Wasafirishwa Hadi Botany Bay
Wasafirishwa Hadi Botany Bay
Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Australia
“NILIKIOKOTA kitabu hicho njiani,” akajitetea kijana aitwaye Job. Kijana huyo mwenye madoadoa usoni aliye na umri wa miaka 19 alikamatwa alipokuwa akivuka barabara moja jijini London, na kushtakiwa kuwa aliiba kitabu hicho. Kiligharimu fedha ngapi? Senti themanini! Hakimu hakuridhishwa na sababu alizotoa kijana huyo, hivyo akamhukumia adhabu ya kufungwa miaka saba katika koloni ya wafungwa.
Katika upande mwingine wa ulimwengu, katika eneo ambalo sasa linaitwa Quebec, Kanada, mwanamume mmoja aitwaye François-Maurice Lepailleur alishikwa. Alihukumiwa kifo kwa sababu ya kushiriki katika hujuma iliyoshindwa ya waasi wenye silaha dhidi ya serikali ya Uingereza. Hata hivyo, mahakama iliamua kumpa adhabu tofauti.
Mbali na kukiuka sheria ya Uingereza, vijana hao wawili walikabili hali moja. Punde si punde walijikuta wakisafirishwa kwa merikebu hadi mahali paitwapo Australia na kufikishwa katika koloni mpya ya wafungwa ya Botany Bay.
Maisha ya mfungwa nchini Australia yalikuwaje? Ni watu wangapi waliopelekwa huko? Na kwa nini vijana hao wawili wakasafirishwa mbali na nyumbani?
Mbona Wakahamishwa Hadi Australia?
Mwaka wa 1718 serikali ya Uingereza iliamua kupunguza idadi kubwa ya wafungwa magerezani kwa kuwahamisha wahalifu hao. Kufikia mwaka wa 1770 walikuwa wakihamisha wafungwa wapatao elfu moja kila mwaka, wengi wao walipelekwa hasa katika koloni zake huko Maryland na Virginia. Kufikia mwaka wa 1783 Waingereza walikuwa wamepoteza koloni hizo za wafungwa wao katika Vita ya Mapinduzi katika Amerika Kaskazini. Hata hivyo, kufikia wakati huo walikuwa tayari wamepeleka wafungwa 50,000 huko.
Sehemu nyingine ambayo wangehamishia wafungwa ilikuwa eneo la jangwa upande mwingine wa ulimwengu. Ramani ya pwani ya mashariki ilikuwa imechorwa na kufanywa milki ya Uingereza miaka 13 mapema na ofisa wa jeshi la majini aitwaye James Cook. Joseph Banks alikuwa mvumbuzi mwenzi wakati wa safari hiyo, naye alidokeza kwamba nchi hiyo ingekuwa mahali pafaapo pa raia wasiofaa wa Milki ya Uingereza. Kwa hiyo, katika Mei 1787 kundi la kwanza lenye meli ndogo 11 lilianza safari ya umbali wa kilometa 26,000 kuelekea Botany Bay. Kwa muda wa miaka 80 iliyofuata, hadi mwaka wa 1868, jumla ya wafungwa 158,829 walipelekwa Australia.
Safari ya Baharini Isiyo na Kifani
Mnamo mwaka wa 1833, kijana Job na wasafiri wenzake 300 waliwasili katika Ghuba ya Sydney, katika Bandari ya Jackson. Ijapokuwa koloni hiyo iliitwa Botany Bay, sehemu yenye jina hilo iko kilometa kadhaa kusini ya mahali ambapo makazi hayo yalijengwa mwishowe.
Safari hiyo ilikuwa adhabu kali sana kwa baadhi ya wafungwa. Dondoo ifuatayo kutoka kwa maandishi ya kibinafsi ya François Lepailleur yaonyesha kifupi jinsi maisha yalivyokuwa melini: “Mnamo mwaka wa 1840 tulikuwa tukipita Cape of Good Hope [Afrika Kusini] tukiwa katika sehemu inayopakiwa shehena ya meli iitwayo Buffalo, ambayo ilikuwa yenye kuogofya kupita zote, kwa sababu ya giza lililokuwamo daima, sheria kali ambazo zilipasa kufuatwa, wadudu hatari na joto, na pia njaa ilizidisha taabu yetu.”
