

Kuvinjari kwenye magofu ya Nan Madol kulitusaidia tuthamini jitihada ambayo ilihusika katika ujenzi. Vifusi vya matumbawe hufanyiza misingi ya vijisiwa hivyo. Misingi hiyo ilijengwa ili iweze kustahimili mabonge mazito ya nguzo ndefu za gumawesi. Nguzo hizo zina umbo la kuvutia sana hivi kwamba wageni waliozuru zamani walidhani zilifinyangwa kwa mikono. Baadaye, iligunduliwa kwamba umbo lake la asili ni kama la mche, kila nguzo ikiwa na pande tano hadi nane.

Maelfu ya majabali hayo ya nguzo—baadhi yake yakiwa na urefu wa meta tano hivi na uzito wa zaidi ya tani tano—yalisafirishwa hadi hapo. Mojawapo ya mawe ya msingi linakadiriwa kuwa na uzito wa zaidi ya tani 50! Kwa kuwa chelezo chenye kubeba uzito kama huo huzama kwenye maji yasiyo na kina hatuna budi kujiuliza hivi, ‘Majabali hayo makubwa sana yalisafirishwaje hadi Nan Madol kisha kusimamishwa mahali pafaapo?’ Lakini, mgodi wa gumawesi ulio karibu zaidi uko mbali sana—karibu upande wa pili wa kisiwa cha Pohnpei!

Katika miaka iliyopita, fumbo la Nan Madol limezusha hekaya fulani zilizobuniwa. Hekaya moja husema kwamba karne nyingi zilizopita ndugu wawili walipewa uwezo wa kimizungu na miungu ili “kuruka” na kusafirisha mawe mazito mahali hapo pa ujenzi. Hekaya nyingine husema kwamba, wakati mmoja Kisiwa cha Pohnpei kilikaliwa na jamii iliyoendelea sana ambayo ilifahamu siri ya kudhibiti mawimbi ya sauti, na hivyo kufaulu kufanya mawe hayo makubwa yaelee hewani na kusimama mahali pake muafaka.

Wale waliokuwa wakitutembeza walitueleza habari yenye kusadikika zaidi—ya kwamba Kisiwa cha Nan Madol kilijengwa na watu wengi sana na kilichukua karne nyingi kukamilika. Yaelekea kwamba nguzo za gumawesi ziliinuliwa na kuwekwa mahali pake kwa kazi ya sulubu, huku wakitumia mashina ya michikichi yaliyobetuka kuwa maegemeo. Lakini bado, twauliza, “Mawe haya mazito yalisafirishwaje hadi Nan Madol?”

Je, Fumbo Hilo Litatatuliwa?

Hakuna mtu awaye yote awezaye kusema kwa hakika namna Kisiwa cha Nan Madol kilivyojengwa au, labda hata lenye kutatanisha zaidi, kilichofanya wakazi wahame. Wengi hudai kwamba Kisiwa cha Nan Madol kilishambuliwa na kushindwa. Wengine husema kwamba wageni walileta maradhi katika Kisiwa cha Pohnpei, ambayo yaliwaangamiza wakazi wengi. Dhana nyingine husema kwamba kimbunga kikali sana kiliharibu chakula kilichokuwa kisiwani, ikabidi wakazi wake wahamishwe. Haidhuru sababu ni gani, Kisiwa cha Nan Madol kimeachwa mahame kwa angalau miaka 200.

Kwa hiyo, ujenzi huo wa kale wa kustaajabisha hutuacha tukiwa na maswali mengi yasiyo na majibu. Mashua yetu ilipokuwa ikiondoka, hatukuwa na budi kufikiria sana swali, Je, mtu awaye yote atawahi kutatua fumbo la Nan Madol?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Kisiwa cha Pohnpei kiko karibu na ikweta, takriban kilometa 5,000 kusini-magharibi ya Hawaii.

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Pohnpei

[Picha katika ukurasa wa 16]

Gati na mwingilio mkuu wa ngome

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ukuta mkubwa sana wa nje

[Picha katika ukurasa wa 18]

Chumba kikuu cha mawe kilicho ardhini cha kuzikia wafu

[Picha katika ukurasa wa 18]

Baadhi ya mifereji yenye ukubwa wa ekari 200 iliyotengenezwa na watu

[Hisani]

© 2000 Nik Wheeler