Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Twajifunza Nini Kutokana na Mambo Yaliyopita?

Twajifunza Nini Kutokana na Mambo Yaliyopita?

Twajifunza Nini Kutokana na Mambo Yaliyopita?

“Wanahistoria wanathamini sana ubainishaji wa kisababishi na matokeo.”—GERALD SCHLABACH, PROFESA-MSAIDIZI WA HISTORIA.

WANAHISTORIA huuliza hivi mara nyingi, Ni jinsi gani na kwa nini mambo fulani yalitukia? Kwa mfano, twajua kutokana na historia kwamba Milki ya Roma iliporomoka. Lakini kwa nini iliporomoka? Je, ni kwa sababu ya ufisadi au anasa? Je, ilikuwa vigumu mno kuongoza milki hiyo na gharama za kudumisha majeshi yake zikawa juu sana? Je, maadui wa Roma walikuwa wengi mno na wenye nguvu mno?

Hivi majuzi, Ukomunisti wa Ulaya Mashariki, ambao pindi moja ulikuwa tisho kwa nchi za Magharibi, uliporomoka kana kwamba kwa usiku mmoja nchi baada ya nchi. Lakini kwa nini? Na twaweza kujifunza masomo yapi? Hayo ni baadhi ya maswali ambayo wanahistoria hujaribu kujibu. Lakini wanapojibu maswali hayo, maamuzi yao huathiriwa na upendeleo kadiri gani?

Je, Historia Yaweza Kutumainiwa?

Wanahistoria ni kama wapelelezi wala si kama wanasayansi. Wao huchunguza, hufanya udadisi, na kuchanganua rekodi za mambo yaliyopita. Lengo lao ni kubaini ukweli, lakini mara nyingi mradi wao si dhahiri. Kwa sehemu ni kwa sababu kazi yao huhusu hasa watu, na wanahistoria hawawezi kusoma akili za watu—hasa akili za wafu. Wanahistoria wanaweza pia kuwa na dhana na upendezi fulani wa kibinafsi. Kwa hiyo, nyakati nyingine historia inayoonwa kuwa bora kwa kweli huwa ni fasiri inayotegemea maoni ya mwandishi.

Bila shaka, hatuwezi kusema kwamba kazi ya mwanahistoria si sahihi kwa sababu ya maoni yake. Masimulizi ya Biblia ya Samweli, Wafalme na Mambo ya Nyakati yatia ndani masimulizi sambamba ambayo yaliandikwa na watu watano mbalimbali, na bado yaweza kuthibitishwa kwamba hayapingani wala hayana makosa. Ndivyo ilivyo kuhusu zile Gospeli nne. Waandikaji wengi wa Biblia hata walirekodi dosari na makosa yao ya kipumbavu—jambo ambalo ni nadra sana katika vitabu vya kilimwengu.—Hesabu 20:9-12; Kumbukumbu la Torati 32:48-52.

Mbali na uwezekano wa kuwapo kwa upendezi wa kibinafsi, jambo jingine muhimu la kuzingatia unaposoma historia ni madhumuni ya mwandikaji. “Historia yoyote inayosimuliwa na wenye mamlaka, au na wale wenye tamaa ya uongozi au na rafiki zao, ni sharti ichunguzwe kwa uangalifu sana,” asema Michael Stanford katika kitabu A Companion to the Study of History. Madhumuni yenye kutiliwa shaka hudhihirika pia vitabu vya historia vinapotetea utaifa na uzalendo kwa hila au hata waziwazi. Kwa kusikitisha, nyakati nyingine dhana hizo huandikwa katika vitabu vya mafunzo shuleni. Sheria ya serikali ya nchi moja ilitaarifu waziwazi kwamba kusudi la kufunza historia ni “kuimarisha hisia za utaifa na uzalendo katika mioyo ya watu . . . kwa sababu kujua historia ya taifa ni mojawapo ya mambo muhimu sana katika kusitawisha uzalendo.”

Historia Iliyopotoshwa

Mbali na kupendelea, nyakati nyingine historia huwa imepotoshwa. Kwa mfano, ule uliokuwa Muungano wa Sovieti “ulifuta jina Trotsky kutoka kwenye rekodi, hivi kwamba uthibitisho wa kuwapo kwa kiongozi huyo wa kisiasa ulitokomea,” chasema kitabu, Truth in History. Trotsky alikuwa nani? Alikuwa kiongozi wa Mapinduzi ya Bolsheviki ya Urusi naye alikuwa na cheo cha pili baada ya Lenin. Baada ya kifo cha Lenin, Trotsky alikosana na Stalin, akafukuzwa kutoka Chama cha Kikomunisti, kisha akauawa baadaye. Jina lake hata lilifutwa kutoka katika ensaiklopedia za Sovieti. Kupotoshwa kama huko kwa historia, hata kufikia hatua ya kuteketeza vitabu visivyokubaliana na malengo fulani, ni zoea la kawaida la serikali nyingi za kimabavu.

