Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kifukofuko Makala “Upendo Unaposhindwa Kuona” (Machi 22, 2000) yamtaja nondo akiibuka kutoka kwenye pupa (buu). Hata hivyo, ni vipepeo wanaotengeneza pupa. Nondo hutengeneza vifukofuko.
V. L., Marekani
Kulingana na “Webster’s Ninth New Collegiate Dictionary,” neno linalotafsiriwa “buu” laweza kutumiwa kwa upana kumaanisha “pupa ya mdudu.” Kwa wazi, neno hilo kwa kawaida hutumiwa kuhusiana na vipepeo. Lakini, vichapo fulani hutumia neno hilo kuhusiana na nondo.—Mhariri.
Vasa Ningependa kueleza uthamini wangu kwa ajili ya makala “Vasa—Kutoka Katika Msiba Hadi Kuwa Kivutio.” (Aprili 8, 2000) Nikiwa mwanahistoria aliyechunguza habari hiyo kwa kiasi fulani, naweza kuthibitisha kwamba makala hiyo ilifanyiwa utafiti wa hali ya juu sana. Ilieleza matukio hayo kwa njia bora kabisa na kwa usawaziko.
T. W., Ujerumani
Ushindi wa Kisheria Hivi karibuni nilienda mahakamani ili kuomba idhini ya kuwatunza watoto wangu, yule aliyekuwa mume wangu amezusha ubishi kuhusu itikadi zangu za kidini. Mambo yamekuwa magumu. Niliposoma makala “Vita Si Yenu Bali Ni ya Mungu” (Aprili 22, 2000), nilibubujikwa na machozi.
D. B., Marekani
Baada ya kusoma makala hiyo, niliwaonyesha wanasheria wa eneo letu. Hakuna yeyote aliyekataa. Hata baadhi yao walinialika ofisini mwao ili ninywe kahawa na kuzungumza nao zaidi. Baadhi yao waliomba nakala zaidi kwa ajili ya wanasheria wenzao. Wanasheria wote walishangaa nilipowaonyesha kwamba Hayden Covington alishinda kesi 36 kati ya 45 katika Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani.
C. M., Marekani
Baba Vijana Naandika ili kueleza uthamini wangu wa kutoka moyoni kwa ajili ya makala “Vijana Huuliza . . . Kuzaa Watoto—Je, Humfanya Mtu Awe Mwanamume?” (Aprili 22, 2000) Mimi ni mseja mwenye umri wa miaka 28, nami hutumikia nikiwa painia wa pekee, au mweneza-evanjeli wa wakati wote. Katika sehemu hii ya Afrika Magharibi, mtu yeyote mwenye umri kama wangu asiye na mke au rafiki wa kike huonwa kuwa mshamba na gumba. Mara nyingi mimi hudhihakiwa na kudharauliwa kwa sababu hiyo. Hata hivyo, makala yenu iliimarisha azimio langu la kubaki safi.
A. E., Ghana
Nilipoteza ubikira wangu nikiwa kijana nami nilifanya uasherati na mvulana mmoja baada ya mwingine. Nilibaki nikijihisi mchafu kila mara, na mara nyingi nilikuwa nikitumiwa vibaya. Hilo lilinifanya nishuke moyo. Yehova alinisaidia kurekebisha maisha yangu, na hivi sasa nina furaha kwa kuwa nimeolewa na mwanamume mzuri. Lakini mwafanya vema kuchapisha makala kama hizo ili kuwasaidia vijana wanaume wang’amue kwamba yale wanayotenda yanaweza kumwumiza msichana maisha yake yote.
F.A.S., Ujerumani
Nimeguswa moyo sana kiasi cha kutaka kuwashukuru kwa kuonyesha ifaavyo kwamba angalau nusu ya wajibu wa akina mama wasioolewa—ni wa akina baba! Watu wengi sana huamini kwamba kwa kuwa ni wanawake tu wanaopata mimba, hali ya maumbile yaonyesha kwamba ni tatizo la wanawake na kwamba wanaume hawahitaji kuwajibika kwa vyovyote. Endeleeni kuwaelimisha vijana wanaume wafahamu jinsi Mungu anavyotaka wanawake watendewe.
J.M.O., Italia