Takwimu za UKIMWI Zenye Kushtua!
Takwimu za UKIMWI Zenye Kushtua!
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI
THEMBEKA ni msichana wa miaka 12 anayeishi kwenye kijiji cha mashambani kusini mwa Afrika. Wazazi wake walikufa kwa UKIMWI, akaachwa na daraka la kutunza dada zake wadogo watatu, wa miaka kumi, miaka sita, na miaka minne. Mwandishi mmoja alisema kwamba “wasichana hao hawawezi kujikimu na hivyo wanategemea majirani . . . ili kupata mkate, viazi vichache.” Picha ya wasichana hao wanne mayatima ilionyeshwa kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti moja la Afrika Kusini lililoripoti kuhusu Kongamano la 13 la Kimataifa Juu ya UKIMWI lililofanywa Julai 2000 huko Durban, Afrika Kusini.
Mamilioni ya mayatima wa UKIMWI wanakabili hali kama ile ya Thembeka na dada zake. Kongamano hilo lilijadili njia za kukabiliana na tatizo linaloenea sana la UKIMWI, kama vile kuelimisha watu wajikinge na UKIMWI kwa kutumia kondomu, kutumia dawa za bei nafuu za kupambana na UKIMWI zilizopo; na kuandaa fedha zaidi kwa minajili ya kutokeza chanjo za UKIMWI. Jinsi ugonjwa huu unavyowaathiri kwa urahisi wanawake na hasa wasichana wachanga ilijadiliwa pia.
Kwa kusikitisha, mayatima wa UKIMWI ni shabaha ya wanaume wanaoamini kwamba kufanya ngono na msichana bikira ni tiba ya magonjwa yanayoambukizwa kingono. Isitoshe, wanaume wengi hawawezi kumwoa msichana asipozaa kwanza. Ndiposa kutumia kondomu kunaonwa kuwa kunawazuia wasichana kuolewa na kuzaa watoto.
Kwa kusikitisha, wasichana wengi hawajui hatari ya UKIMWI. Likizungumzia ripoti moja iliyotolewa na kongamano la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF), gazeti la Sowetan la Afrika Kusini lilisema hivi: “Uchunguzi wa Unicef uligundua kwamba asilimia 51 ya wasichana wa miaka 15 hadi 19 huko Afrika Kusini hawajui kwamba mtu anayeonekana kuwa na afya njema aweza kuwa na UKIMWI na kwamba anaweza kuwaambukiza.”
Njia nyingine inayosambaza UKIMWI ni wanawake kutendwa vibaya kingono. Ranjeni Munusamy, aliyehudhuria kongamano hilo, aliripoti hivi katika gazeti la Sunday Times la Johannesburg, Afrika Kusini: “Jeuri inayofanywa na wanaume wakatili dhidi ya wanawake bado ni kizuizi kikubwa kuelekea kudhibiti virusi vya UKIMWI na kutoa utunzaji. Jeuri mbalimbali—ubakaji, ngono ya maharimu, wanawake kupigwa na kutendwa vibaya kingono—zadhihirisha kwamba mara nyingi wanawake hulazimishwa kufanya ngono, jambo hatari ambalo huchangia sana uambukizaji wa UKIMWI.”
Takwimu zilizowasilishwa kwenye kongamano hilo zilikuwa zenye kushtua, kama chati inavyoonyesha. Vijana wapatao 7,000 na watoto wachanga 1,000 wanaambukizwa virusi vya UKIMWI kila siku. Katika mwaka mmoja, 1999, watoto wapatao 860,000 katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Sahara walipoteza walimu wao kwa sababu ya UKIMWI.
Kulingana na uchunguzi uliochapishwa na Baraza la Utafiti wa Kitiba la Afrika Kusini, watu milioni 4.2 huko Afrika Kusini wana virusi vya UKIMWI, yaani raia 1 kati ya kila raia 10. Hali katika nchi jirani ni mbaya zaidi. Gazeti la The Natal Witness likiripoti juu ya kadirio lililotolewa na Shirika la Marekani la Sensa lilisema hivi: “Watu katika nchi za Afrika zinazokumbwa na UKIMWI wataanza kupungua kwa sababu mamilioni watakufa kwa ugonjwa huo, na muda ambao watu wanatarajia kuishi utashuka kufikia takriban miaka 30 mwishoni mwa mwongo huu.”
Janga la UKIMWI ni uthibitisho mwingine unaoonyesha kwamba wanadamu wanaishi katika “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo” zilizotabiriwa na Biblia kuwa zingekuwepo katika “siku za mwisho.” (2 Timotheo 3:1-5) Wapendao Neno la Mungu, Biblia, wanatarajia suluhisho kamili na la kudumu la UKIMWI na matatizo mengine yote yanayohangaisha binadamu. Karibuni, Ufalme wa Mungu utachukua hatamu ya uongozi wa dunia. Katika ulimwengu mpya wenye uadilifu, umaskini na uonevu utaondolewa mbali. (Zaburi 72:12-14; 2 Petro 3:13) Badala yake, wenyeji wa dunia watarudishwa kwenye afya kamilifu na hakuna mmoja wao atakayesema kamwe: “Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.
[Blabu katika ukurasa wa 14]
Kuna mayatima wa UKIMWI 13,000,000 ulimwenguni kote
[Chati/Ramani katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
WATU WAZIMA (UMRI 15 hadi 49) WALIO NA UKIMWI, MWISHONI MWA 1999
Amerika Kaskazini 890,000
Karibea 350,000
Amerika ya Latini 1,200,000
Ulaya Magharibi 520,000
Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati 210,000
Ulaya Mashariki na ya Kati 410,000
Asia Kusini na Kusini-mashariki 5,400,000
Asia Mashariki na Pasifiki 530,000
Australia na New Zealand 15,000
Nchi za Afrika Zilizo Kusini mwa Sahara 23,400,000
[Hisani]
Kutoka kwa: UNAIDS
[Grafu/Picha katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
ASILIMIA YA WATU WAZIMA (UMRI 15 hadi 49) WALIO NA UKIMWI NCHI 16 ZA AFRIKA, MWISHONI MWA 1999
1 Botswana 35.8%
2 Swaziland 25.2
3 Zimbabwe 25.0
4 Lesotho 23.5
5 Zambia 20.0
6 Afrika Kusini 20.0
7 Namibia 19.5
8 Malawi 16.0
9 Kenya 14.0
10 Jam. ya Afrika
ya Kati 14.0
11 Msumbiji 13.2
12 Jibuti 11.7
13 Burundi 11.3
14 Rwanda 11.2
15 Côte d’Ivoire 10.7
16 Ethiopia 10.6
[Hisani]
Kutoka kwa: UNAIDS
[Picha]
Thembeka akiwa na dada zake
[Hisani]
Picha: Brett Eloff