Hata hivyo, kupotosha historia ni zoea la kale sana, lililoanza mapema angalau katika Misri na Ashuru. Mafarao, wafalme, na maliki wenye kiburi na majivuno walihakikisha kwamba waliacha historia ya matendo yenye kusifika. Kwa hiyo mafanikio yalitiliwa chumvi mara nyingi, ilhali mambo yoyote yenye kufedhehesha au ya aibu, kama vile kushindwa vitani, yalifichwa, yalisahauliwa kabisa, au hata kutoripotiwa nyakati nyingine. Kinyume kabisa cha hilo, historia ya Waisraeli iliyorekodiwa kwenye Biblia inatia ndani makosa na sifa nzuri za wafalme na raia pia.

Wanahistoria huchunguzaje usahihi wa maandishi ya kale? Wao huyalinganisha na rekodi za kale za kodi, mifumo ya sheria, matangazo ya minada ya watumwa, barua za kibiashara na za kibinafsi, maandishi yaliyoandikwa kwenye vipande vya vyungu, maandishi ya safari za meli, na vifaa vilivyopatikana makaburini. Vitu hivyo hutoa habari zaidi au habari mpya kuhusu maandishi rasmi yaliyopo. Kunapokuwa na mapengo au tashwishi, wanahistoria waaminifu kwa kawaida hukiri jambo hilo, japo wanaweza kubuni nadharia zao wenyewe ili kujaza mapengo hayo. Kwa vyovyote vile, wasomaji wenye hekima huchunguza vichapo mbalimbali endapo wanataka maelezo yenye usawaziko kuhusu matukio.

Licha ya magumu yote yanayowakabili wanahistoria, kazi yao huandaa habari muhimu sana. Kitabu kimoja cha historia chaeleza hivi: “Ijapokuwa si rahisi kuandika historia ya ulimwengu, . . . historia hiyo ni ya maana, hata ni muhimu sana kwetu.” Mbali na kutuelewesha kuhusu mambo yaliyopita, historia inaweza kutufahamisha mengi zaidi kuhusu hali ya sasa ya mwanadamu. Mathalani, sisi hugundua mara moja kwamba hata watu wa kale walidhihirisha sifa zilezile za kibinadamu zinazodhihirishwa na watu leo. Sifa hizo za kawaida zimeathiri sana historia, na labda zimetokeza msemo wa kwamba hakuna jambo jipya duniani. Lakini je, mkataa huo unategemea uhakika na kufikiri kuzuri?

Je, Hakuna Jambo Jipya Duniani?

Je, kweli tunaweza kutabiri kwa uhakika mambo ya wakati ujao tukitegemea mambo yaliyopita? Matukio fulani-fulani hutukia tena. Kwa mfano, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Henry Kissinger alisema hivi: “Kila ustaarabu uliowahi kuwapo uliporomoka hatimaye.” Akaongezea hivi: “Historia ni simulizi la jitihada zilizoambulia patupu, na miradi isiyotimizwa. . . . Kwa hiyo, mtu akiwa mwanahistoria, hana budi kukubali kwamba misiba haiepukiki.”

Hakuna milki zozote mbili zilizoporomoka kwa njia ileile. Babiloni ilishindwa usiku mmoja na Wamedi na Waajemi mwaka wa 539 K.W.K. Ugiriki ilisambaratika na kuwa falme kadhaa baada ya kifo cha Aleksanda Mkuu, hatimaye ilishindwa na Milki ya Roma. Hata hivyo, kuporomoka kwa Roma kumezusha ubishi. Mwanahistoria Gerald Schlabach auliza hivi: “Roma iliporomoka lini? Je, kweli iliporomoka? Jambo fulani lilibadilika huko Ulaya Magharibi kati ya mwaka wa 400 W.K. na 600 W.K. Lakini mengi zaidi yalibaki vilevile.” * Ni wazi kwamba mambo fulani ya historia hutukia tena, ilhali mengine hayatukii tena.

Somo moja la historia linalotokea tena na tena ni kushindwa kwa utawala wa mwanadamu. Miaka nenda miaka rudi jitihada za kutafuta serikali nzuri zimeharibiwa na ubinafsi, kutozingatia wakati ujao, pupa, ufisadi, ubaguzi, na hasa tamaa ya kupata na kushikilia mamlaka. Hivyo basi, enzi zilizopita zilikuwa na harakati za kurundika silaha, mikataba isiyofua dafu, vita, michafuko ya kijamii na jeuri, ubaguzi katika ugawanyaji wa mali, na kuzorota kwa uchumi wa nchi mbalimbali.

