Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kushinda Vipingamizi kwa Kuweka Miradi

Kushinda Vipingamizi kwa Kuweka Miradi

Kushinda Vipingamizi kwa Kuweka Miradi

WILLIAM (Bill) Meiners na mkewe, Rose, wanaishi katika chumba kimoja karibu na Uwanja wa Ndege wa LaGuardia huko New York. Humo Rose, mkaribishaji mwenye haiba aliye na umri wa kati ya miaka ya 70, amkaribisha mgeni wake kwa uchangamfu. Mtu aingiapo chumbani anaona mara moja kwamba sebule yenye kustarehesha inapendeza na kulandana na uchangamfu wa Rose. Mpangilio maridadi wa maua karibu mlangoni na picha zenye kuvutia zilizo ukutani huleta hisia ya shangwe na shauku kubwa ya kuishi.

Kuna chumba chenye kuvutia sana karibu na sebule ambamo Bill, mwenye umri wa miaka 77, amelala kitandani, mgongo wake ukiwa umetegemezwa na godoro linalorekebishika. Mara tu anapomwona mgeni wake, macho yake ya fadhili yanang’aa naye anatabasamu kwa shauku. Angependa kuinuka, kumsalimu kwa mikono, na kumkumbatia, lakini hawezi. Bill amepooza mwili wote ila mkono wake wa kushoto.

Kwa kuwa Bill amekuwa na matatizo ya afya tangu alipokuwa na umri wa miaka 26, yeye aulizwa kile ambacho kimemsaidia kukabiliana na ugonjwa wake kwa zaidi ya miaka 50. Bill na Rose waangaliana kwa kicheko. “Hatumjui mgonjwa yeyote!” asema Rose, huku kicheko chake cha kutoka moyoni kikisambaa chumbani. Macho ya Bill yang’aa kwa furaha; acheka-cheka na kutikisa kichwa chake kwa kuitikia. “Hakuna mgonjwa hapa,” yeye asema kwa kusitasita kwa sauti nzito yenye kukwaruza. Rose na Bill wataniana kwa mchezo, na punde si punde, kicheko chazagaa chumbani. Ni dhahiri kwamba Bill na Rose wangali na upendo waliokuwa nao walipokutana mara ya kwanza mnamo Septemba 1945. Bill aulizwa tena: “Lakini bila utani wowote, umekabili vipingamizi gani? Ni nini ambacho kimekusaidia kukabiliana navyo na kudumisha mtazamo chanya maishani?” Baada ya kumsihi, Bill akubali kusimulia yaliyompata. Yafuatayo ni madondoo ya mazungumzo kadhaa kati ya Amkeni!, Bill na mkewe.

Vipingamizi Vyaanza

Mnamo Oktoba 1949—miaka mitatu baada ya kumwoa Rose na miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwa binti yao, Vicki—Bill alijulishwa kwamba ana uvimbe wenye kusababisha kansa katika moja ya nyuzi zake za sauti, uvimbe huo uliondolewa. Miezi michache baadaye, daktari wa Bill alimjulisha kipingamizi kingine—kansa hiyo ilikuwa imeathiri zoloto yote. “Niliambiwa kwamba bila kupasuliwa na kuondolewa zoloto yote, ningekufa baada ya miaka miwili tu.”

Bill na Rose walielezwa matokeo ambayo yangesababishwa na upasuaji huo. Zoloto huanzia kwenye shina la ulimi hadi kwenye mwingilio wa koromeo. Ndani ya zoloto mna nyuzi mbili za sauti. Hewa inayotoka mapafuni inapopita kwenye nyuzi hizo, zinatikisika na kutoa sauti za usemi. Zoloto inapoondolewa, sehemu ya juu ya koromeo huunganishwa na shimo lililotobolewa upande wa mbele wa shingo. Baada ya upasuaji, mgonjwa hupumua kupitia kwa shimo hilo—lakini huwa amepoteza sauti yake.

