Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mkalatusi Ni Wenye Manufaa Kadiri Gani?

Mkalatusi Ni Wenye Manufaa Kadiri Gani?

Mkalatusi Ni Wenye Manufaa Kadiri Gani?

Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Australia

MINGINE ni mikubwa mno—ikiwa na urefu unaozidi meta 90—na ni mojawapo ya miti mirefu zaidi ulimwenguni. Mingine ni mifupi na imejipinda, na hutambaa kwenye ardhi iliyokauka kwa jua. Majani yake yana umbo la kustaajabisha, na maua yake huvutia sana. Yaelekea kwamba umetumia sehemu ya mti huu kwa njia moja au nyingine.

Mikalatusi michache ina majina ya pekee kama vile alpine ash na Tasmanian oak, lakini jamii nyingi huitwa tu mikalatusi ya kawaida (common gum tree). Kwa kweli, ingawa neno la Kiingereza gum hurejezea dutu fulani mumunyifu inayofanyizwa na kabohidrati, hakuna mkalatusi unaofanyiza dutu hiyo. Kwa hiyo jina la Kiingereza gum tree ni jina lisilofaa. Kwa hiyo jina sahihi la Kiingereza la miti hiyo ni Eucalyptus (mikalatusi), na kuna zaidi ya jamii 600 za miti hiyo iliyotoka Australia.

Mikalatusi husitawi katika joto la kitropiki la Jimbo la Kaskazini mwa Australia vilevile katika nyanda kame zilizo mbali na miji. Lakini inasitawi pia katika eneo lenye pepo za Antaktiki zinazotoka kusini mwa Tasmania na ukungu unaotanda kwenye safu ya milima ya pwani. Imeenea sana kiasi cha kwamba mvumbuzi na mwanazuolojia mmoja wa karne ya 19 alilalamika hivi: “Mikalatusi imeenea sana isivyowazika: na majani yake yote yanafanana kabisa.”

Tangu walowezi wa Ulaya walipomiminika Australia katika karne ya 19, mikalatusi imezidi kutokomea. Msitu wa mikalatusi wenye ukubwa wa takriban kilometa 300,000 za mraba umeng’olewa wote kwa sababu ilidhaniwa kwamba miti hiyo inazuia maendeleo. Hata hivyo, si kila mtu aliyekosa kuthamini rasilimali hii muhimu. Katika karne ya 19, mikalatusi mbalimbali ilienea sana ulimwenguni pote.

Maliki, na Daktari

Katika miaka ya 1880, Maliki Menelik wa Pili wa Abyssinia, ambayo sasa inaitwa Ethiopia, alitaka miti yenye kivuli na chanzo cha kuni kwa ajili ya mji wake mkuu mpya wenye ukame, Addis Ababa. Hakuna mti wowote uliotoka Afrika uliofaa eneo hilo lililofyekwa misitu. Kwa hiyo wataalamu wa maliki walitafuta kwingineko mti uliositawi kwenye sehemu yenye jua kali sana kama nchi yao. Jina “Addis Ababa” humaanisha “Ua Jipya,” na huenda jina hilo lilibuniwa kwa sababu ya mkalatusi, mti muhimu wa kigeni ulionufaisha sana uchumi wa Ethiopia baadaye.

Mwanamume mwingine aliyechangia sana kuhamishwa kwa kisasa kwa mkalatusi ni Dakt. Edmundo Navarro de Andrade. Akiwa ameazimia kupanda upya misitu ya Brazili iliyokuwa ikitokomea, alianza kuingiza mikalatusi nchini humo kutoka Australia mnamo mwaka wa 1910. Alipanda mikalatusi milioni 38. Leo mikalatusi zaidi ya bilioni mbili imepandwa nchini Brazili.

Hivyo basi, pamoja na misitu yake ya kiasili ya mvua, Brazili ndiyo nchi yenye mikalatusi mingi zaidi mbali na Australia. Dakt. Navarro alitunukiwa nishani maaulmu kwa sababu ya kazi yake ya pekee ya kunufaisha uchumi wa nchi yake ya Brazili kwa kuleta rasilimali hiyo yenye thamani.