Kwa mfano, ona mambo yanayosemwa na kichapo The Columbia History of the World kuhusu jinsi ustaarabu wa Magharibi ulivyoathiri ulimwengu wote: “Baada ya Colombus na Cortes kuwahamasisha wenyeji wa Ulaya Magharibi kuhusu fursa zilizopo, tamaa yao ya kupata wafuasi, faida, na umashuhuri ilichochewa sana na ustaarabu wa Magharibi ukaenezwa kwa lazima karibu ulimwenguni pote. Wakiwa na tamaa kubwa ya kusambaa na kwa kutumia silaha kali, washindi hao waliutiisha ulimwengu kwa nguvu chini ya mamlaka ya serikali kubwa za Ulaya . . . Kwa ufupi, wenyeji wa mabara hayo [Afrika, Asia, na Amerika] walitumiwa vibaya sana na kikatili.” Maneno yapatikanayo kwenye Biblia katika Mhubiri 8:9 (Chapa ya 1989): ‘Mtu amekuwa na mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake’ ni ya kweli kama nini!

Huenda rekodi hiyo yenye kusikitisha ndiyo iliyomchochea mwanafalsafa mmoja Mjerumani aseme kwamba somo pekee tunalojifunza kutokana na historia ni kwamba wanadamu hawajifunzi jambo lolote kutokana na historia. Andiko la Yeremia 10:23 lasema: “Njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” Twapaswa kuhangaikia kushindwa kwetu kuelekeza hatua zetu hasa leo. Kwa nini? Kwa sababu tunakumbwa na matatizo mabaya sana yasiyo na kifani. Basi tutakabilianaje nayo?

Matatizo Yasiyo na Kifani

Katika historia yote ya wanadamu, dunia nzima haijawahi kamwe kutishwa na matatizo chungu nzima kama ya kuharibiwa kwa misitu, mmomonyoko wa udongo, kuenea kwa jangwa, kuangamia kwa jamii nzimanzima za mimea na wanyama, kuharibiwa kwa ozoni ya angahewa, uchafuzi, kuongezeka kwa joto duniani, kuchafuliwa sana kwa bahari, na kuongezeka kasi kwa idadi ya watu.

“Tatizo jingine linalokabili jamii za kisasa ni jinsi mabadiliko hufanyika haraka,” chasema kitabu A Green History of the World. Ed Ayres, mhariri wa gazeti la World Watch, aandika hivi: “Tunakabili jambo fulani tusiloweza kuelewa kamwe kiasi cha kutolitambua, kujapokuwa na ushuhuda wa kutosha. Kwetu sisi, ‘jambo’ hilo ni kutokea ghafula kwa mabadiliko makubwa sana ya kibiolojia katika ulimwengu ambao umekuwa ukitutegemeza.”

Kwa sababu ya matatizo hayo na mengine mengi, mwanahistoria Pardon E. Tillinghast asema hivi: “Mwelekeo wa jamii umezidi kuwa tata zaidi, na utata huo unaogofya wengi wetu. Wanahistoria wenye ujuzi wanaweza kuandaa mwelekezo gani kwa watu waliotatanika leo? Yaonekana si mwelekezo madhubuti.”

Huenda wanahistoria wenye ujuzi wasijue jambo la kufanya wala shauri la kutoa, lakini bila shaka Muumba wetu hawezi kushindwa. Isitoshe, alitabiri kwenye Biblia kwamba katika siku za mwisho, kungekuwa na “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo,” ulimwenguni. (2 Timotheo 3:1-5) Lakini Mungu amefanya jambo ambalo hata wanahistoria hawawezi kufanya—ameandaa suluhisho, kama tutakavyoona kwenye makala inayofuata.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 16 Maoni ya Schlabach yanapatana na utabiri wa nabii Danieli kwamba mahali pa Milki ya Roma pangechukuliwa na ufalme mwingine ulioibuka kutoka kwa Roma. Ona sura ya 4 na 9 ya kitabu Sikiliza Unabii wa Danieli!, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Blabu katika ukurasa wa 5]

“Historia yoyote inayosimuliwa na wenye mamlaka . . . ni sharti ichunguzwe kwa uangalifu sana.”MICHAEL STANFORD, MWANAHISTORIA

[Picha katika ukurasa wa 4]

Maliki Nero

[Hisani]

Roma, Musei Capitolini

[Picha katika ukurasa wa 7]

Katika miaka yote ‘mtu amekuwa na mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake’

[Hisani]

“The Conquerors,” na Pierre Fritel. Kutia ndani (kushoto hadi kulia): Ramses wa Pili, Attila, Hannibal, Tamerlane, Yulio Kaisari (katikati), Napoléon wa Kwanza, Aleksanda Mkuu, Nebukadneza, na Charlemagne. Kutoka kwa kitabu The Library of Historic Characters and Famous Events, buku la Tatu, 1895; ndege: USAF photo