Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Moto! Je, Utatumia Kizima-Moto Kipi?

Moto! Je, Utatumia Kizima-Moto Kipi?

Moto! Je, Utatumia Kizima-Moto Kipi?

NI MARA nyingi sisi hupita kidude hicho kidogo kilicho ukutani bila hata kukiangalia! Hata hivyo, siku moja huenda kitazuia ofisi yetu au kiwanda au hata nyumba yetu kuteketea. Vizima-moto vidogo vyaweza kuzima moto mdogo—sufuria yenye kuwaka moto mekoni, pazia iliyoshika moto kutokana na kipasha-joto—kabla ya kusambaa. Kama silaha zilizo tayari, vimekusudiwa kumaliza adui kabla hajapata nguvu.

Kwa kuwa adui huyo huzuka kwa njia mbalimbali—mioto ya mbao, mioto ya mafuta na gesi, mioto ya umeme—vizima-moto vidogo vilevile huwa vya aina mbalimbali. Bila shaka, utapendezwa kufahamu adui yako na silaha uliyo nayo. Hilo halimaanishi kuwa na ujuzi wa mzima-moto stadi, bali yamaanisha kuelewa kanuni fulani za msingi. Kwa kielelezo, ungalifanya nini chini ya hali ifuatayo?

Mwokaji mmoja alikuwa akipasha joto rafu ndani ya oveni iliyokuwa na vikaango vipya 20, vilivyopakwa mafuta akijitayarisha kuoka mikate. Kirekebisha-joto kilikuwa na kasoro na hivyo joto likazidi hadi mafuta yakaanza kufuka moshi. Upesi yule mwokaji, akiwa amesitiri mikono yake na glavu, alifungua oveni na kuburuta nje ile rafu. Jambo hilo likawa kama kupuliza moto. Pu! Moto mkali ulilipuka mara hiyo na miali ikapaa kuelekea dari. Yule mwokaji hakupatwa na dhara lolote, alikimbia nje chapuchapu na kurejea hima na kizima-moto kilichokuwa na kaboni dioksidi na kuuzima moto huo upesi. Lakini punde si punde moshi ulizuka na mafuta yakashika moto tena. Hali hiyo ilizuka mara nne! Akihofia kwamba kaboni dioksidi ingemalizika kabla ya moto kuzimika, alichukua blanketi ya kuzima moto kutoka kifuko chake kilichokuwa karibu na kuifunika ile rafu. Alifarijiwa kuona ule moto ukizimika—kabisa.

Kwa kawaida, sisi huelekea kutumia kizima-moto kilicho karibu ili kuzima moto mdogo lakini unaotisha kusambaa. Hata hivyo, iwapo yule mwokaji angeelewa uwezo wa hewa kuchochea moto—jambo linaloelekea kutukia kunapokuwa na moshi—angezima tu umeme kwenye oveni, kufunga mlango wa oveni, na kuruhusu vilivyo ndani ya oveni kupoa tu vyenyewe. Au angalifunika moto kwa blanketi ya kuzima moto kwanza, kisha iwapo ni lazima, atumie kizima-moto chenye kaboni dioksidi. Kwa vyovyote vile, kisa hiki chaonyesha uhitaji wa kufahamu kimsingi namna moto unavyoanza na njia bora ya kuuzima.

“Pembetatu” ya Moto

Ile inayojulikana kama pembetatu ya moto ni kanuni madhubuti inayoonyesha hali zinazosababisha moto: fueli + oksijeni + joto = moto. Ukiondoa mojawapo ya vitu hivyo moto huzimika mara hiyo na huzuia pia moto kulipuka tena. Acheni tuone ukweli wa jambo hilo.

FUELI: Kama tunavyokufa tukikosa chakula ndivyo inavyotukia kwa moto pasipo fueli. Wazima-moto hutumia kanuni hii kuzima moto wa misitu na vichaka wanapokata kijia mbele ya moto. Ili kuondoa fueli jikoni, huenda linalohitajiwa tu ni kuzima gesi. Hata hivyo, katika sehemu nyinginezo huenda ikawa vigumu au hata isiwezekane kabisa kuondoa fueli.