Jambo la kushangaza ni kwamba, meli hizo za wafungwa zilikuwa na rekodi bora ya afya na usalama kuliko meli nyingine zote zilizoabiri wakati huo. Kwa sababu ya misaada kutoka kwa serikali ya Uingereza, idadi ya waliokufa kati ya mwaka wa 1788 na 1868 haikuzidi asilimia 1.8. Kinyume chake, kuanzia mwaka wa 1712 hadi 1777, kati ya asilimia 3 na asilimia 36 ya abiria waliokuwa hoi katika meli hizo za wafungwa walifia safarini. Kwani, hata meli zilizosafirisha wahamiaji walio huru kutoka Ulaya hadi Amerika zilikuwa na idadi kubwa sana ya waliokufa kuliko ile ya meli za wafungwa!
Mchanganyiko wa Wafungwa
Idadi kubwa hawakufa kwa sababu wafungwa wengi walikuwa vijana. François alikuwa na umri wa katikati ya miaka ya 30, alikuwa na umri mkubwa akilinganishwa na wafungwa wengine. Wengi wao walikuwa na umri wa kati ya miaka 16 na 25, ilhali wengine walikuwa na umri wa miaka 11 tu. Wafungwa wanaume waliwazidi wafungwa wanawake kwa uwiano wa zaidi ya 6 kwa 1.
Idadi kubwa ya watu waliosafirishwa walitoka katika Muungano wa Uingereza. Zaidi ya nusu walikuwa Waingereza, thuluthi moja walitoka Ireland, na maelfu kadhaa ya wafungwa walitoka Scotland. Baadhi yao, kama François, walitoka sehemu za mbali sana za Milki ya Uingereza kama vile nchi zinazoitwa leo India, Kanada, Malaysia, Sri Lanka, na hata kisiwa kidogo cha Malta.
Watu hao waliohamishwa kwa nguvu walikuwa na vipawa na ustadi mbalimbali wenye kuvutia. Baadhi yao walikuwa mabucha, mafundi wa boila, wahunzi wa shaba nyeupe, maseremala, wapishi, watengenezaji wa kofia, washonaji, na wafumaji. Rekodi rasmi zaonyesha walikuwa na ustadi mbalimbali elfu moja, na hilo laonyesha sifa ya ujumla ya wafanyakazi wa Uingereza.
Yaonekana kwamba mara nyingi wafungwa hao walikuwa na elimu zaidi kuliko wafanyakazi waliobaki nyumbani. Robo tatu ya wale waliowasili New South Wales walijua kusoma na kuandika. Kwa ulinganisho, karibu nusu tu ya watu waliobaki Uingereza waliweza kutia sahihi cheti cha ndoa.
Mtu angeweza kuhamishwa hadi Botany Bay kwa sababu ya makosa kama vile kuteka nyara, kuua, na uhaini, lakini mtu angehamishwa pia kwa sababu ya mambo mengine mengi. Kufungua kituo cha burudani siku ya Jumapili, kuiba kitambaa kidogo, au kuwa na mijadala ya Maandiko Matakatifu bila kibali kungemfanya mtu asafirishwe hadi Kizio cha Kusini.
Maisha Katika Nchi Ngeni
Maisha ya wafungwa wa mapema nchini Australia huwakumbusha wengi jinsi walivyopigwa kikatili, kuteswateswa kinyama, na kudhalilishwa. Baadhi yao walipatwa na hali hizo kihalisi, lakini wengi walikuwa na maisha bora kuliko awali.
Mpango fulani ulibuniwa ambapo wafungwa wangeweza kuagizwa kufanyia kazi walowezi na maofisa au hata kufanya kazi za kibinafsi. Kwa hiyo, badala ya kuwa wafungwa wenye minyororo wanaotengeneza barabara muda wote wa kifungo, wangeweza kufanya kazi zao wenyewe au kujifunza kazi mpya. Kwa mfano, Job aliagizwa amfanyie kazi mmiliki mmoja wa shamba aliye tajiri na mwenye fadhili, Job alijifunza ufugaji wa ng’ombe kwenye shamba moja la mmiliki huyo viungani mwa Sydney.