“Niliposikia maelezo hayo, nilikasirika sana,” asema Bill. “Tulikuwa na binti mchanga, nilikuwa na kazi nzuri, tulikuwa na mataraja bora maishani, na sasa matumaini yangu yote yalididimia kabisa.” Lakini kwa kuwa kuondolewa zoloto kungeokoa uhai wake, Bill alikubali kufanyiwa upasuaji huo. “Baada ya upasuaji,” asema Bill, “singemeza kitu chochote. Singesema hata neno moja. Nilikuwa bubu.” Rose alipomtembelea Bill, aliweza kuwasiliana naye kwa kuandika maneno kwenye kijitabu. Ulikuwa wakati mgumu sana. Ili kushinda kipingamizi hicho, walihitaji kuweka miradi mipya.

Asiyeweza Kusema na Asiye na Kazi

Upasuaji wa kuondoa zoloto mbali na kumwacha Bill akiwa bubu, ulimwacha bila kazi. Awali alikuwa akifanya kazi kwenye karakana ya mashine, lakini sasa kwa kuwa alipumua kupitia tu kwa shimo lililo shingoni, vumbi na moshi vingeweza kuhatarisha mapafu yake. Alihitaji kutafuta kazi nyingine. Huku akiwa hawezi kusema, alijiandikisha katika shule moja ili ajifunze kutengeneza saa. “Ilikuwa kama kazi yangu ya awali,” asema Bill. “Nilijua jinsi ya kuunganisha sehemu za mashine, na unapotengeneza saa, unaunganisha pia visehemu pamoja. Tofauti ni kwamba visehemu hivyo havikuwa na uzito wa kilogramu 23!” Mara tu baada ya kukamilisha masomo ya kutengeneza saa, aliajiriwa kazi ya kutengeneza saa. Alikuwa ametimiza mradi wa kwanza.

Wakati huohuo, Bill alikuwa ameanza kuhudhuria masomo ya kusema kwa umio. Katika usemi wa umio, sauti haitokezwi na nyuzi za sauti bali na mitetemo katika umio, njia ya chakula kutoka shingoni hadi tumboni. Kwanza, mtu hujifunza kumeza hewa na kuilazimisha kuingia kwenye umio. Halafu, mtu huteuka hewa hiyo kwa njia fulani maalum. Hewa inapotoka, inasababisha kuta za umio zitetemeke. Mtetemo huo hutokeza sauti nzito inayokwaruza, ambayo inaweza kudhibitiwa kwa mdomo na kuwa usemi.

“Hapo awali, niliteua tu baada ya kula sana,” asema Bill kwa tabasamu, “lakini sasa nilihitaji kujifunza kuteua kwa kawaida. Mwanzoni, niliweza kusema neno moja tu kwa wakati, kwa njia hii: ‘[Pumua, meza, teua] Habari [pumua, meza, teua] yako?’ Haikuwa rahisi. Kisha, mwalimu wangu akaniambia ninywe kinywaji kingi cha tangawizi kwa sababu gesi iliyomo ingenisaidia kuteua. Kwa hivyo wakati wowote Rose alipoenda matembezini na Vicki, nilikunywa na kuteua, kunywa na kuteua. Nilijitahidi mno!”

Ijapokuwa asilimia 60 ya wagonjwa wote wasio na zoloto hushindwa kusema kwa kutumia umio, Bill alifanya maendeleo. Vicki, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka miwili hivi, alimshurutisha pasipo kujua. Bill aeleza: “Vicki angeongea nami kisha angenitazama, akisubiri jibu. Lakini singeweza kumjibu hata kwa neno moja. Alizidi kuongea, lakini kwa mara nyingine sikujibu. Kwa hamaki, Vicki alimgeukia mke wangu na kusema: ‘Mfanye Baba aongee nami!’ Maneno yake yalinichoma sana na kunifanya niazimie kuongea tena.” Vicki, Rose, na wengineo walifurahi sana Bill alipofaulu. Alitimiza mradi mmoja zaidi.

Akumbwa na Pigo Jingine

Kufikia mwishoni mwa mwaka wa 1951, Bill na Rose walikabili tatizo jipya. Madaktari, huku wakihofia kwamba kansa ingeibuka tena, walimshauri Bill apate matibabu ya mnururisho. Bill akakubali. Matibabu yalipokamilika, alikuwa na hamu ya kurejelea maisha ya kawaida. Hakutambua kamwe kwamba pigo jingine kwa afya yake lilikuwa likija!

