Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hali ya Mapigano ya Kisasa

Hali ya Mapigano ya Kisasa

Hali ya Mapigano ya Kisasa

KAMBII hiyo ya wakimbizi ilijengwa upesi ili kuwapa makazi watu 1,548 waliowasili ghafula kutoka nchi jirani ya Afrika. Mahema ya rangi ya buluu na kaki yalikuwa yamesimamishwa kwenye uwanja wenye matope uliokuwa ndani ya msitu wa michikichi. Hakukuwa na umeme, matandiko, wala mabomba ya maji au vyoo humo kambini. Kulikuwa kukinyesha. Wakimbizi walichimba mitaro kwa vijiti ili kuzuia maji kuingia ndani ya mahema. Mashirika mawili ya kimataifa ya kutoa misaada yalifanya kazi kwa bidii nyingi ili kuboresha hali ya maisha kambini.

Mapema, wakimbizi hao walikuwa wamefanya bidii kupanda ndege moja kuukuu ya kubeba mizigo ili kukimbia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yamekumba nchi yao kwa miaka mingi. Mapigano hayo hayakufanywa kwa vifaru wala ndege za kumimina mabomu. Yalianza wakati wanajeshi 150 hivi wenye bunduki za rashasha walipovamia nchi. Katika miaka iliyofuata, wanajeshi hao waliteka kijiji kimoja baada ya kingine, wakalazimisha raia kutoa kodi, wakafanya wengine wajiunge nao, na kuua mtu yeyote aliyejaribu kupinga. Hatimaye, waliteka nchi nzima.

Miongoni mwa wakimbizi palikuwa na mwanamke mmoja kijana aitwaye Esther. “Kumpoteza mume wangu katika mapigano hayo ndilo tukio baya zaidi kuwahi kunipata,” akasema. “Walimpiga risasi. Kuna hofu nyingi. Unaposikia kilio, unafikiri kuna mtu anayekuja kukuua. Kila unapomwona mtu akiwa na bunduki, unafikiri atakuua. Sikutulia kamwe. Ni katika kambi hii tu ndipo nimeweza kulala usiku. Nilipokuwa nyumbani singeweza kulala. Hapa nalala fofofo.”

“Unamaanisha unapata usingizi kwenye hema hii iliyolowa maji?” akauliza mwandishi mmoja wa Amkeni!

Esther akaangua kicheko. “Hata nikilala kwenye tope hili, bado nitapata usingizi wa kutosha kuliko nilikotoka.”

Ambrose, mwenye umri wa miaka kumi, alikuwa akikimbia maeneo yenye mapigano akiwa na familia yao karibu muda wote wa maisha yake. “Ningependa kuwe na amani ili niweze kurudi shuleni,” akasema. “Miaka inasonga.”

Kpana, mwenye umri wa miaka tisa, ana macho ya hudhurungi yenye kuvutia. Alipoulizwa ni jambo gani analokumbuka tangu utotoni, alijibu hivi bila kusita: “Mapigano! Mzozano!”

Mapigano ambayo watu hao walikuwa wameyakimbia yamekuwa ya kawaida katika miaka ya karibuni. Kulingana na ripoti moja, kati ya mapigano makubwa 49 ambayo yamekuwapo tangu mwaka wa 1990, silaha nyepesi zimetumiwa kwenye mapigano 46. Tofauti na mapigano yenye kutumia upanga au mkuki ambayo huhitaji wapiganaji kuwa na uzoefu mkubwa, silaha nyepesi zinaweza kutumiwa na mtu yeyote, awe ana uzoefu au la. * Mara nyingi vijana na watoto huandikishwa jeshini na kulazimishwa kupora, kukata watu viungo, na kuua.

Mengi ya mapigano hayo si kati ya nchi moja na nyingine, bali ni ya wenyewe kwa wenyewe. Wapiganaji si wanajeshi waliozoezwa katika viwanja vya vita, bali wengi wao ni wakazi wa majiji, miji na vijiji. Kwa sababu mengi ya mapigano hayo hufanywa na watu wasio na mafunzo ya kijeshi, sheria za kawaida za mapigano huvunjwa mara nyingi. Kwa sababu hiyo, imekuwa kawaida kwa wanaume, wanawake na watoto wasio na silaha kushambuliwa vikali. Inaaminika kwamba zaidi ya asilimia 90 ya watu wanaouawa katika mapigano ya siku hizi ni raia wa kawaida. Katika mapigano hayo silaha ndogo-ndogo na silaha nyepesi zimetumika sana.

Bila shaka, bunduki hazisababishi mapigano moja kwa moja—watu walikuwa wakipigana hata kabla ya baruti kugunduliwa. Hata hivyo, akiba kubwa ya bunduki huenda ikachochea mapigano badala ya kuchochea majadiliano ya amani. Kuwapo kwa silaha huenda kukarefusha muda wa pigano na kuzidisha mauaji.

Silaha nyepesi zinazotumika katika mapigano ya siku hizi zimesababisha hasara kubwa. Katika miaka ya 1990, silaha nyepesi zilitumiwa kuua watu zaidi ya milioni nne. Watu wengine zaidi ya milioni 40 wamekuwa wakimbizi au wamekosa makao. Silaha ndogo-ndogo zimeharibu utaratibu wa kisiasa, kijamii, kiuchumi na mazingira ya watu wanaoishi kwenye maeneo yenye mapigano. Shughuli za kutoa msaada wa dharura, kutunza wakimbizi, kudumisha amani, na kuingilia mambo ya kijeshi zimegharimu jamii ya kimataifa makumi ya mabilioni ya dola za Marekani.

Kwa sababu gani silaha ndogo-ndogo zimetumiwa sana katika mapigano ya siku hizi? Zinatoka wapi? Je, ni jambo gani liwezalo kufanywa ili kupunguza au kumaliza hatari yake? Tutazungumzia maswali hayo katika makala zifuatazo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Mtajo “silaha ndogo-ndogo” humaanisha bunduki na bastola—silaha zinazobebwa na mtu mmoja; na “silaha nyepesi” hutia ndani bunduki za rasharasha, mizinga na vyombo vya kurushia makombora, ambazo nyakati nyingine huhitaji kushughulikiwa na watu wawili.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

UN PHOTO 186797/J. Isaac