Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Walinzi Wanaolinda Afya Yako

Walinzi Wanaolinda Afya Yako

Walinzi Wanaolinda Afya Yako

“BI. YANGU MPENDWA,” akasema daktari huku akichunguza matokeo ya upimaji wa damu, “uwezo wako wa kukinga maradhi ni dhaifu sana.” Veronica alikuwa mgonjwa kwa muda fulani. Alidhoofika sana kwa sababu ya kuugua mkamba mara nyingi, na hivi karibuni sikio lake pia liliambukizwa ugonjwa na akawa na uvimbe wenye kukera kwenye mianzi ya pua.

Mfumo wa kukinga maradhi ukoje, na kwa nini ni muhimu sana? Unafanyaje kazi?

Kulindwa Kutokana na Mashambulizi

Mfumo wa kinga hufanyizwa na molekuli mbalimbali tata na chembe maalumu ambazo hushirikiana katika kupambana na maambukizo. Sisi hutegemea mfumo wetu wa kinga kutulinda kutokana na shambulio la maadui, kama vile bakteria au virusi.

Kwa kielezi, twaweza kulinganisha mwili wetu na jiji la kale. Jiji lilijengwa kwenye kilima ili kuweza kuona majeshi yoyote yenye uhasama yakiwa mbali. Na jiji lililindwa na kuta nyingi na malango, yaliyolindwa na walinzi. Ulinzi huo ulifanya jiji hilo kuwa mahali salama kuishi. Kwa kulinganisha mwili wetu na jiji la aina hiyo, twaweza kuelewa vyema mambo yanayohitajiwa ili kuulinda kutokana na mashambulizi.

Kinga moja dhidi ya mashambulizi ya viini mwilini mwetu ni ngozi na tando-telezi (kwa mfano, utando ulio puani na kooni.) Ngozi yetu huwa kama kizuizi muhimu sana cha asili. Viini vingi kati ya mabilioni ya viini tulivyo navyo kwenye ngozi huondolewa vinapoambuliwa pamoja na matabaka ya nje ya ngozi.

Tando-telezi si ngumu sana kama ngozi na zaweza kudhuriwa kwa urahisi. Hata hivyo, zina dutu nyingi za asili za kupambana na viini vya maradhi. Mojawapo ya dutu hizo, inayoitwa lisozimi, huwa katika machozi, mate, na jasho. Ingawa hali ya asidi ya jasho yatosha kuzuia ukuzi wa viini vingi vya maradhi, lisozimi huviua kwa kuharibu ukuta wa chembe zake. Ndiyo sababu, mnyama anaweza kuponya majeraha yake kwa kuyaramba-ramba tu.

Walinzi Muhimu Sana—Chembe Nyeupe za Damu

Tuseme kwamba bakteria zinazoweza kuleta maradhi zafaulu kupenya “jiji” letu kupitia kwa jeraha au ambukizo. Jeshi la chembe huanza kazi mara moja, chembe zote huwa na kusudi moja tu—kuondolea mbali kiini cha maradhi kinachoshambulia na kuponya maradhi hayo. Chembe zinazopambana ili kuulinda mwili huitwa leukocytes, au chembe nyeupe za damu. Aina tatu muhimu za chembe nyeupe za damu zinazopambana wakati huo ni monocytes, neutrophils, na chembe za limfu (lymphocytes).

Chembe za monocytes “zinapopata” ishara za kemikali zinazoonyesha sehemu fulani imeumia, zinaibuka katika damu na kupenya tishu iliyoshambuliwa, ambamo zinakuwa macrophages, yaani, “wabugiaji.” Zinabugia maadui wote walio mwilini mwa kiumbe. Kwa kuongezea, zinatoa dutu muhimu zinazoitwa sitokini, ambazo huutayarisha mwili kupambana na ambukizo. Mojawapo ya kazi za sitokini ni kuleta homa. Homa ni muhimu sana kwa sababu ni dalili ya kwamba mfumo wa kinga unafanya kazi. Inaweza kuharakisha muda wa kupona na pia kuwa njia muhimu sana ya kupima ugonjwa.

