Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sanaa za Jangwa la Namibia

Sanaa za Jangwa la Namibia

Sanaa za Jangwa la Namibia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI

MTINDO wa msanii huyu hubadilika daima, na bado, hutokeza kitu chenye kupendeza. Msanii hutumia mchanga. Msanii huyo ni nani? Ni upepo ambao hufanya marundo ya mchanga yawe na maumbo ya kipekee. Labda umbo linalojulikana hasa ni umbo la mwezi mwandamo. Upande wa rundo la mchanga unaoelekea upepo ni mteremko usio mkali. Mteremko usioelekea upepo ni mkali na mfupi kuliko ule mwingine. Mgongo wa juu wa marundo waonekana kuwa wenye ncha kali, hata hivyo ukipigwa teke ovyoovyo waweza kwa urahisi kufanywa kuwa butu.

Jangwa la Namibia, lililoko sehemu ya kusini-magharibi mwa Afrika, ni mahali pazuri pa kutazama sanaa hizo. Katika jangwa hilo kuna marundo ya mchanga yenye urefu wa zaidi ya meta 400, nayo ni kati ya yale marefu zaidi ulimwenguni. Hata hivyo, Jangwa la Namibia ni dogo kuliko majangwa makubwa ya ulimwengu. Laanzia Bahari ya Atlantiki na kufikia kilometa 160 kuelekea barani, na urefu wake ni kilometa 1,900.

Wasanii Wengine Kazini

Upepo si msanii pekee katika ‘nyumba hiyo ya sanaa’ iliyoko mbali. Unapotazama kwa makini marundo ya mchanga utaona michoro ya kipekee ya wasanii wengine. Kwa mfano, waweza kuona alama inayofanana na nyororo ndefu nyembamba iliyojipinda mchangani. Ukingoja kwa muda, huenda hata ukamwona msanii akifanya kazi. “Nyororo” hiyo ni alama za mguu za mbawakawa wanaotembea mchangani usiku. Karibu na “nyororo,” hiyo kuna mstari wa mashimo madogo yanayofanana. Hayo pia ni alama za mguu, za panya-tembo (elephant shrew) arukaye kuelekea aendapo. Ghafula watambua kwamba ijapokuwa nyumba hiyo ya sanaa iliyoko mbali inaonekana ukiwa inakaa wakazi wengi.

Kaskazini, kwenye pwani ya Skeleton Coast, huenda ukaziona kazi za wasanii wengine wa jangwani. Hao hawafanyi usanii wao kwa utaratibu, kwa hiyo usanii wao unakaa shaghalabaghala. Jihadhari! Wanakuja kwa kasi juu ya rundo la mchanga. Jambo moja ni la hakika, hao hufurahia usanii wao. Viumbe hao wakubwa wateremka rundo la mchanga kwa kasi ajabu, huku wakirusha mchanga kiholela. Hawaridhiki kukimbia, pia wanateleza wakiburuta miguu ya nyuma na kuacha mitaro mchangani. Wanakimbilia dimbwi la maji la karibu, wajirusha ndani, na kucheza kama watoto wenye furaha. Wasanii hao, tembo wa Afrika, wana uzito wa kilogramu 6,000!

Kuna msanii mwingine aitwaye kifutu wa Péringuey ambaye ni mwenye utu na tabia zisizo za kawaida, lakini mpole kuliko tembo. Michoro yake mchangani yafanana na vijiti vilivyojipinda. Nyoka huyo hufanya alama hizo anapotambaa kwa kupinda mwili wake upande mmoja. Ghafula alama zakoma, na kifutu haonekani popote. Yuko wapi? Ukitazama kwa umakini, huenda ukayaona macho membamba mawili yanayokuchungulia mchangani. Mwili wa nyoka huyo umefunikwa kwa mchanga. Akiwa amejificha hivyo, angoja mlo, ambao mara nyingi ni mjusi anayepita.

Aina moja ya alama huenda isifurahishe sana. Ni alama pana za pikipiki zenye magurudumu matatu, zilizoundwa kwa ajili ya kusafiri kwenye nchi kama hiyo. Wanadamu pia wameacha alama zao.

Msanii Anayebadilika-badilika

Wengi sana, wasiohesabika, huacha alama zao mchangani huku. Hao watia ndani kifaru, simba, twiga, na mbweha, ambao wote waweza kutazamwa katika mbuga ya wanyama ya Skeleton Coast na penginepo.

Lakini upepo ni msanii mkuu. Huo waamua jinsi jangwa litakavyokaa na hubadili maumbo yake atakavyo. Sikuzote hufanya mabadiliko. Ukirudi baada ya mwaka mmoja, huenda ukaona kwamba marundo ya mchanga yamesonga meta 30 katika mwaka huo! Hilo ndilo jambo ambalo upepo wa Namibia unaweza kufanya.

[Ramani katika ukurasa wa 27]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

AFRIKA

NAMIBIA

[Picha katika ukurasa wa 26]

Panya-tembo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

Des na Jen Bartlett