Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sili-Watawa wa Mediterania—Je, Wataendelea Kuwapo?

Sili-Watawa wa Mediterania—Je, Wataendelea Kuwapo?

Sili-Watawa wa Mediterania—Je, Wataendelea Kuwapo?

Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Ugiriki

WANYAMA hao wanaonyeshwa wakiota jua kwenye fuo za Ugiriki katika shairi la Homer liitwalo Odyssey. Katika jiji moja la kale la Asia Ndogo sarafu zenye picha yao zilitengenezwa. Zamani Bahari za Mediterania na Bahari Nyeusi zilijaa nao. Hata hivyo, leo ni nadra kuona mmoja wa viumbe hao waoga—sili-watawa (monk seal) wa Mediterania.

Sili-watawa wa Mediterania waliwindwa sana katika karne ya 18 na 19, kama vile wanyama wa baharini wengi wenye manyoya walivyowindwa. Maelfu walichinjwa kwa sababu ya manyoya, mafuta, na nyama zao.

Wakati huu madhara yanaonekana wazi kabisa. Sili-watawa wa Mediterania wanaosalia wanakadiriwa kuwa kati ya 379 hadi 530. Huenda wakatoweka kabisa. Hata hivyo, jarida la habari la Monachus Guardian lataarifu kwamba makadirio ya idadi ya sili hao ni “sayansi isiyo sahihi hata kidogo.”

Je, msaada umechelewa mno? Ni jitihada gani zinazofanywa kuhifadhi sili-watawa?

Mapambano Magumu

Huenda sili-mtawa alipewa jina hilo kwa sababu manyoya yake yana rangi inayofanana na rangi ya mavazi maalum ya dini mbalimbali. Wengi wao huishi kwenye majabali yasiyofikika kwa urahisi na katika mapango ya baharini ya visiwa vya Sporades Kaskazini katika Bahari ya Aegea. Vikundi vidogo vyaweza kupatikana ufukoni mwa Afrika kaskazini-magharibi na visiwa vya Desertas vya Ureno. Sili-watawa ni mmojawapo wa sili wakubwa zaidi ulimwenguni, naye aweza kufikia urefu wa zaidi ya meta tatu na uzito wa zaidi ya kilogramu 275.

Sili-mtawa ana kichwa chenye umbo la kitunguu na manyoya yenye rangi ya fedha, macho meusi tii, pua yenye mianzi mikubwa, masikio yaliyo nyufa ndogo, masharubu yaliyopinda, na videvu vingi vinono. Mwili umefunikwa kwa manyoya mafupi meusi au kahawia na meupemeupe sehemu ya chini. Kwa upande mwingine, sili aliyezaliwa karibuni ana manyoya meusi marefu mgongoni na manyoya meupe machache tumboni.

Kuendelea kuwapo kwa sili-mtawa kwazuiwa na kiwango chake cha chini cha kuzaa. Sili-mtawa wa kike huzaa kitoto kimoja tu kwa mwaka. Na jambo baya hata zaidi ni kwamba, baadhi ya sili-watawa wa kike waliokomaa hawazai kila mwaka.

Lakini si kiwango cha chini cha kuzaa tu kinachosababisha idadi ya sili-watawa kupungua. Dakt. Dennis Thoney, msimamizi wa Matangi ya Viumbe vya Baharini ya New York asema hivi: “Ingawa kiwango cha kuzaa cha sili-mtawa wa Mediterania ni cha chini, hata hivyo idadi ya sili bandari (harbor seal) haipunguki ijapokuwa kiwango chake cha kuzaa ni sawa na cha sili-mtawa. Kwa hiyo, kwa hakika kuna mambo mengine yanayosababisha kufa kwao.”

Washambuliwa

Wazia hali ya nyumba yako baada ya moto kuiteketeza. Mali yako yote—vyombo, nguo, vitu vya thamani vya binafsi na vya ukumbusho—ingekuwa imepotezwa. Maisha yako yangebadilika kabisa. Makazi ya sili-mtawa wa Mediterania yamepatwa na hali kama hiyo. Uchafuzi, utalii, viwanda, na shughuli nyingine za wanadamu zimeharibu makazi ya asili ya sili hao.

Isitoshe, chakula cha sili-mtawa kimepungua sana kwa sababu ya uvuvi wa kupita kiasi. Mwanazuolojia Dakt. Suzanne Kennedy-Stoskopf asema hivi: “Wakati ambapo mawindo hayapatikani kwa urahisi, sili huhitaji kutumia nguvu nyingi zaidi ili ajilishe.” Kwa hiyo, si tu bahari—makazi yao—ambayo imechafuliwa bali pia imekuwa vigumu kwao kupata chakula!

Zaidi ya hayo, uvuvi wa kupita kiasi husababisha sili kadhaa kunaswa katika nyavu na kufa maji. Hata hivyo, mara nyingi sili hao wanauawa moja kwa moja na wavuvi. Kwa nini? Kwa sababu wamejua jinsi ya kuiba chakula kutoka katika nyavu, na huziharibu nyavu wafanyapo hivyo. Hivyo, wanadamu na wanyama wanashindania samaki wanaopungua. Mapambano hayo yamefanya sili-mtawa wakaribie hali ya kutoweka.