Mti wa Uhai

Mikalatusi fulani kama ile iitwayo mallees, hustahimili sana katika ardhi kavu kwa kuhifadhi maji mengi mizizini. Wakazi wa asili wa Australia na wavumbuzi wa kale waliendelea kuishi katika majangwa yaliyokuwa mbali na miji kwa kunywa maji yaliyo katika mizizi hiyo. Vipande virefu vya mizizi iliyo juu vilifukuliwa na kukatwakatwa vipande vidogo-vidogo. Hewa inapopulizwa ndani ya kipande cha mzizi, utomvu wenye rangi ya dhahabu-hudhurungi huibuka. Ijapokuwa si kinywaji kitamu, inakadiriwa kwamba lita 1.5 za kinywaji hicho kinachookoa uhai zinaweza kukamuliwa kutoka kwa mzizi wenye urefu wa meta tisa.

Jamii nyingine za mikalatusi husitawi kwenye vinamasi, zinafyonza maji mengi sana kutoka kwenye udongo uliojaa maji. Waitalia walitumia mikalatusi inayositawi kwenye vinamasi ili kukausha vinamasi vya Pontine vilivyokuwa na mbu wengi. Eneo hilo sasa limegeuzwa kuwa ardhi muhimu ya kilimo.

Zaidi ya nchi 50 barani Afrika, Amerika, Asia, na Ulaya zimepanda mikalatusi kwa sababu ya kibiashara na kuboresha mandhari. Watengenezaji-fanicha hupenda sana mbao zake zenye rangi nyekundu na ya kaharabu. Kichapo kimoja chasema hivi: “Mbao za mikalatusi ni mojawapo ya mbao nzito, ngumu na zenye kudumu zaidi. Ubora wa mbao zake, pamoja na ukuzi wake wa haraka . . . , hufanya miti hiyo iwe chanzo muhimu sana cha mbao ngumu ulimwenguni.”

Mikalatusi isiyopenywa na maji hutumiwa katika ujenzi wa meli, magati, milingoti ya simu, nyuzio, na vizuizi vilivyo pembeni mwa barabara. Isitoshe, mikalatusi aina ya yellow box na ironbark huchanua makokwa maridadi ambayo hutokeza mbochi tamu, inayotumiwa na nyuki kutengenezea asali tamu sana. Katika miaka ya majuzi, tani milioni 4.5 za vibanzi vya mikalatusi zimeuzwa nje ya Australia, na hivyo kuleta faida ya dola milioni 250 za Marekani kwa mwaka.

Kino, Mafuta, na Tanini

Dutu nyekundu sana iliyo kama gundi inayoitwa kino huchirizika kutoka kwenye magamba na mbao za mikalatusi. Baadhi ya dutu za kino hutumiwa kuhifadhi mbao zisiliwe na wadudu waitwao shipworm. Dutu hiyo hutumiwa pia katika utengenezaji wa dawa inayokomesha uvujaji wa damu. Magamba ya mikalatusi fulani hutokeza tanini, inayotumiwa kugeuza rangi ya ngozi na kutia nguo rangi.

Majani yake yanayohifadhi mafuta muhimu yana umbo la kustaajabisha sana. Huning’inia kama vidole vilegevu vya mkono ulionyong’onyea, ncha zake huinama chini. Majani hayo hutenda kama faneli kubwa kwa sababu ya umbo hilo. Unyevunyevu unaohitajiwa sana hutulia kwenye majani hayo, kisha hutonatona kutoka kwenye ncha zake hadi mizizini.

Mafuta ya mkalatusi, yanayonukia vizuri na yenye kusisimua, hutengenezwa kutoka kwa majani yake baada ya kuchemshwa na kutoneshwa. Mafuta hayo hutumiwa kwa njia mbalimbali, kwa mfano, hutiwa katika marashi, sabuni, dawa, upishi, na bidhaa za usafi. Kiasili, mafuta hayo huibuka kwenye jani yakiwa mvuke na kusambaza hewani matone madogo ambayo hupinda nuru ya jua, hufanya msitu wa mikalatusi uwe na rangi ya pekee ya buluu. Milima ya Blue Mountains, iliyo magharibi kabisa mwa jiji la Sydney, iliitwa jina hilo la pekee kwa sababu ya rangi ya msitu huo.