Kisha, neutrophil “hupata” ishara ya kemikali kutoka katika sehemu yenye maumivu nazo huelekea kasi kusaidia macrophages. Hizo pia huzingira, au kumeza, bakteria. Chembe hizo za neutrophil zinapokufa, zinaondolewa mwilini zikiwa usaha. Kwa hiyo, kutungwa kwa usaha ni njia nyingine ya ulinzi. Hivyo basi, usemi wa Kilatini ambao umetumiwa na madaktari kwa karne nyingi unafaa: pus bonum et laudabile. Wamaanisha “usaha mzuri unaostahili sifa.” Kutungwa kwa usaha husaidia kuzuia ambukizo. Baada ya kumeng’enya viini vya maradhi, rafiki zetu macrophages “huwasilisha,” vipande vya viini hivyo vya maradhi mbele ya chembe za limfu ili kuonya kuhusu wavamizi hao.

Chembe za limfu ni kikundi cha chembe zenye uwezo maalumu wa kupambana na maambukizo. Zinatengeneza kinga-mwili, ambazo hujiambatisha kwa kipande hususa cha kiini cha maradhi. Kuna vikundi viwili vikuu vya chembe za limfu vyenye uwezo mbalimbali. Kwanza kuna chembe za limfu aina ya B, ambazo hutengeneza kinga-mwili na kuzitia katika damu. Chembe hizo aina ya B zimeitwa kundi la wanajeshi wenye silaha wa mfumo wa kinga, nazo hufuma mishale yake, kinga-mwili, kwa usahihi kabisa. Hizo kinga-mwili “husaka” kiini cha maradhi ambacho zinatambua na kushambulia sehemu muhimu ya kiini hicho. Kikundi kingine muhimu cha chembe za limfu, chembe aina ya T, huhakikisha kwamba kinga-mwili zinazozitambua zinabaki juu ya mwili wake. Chembe hizo hutumia kinga-mwili zake kushambulia adui—humenyana ana kwa ana na adui.

Suala hilo huwa tata hata zaidi. Kikundi kidogo cha chembe aina ya T, zinazoitwa chembe-saidizi za T, husaidia chembe-andamani, chembe aina ya B, kutengeneza kiasi kikubwa cha kinga-mwili. Chembe-saidizi za T huwasiliana kabla ya kushambulia. Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kwamba chembe hizo “huwasiliana” kwa msisimuko kupitia kwa ishara za kemikali, na kujadiliana kuhusu adui huyo, maongezi hayo huitwa maongezi ya shauku.

Usaidizi mkubwa hutoka kwa kikundi kingine muhimu, chembe-uaji za asili. Chembe hizo hazitengenezi kinga-mwili, lakini ziko tayari kuua chembe ambazo zimeambukizwa na kuwa “hatari.” Hivyo basi chembe-uaji za asili husaidia pia kulinda hali njema ya mwili.

Mwishowe, kwa sababu ya kuwa na kumbukumbu ya kinga za maradhi, chembe za limfu zinaweza kukumbuka tabia ya kiini cha maradhi, ni kana kwamba zimehifadhi rekodi yake katika faili. Kwa hivyo, endapo kiini cha aina hiyo kitazuka tena, chembe hizo za limfu huwa na kinga-mwili mahususi za kukiangamiza mara moja.

Chembe za macrophages, ambazo huchochea mfumo wa kinga, husaidia pia kwa kubaki kwenye sehemu iliyoshambuliwa na kusaidia kupunguza maumivu. Zinaondoa uchafu wote kutoka katika sehemu iliyoathiriwa, chembe zilizokufa, au mabaki ya chembe yaliyosalia kwenye “uwanja wa mapigano” baada ya pambano, na hivyo hudumisha utulivu na utengamano katika “jiji.”

Mfumo wa Kinga Unapokuwa Dhaifu

Habari hiyo ni muhtasari tu wa jinsi mfumo wa kinga unavyodhaniwa kufanya kazi. Lakini mfumo wa kinga waweza kuwa dhaifu kwa sababu kadha wa kadha: Huenda kukawa na kasoro za asili za mfumo wa kinga na kasoro zinazoibuka katika maisha ya mtu kwa sababu ya kuambukizwa magonjwa.

