Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Mabomu ya Ardhini Niliguswa sana na ule mfululizo wa makala “Mabomu ya Ardhini—Ni Nini Kinachoweza Kufanywa?” (Mei 8, 2000) Inasikitisha kwamba raia wengi sana wasio na hatia hufa kila mwaka kutokana na mabomu ya ardhini.
E. U., Finland
Niliaibika sana niliposoma juu ya chombo hiki cha kutisha kinachotumiwa na wanadamu kuwaumiza wengine. Mungu ana sababu tosha za kuingilia mambo na kuondolea mbali uovu kutoka katika dunia yetu.
G. S., Brazili
Mfululizo huo ulikuwa muhimu sana katika kuchangia kujulisha umma kuhusu suala hili. Picha ya jalada iliamsha upendezi sana.
R. H., Marekani
Matibabu Bila Damu Makala “Utakufa!” (Mei 8, 2000) ilinikumbusha kisa cha baba yangu. Miaka fulani iliyopita alipatwa na kiharusi alipokuwa akiendesha gari. Gari lilipinduka, na alipopata fahamu, daktari alimjulisha kwamba alihitaji kutiwa damu mishipani. Baba yangu alipokataa, daktari alisema hivi: “Usipokubali kutiwa damu utakufa.” Baba alisimama imara. Siku iliyofuata daktari aliingia chumbani mwake na kumuuliza hivi: “U hali gani?” Baba yangu akajibu: “Niko hai!” Baba yangu angali hai akimtumikia Yehova kadiri awezavyo.
T. M., Marekani
Ninaugua kansa ya damu iliyo nadra, na ilipogunduliwa, daktari aliniarifu kuwa ningekufa baada ya miezi sita kama singeanza kutiwa damu mishipani mara moja. Hilo lilitukia mwaka wa 1991. Nilimpata daktari mwenye kuheshimu msimamo wangu juu ya damu na nikaamua kibinafsi kudungwa sindano ya erythropoietin kila juma chini ya usimamizi wake. Sindano hiyo imesaidia kuongeza kiwango changu cha damu.
E. G., Marekani
Nilisoma kisa cha Leanne Karlinsky, na kwa sababu mimi ni daktari, nilisikitishwa sana na unyama aliofanyiwa na watu waliokataa kumhudumia baada ya upasuaji [kwa sababu alikataa kutiwa damu mishipani]. Ni vigumu kuwazia watu wenye akili finyu jinsi hiyo!
C. C., Marekani
Kupambana na Hali ya Kukata Tamaa Kwa sababu nina mshuko-moyo, nilisoma makala “Maoni ya Biblia: Jinsi ya Kukabiliana na Hali ya Kukata Tamaa” (Mei 8, 2000) baada tu ya kuipokea. Kama mlivyosema, kuzungumza na mtu mwenye hisia-mwenzi hutia moyo sana. Ningependa kuwashukuru kwa ajili ya makala zenu murwa.
A. D., Lithuania
Kuathiriwa na Laktosi Mke wangu alimwona daktari kwa sababu alikuwa na maumivu makali. Daktari alisema huenda alikuwa akiathiriwa na laktosi. Sikuwa nimewahi kusikia jambo kama hilo, hivyo tulithamini makala “Je, Wewe Huathiriwa na Laktosi?” (Mei 8, 2000) Habari hiyo bora ilikuja kwa wakati ufaao.
E. P., Marekani
Brazili Ile makala “Pantanal—Hifadhi Yenye Kuvutia Sana” (Septemba 8, 1999) ilinichochea kwenda kujionea mwenyewe sehemu hiyo ya uumbaji wa Yehova. Kwa hiyo, mimi na dada yangu tulipanga kuzuru Brazili, na tulipokea ile makala “Historia Yenye Kuvutia ya ‘Nchi Iliyo na Utofautiano’” (Mei 8, 2000) majuma mawili kabla ya sisi kufika huko. Tuliitumia makala hiyo kama ramani ya kutuelekeza kwenye sehemu bora za kutembelewa.
E. V., Uingereza
Ndege na Wafungwa Nimefurahia kuwatunza—na hatimaye kuwaacha huru mwituni—ndege kadhaa. Ile makala “Mfungwa Aweza Kujifunza Nini Kutokana na Ndege?” (Mei 8, 2000) ilinikumbusha vile ambavyo hata kiumbe mdogo wa Yehova awezavyo kutufundisha mambo mengi.
E. D., Marekani