Wafungwa walihitajiwa kufanya kazi siku tano na nusu, au saa 56, kila juma. Kwa kushangaza, muda huo ulikuwa mchache sana ukilinganishwa na ule ambao wafanyakazi wengi wa viwandani nchini Uingereza walikuwa wakitumika wakati huo, walikuwa wakifanya kazi ngumu mchana kutwa kila siku. Wafungwa wangeweza kudai malipo kwa kazi ya ziada, na kwa kawaida waliendesha biashara ndogondogo baada ya kazi, kama vile kuuza nyasi zilizokatwa kuwa chakula cha mifugo.
Na ijapokuwa wengi walicharazwa sana mijeledi, uchunguzi mmoja waonyesha kwamba asilimia 66 ya wafungwa katika New South Wales hawakucharazwa mijeledi hata kidogo au walicharazwa mara moja tu muda wote waliofungwa. Hilo lilimaanisha kwamba mapigo hayo hayakuzidi mapigo waliyopata wanaume katika Jeshi la Uingereza la Nchi Kavu au la Majini.
Mambo hayo hakika, pamoja na taraja la kwamba wafungwa wangeweza kupokea ardhi yao wenyewe mwishoni mwa kifungo, kuliwafanya wengine wapendezwe na safari hiyo. Mwaka wa 1835, W. Cope, msimamizi wa Gereza la Newgate lenye sifa mbaya huko London, aliripoti hivi kuhusu wafungwa waliotishwa kusafirishwa: “Kumi na tisa kati ya ishirini wanafurahia kwenda.” Na msimamizi wa gereza jingine alisema hivi kuhusu wafungwa wake: “Tisini na tisa kati ya mia moja wana hamu sana ya kwenda.”
Mambo Yenye Kuchukiza
Maisha ya wale walioendelea kukiuka sheria yaliweza kuwa mabaya sana. Ripoti moja ilisema hivi: “Kusafirishwa si adhabu nyepesi, bali ni mfululizo wa adhabu, inayohusisha mateso ya kila aina.” Gurudumu la kinu lilikuwa mojawapo ya adhabu hizo. François alieleza hivi kuhusu gurudumu moja: “Ni kinu kinachosaga nafaka ambacho huzungushwa na wafungwa. Wanaume 18 hupanda gurudumu hilo kwa kuendelea na uzani wao huzungusha gurudumu na kinu. Kwa kawaida wanaume hao huwa na jozi ya pingu miguuni mwao, lakini mara nyingi wanakuwa na jozi tatu au nne miguuni mwao, nao hulazimishwa kufanya kazi kama wengine, la sivyo, wanacharazwa bila huruma.”
Wafungwa wanawake wenye utovu wa nidhamu walilazimishwa kuvaa mkanda wa chuma shingoni. Mkanda huo wa chuma wa shingoni ulikuwa na misumari miwili, kila msumari ukiwa na urefu wa angalau futi moja, kutoka kwenye mkanda huo. Vifaa hivyo vizito sana vya kikatili vilionwa kuwa njia pekee ya kuwatia nidhamu wanawake hao.
Makao ya wafungwa kama vile Port Arthur, mashariki ya Hobart huko Tasmania, yalikusudiwa kuwa mahali pa kuwatia adhabu kali wahalifu walioshtakiwa mara ya pili. Ukatili uliotukia humo wafunuliwa na ripoti moja rasmi iliyosema hivi: “Baadhi ya wafungwa . . . walipendelea kifo badala ya kuishi kifungoni, nao walitenda uhalifu ili wahukumiwe kifo.”
