Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Madoa Makala ya “Je, Macho Yako Yana Madoa?” (Juni 8, 2000) ilinisaidia sana. Siku tatu baada ya kupata gazeti hilo sehemu ndogo ya retina ya jicho langu la kulia ilibanduka. Nilipoona dalili za ugonjwa huo katika makala hiyo niliamua mara moja kumwona daktari. Matibabu ya leza yalitumiwa kurekebisha tatizo hilo, kwa hiyo uwezo wangu wa kuona haukufifia. Asanteni kwa makala za aina hiyo zenye habari zilizotafitiwa vizuri, na zenye kusaidia maishani.

C. V., Afrika Kusini

Uenezaji-Habari Nimemaliza tu kusoma nakala ya Juni 22, 2000, na ninawashukuru kwa mfululizo wa makala “Je, Wapaswa Kuamini Kila Jambo Usikialo?” Mahali ninapoishi watu wameanza kuzoea kudhihaki Waromany (Wazururaji). Watu hufanya mzaha juu ya jinsi wanavyodhaniwa kuiba. Makala hizo zimenisaidia kuona kwamba mzaha wa aina huo haufai, nami sitashiriki jambo hilo.

K. M., Jamhuri ya Cheki

Kuishi Ng’ambo Asanteni kwa makala ya “Vijana Huuliza . . . Je, Nikaishi Ng’ambo?” (Juni 22, 2000) Mimi husoma kwa ukawaida mfululizo huo wa makala, lakini mara nyingi nimekuwa nikiwaza kwamba hatari nyingine mnazoeleza zimetiwa chumvi. Mwaka uliopita nilisafiri ng’ambo kwa ajili ya mabadilishano ya kitamaduni kati ya shule yangu na chuo kikuu kingine. Hata ingawa jambo hilo lilipendeza halikuwa lenye manufaa upande wa kiroho.

M. P., Italia

Makala hiyo na makala ya “Vijana Huuliza . . . Naweza Kufanikishaje Maisha Yangu Ng’ambo?” (Julai 22, 2000) zilikuwa ‘chakula cha wakati ufaao’ kwangu. (Mathayo 24:45) Tayari nilikuwa nimeamua kuishi ng’ambo kwa muda wa mwaka mmoja ili nijifunze lugha ya kigeni. Kwa hiyo, nashukuru kwa mapendekezo na madokezo yenye kusaidia.

I. Z., Uswisi

Kisiwa cha Ista Makala ya “Somo Muhimu Kutoka kwa Kisiwa Kidogo Sana” (Juni 22, 2000) yaonyesha mahangaiko ya watu wengi wenye wasiwasi juu ya mazingira. Lakini naona kwamba wanaotambua hatari tunayokabili ni wachache. Ninapofikiria jinsi ambavyo watu wameharibu dunia hii, nalia machozi.

K. M., Japani

Kurekebisha Saa Je, kurekebisha saa ni jambo lenye manufaa? Hilo ni swali linalozuka kuhusu makala ya “Kurekebisha Saa—Je, Ni Wazo Lililotolewa Mapema Mno?” (Julai 8, 2000) Muumba wetu mkuu aliweka majira. Ni nani aliye na haki ya kubadili jambo hilo? Kile kinachoitwa kurekebisha saa si jambo la kawaida!

I. L., Ujerumani

Makala yetu haikusifu wala kushutumu desturi ya kurekebisha saa. Tulionyesha tu jinsi ilivyoanzishwa. Mungu hakuweka maagizo maalum jinsi ya kuratibu wakati. Njia za siku hizi za kuratibu wakati hazikuagizwa na Mungu. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba kurekebisha saa zetu mara mbili kwa mwaka hakubadili majira. Na kwa sababu hizo, hakuelekei kuvunja kanuni yoyote ya Mungu.—Mhariri.

Tabasamu Asanteni kwa kuchapisha makala yenye maana ya “Tabasamu—Ni Yenye Manufaa Kwako!” (Julai 8, 2000) Nakubaliana kabisa na habari iliyomo. Ilinikumbusha kuwa na mtazamo unaofaa kila wakati ili tabasamu yangu iwe ya kutoka moyoni. Naam, kutabasamu kwatusaidia kufanya marafiki. Kwasaidia pia kuondoa wasiwasi.

P. C., China