Mwaka mmoja hivi ulipita. Halafu, siku moja vidole vya Bill vikafa ganzi. Kisha, akashindwa kupanda ngazi. Muda mfupi baadaye, alianguka alipokuwa akitembea na hangeweza kunyanyuka tena. Uchunguzi ulionyesha kwamba matibabu ya mnururisho ambayo Bill alikuwa amepokea (ambayo, wakati huo, hayakuwa sahihi kama yalivyo leo) yalikuwa yameharibu uti wake wa mgongo. Alielezwa kwamba hali yake ingezidi kuzorota. Daktari mmoja hata alimwambia kwamba hakuwa na tumaini “lolote” la kupona. Hilo lilikuwa pigo kubwa sana kwa Bill na Rose.

Hata hivyo, katika jitihada za kushinda kipingamizi hicho, Bill alilazwa hospitalini kwa miezi sita ili kupata matibabu ya maungo. Ingawa matibabu hayo hayakubadili hali ya mwili wake, kulazwa hospitalini kulibadili maisha yake—badiliko ambalo hatimaye lilimwezesha amjue Yehova. Hilo lilitukiaje?

Atiwa Nguvu Baada ya Kuelewa Chanzo cha Vipingamizi

Kwa hiyo miezi sita, Bill alikaa katika chumba kimoja katika hospitali moja ya Kiyahudi na wanaume 19 waliopooza—wote walikuwa Wayahudi Waothodoksi. Kila alasiri wanaume hao walikuwa wakizungumzia Biblia. Bill, mhudhuriaji wa kanisa la Baptisti, alisikiliza tu. Lakini wakati wa kuondoka hospitalini ulipofika, aliyosikia yalimsaidia afikie mkataa wa kwamba Mungu Mweza Yote ni mtu mmoja tu na kwamba fundisho la Utatu hupingana na Biblia. Kama tokeo, Bill hakurudi tena kanisani. Hata hivyo, aliona uhitaji wa kupata mwelekezo wa kiroho ili kukabiliana na vipingamizi maishani. “Nilizidi kumwomba Mungu msaada,” asema Bill, “na sala zangu zilijibiwa.”

Jumamosi moja mnamo mwaka wa 1953, Roy Douglas, mwanamume mzeemzee aliyewahi kuwa jirani yake alimtembelea Bill baada ya kuelezwa hali yake. Roy, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alimwomba Bill ajifunze Biblia naye, Bill akakubali. Mambo ambayo Bill alisoma kwenye Biblia na katika kitabu “Let God Be True” * yalimshangaza sana. Alimwambia Rose mambo ambayo yeye alijifunza, naye akajiunga na funzo hilo. Rose akumbuka hivi: “Kanisani tulielezwa kwamba ugonjwa ni adhabu kutoka kwa Mungu, lakini katika funzo letu la Biblia tulijifunza kwamba huo ni uwongo. Hilo lilitutuliza sana.” Bill aongezea: “Kujifunza kutoka kwa Biblia kisababishi cha matatizo yote, kutia ndani ugonjwa wangu, na kujua kwamba kutakuwa na wakati ujao mzuri kulitusaidia kukabili hali yangu.” Mwaka wa 1954, Bill na Rose walitimiza mradi mwingine. Wote wawili walibatizwa kuwa Mashahidi wa Yehova.

Kufanya Marekebisho Zaidi

Wakati huo, Bill alikuwa amepooza kiasi cha kutoweza kuendelea na kazi yake ya kuajiriwa. Ili kujiruzuku, Bill na Rose walibadilishana mafungu yao: Bill alibaki nyumbani na Vicki, naye Rose akaanza kufanya kazi kwenye kampuni ya kutengeneza saa—alifanya kazi hiyo kwa miaka 35!

“Kumtunza binti yetu kuliniletea shangwe sana,” asema Bill. “Vicki aliye mchanga alifurahia pia. Kwa fahari, alikuwa akimweleza hivi kila mtu aliyekutana naye: ‘Mimi humtunza Baba!’ Baadaye, alipokuwa akienda shuleni, nilimsaidia kufanya mazoezi yake ya shuleni, na mara kwa mara tulicheza michezo. Isitoshe, nilikuwa na fursa nzuri ya kumfundisha Biblia.”

