Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hekaheka za Ulimwengu Huu

Hekaheka za Ulimwengu Huu

Hekaheka za Ulimwengu Huu

Je, Wewe Huhisi Nyakati Nyingine Umelemewa Na Hekaheka Za Maisha? Je, Hali Hiyo Hukuacha Umevunjika Moyo, Mchovu, Na Hoi? Ikiwa Ndivyo, Basi Si Wewe Peke Yako.

KWA mamilioni ya watu, hasa wakazi wa mijini, maisha yamekuwa ya kutatanisha na yenye hekaheka zenye kuchosha. Ndivyo ilivyo hasa katika nchi za Magharibi. Kwenye mkutano mmoja wa kidini huko Marekani, msemaji mmoja aliwaomba wasikilizaji wake wainue mikono iwapo ni kawaida yao kuhisi wamechoka. Papo hapo, mikono ikajaa hewani.

Kitabu Why Am I So Tired? chasema hivi: “Maisha ya kisasa yamejaa mikazo isiyokuwepo awali—kuwahi ndege, mambo ambayo lazima yatimizwe kwa wakati barabara, kupeleka watoto shule ya watoto wadogo na kuwarudisha nyumbani wakati ufaao—hakika orodha ni ndefu.” Haishangazi kwamba uchovu umetajwa kuwa chanzo cha madhara cha wakati wetu. *

Katika nyakati za kale maisha yalikuwa sahili na hekaheka zilikuwa chache. Watu walielekea kuishi kupatana na majira ya asili—mchana walifanya kazi na usiku walikuwa na familia zao kisha kulala. Leo, kuna sababu kadhaa zinazofanya watu wazidi kuhisi wakiwa hoi na wachovu sana.

Kwa Ghafula, Siku Zimekuwa Ndefu Zaidi

Mojawapo ya sababu huenda ikawa kwamba watu hulala muda mfupi zaidi. Kisababishi kimoja kikuu kilichopunguza wakati wa kulala ni kubuniwa kwa mwangaza wa umeme. Kwa kubonyeza swichi tu, mwanadamu angeweza kurefusha “siku,” na punde watu wakaanza kuchelewa kulala. Kwa kweli, watu hawangeepuka jambo hilo kwa sababu viwanda na mashirika ya kutoa huduma yalianza kufanya kazi saa 24. Mwandikaji mmoja alisema hivi: “Ukawa mwanzo wa jamii yenye shughuli saa 24.”

Kusitawi kwa tekinolojia nyinginezo, kama vile redio, televisheni, na kompyuta za kibinafsi, kumechangia kunyang’anya watu usingizi wao. Katika nchi nyingi, programu za televisheni huendelea saa 24 kwa siku. Ni jambo la kawaida kwa wapenzi wa sinema au wa michezo kufika kazini wakiwa wamelemewa na usingizi na uchovu baada ya kuzitazama usiku kucha. Kompyuta za nyumbani zenye vikengeusha fikira vingi huwafanya mamilioni ya watu kuchelewa sana kulala usiku. Bila shaka, hatuwezi kuzilaumu bidhaa hizo; hata hivyo watu huzitumia kuwa udhuru wa kupuuza uhitaji wao wa kupumzika.

Maisha Yasonga Kasi Zaidi

Mbali na siku zetu kuwa ndefu, maisha yaonekana yakisonga kasi zaidi—hali hiyo pia inachochewa na tekinolojia. Mwendo wa gari lenye kukokotwa na farasi lililotumika karne moja hivi iliyopita, ulikuwa wa chini sana ukilinganishwa na ule wa magari, treni, na ndege za kisasa zenye kasi sana. Kwa hakika, mfanyabiashara wa siku hizi, ambaye yamkini babu yake alienda kazini kwa miguu, kwa farasi, au baiskeli, anaweza kuvuka Bahari ya Atlantiki kwa ndege katika muda unaopungua nusu siku!

Vilevile, kumekuwa na mabadiliko makubwa yasiyokuwa wazi katika ofisi ili kuongeza mwendo wa kufanya kazi. Mahali pa taipureta na barua za kawaida pamechukuliwa na kompyuta, mashine za faksi na E-mail. Nyumbani kumekuwa kama ofisini kwa sababu ya kompyuta ndogo, simu za mkononi na bipa (pager).

Bila shaka, hakuna mtu awezaye kupunguza mwendo wa ulimwengu unaozidi kuongezeka. Hata hivyo, sisi wenyewe tunaweza kufanya marekebisho ili tuishi maisha matulivu na yenye usawaziko. Lakini kabla ya kuzungumzia jambo hilo, acheni tuchunguze baadhi ya athari za hekaheka za siku hizi zinazoweza kutupata sisi wenyewe na jamii kwa ujumla.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Uchovu wa daima unaweza kusababishwa au kuchochewa na sababu nyinginezo mbali na mikazo ya kila siku. Sababu hizo zinaweza kutia ndani matatizo ya afya, lishe isiyofaa, dawa, uchafuzi wa kemikali, matatizo ya kihisia na kiakili, uzee, au mchanganyo wa mambo hayo.