OKSIJENI: Kwa mara nyingine tena, sawa na sisi, lazima moto upate hewa. Rusha mchanga kwenye moto au funika moto kwa blanketi ya kuzima moto na moto utazimika. Hata hivyo, si lazima oksijeni iishe kabisa ili moto uweze kuzimika. Ukipunguza tu kiwango cha oksijeni kutoka kile cha kawaida cha asilimia 21 katika hewa hadi asilimia 15, vitu vingi kama vile, vioevu vinavyoweza kuwaka moto na hata vitu vingine mango, vitakoma kuwaka moto.

JOTO: Chanzo cha joto liwezalo kuanzisha moto chaweza kuwa, kipasha-joto, jiko, soketi zenye vifaa vingi kupita kiasi, cheche au kaa lenye moto, radi, au joto linalotoka kwenye mimea inayooza, kemikali zinazotoa mvuke, na vitu vingine vingi. Kumbuka kwamba uonapo moshi, na hasa ukifuka kwenye mafuta ya kupikia au kukaangia yaliyo jikoni, tahadhari kwamba moto unaweza kulipuka wakati wowote.

Vimekusudiwa Kuzima Moto Wowote Mdogo

Ingawa vizima-moto havipatikani katika nyumba nyingi, sheria hudai kwamba majengo ya umma, viwanda, na ofisi ziwe navyo. Vizima-moto vya kawaida huwa na maji, kemikali nyevu, povu, poda kavu, na kaboni dioksidi. Vizima-moto vyenye gesi ya haloni havitengenezwi tena kwa sababu inadhaniwa kwamba haloni inaharibu tabaka la ozoni kwenye anga la dunia. Ili kuwasaidia watumiaji kuchagua kizima-moto kifaacho wakati wa dharura, vingi huwa na picha au rangi mbalimbali zinazoonyesha mahali viwezapo kutumiwa au visipoweza kutumiwa. Na vizima-moto vingi huwa na herufi, kama vile A, B, au C, kuainisha moto hususa ambao vinaweza kuzima. Gesi iliyoshinikizwa hutumiwa kusukuma nje kwa nguvu nyingi mkorogo unaozima moto vali inapofunguliwa. Kwa sababu vizima-moto vimejaa gesi iliyoshinikizwa, vyahitaji kukaguliwa mara kwa mara. Vizima-moto vyapasa kuwekwa karibu na milango, mahali vinavyoweza kuchukuliwa kwa urahisi. Acheni sasa tuchunguze kifupi kila aina ya kizima-moto.

Vizima-moto vya poda kavu hudhibiti moto kwa kutumia kemikali na ndiyo aina inayopendwa sana kote ulimwenguni. Poda kavu inaweza kukabiliana na mioto aina ya A na B na hata inazima mioto aina ya C (inayotokana na vifaa vinavyotumia umeme). Kwa sababu hiyo, kizima-moto hicho chenye uwezo mkubwa chatosha kulinda nyumba yako. Poda kavu huchafua—lakini afadhali kuchafua nyumba kuliko ichomeke!

Vizima-moto vya maji yaliyoshinikizwa hufaa katika kuzima mioto ya karatasi, miti, plastiki, takataka, au nguo. Kwa kawaida mioto hiyo ni aina ya A. Maji huzima moto kwa urahisi kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kufyonza joto. Yanapokuwa mengi vya kutosha, maji hufyonza joto haraka na kuushinda moto nguvu. Hata hivyo, usitumie maji kuzima moto wa vioevu vinavyoweza kuwaka moto. Moto utasambaa tu—kwa kulipuka! Pia, kwa sababu maji hupitisha umeme, usitumie kizima-moto cha maji au chenye mchanganyiko wa maji kuzima moto palipo na nyaya zenye umeme.