Kuhudhuria mikutano ya Kikristo kwenye Jumba la Ufalme pia kulimletea Bill na familia yake shangwe. Alichechemea kwa saa nzima kutoka nyumbani kwake hadi kwenye Jumba la Ufalme, lakini hakukosa mikutano. Baadaye, baada ya kuhamia eneo jingine jijini, Bill na Rose walinunua gari dogo, na Rose alipeleka familia kwenye jumba. Hata ingawa Bill angeweza kuongea kwa vipindi vifupi tu, alijiandikisha kuwa mwanafunzi katika Shule ya Huduma ya Kitheokrasi. Bill aeleza: “Niliandika hotuba yangu, na ndugu mwingine aliitoa. Baada ya hotuba, mwangalizi wa shule alinishauri kuhusiana na muhtasari huo.”

Watu mbalimbali kutanikoni walimsaidia pia Bill kushiriki kikawaida katika kazi ya kuhubiri. Na wale waliokuwa wakiona ujitoaji wake hawakushangaa wakati Bill aliwekwa rasmi baadaye kuwa mtumishi wa huduma kutanikoni. Halafu, miguu yake ilipodhoofika kabisa naye akazidi kupooza, alikaa tu kwenye chumba chake na hatimaye akawa habanduki kitandani. Je, angeweza kushinda kipingamizi hicho?

Burudani Yenye Kuridhisha

“Nilitafuta burudani kwa sababu ya kushinda nyumbani siku nzima,” asema Bill. “Kabla ya kupooza nilikuwa nikifurahia kupiga picha. Kwa hiyo nilifikiria kujaribu kuchora picha, hata ingawa sikuwahi kuchora picha maishani mwangu. Awali niliandika kwa mkono wa kulia, lakini sasa mkono huo wote na vidole viwili vya mkono wangu wa kushoto vilikuwa vimepooza. Haidhuru, Rose alinunua vitabu vingi kuhusu mbinu za uchoraji. Nilivisoma na nikaamua kuchora kwa mkono wangu wa kushoto. Picha zangu nyingi ziliishia kwenye moto, lakini hatimaye nikaanza kuwa stadi.”

Picha maridadi chungu nzima zilizochorwa kwa rangi ya maji ambazo sasa zinaremba chumba cha Bill na Rose zathibitisha kwamba Bill alifanikiwa zaidi ya alivyotarajia. “Miaka mitano hivi iliyopita,” aongezea Bill, “mkono wangu wa kushoto ulianza kutetemeka sana hivi kwamba ilinibidi kuacha kabisa kuchora, lakini kwa miaka mingi burudani hiyo iliniridhisha sana.”

Mradi Unaosalia

Bill akumbuka: “Zaidi ya miaka 50 imepita sasa tangu nilipoanza kukumbwa na matatizo ya afya. Usomaji wa Biblia ungali unanifariji, hasa ninaposoma Zaburi na kitabu cha Ayubu. Nami hufurahia kusoma vichapo vya Watch Tower Society. Mimi pia hutiwa moyo sana wakati washiriki wa kutaniko letu na waangalizi wasafirio wanaponitembelea na kushiriki nami mambo yaliyoonwa yenye kuchangamsha. Zaidi ya hayo, simu iliyounganishwa kwenye Jumba la Ufalme huniwezesha kusikiliza mikutano, na hata mimi hupokea kanda za vidio za programu za mikusanyiko.

“Ninashukuru sana kwa kuwa nimebarikiwa kuwa na mke mwenye upendo. Kwa miaka mingi, amekuwa mwandamani wangu wa karibu. Pia, binti yetu, ambaye leo anamtumikia Yehova pamoja na familia yake mwenyewe, angali anatuletea shangwe sana. Namshukuru hasa Yehova kwa kunisaidia niwe karibu naye. Hivi leo, kadiri sauti yangu na mwili wangu unavyodhoofika zaidi na zaidi, mara nyingi mimi hufikiria maneno haya ya mtume Paulo: ‘Hatufi moyo, lakini hata ikiwa mtu tuliye kwa nje anachakaa, hakika mtu tuliye kwa ndani anafanywa upya siku kwa siku.’ (2 Wakorintho 4:16) Naam, kudumu nikiwa macho kiroho maadamu ninaishi—ungali mradi wangu.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 20 Kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.; sasa hakichapishwi tena.

[Blabu katima ukurasa wa 12]

“Baada ya upasuaji, singemeza kitu chochote. Singesema hata neno moja. Nilikuwa bubu”

[Picha katika ukurasa 13]

Bill na Rose walivyo leo