Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Machungwa Yanapokosa Rangi ya Machungwa

Machungwa Yanapokosa Rangi ya Machungwa

Machungwa Yanapokosa Rangi ya Machungwa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

MACHUNGWA hukosa rangi ya machungwa lini? Huenda hilo likasikika kuwa ulimbuaji wa maneno katika Kiswahili, lakini sivyo ilivyo. Kwenye kisiwa cha Sicily nchini Italia, jibu la wazi ni, “Yanapokuwa mekundu!”

Tunaongea juu ya machungwa mekundu ya Sicily (Sicilian blood oranges), yanaitwa hivyo kwa sababu ya rangi nyangavu sana ya nyama yake, ambayo yaweza kuwa na rangi ya machungwa na vishipajani vyenye rangi ya rubi na rangi nyekundu sana hadi nyekundu iliyoiva na rangi inayokaribia kuwa nyeusi. Ganda lake lina rangi ya machungwa iliyochanganyika na rangi nyekundu au rangi hafifu ya zambarau, na harufu yake nzuri huchochea sana hamu. Ladha yake ni tamu kupindukia, watu fulani husema kwamba yana “ladha ya rasiberi.”

Miti ya jamii ya mchungwa imepandwa Italia tangu nyakati za kale. Yamkini machungwa yaliletwa Sicily kutoka Asia katika karne ya nne W.K., lakini machungwa hayo yalikuwa makali na yenye rangi ya manjano. Machungwa matamu yaliletwa Ulaya na Wareno katika karne ya 14 na 15 na kutoka huko yalipelekwa Amerika pamoja na matunda mengine ya jamii hiyo. Hata hivyo, machungwa mekundu yalitambuliwa rasmi kwa mara ya kwanza katika Sicily mwanzoni mwa karne ya 20.

Mbona Ni Mekundu?

Machungwa yote huwa na karotini, rangi ileile ya asili ya machungwa na manjano inayofanya viini vya yai na karoti ziwe na rangi zake. Jambo la kushangaza kuhusu machungwa mekundu ya Sicily aina ya Moro, Tarocco, na Sanguinello ni kwamba yanatokeza dutu nyekundu inayoitwa anthosianini, ambayo hufanya matunda mabivu yawe na rangi nyekundu. * Lakini ukihamisha mchungwa wa Sicily kutoka hapa—sehemu mahususi katika majimbo ya Katania, Sirakusi, na Enna—na kuupanda kwingineko, matunda yanayozaliwa huenda yasiwe mekundu hata kidogo. Kwa nini? Kwani kuna nini cha pekee mashariki mwa Sicily?

Hali zote zinazochangia kuwapo kwa anthosianini katika machungwa mekundu ya Sicily hazijulikani. Lakini bado inahitaji kuchunguzwa ikiwa udongo unachangia kwa vyovyote rangi ya matunda hayo. Hali nyingine zenye kubadilika huzidisha au kuzuia usitawi wa rangi nyekundu wakati tunda linapoiva. Kwa mfano, imeonekana kwamba rangi huanza kuwa nyekundu kunapokuwa na baridi kali usiku na mwangaza unapokuwa mwingi wakati wa mchana. Kuhusu ladha ya tunda, mwangaza mwingi wa jua hutokeza kiasi barabara cha sukari sahili, ilhali mvua ya kadiri huhakikisha kwamba tunda lina ladha murua kabisa.

Hali hizo za pekee kwa ujumla hudhaniwa kuwa zinachangia sifa za pekee za machungwa mekundu ya Sicily. Matunda kama hayo yamekuzwa sehemu nyinginezo kusini mwa Italia vilevile Hispania, Moroko, Florida, na California, lakini, yasemekana kwamba hakuna mtu aliyefaulu kupanda matunda yenye sifa sawa kabisa na machungwa mekundu ya Sicily.

Tunda Linalohitaji Kuthaminiwa

Mbali na rangi yake ya pekee, matunda hayo yana kiwango kikubwa cha lishe. Machungwa aina ya Tarocco yana kiasi kikubwa zaidi cha vitamini C katika jamii yote ya machungwa. Chungwa lenye ukubwa wa kadiri tu lina vitamini ya kutosha kiasi kinachopendekezwa kila siku. Yadaiwa kwamba machungwa mekundu ya Sicily yana manufaa tele. Baadhi ya manufaa hayo ni, glasi ya maji mazito ya matunda yaliyotengenezwa hivi sasa ni matamu na huwa na kabohidrati sahili, madini, na nyuzi zinazofyonzwa mara moja na mwili na kutokeza nishati muhimu kwa afya. Ndiyo sababu, wakuzaji wa machungwa mbalimbali katika Sicily wanajitahidi kulinda bidhaa zao za pekee na kufanya watu wazithamini zaidi.

Wataalamu wanaamini kwamba matunda hayo ya Sicily ni “miongoni mwa machungwa bora zaidi ya kitindamlo kwa sababu ya ladha yake tamu sana, yenye kiasi kinachofaa cha asidi na sukari, ladha hiyo hudumu mdomoni kwa muda mrefu.” Siku moja huenda ukapata fursa ya kuyaonja na kuona iwapo unakubaliana nao.

Ijapokuwa chungwa jekundu la Sicily liligunduliwa hivi karibuni, ni mojawapo ya vyakula chungu nzima vyenye kupendeza ambavyo Yehova aliumba ili kumfurahisha mwanadamu. Kwa hiyo, kwa mtu yeyote anayethamini ukarimu wa Mungu, hata ‘miti yenye matunda . . . hulisifu jina la BWANA.’—Zaburi 148:9, 13; Mwanzo 1:29.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Karotini na anthosianini ni dutu sawa za asili zinazofanya majani yanayopukutika yawe na rangi ya manjano, ya machungwa, na nyekundu hafifu wakati wa majira ya kupukutika.—Ona Amkeni!, la Septemba 22, 1987, ukurasa wa 16-18, Kiingereza.