Vizima-moto vya kemikali nyevu huwa na mchanganyo ulioshinikizwa wa maji na chumvi za alkali na vinafaa sana kuzima moto unaotokana na mafuta ya kupikia na kukaangia lakini havina uwezo wa kupambana na moto wa petroli. Vinaweza pia kupambana na mioto aina ya A.

Vizima-moto vya povu ni vifaa tosha kwa mioto aina ya A na hasa mioto aina ya B inayohusisha vioevu vinavyoweza kuwaka moto (mafuta ya viwandani, fueli mbalimbali, rangi). Kuna aina mbili za vizima-moto vya povu, kwa hivyo chagua kinachokufaa zaidi. Povu hiyo hudhibiti moto kwa kufanyiza utando juu ya kioevu kinachoungua na kuzuia mvuke na oksijeni kupenya. Hivyo basi, ili povu ifanyize utando juu ya kioevu inafaa kunyunyizwa kwa uangalifu ili isipenye. Jihadhari usitumie povu karibu na umeme.

Vizima-moto vya kaboni dioksidi vyaweza kutumiwa kwa aina zote za mioto ila mioto ya gesi. Hufanya kazi kwa kanuni ya kwamba kaboni dioksidi humaliza oksijeni. Lakini kama tulivyoona awali, ikiwa kitu kinachoungua kinabaki na joto, basi moto unaweza kulipuka tena. Kaboni dioksidi ni gesi na haitafaa mahali penye upepo. Hata hivyo, kwa sababu ni safi inafaa zaidi kwa mashine ziwezazo kuharibika upesi na vyombo vya kielektroni. Lakini, kaboni dioksidi inaweza kufisha kwenye sehemu zisizo na hewa, hivyo mara tu moto uzimikapo toka nje na ufunge mlango.

Blanketi ya kuzima moto * inafaa katika kupambana na mioto midogo kama ile inayoweza kuzuka juu ya jiko au kwenye sehemu ndogo ya zulia. Ivute hiyo blanketi kutoka kwenye kifuko chake nadhifu ukutani, ikunjue mbele yako ili ujikinge na miale ya moto, kisha itandaze juu ya moto. Ikiwa bado hujazima chombo chenye kutoa joto fanya hivyo mara moja iwapo yawezekana.

Blanketi za kuzima moto zaweza kuokoa uhai iwapo nguo zako zashika moto. Hilo linapotukia, kumbuka onyo hili muhimu: “Simama, jilaze chini na ujibingirishe.” Usikimbie Kamwe; utachochea moto tu. Iwapo wewe au mtu mwingine aweza kukufunika blanketi unapobingirika, moto utazimika haraka zaidi.

Bora Kuliko Vizima-Moto

Bila shaka, ulinzi madhubuti dhidi ya mioto ni kuizuia; hivyo uwe mwangalifu. Weka viberiti na vitu vingine vya kuwasha moto mbali na watoto. Weka mbali na jiko vitu vyote viwezavyo kushika moto. Unapopika usivae kamwe nguo zenye mikono yenye kuning’inia inayoweza kushika moto. Weka vifaa vya kugundua moshi katika nyumba yako.

Yafuatayo ni madokezo zaidi. Usijaze kamwe vifaa vingi kupita kiasi kwenye soketi za umeme. Usiache kamwe mafuta ya kupikia au ya kukaangia kwenye moto bila mtu kuwepo. Hakikisha mahali unapoweka vipasha-joto ni salama. Iwapo una mitungi ya gesi karibu na nyumba, elekeza vali za usalama—ambazo hulipuka moto unapozuka—mbali na nyumba. Tumia fyuzi za umeme za saizi ifaayo. Badilisha nyaya za umeme zilizochakaa.