Ni Makao ya Walaji Fulani Wachaguzi Mno

Mnyama mdogo mnono na maridadi sana mwenye manyoya mengi anayeitwa koala ndiye mwenyeji anayejulikana sana wa msitu wa mikalatusi. Mnyama huyo alaye majani fulanifulani hupendelea kula ncha za majani ya jamii 12 hivi za mikalatusi. Chakula hicho cha pekee chaweza kuwaua wanyama wengine lakini si koala. Mbona?

Hiyo ni kwa sababu ya mfumo wa umeng’enyaji wa koala uliobuniwa kwa njia ya pekee, una kidole-tumbo chenye urefu wa meta moja hadi mbili. Kwa ulinganisho, kidole-tumbo cha mwanadamu kina urefu wa sentimeta 8 hadi 15 tu. Kidole-tumbo cha pekee cha koala humwezesha mnyama huyo mdogo kupata protini zote, kabohidrati, na mafuta anayohitaji kutoka kwenye majani hayo.

Mnyama mwingine wa Australia asiyejulikana sana aliye mlaji mchaguzi wa majani ya mkalatusi kama koala ndiye mnyama mkubwa zaidi wa jamii ya opossum wanaoruka. Mnyama huyo mwenye manyoya mengi na mbeleko analingana na paka wa nyumbani. Ana mkia wenye urefu wa sentimeta 40 hivi ulio na manyoya mengi marefu na mwili wake una utando wa ngozi unaoanzia miguu ya mbele hadi ya nyuma. Kwa kutumia mabawa hayo ya ngozi, opossum huruka kutoka kwa tawi moja hadi jingine, na kunyiririka kwa umbali wa meta 100, hugeuka kwa pembe mraba hewani, na kisha hutua kwenye tawi jingine kwa usalama.

Mioto ya Misitu na Ukuzi Mpya

Mioto ya misitu, kama inavyoitwa nchini Australia, ni tisho kwa msitu wa mikalatusi. Lakini miti hiyo ina uwezo wa kukinza mioto hiyo. Jinsi gani?

Chini ya gamba la mti huo, kwenye shina lake kuna machipukizi bwete ya majani. Gamba na majani ya mti huo yanapoteketezwa kabisa na moto, machipukizi hayo huanza kuota. Shina jeusi la mti huo hufunikwa na majani mengi ya kijani kibichi. Kama tokeo, mti huo huendelea kuishi. Isitoshe, mbegu za mti huo zilizo bwete ardhini mara nyingi huanza kuota, na mmea mpya huchipuka.

Mti Unaostahili Kuthaminiwa

Je, umewahi kuburudisha koo lako kwa dawa inayotokana na mkalatusi au peremende iliyotengenezwa kwa asali ya mkalatusi? Je, umewahi kusafirishwa kwa mashua au kuishi katika nyumba iliyojengwa kwa mbao za mti huo, au kuota moto wa kuni za mkalatusi? Kuna uwezekano mkubwa kwamba kwa njia moja au nyingine umenufaishwa na mti huo usio na kifani. Kwa hivyo, pindi utakapoona koala mwenye manyoya mengi—au kufurahia picha ya koala—na ukumbuke mti huo uliobuniwa kwa njia ya ajabu ambao ni makazi ya koala.

Kwa kweli, mkalatusi ulio mgumu ni mti wenye matumizi mengi.

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Mikalatusi ni mojawapo ya miti mirefu zaidi ulimwenguni

[Picha katika ukurasa wa 17]

Nyuki hutumia mbochi ya mkalatusi kutengenezea asali ya pekee

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mbao za mikalatusi ni “mojawapo ya mbao nzito, ngumu na zenye kudumu zaidi”

[Picha katika ukurasa wa 18]

Koala (kushoto) na “opossum” mwenye mwendo wa kasi (juu) hula majani ya mkalatusi

[Hisani]

© Alan Root/Okapia/PR

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Geoff Law/The Wilderness Society

[Picha katika ukurasa wa 17]

Courtesy of the Mount Annan Botanic Gardens