Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Ugonjwa wa Kudumu Tuna watoto watatu—mmoja ana ugonjwa wa Down’s syndrome na mwingine ana anemia aina ya sickle-cell. Hivi majuzi, mtoto huyo mwenye anemia aina ya sickle-cell alikuwa na tatizo kubwa naye alilazimika kulazwa hospitalini, sote tulisononeka sana. Nilihisi kwamba Yehova amejibu sala zangu nilipopokea nakala ya Amkeni!, Mei 22, 2000, yenye mfululizo wenye kichwa “Ugonjwa wa Kudumu—Kukabiliana Nao Mkiwa Familia.” Makala hizo zilinipa mimi na mke wangu kitia-moyo cha kuendelea kuvumilia. Pia ziliimarisha tumaini letu kwamba hivi karibuni hakuna mtu atakayesema: “Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.

E.J.M., Brazili

Tuna mwana mwenye umri wa miaka 19 ambaye ana ugonjwa wa kuchanganyikiwa kiakili (schizophrenia). Tumeona vitabu vingi ambavyo huzungumzia ugonjwa lakini hatujapata kamwe kusoma kichapo chochote ambacho huzungumzia jinsi familia inavyoweza kukabiliana na ugonjwa, kama zilivyofanya makala hizo. Zilisimulia kabisa msononeko wangu na mateso yangu, kana kwamba kuugua kwangu moyoni kulikuwa kumeandikwa.

H. T., Japani

Kwa miaka kumi iliyopita, nimekuwa na ugonjwa wa kudumu unaodhoofisha, niliguswa moyo sana na jinsi mlivyosimulia vile ambavyo mtu huhisi. Nyakati nyingine ni rahisi mtu kupoteza usawaziko wa kiakili na kiroho, lakini akina ndugu katika kutaniko langu wameonyesha kwamba wanataka kuelewa mateso yangu. Kwa maneno yenye busara, wananitia nguvu ya kuendelea kuishi.

M. M., Italia

Tulisoma makala hizo tukiwa familia. Binti yangu alipatwa na tatizo la mafigo na amekuwa akisafishwa damu kupitia mashine ya figo kwa miaka mitano. Imekuwa vigumu sana kukabiliana na hali hiyo. Mara nyingi ameponea chupuchupu kufa hivi kwamba twaishi katika hali ya wasiwasi, hatujui tatizo jingine litatokea lini. Lakini ushauri wenu ulisaidia sana. Lazima tuthamini kila siku. Sala ni muhimu pia. Kujua kwamba Yehova huelewa hisia zangu hunisaidia.

S. J., Marekani

Moyo wangu ulisisimuka kujua kwamba mtu fulani anaelewa uchungu wa kuwa na ugonjwa wa kudumu! Nimetazama wasichana wangu wote watatu mmoja baada ya mwingine wakiteseka kutokana na kifafa, kama mimi. Makala kama hizi hutusaidia kupata kuelewa na kuonyesha akili ya Kristo.

G. L., Marekani

Anaconda Naishi sehemu ambayo ina anaconda. Mara nyingi watu husimulia mengi juu ya nyoka hawa, lakini ni vigumu kujua kama uamini au usiamini. Makala yenu “Anaconda—Je, Wanafunua Siri Fulani?” (Mei 22, 2000) ilinisaidia kutofautisha ukweli na hadithi yenye kubuniwa, nayo ilijibu maswali yangu yote kuhusu viumbe hawa wa ajabu.

J. S. P., Brazili

Akina Baba Wanaotoroka Wajibu Nimekuwa nikisoma Amkeni! kwa miaka 25, nami naamini kwamba habari hii haijapata kuzungumziwa. (“Vijana Huuliza . . . Akina Baba Wanaotoroka Wajibu—Je, Kweli Waweza Kutoroka?” Mei 22, 2000) Habari ya akina mama wasio na wenzi, imepata kuzungumziwa, lakini daraka la baba mchanga bado halijazungumziwa. Sikuweza kuelewa kwa nini baada ya watu wawili kufanya uasherati, ni mama na mtoto tu ndio huathiriwa na matokeo ya baadaye. Nilipata mimba nilipokuwa na umri wa miaka 19. Mvulana huyo hakutaka kamwe kuchukua daraka lake. Tafadhali endeleeni kuwaambia vijana ‘waukimbie uasherati.’—1 Wakorintho 6:18.

C. C., Hispania

Ukumbi wa Michezo wa Ugiriki Laiti ningeweza kuwaambia zaidi jinsi nilivyothamini makala “Ukumbi wa Michezo ya Kuigiza wa Epidaurus—Haujabadilika kwa karne Nyingi.” (Juni 8, 2000) Nilitazamia kwamba makala hiyo ingevuta fikira, na kweli ikawa hivyo. Hata hivyo, sikutazamia kwamba ingekuwa na habari nyingi za kiroho jinsi hiyo!

K. S., Marekani