Je, umefikiria kufanya mazoezi kuhusu hatua za kuchukua moto unapotokea nyumbani? Hilo laweza kuokoa uhai. Panga mahali mahususi pa washiriki wa familia kukutania—mahali popote palipo wazi na salama na pawezapo kufikika kwa urahisi mchana au usiku. Gawia wengine madaraka: Ni nani atakayewaondoa hatarini watoto au walemavu? Ni nani atakayewasiliana na idara ya moto? Naam, mazoezi huokoa uhai kwa sababu huzoeza watu kutenda kwa haraka na bila kusitasita.

Balaa Itokeapo

Kumbuka kwamba vitu vinaweza kununuliwa lakini uhai hauwezi kununuliwa. Usihatarishe uhai wako ukijaribu kupambana na moto. Hata hivyo, iwapo ni salama unaweza kujaribu kuuzima moto lakini uwe katika eneo lenye mlango wa kutokea. Lakini, iwapo unafikiri kwamba kizima-moto ulicho nacho hakifai au moto ni mkali mno ondoka mara moja na uwasiliane na idara ya moto.

Pia, kumbuka kwamba watu wengi hufa kutokana na moshi wenye sumu unaotoka kwa plastiki kuliko moto wenyewe—unaweza kufisha katika muda usiozidi dakika mbili! Kwa hivyo, inama unapokuwa ukitoka katika jengo linalochomeka. Kuna moshi mchache karibu na sakafu, na hewa huwa baridi kidogo. Ikiwezekana, funika mdomo kwa kitambaa kinyevu. Kabla ya kufungua mlango, uguse kwa sehemu ya nyuma ya kiganja. Ikiwa ni moto, basi moto uko upande wa pili; hivyo tafuta mlango mwingine. Funga kila mlango unaopitia. Jambo hilo hupunguza kiwango cha oksijeni inayofikia moto. Bila shaka, lifti hazipasi kamwe kutumiwa wakati wa moto—unaweza kunaswa humo kisha uchomeke kabisa!

Kwa hiyo, iwapo unataka kununua kizima-moto cha nyumbani, cha gari au cha biashara yako, inafaa kuzungumza kwanza na idara ya moto ya kwenu. Mambo mengine hususa huenda yakatofautiana kati ya nchi moja na nyingine na hivyo hayazungumziwi katika makala hii.

Kwa vyovyote vile, utakapopita karibu na mojawapo ya vidude hivyo vidogo, tua na ukichunguze zaidi. Huenda kitakusaidia sana siku moja.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 18 Iwapo blanketi ya kuzima moto hutumika kwa ukawaida katika nchi yenu, basi hakikisha unajua jinsi ya kuitumia ifaavyo. Shirika la Kujikinga na Moto la Kitaifa la Marekani lasema hivi: “Inapasa kukaziwa kwamba . . . blanketi ya kuzima moto si muhimu sana. Zapasa kutumiwa tu iwapo zapatikana kwa urahisi. . . . Kutumia blanketi ya kuzima moto isivyofaa kwaweza kuzidisha majeraha ya moshi na moto iwapo blanketi yapeperusha moshi kuelekea uso au ikiwa blanketi haiondolewi mara moto uzimikapo.”

[Mchoro/Picha katika ukurasa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MOTO

fueli

joto

oksijeni

[Picha]

AINA YA A

AINA YA B

[Hisani]

Chubb Fire Safety

[Mchoro katika ukurasa wa 26]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Nguo zako zikishika moto, usikimbie

1. SIMAMA

2. JILAZE CHINI

3. JIBINGIRISHE

[Hisani]

© Coastal Training Technologies Corp. Reproduced by Permission

[Picha katika ukurasa 24]

Kuna aina nyingi za vizima-moto vinavyoweza kutumiwa nyumbani kupambana na mioto mbalimbali

[Hisani]

Picha iliyo juu: Reprinted with permission from NFPA 10 - 1998, Portable Fire Extinguishers, Copyright © 1998, National Fire Protection Association, Quincy, Massachusetts 02269. This reprinted material is not the complete and official position of the NFPA on the referenced subject which is represented only by the standard in its entirety.