Sili-watawa hula samaki, na samaki hao hula viumbe wengine wadogo wa baharini. Hivyo, ikiwa sili-watawa hawasitawi kwa sababu ya upungufu wa chakula, ni ishara inayotegemeka kwamba viumbe wengine wa baharini pia hawana chakula cha kutosha. Ikiwa hivyo ndivyo ilivyo, viumbe wote wa bahari ya Mediterania wamo hatarini.

Je, Wataendelea Kuwapo?

Kwa kushangaza, wanadamu ni adui wakubwa zaidi wa sili-mtawa, na vilevile wao ni wasaidiaji wake wakubwa zaidi. Mashirika ya watu binafsi na ya serikali yameanzishwa ili kuhifadhi sili hao. Mahali pa hifadhi pametengwa kwa ajili yao. Uchunguzi mbalimbali wa wanyama hao wazuri umefanywa mahali wanapoishi ili kujifunza jinsi ya kuwasaidia.

Katika mwaka wa 1988 Shirika la Ugiriki la Uchunguzi na Uhifadhi wa Sili-Mtawa wa Mediterania (MOm) lilianzishwa. Kwa ukawaida watafiti wa MOm huenda kwenye eneo la makazi ya sili-watawa ili kuwahesabu na kukusanya habari zitakazotumiwa katika jitihada za kuwahifadhi.

Hifadhi za wanyama hao hulindwa na kikundi cha walinzi wafanyao doria wakitumia mashua zinazoenda kasi. Walinzi hao pia huwaarifu na kuwafundisha wageni na wavuvi wanaosafiri kwenda Hifadhi ya Taifa ya Viumbe wa Baharini ya Ugiriki kisiwani Alónnisos, ambacho ni mojawapo ya visiwa vya Sporades Kaskazini. Sili wagonjwa au waliojeruhiwa wanapopatikana, kikundi hicho huwatibu na vilevile kuwasafirisha kwenye kituo cha matibabu cha MOm.

Katika Kituo cha Matibabu cha Sili kuna nafasi kwa sili wadogo wasio na wazazi, wagonjwa, au waliojeruhiwa. Hao hutibiwa na kutunzwa hadi wawezapo kuishi pasipo utunzaji. Kufikia sasa, matokeo ni mazuri. Sili-watawa katika visiwa vya Sporades Kaskazini wanaanza kuongezeka baada ya kupunguka haraka kwa miaka mingi.

Je, jitihada hizi zitaendelea kufanikiwa? Tutaona. Hata hivyo, ni wazi kwamba kazi nyingi itahitajika ikiwa mnyama huyo aliye hatarini ataendelea kuwapo. Dakt. David Wildt wa Taasisi ya Smithsonia alisema hivi alipohojiwa na gazeti la Amkeni!: “Viumbe wa baharini kwa ujumla hawaendelei vizuri. Tatizo ni kwamba hatujui vya kutosha juu ya kilichomo baharini, na hatujajua hata kidogo jinsi ya kukihifadhi.”

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

Binamu Hatarini

Sili-watawa wapatikana pia katika bahari nyingine ulimwenguni, na hata sili hao wamo hatarini. Gazeti la National Geographic lasema kwamba sili-watawa wa Karibea, au wa West Indies, walikuwa “sili wa kwanza ambao Columbus aliwaona katika Ulimwengu Mpya. Kwa sababu sili-watawa hupenda kukaa ufukoni na ni wenye manufaa, punde walichinjwa kwa wingi. . . . Sili-mtawa wa Karibea alionekana mara ya mwisho mwaka wa 1952.”

Visiwa vidogo vya French Frigate Shoals, katika Hifadhi ya Taifa ya Wanyama ya Visiwa vya Hawaii, huenda ni kimbilio la mwisho la sili-mtawa wa Hawaii, au wa Laysa. Hata hivyo, wale sili 1,300 waliopo “wanasumbuliwa na matatizo,” ijapokuwa jitihada nyingi za kuwalinda.

Tangu majira ya kuchipua ya mwaka wa 1997, karibu robo tatu ya wale sili-mtawa wa Mediterania 270 wanaoishi pwani ya Mauritania, Afrika Magharibi, wamekufa kwa ugonjwa. Kulingana na ripoti ya gazeti la Science News, sili wengi waliochunguzwa walikuwa wameambukizwa “kirusi cha morbillivirus cha kijinyangumi, ambacho chafanana na kirusi kinachosababisha ugonjwa wa mbwa.”

[Picha katika ukurasa wa 16]

Sili-watawa wana sura ya kipekee, kama vile kichwa chenye umbo la kitunguu na mianzi mikubwa

Mashirika yameanzishwa ili kuhifadhi sili hao

[Hisani]

Panos Dendrinos/HSSPMS

[Picha katika ukurasa wa 17]

Sili-watawa katika visiwa vya Sporades Kaskazini wanaanza kuongezeka baada ya kupunguka haraka kwa miaka mingi

[Hisani]

P. Dendrinos/MOm

D. Kanellos/MOm

[Picha katika ukurasa wa 17]

Sili-mtawa wa Hawaii

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Panos Dendrinos/HSSPMS