Mojawapo ya magonjwa mabaya zaidi ya kinga ni UKIMWI, ugonjwa wenye kutisha unaoenea kasi ulioibuka katika miaka ya 1980. Unasababishwa na virusi vinavyoharibu kinga ya mwili wa binadamu (HIV), virusi hivyo vyaweza kushambulia kitovu cha mfumo wa kinga, na kuharibu chembe hususa za limfu hatua kwa hatua. Tokeo ni kwamba sehemu muhimu ya mfumo wa kinga wa mtu huharibiwa kabisa. Baada ya hilo, maambukizo huzuka na kuwa sugu. Kwa kweli, hali huzidi kuwa mbaya, na mwili hukosa njia ya kujikinga. Huwa kama jiji lililo magofu, bila kuta, ambalo linaweza kushindwa na mtu yeyote.

Jambo zuri ni kwamba si kasoro zote za mfumo wa kinga zinazokuwa mbaya hivyo. Veronica, aliyetajwa mwanzoni, alikuwa na kasoro kidogo katika utengezaji wa kinga-mwili mahususi ambayo kwa kawaida huwa katika utando-telezi, hasa katika mianzi ya pua. Ndiyo sababu alikuwa akishikwa na maambukizo mara kwa mara.

Veronica alipata nafuu. Baada ya kusikiliza maelezo ya daktari wake, aliamua kufuata kikamili tiba aliyoagiziwa na daktari. Uvimbe wake wa puani ulipopona, alikubali kupigwa sindano ambazo zingechochea utengenezaji wa kinga-mwili. * Aliacha pia kuvuta sigareti na akajitahidi kupumzika vya kutosha. Muda si muda, afya yake ikawa bora zaidi.

Naam, tumeumbwa ili tuweze kufurahia maisha tukiwa na afya njema. Tunapotafakari hali tata ya mfumo wetu wa kinga na mifumo mingine ya ajabu katika mwili wa binadamu, tunavutiwa na kuchochewa kutoa shukrani kwa ajili ya hekima ya Muumba wetu. (Zaburi 139:14; Ufunuo 15:3) Na ijapokuwa sasa hatufurahii afya njema sikuzote kwa sababu ya kukosa ukamilifu kwa wanadamu, Neno la Mungu lililovuviwa hutuhakikishia kwamba katika ulimwengu mpya utakaokuja karibuni, wanadamu watakuwa tena wakamilifu kiakili na kimwili, hivi kwamba “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 22 Gazeti la Amkeni! halipendekezi tiba yoyote hususa, kwa kuwa linatambua kwamba hilo ni suala linalopasa kuamuliwa na mtu binafsi.

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

MFUMO WA KINGA:

NGOZI NA UTANDO-TELEZI

LEUKOCYTES, AU CHEMBE NYEUPE ZA DAMU

“Monocytes” hupenya tishu iliyoshambuliwa na kubugia bakteria zinazovamia

“Neutrophils” husaidia kumeza bakteria nazo huondolewa mwilini zikiwa usaha

Chembe za limfu zina kumbukumbu ya kinga za maradhi; endapo kiini cha maradhi cha aina hiyo kitazuka tena, kinga-mwili hukiharibu mara moja

Chembe aina ya B hutengeneza kinga-mwili kama mishale iliyofumwa barabara; hizo “husaka” viini vya maradhi na kuvishambulia

Chembe aina ya T hutengeneza kinga-mwili ambazo humenyana “ana kwa ana” na viini vya maradhi

—Chembe-saidizi za T husaidia chembe aina ya B kutengeneza kiasi kikubwa cha kinga-mwili

—Chembe-uaji za asili huua moja kwa moja chembe zilizoambukizwa bila kutengeneza kinga-mwili

[Picha katika ukurasa 15]

Chembe nyeupe za damu zikishambulia bakteria

[Hisani]

Lennart Nilsson