Kwa wafungwa fulani waliohamishwa, jambo baya zaidi lilikuwa kutengwa na familia zao. François aliandika hivi: “Familia yangu penzi, je, uhamisho utanitenga nanyi, wapendwa wangu wa moyoni, kwa muda mrefu sana? Jamani, nahuzunika na kusononeka kwa sababu ya kutengwa nanyi! Kutengwa na mke mpenzi na watoto wachanga wanaohitaji kutunzwa na baba mwenye upendo! Familia penzi, sikuzote mimi humsihi Mungu kwa moyo wangu wote aniondolee minyororo inayonizuia hapa, aniweke huru toka uhamishoni ili niweze kurejea kwa familia yangu penzi, wapenzi wote wa moyo wangu.”
Mchango wa Wafungwa
Mnamo mwaka wa 1837, Gavana Bourke alisema hivi: “Katika New South Wales, walowezi wenye bidii na wenye ujuzi wamegeuza jangwa kuwa koloni nzuri yenye ufanisi kwa muda wa miaka hamsini, kwa msaada wa wafungwa.” Wakati huo zaidi ya thuluthi mbili ya wafanyakazi wanaume walikuwa wafungwa au wafungwa waliowekwa huru, walisaidiana na wahamiaji wengineo wasio watumwa kutekeleza kazi hiyo ya ajabu. Kwa sababu ya hali yao au hiari yao, zaidi ya asilimia 90 ya wafungwa wote waliendelea kuishi Australia.
Kijana Job pia alikuwa mmojawapo wa wakazi hao wa kudumu, kwa kuwa alipowekwa huru, alioa, na kuishi huko, hatimaye alikuja kuwa babu ya mamia ya wenyeji wa Australia na New Zealand. Kwa upande mwingine, François alikuwa baadhi ya wafungwa wachache waliorejea makwao na kwa familia zao penzi baada ya kuwekwa huru.
Maendeleo makubwa yalifanywa siku hizo za mapema, na baada tu ya vizazi vitatu mfululizo, hiyo “koloni nzuri yenye ufanisi” ilisitawi na kuwa taifa lenye utamaduni mbalimbali. Kila mwaka sasa, maelfu ya watu kutoka Asia, Kanada, na Ulaya, hata Uingereza, huzuru Australia kwa hiari au huomba uraia. Wanapowasili, wao huona majengo marefu ya zege yakiwa yameenea kwenye ardhi iliyofyekwa na wafungwa na barabara kuu nzuri palipokuwa na vijia vilivyochimbwa na wafungwa hao. Lakini, hata katikati ya barabara za kisasa za Australia, majengo ya kale ya mawe yangali yanadhihirisha kazi ngumu ya wale watangulizi wa mapema waliosafirishwa bila hiari hadi Botany Bay.
[Ramani/Picha katika ukurasa 20]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
BOTANY BAY
[Picha]
JAMES COOK
JOSEPH BANKS
[Hisani]
Cook: Painting by John Weber/Dictionary of American Portraits/Dover; Banks: Dickinson, W. Portrait of Sir Joseph Banks when Mr. Banks. Rex Nan Kivell Collection; NK10667. By permission of the National Library of Australia; mandhari ya ghuba: Fittler, James. Sydney, New South Wales, with entrance into Port Jackson. By permission of the National Library of Australia
[Picha katika ukurasa 23]
(Juu) Eneo Kuu la Kibiashara la Sydney limesitawi palipokuwa na ile iliyoitwa koloni ya wafungwa ya Botany Bay
[Picha katika ukurasa 23]
Old Sydney Hospital, ambayo sasa ni Jumba la Kitaifa la Maonyesho ya Sarafu, ilijengwa na wafungwa
[Hisani]
Image Library, State Library of New South Wales
[Picha katika ukurasa 23]
Hyde Park Barracks, ni gereza lililochorwa na kujengwa na wafungwa
[Hisani]
Hyde Park Barracks Museum (1817). Historic Houses Trust of New South Wales, Sydney, Australia
[Picha katika ukurasa 23]
The Great North Road. Wafungwa walichimba kwa mikono barabara hii kuu yenye umbali wa kilometa 264 katikati ya vilima vya mawe ya mchanga. Iliunganisha jiji la Sydney na Hunter Valley, karibu na Newcastle. Ilikuwa mojawapo ya miradi muhimu sana ya uhandisi-ujenzi katika koloni hiyo
[Hisani]
Managed by the National Parks and Wildlife Service, N.S.W.